WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, October 16, 2012

TUMO HATARINI, UDINI, UKABILA UMEINGIA KATIKA TAIFA LETU



MOJA ya kitu tunachojivunia Watanzania ni undugu wetu ambao unafanya mtu yeyote kuweza kuishi katika ardhi ya nchi yetu popote bila kujali dini au kabila lake. Hili ni jambo la kujivunia sana.
Lakini taratibu udini na ukabila umeanza kuingia kwa kasi katika nchi yetu, kitu ambacho naona ni hatari sana kwa vizazi vyetu na vijavyo. Matukio ya wiki iliyopita huko Mbagala jijini Dar es Salaam ni sawa na yaliyotokea Zanzibar. Makanisa yamechomwa moto. Siku hizi kiongozi anadiriki kusimama jukwaani na kudai chama fulani ni cha dini au mtu fulani achaguliwe kwa kuwa ni kutoka ‘kanda yetu.’ Hili ni jambo la hatari.

Binafsi nakumbuka sana hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa Hoteli ya Kilimanjaro mbele ya Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania Machi 13, 1995, ambapo alitaja nyufa tano zinazolitikisa taifa letu hadi kufikia katika msingi ule imara wa utaifa uliojengwa kwa muda mrefu. Nyufa zipo kwenye muungano, kuendesha mambo bila kujali sheria, rushwa na udini na ukabila.
Kwa muda mrefu sasa, nchini mwetu kumesikika malalamiko au manung’uniko ya wafuasi wa dini moja kudai kukandamizwa au kunyimwa fursa sawa za elimu katika nchi yetu, ni wazi walalamikaji wanaona kuna udini. 
Huko nyumba yalitolewa madai ya haki za Waislam kama yalivyotolewa na kauli ya Baraza Kuu la Jumuia na Taasisi za Kiislam Tanzania mwaka 1993. Mwaka 1998 kulitolewa waraka kwa serikali kulaumu Kanisa Katoliki na Serikali ya CCM katika hili. Kuna malalamiko yanayojirudiarudia licha ya kutolewa majibu na mamlaka husika. 
Mwalimu alipokuwa akila kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika alizungumzia tofauti ya elimu kati ya Wakristu na Waislam, hiyo ilikuwa Desemba 10, 1962 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na alisema, nanukuu:
“…uhasama baina ya waumini wa Kiislam na Kikristo ambao unaweza kuenezwa na fikra potofu , kama tunavyojua, ni matokeo ya serikali ya kikoloni kutojihusisha hata kidogo na elimu kwa Waafrika na kwa maana hiyo wengi wa wale walioipata kwa kiwango chochote, walifanya hivyo kupitia shule za misheni na kwa hiyo ni Wakristo, hivyo wengi wao ni Wahaya, Wanyakyusa na Wachaga…”
Kwangu mimi haya yalikuwa mawazo sahihi ya Mwalimu na hakuna aliyebisha, lakini watu wasioitakia mema nchi hii wakachukulia maneno hayo kwa kugeuza kibao na kudai Waislam hawajapewa elimu kwa makusudi. 
Mwaka 1970 serikali ya Nyerere iliamua kutaifisha shule zote za misheni na za binafsi katika nchi yetu kama hatua muhimu ya kupunguza tofauti katika elimu kwa Waislam na Wakristo maana kuanzia hapo hapakuwepo tena shule za misheni. Matokeo ya utaifishwaji ule, yameharakisha sana upatikanaji wa elimu kwa Waislam wengi hapa nchini. 
Alhaji Ally Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili aliliona tatizo la elimu kwa Waislam na wakati anafungua Ofisi za Shirika la World Muslim League mwaka 1998 jijini Dar es Salaam, alisema “… Ndugu Waislam, punguzeni malalamiko dhidi ya serikali na muanze kufanya kazi… tujenge vyuo vya elimu ya kizungu ili tuwaandae watoto wetu kushika nafasi za uongozi…” naamini huu ulikuwa mwongozo bora na safi kwa Waislam.
Mwaka huu, 2012 baadhi ya Waislam wamelalamikia matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita kwa shule za Waislam hata kuwafanya wengine wasiwe na imani na uongozi wa Baraza la Mitihani (NECTA) lakini Sadiki Godigodi ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation alitoa maelezo ya kueleweka sana katika gazeti la Majira la Jumatatu, Juni 25, mwaka huu. 
Alisema wasahishaji wakati wa kufanya kazi hiyo huwa wanaona namba za watahiniwa wala siyo majina yao, hivyo hawajui karatasi hii ya Mwislam au ya Mkristo! Akaonya kuwa wote wanaopandikiza chuki na kunufaika na mgogoro huo waache kwani wataangamiza taifa. 
Gazeti la Uhuru la Jumatatu, Juni 28, 1993 lililoandika wazi upendeleo uliofanywa hapa Dar es Salaam katika kuchagua watoto wa kuingia kidato cha kwanza, majina ya watoto 84 Wakristo yakiachwa na nafasi zao wakapatiwa wenzao wa Kiislam matokeo yake gazeti hilo la Jumatano, Juni 30, 1993 yalitangazwa majina ya walimu 58 waliohusika na kashfa hiyo ya upendeleo kwa watoto wa Waislam na kwa mujibu wa sheria walisimamishwa kazi hapa Dar es Salaam.
Nimetoa mifano hii kuonesha kuwa udini katika nchi yetu upo na umeanza kugawa taifa na sijaona viongozi wakikemea kwa nguvu zote. Nawasihi Watanzania kwamba tusiupe mwanya ufa huu wa udini na ukabila utumalize kwani tutajuta.
Naamini wale wote wanaoujua Ukristo au Uislam hawapayuki ovyo, ni wasikivu, hawana dharau kwa wasiokuwa wa dini yao badala yake wanashirikiana kutunza amani. Maalim Hassan Yahya Hussein aliwahi kuniambia kuwa sura ya IV Maidah aya ya 82 inasema, Uislamu hauchukii Ukristo, sasa vipi Waislam halisi wachome makanisa? Matukio kama yale ya Zanzibar na juzijuzi Mbagala ni ya kulaaniwa kwa wapenda amani wote. 
Nawasihi Waanzania kwamba tuepuke vishawishi vya kutugawa kwa misingi ya udini na ukabila, tuendelee kuwa Watanzania wenye imani za kiroho tofauti kutokana na mapokeo tuliyonayo, bila kufanya hivyo, tutaiingiza nchi katika matatizo mazito.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

source Vujimambo blog

No comments:

Post a Comment