WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, December 31, 2015

BAADHI YA MATUKIO YALIYO TIKISA TAIFA KATIKA MWAKA 2015



mwaka 2015 kama taifa tumeshuhudia ajali nyingi sana zikiendelea kudhoofisha uchumi wa taifa letu kwa kuwapoteza watanzania wenzetu wengi ambao wamefarika katika ajali zilizosababishwa na ajali nyingi za barabarani kama makala ya hapo juu ilivyoelezea. umekuwa mwaka wa huzuni kubwa kwani kuna baadhi ya ajali tungeweza kuzizuia kama wahusika wangekuwa makini.




Katka mwaka wa 2015 Mheshimiwa Zitto aliaga rasmi kuachana na chama cha CHADEMA; lilikuwa ni tukio ambalo liligusa nyoyo za wapenzi wengi wa siasa wale wa upinzani na wa chama tawala pia.



Katika Mwaka huu wa 2015 Mheshimiwa Lowassa alikihama chama cha mapinduzi na kujiunga na chama cha Upinzani CHADEMA ili kuweza kuwania kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.



DR. John Pombe Magufuli aliteuliwa na chama chake ili kuogombea nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania, kitu ambacho hakikutarajiwa na wengi, kutoka kuwa hakuwa na makundi ndani ya chama hicho , uwajibikaji wake uadilifu wake ndivyo vilimfikisha hapo alipofika.



Katka Mwaka wa 2015 tulishuhudia Prof Ibrahim Lipumba akiamua kuacha na siasa kama mwenyekiti wa CUF na Mwenyekiti Pacha wa UKAWA, kwa kuto ridhika na taratibu ndani ya UKAWA katika harakati za kumpata mgombea urais kupitia muungano huo.


Dr Slaa pia katika mwaka huu wa 2015 aliamua kuachana na siasa akiwa kama katibu mkuu wa CHADEMA. hilo lilitoka na tofauti zilizojitokeza ndani ya UKAWA. lilikuwa ni tukio lililovuta hisia za wengi.



Tukio nyingine kubwa katika mwaka wa 2015 ni CCM kushinda uchaguzi Mkuu uliofanyika October 2015 ; ambapo mgombea wa urais wa CCM Dr. JPM na Makamu wa Kwanza Mwanamke katika historia ya Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan walikabidhiwa vyeti vya ushindi.



DR. JPM awashukuru wana CCM kwa kumchagua na kuanza kuwasha cheche kuhusu unafiki wa baadhi ya wanachama wa chama hicho


Tumeshuhudia Rais DR. JPM akianza kazi kwa ujasili wa kuwa tayari kutumbua majipu ambayo yamerudisha sana nyuma maendeleo ya watanzania.

katika mwaka huu 2015 tuliona wananchi kuguswa na hotuma ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alipofungua Bunge la 11 kwani ilikuwa imegusa kiu yao na matarajio yao ya muda mrefu. ilikuwa hotuba ambayo imeonyesha mwelekeo wa serikali yake kwa kipindi cha miaka 5 ya utumishi wake kwa umma wa watanzania hasa wanyonge.


Ilikuwa shangwe na vigelegele wakati DR.JPM alivyofanya ziara za kushitukiza na kugundua jinsi watanzania walivyokuwa wakikosa hudumu muhimu kwa uzembe wa wa watendaji, hivyo Katibu Mkuu Kiongozi alitoa mchumuisho wa ziara ya Mheshimiwa Rais na majumuisho ya uwajibikaji kwa wazembe.


Katika mwaka huu wa 2015 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa alifanya ziara ya Ghafla Bandarini Na TRA na kujionea njinsi Taifa lilivyokuwa likipoteza kiasi kukubwa cha mapato kwa Tamaa ya watendaji wachacche ambao walikuwa hawana maadili.  ziara hiyo iliweza kubadilisha ukusanyaji wa mapato na serikali kuanza kupata mapato mengi zaidi.


Katika mwaka wa 2015 tumeshuhudia jinsi Rais Dr. JPM akishiriki kufanya usafi wa mazingira. Lilikuwa ni tukio ambalo liliweza kumjumuisha kila mtu kushiriki kufanya usafi ikiwa na sehemu ya kusherekea siku ya kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu.

Tunawatakieni sherehe njema za kuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 kwa amani na utulivu na tuendelee kumwombea Rais wetu ili katika mwaka huu wa 2016 aendelee kutekeleza majuku yake, kwa kasi kwa faida ya watanzania kama alivyoanza. Mwenyezi Mungu amjalie afya njema  Amen
.

Monday, December 28, 2015

MCHANGO WA WAPINZANI KATIKA MAENDELEO YA TAIFA;


MCHANGO WA WAPINZANI KATIKA MAENDELEO YA TAIFA;

BADO TUNAHITAJI MCHANGO WA UPINZANI KATIKA KUBORESHA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA NA WA HAKI TUKIZINGATIA KUWA:

  • “Siasa si mchezo mchafu, ila wachezaji wake ndiyo wachafu.”


  • Litakuwa ni jambo la kuheshimiwa ka viongozi wetu wetu watakuwa wakweli na wenye Uzalendo wa kweli ndani ya mioyo kwa faida ya wananchi wao.


  • Confucius aliwahi sema kuwa  ‘Utajiri na vyeo ndivyo vitu ambavyo kila bianadamu anavitamani; lakini ikiwa njia ya kuvipata ni kwa kwenda kinyume na misingi yake, anapaswa ajiepushe navyo.’


  • Rudolph Giuliani aliwahi sema kuwa ‘Kiongozi huchaguliwa kwa kuwa yeyote anayemuweka pale huwa anaamini maamuzi, tabia na uwezo wa maarifa yake – siyo ujuzi wa kufuata maoni. Ni wajibu wa kiongozi kuchukua hatua kufuatana na sifa hizo.’


  • “kiongozi ajiulize ni vipi atalitumikia Taifa na si Taifa kumtumikia yeye Kiongozi Umashuhuri na uzuri wa Kiongozi unatokana na hekima, busara, uchapakazi, ufanisi, ufuatiliaji, uimara, uungwana, uwajibikaji na unyenyekevu wake. Ama fikra endelevu na upeo wa kuongoza ni muhimu na si kauli tamu za kuwafurahisha viongozi wengine”

 

Demokrasia kama falsafa ya Plato ambayo inahusiana na uendeshaji wa shughuli za kisiasa inalenga zaidi katika  utumishi kwa umma na uendeshaji wa jamii na taifa. Wananchi wote hawawezi ongoza nchi kwa mara moja; Katika msingi huu wananchi kutokana na wingi wao waliridhika itakuwa sio rahisi kwa wao wote kukutana, kufanya maamuzi na kuyasimamia moja kwa moja maamuzi hayo yanayowahusu wao kama jamii; dhana ya kuwachagua viongozi wachache huzaliwa kwa chimbuko hili na kuruhusiwa kuunda serikali.


Tatizo kubwa tulilonalo kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa wachache walio katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi. Kwani inatupasa kutambua kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu. Lakini ridhaa hiyo haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na amana, kwamba waongozi watatekeleza dhamana  na wajibu  wao kwa makubaliano na maelewano ya kufuata barabara na kuheshimu ipasavyo kanuni na maadili fulani yanayoitambulisha na kuiongoza jamii husika. 


Hapa ndipo chimbuko la demokrasia linapochimbuka na dhana ya Upinzani kwa masilahi ya wananchi linapoanzia. Lengo la vyama nya upinzani ni kuleta ushindani wa kisiasa dhidi ya chama kinachotawala katika nchi husika. Upinzani unasimama kama mbaadala wa wananchi katika kukosoa shughuli za serikali ambazo huzitenda kinyume na utaratibu ambao unafaida kwa taifa husika.


Pamoja na hamu kubwa ya upinzani kushika hatamu lakini husaidia kuleta uwajibikaji na uadilifu kwa viongozi ambao wameshika hatamu ya uongozi. ikumbukwe kuwa kiongozi muadilifu hakubali kufuata  au kutoa maamuzi bila kufanya ukadirifu wa hoja na hali husika. Uongozi ni kujitolea na kuweka matwakwa na maslahi ya wengine kuwa mstari wa mbele na si matakwa binafsi na kujinufaisha.


Marehemu John Kennedy rais wa Marekani alitoa kauli moja maarufu iliyosema kuwa. Tuchague viongozi si kwa kuangalia vyama au sura, bali tuangalie uwezo wao wa kuongoza, kuhamasisha na kufanya kazi. Tupime kauli zao na matokeo ya kazi zao kama wanavyojinadi. Hii ndio dhana ya upinzani inapoingia kwani hutupa sisi wananchi nafasi zaidi ya kupima uwezo wa viongozi kupitia vyama vyao nani unafaa kuongoza nchi kwa kipindi Fulani kulingana na mahitaji ya Taifa.

Tukumbuke kuwa, Serikali ni watu, inaundwa na watu tuliowachagua na tunawapa watu hawa na Serikali mamlaka makubwa ya kutuongoza, kupanga na kulinda Taifa na Katiba yetu. Dhamana hii imefanywa kwa kuaminiana kuwa Serikali itafanya kazi kwa manufaa ya Wananchi wake na kwa matakwa na utashi wa Wananchi wake.


Upinzani tunahitaji ni ule ambao unatija kwa taifa, kwani taifa letu linahitaji utulivu, amani na upendo miongoni mwa wananchi wake na kudumisha umoja wa kitaifa kupitia viongozi wake; kiongozi muadilifu pia hufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli katika nchi vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye magomvi na huhasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na haki na uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya maisha na mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi wala upinzani wa kweli ambao haujejaa uroho wa madaraka kwa nia binafsi.

Uadilifu wa uongozi unadai kuheshimu nguvu ya hoja na fikra bora na hayo yanaweza kupatikana tu iwapo nchi inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Hivyo, katika kutoa uongozi sahihi, kwa kuzingatia maslahi bora ya nchi na watu wake, haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu, hapana budi kwa kiongozi kuiamini, kuiheshimu na kuifuata barabara misingi ya kidemokrasia.


Bado binadamu si mkamilifu na kwa vyovyote vile hufikia mahala akafanya maamuzi ambayo si sahihi hata kama yalifanywa kwa nia njema na kwa kuzingatia taarifa zilizopatikana wakati maamuzi hayo yanafanywa. Hayo yanaeleweka na kiongozi muadilifu anapaswa kuyakubali na kuliomba radhi Taifa. Hiki ndiyo kilele na kigezo kikuu cha uadilifu wa uongozi katika siasa. Kukubali kubeba dhamana kwa madhara yaliyotokana na maamuzi yako au yaliyofanywa kwa jina lako.

Maamuzi ya kiongozi wa kisiasa huathiri taifa zima, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila hatua anayochukua. Kama viongozi wetu wa bunge wakikiri kuwa walikurupuka katika kufanya maamuzi hayo bila kuyafanyia kazi vizuri heshima na uwajibikaji wa kuliendesha bunge letu itarudi. Tukubali tu kuwa njia ya kusonga mbele ni kukubali kutofautiana katika fikra lakini tubaki kuwa wamoja.


Kama taifa bado tunahitaji upinzani katika uendeshaji wa taifa letu ili kuweza kuikumbusha na kuibana serikali pale ambapo hukiuka utekelezaji wa majukumu yake ya maendeleo kwa wananchi wake; na pale inapokiuka utaratibu wa demokrasia na kukiuka haki za binadamu na matumizi mabaya ya selikali.

Mungu ibarika Tanzania na watu wake.


                           AMEN

Friday, December 25, 2015

NGUVU YA UTUMBUAJI MAJIPU NA FALSAFA YA MPE KAISARI YALIO YA KAISARI:



Swali la msingi ambalo najiuliza sana hivi sasa hii dhana ya utumbuaji wa majipu ambao umelipatia sana hasara taifa letu asili yake wapi na kwa nini tumefikia hapa ambapo tumefika leo hii kama taifa tukiwa tumepoteza mapato mengi sana ya taifa kwa muda mrefu na taifa kukosa mwelekeo.

Jambo la msingi ambalo halipingiki ni kuwa viongozi wa taifa letu ambao walipewa dhamana ya kutuongoza walikuwa wakitekeleza dhana ya uongozi bora kwa tafsiri binafsi. Dhana ya uongozi inatakiwa ianzie wapi?

Dhana ya uongozi wa namna yeyote ile unafaa uanzie nyumbani kwa kila mtu  uongozi ni uwezo wa kuweza kuyakabili kwanza matatizo  yako mwenyewe na kufanya maamuzi sahihi bila kushawishiwa na mtu mwingine yeyote yule.

kwa kufanya hivyo utakuwa umefanikiwa kuyatawala maisha yako kulingana utaratibu ambao wewe mwenyewe umejiwekea kuanzia ndani ya familia yako;  ukifanikiwa hili unakuwa umefaulu katika mtihani huu wa kwanza wa uongozi ndipo jamii inapoanza kukuona kuwa hata ukipata nafasi ya  kuwaongoza wao pia utaweza kufanya maamuzi sahihi. 

 Kwa maneno mengine ni uwezo au njia ya kuweza kuwashawishi watu ili waweze kufanya kitu au kufikia lengo fulani la kikundi kwa ridhaa yao wenyewe. ili uongozi uwe bora ni lazima kuwe na kiongozi anayeongoza kundi fulani la watu au jamii husika kwa usahihi na kufuata maaadili ya uongozi yanayozingatia uaminifu, ukweli na uadilifu.

Katika kila jamii kuna umuhimu wa kuwa na kiongozi kunatokana na ukweli kwamba watu wanapaswa kuwa na namna ya kuunganisha nguvu zao ili kufikia malengo yao. Katika  kila jamii, ni lazima kuwepo na mikakati ya kuunganisha nguvu, vipaji, uwezo na stadi mbalimbali za wana jamii. 

Wajibu wa msingi wa kiongozi yoyote ni kusaidia kuunganisha uwezo wa watu, kuratibu, kusimamia shughuli za watu, na kila inapobidi aonyeshe njia itakayosaidia kufikia lengo. Hii ndio dhana ya serikali ya awamu ya tano chini ya Dr. John Magufuli ambaye ameonyesha utayari wa kufanya kazi na viongozi ambao wataonyesha uadilifu katika kazi zao za kuwatumikia watanzania ili kuwakwamua  kutoka katika wimbi la umasikini na kuwawajibisha viongozi wote wabadhilifu ambao wamehujumu uchumi wa watanzania.

Kwa dhana ya Plato uongozi ni dhana  au taaluma inayompa muhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaoongozwa kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo ya Taifa lao ili kujikwamua kutoka katika tabaka kandamizi ambalo linawasumbua. Kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao.

Uongozi bora una mchango mkubwa sana katika uimara wa jamii. Lakini tufahamu kuwa Ubora wa kiongozi unachangiwa na vitu vingi lakini tusisahau kuwa vile vile uongozi au kiongozi bora hutoka kwa Mungu. Kama rais wa awamu ya tano alivyowahi sema kuwa serikali yake ina kazi na dhamana nzito wa kuwajengea uchumi wa kati jamii ya watanzania kwa kuelewa kuwa  wakiwatendea watanzania ndivyo sivyo adhabu yao itatoka pande mbili kwa Mungu na kwa jamii iliyowachagua.

Ikumbukwe kuwa viongozi wetu waelewe kuwa ni viongozi muhimu sana ambao wataingia katika vitabu vya kumbukumbu ya Taifa hili kuhusu ubora au ubaya kwa Taifa letu.  

swali la kuwauliza Viongozi wetu wa awamu ya tano Je watendaji wake watampa Kaisari yaliyo ya Kaisari  ili kutimiza yale waliokuwa wamehaidi wakati wa kampeni ili kubadilisha maisha ya watanzania?

Je Viongozi wa awamu ya Tano chini ya mwitikio wa Hapa Kazi Tu chini ya DR. Magufuli   wanafahamu ukubwa na umuhimu wa maamuzi yao kwa jamii ya Tanzania?

Je viongozi wetu wa awamu ya tano  wametawaliwa na maadili gani katika utendaji wa kazi yaokuendesha serikali? Ni ukweli usio fichika kuwa ili waweze kufanikiwa katika kutumiza maendeleo ya wananchi
ni lazima wazingatia maadili ya msingi ya kufanikisha  na kusimamia kwa weledi mkubwa falfasa ya Mpe kaizari yaliyo ya kaizari hasa katika kipengele ya ukusanyaji kodi ili kuimalisha mfuko wa serikali kwa maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Rais Dr Magufuli ameonyesha nia dhabiti katika kutekeleza falfasa hii kwa kuanza kutumbua majipu na kupaisha makusanyo ya kodi katika mwezi huu wa December 2015. Kama taifa tunafarijika kuwa timu nzima ya serikali kwa nia nzuri sasa wanawajibika na kuwawajibisha wale wote ambao walikuwa wanakwenda kinyume na falfasa hii ambayo Yesu aliwambia wafarisayo kuhusu dhana ya kutoa kodi.

Tunaendelea kufarijika kila siku njisi watendaji wakuu wa serikali wanavyowajibika sasa na kuruduisha imani kwa Watanzania masikini kuhusu mabadiliko ya maisha yao na jamii nzima. Hivyo ni vyema waendelee kutimiza wajibu badala ya kujali maslahi yao binafsi yatokanayo na itikadi au faida ambayo wanafikiria wao tu watanufaika nayo na sio taifa;

Daima Rais wetu ameendelee kusisitiza kuwa Tanzania niyetu sote na rasilimali ambazo tumejaliwa ni zetu sote na sio mali ya kikundi Fulani tu. Na ameendelea kusisitiza kuwa  anafafahamu wananchi wanatamani nini; wanatamani watoto wao wapate elimu bora ndio maana sasa serikali imerudisha tena elimu bure kwa watoto wetu;

Anajua watanzania wanataka umoja  ndio maana anaendelea kuhubiri na kuwaomba  wananchi kuendelea kudumisha amani iliyopo katika pande zote mbili za jamuhuri ya Muungano;

Hebu tujikumbushe Busara za Baba wetu wa Taifa  Mwalimu Nyerere alipozungumzia dhana ya uongozi, Mwalimu Nyerere alisema, “uongozi ni kuonyesha njia.” Kwa maana hiyo, viongozi shurti wafahamu vyema matokeo ya uongozi wao. Wasome imani za wanaowaongoza na nyakati zilizopo ili kutambua matumaini ya umma kimaisha.

VIONGOZI GANI TUNAWAHITAJI?

Amabao hawawezi jisahau wamepewa dhamana ya  kushika hatamu ya uongozi la msingi hapa ni kuwa kiongozi amabye yuko tayari kuongoza na  na ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri. Atumie stadi za uongozi mwema kuonyesha njia. Mheshimiwa Dr. Magufuli ameweza kulionyesha hili kuwa kiongozi ambaye anajali Taifa na sio kukitumikia kikundi Fulani.

Wanaepuka kutumia stadi za uongozi kusimamia haki za waliowa wafikisha hapo hasa wanyonge. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki. Ukitaka kulitendea haki jipu lazima ulikamue na ulikamue vizuri na kuhakikisha kuwa kiini kimetoka ili kumpa nafuu mgonjwa. Ugonjwa ambao kama taifa tunao kwa sasa ni uchumi wetu ambao hauendani na maisha ya wananishi wetu. Tunashkukuru majipu haya sasa yanaendelea kutumbuliwa na mgojwa wetu uchumi anaendelea kuimarika.


Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha miongoni mwao  akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu. Kupitia siasa safi kila kitu cha kunufaisha wananchi hupatikana. Bali ni muhimu viongozi wanaotarajiwa kufanikisha ustawi wa wanadamu, wapatikane kwa njia ya haki. Watokane na ridhaa ya watu wenyewe wanaotaka kuongozwa. Na wakisha chaguliwa anatende kazi kwa uadilifu na ustadi mkubwa. Waweze kukusimai uchumi wetu kwa kuhakikisha kuwa yaliyo ya Kaizari anapewa Kaizari kwa faida ya Taifa nzaima.


Watendaji wetu timizeni wajibu wenu ili muweze kumsaidia rais wetu katika kufanikisha adhima ya kulijenga taifa letu kiuchumi kwa faiada ya vizazi vyetu

Mungu ibariki Tanzania

Friday, December 4, 2015

NIMEKUJA KIJIFUNZA KAULI YA WAZIRI MKUU MAJALIWA KASSIM MAJALIWA.



Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa ni waziri mkuu wa awamu ya Tano ambaye anaendana na kasi ya utendaji wa kazi wa Rais wa awamu ya tano Mheshimiwa Dr. Magufuli katika kurudisha uwajibikaji na matumizi mazuri ya fedha za watanzania katika idara za serikali na mashirika ya umma.

Katika hiki kipindi kifupi akiwa kama waziri mkuu ameweza kuonyesha nia dhabiti ya kuwatumikia watanzania wanyonge ambao kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa masikini katika taifa lao ambalo lina utajiri mkubwa ambao ulikuwa ukiishia amikanoni mwa wachache.

Ameanza kazi kwa kutembelea au kufanya ziara za ghafla katika idara nyeti za serikali ambazo ni nguvu ya uchumi wa Taifa na daraja pekee katika kuondoa umasikini wa watanzania wanyonge . kauli ya ambayo alitoa hivi karibuni kuwa amekuja tu kujifunza bila kuhitaji maelezo zaidi ilikuwa ni nzito ambayo kwa kweli watendaji wa serikali na idara zake wanatakiwa kuizingatia na kuwa tayari kuwajibika mara moja.

Mheshimiwa Majaliwa ameonyesha ujasiri wake wa kujifunza nini kinaendelea katika utendaji wa watumishi wa serikali na uma na tayari ameanza kuyapa mgongo mazoea ya kale.  Kwa mhesjimiwa majaliwa ambaye hakuwa maarufu sana katika siasa za Tanzania sasa kwa kushirikiana na mhemishimiwa Rais Magufuli kwa pamoja wameamua kuhakikisha wanabadilisha mifumo ambayo ilikuwa inawanyima watanzania kaktika kuyafikia maendeleo kammili, Lengo kubwa la serikali ya tano chini ya Rais, Magufui, Makamu wa rais Samia Suluhu Hassan na Waziri mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ni kuona kuwa wanabadilisha mifumo yote mibovu  ili kuifanya Tanzmi kuifanya inakuwa bora zaidi kwenye masuala ya uchumi, utawala na maisha ya watanzania masikini.
Waziri Mkuu kwa kushirikia na Uongozi wa awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli wana kila nafasi sasa ya kuandika historia kwa kutumia kauli mbio ya hapa kazi tu na kuhakikisha wanabadilisha mifumo yote mibovu ya kuendesha nchi kwa fiada ya watanzania  
Tukubali kuwa Tanzania ya leo inaweza kuwa tofauti sana na ya jana, na ya kesho ikawashangaza hata watu wa dunia.  Kama Mheshimiwa Majaliwa katika nafasi yake ataweza kuhakikisha kuwa anajenga mfumo ambao, hata kama yeye hatakuwepo madarakani, bado Tanzania na Watanzania watafuata na kuheshimu mifumo mipya itakayowekwa. Ndio maana kauli yake “ nimekuja kujifunza tu ni muhimu sana kwa taifa hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko. Kwa nchi kama ya kwetu, lililo muhimu kwenye mifumo ni kwa wenye kukiuka sheria, kanuni na taratibu zitakazowekwa kuadhibiwa, punde tu wanapokosea.

Je Mheshimiwa Majaliwa amejifunza nini? Na atakuja na somo gani au fundisho gani kwa hao aliowatembelea? Je ataweka mifumo mipya, yenye kutanguliza maslahi ya nchi na si ya watendaji binafsi ambao wameamua kutumia pesa katika kujilipa wao wenyewe? Je hili litakuwa anguko jingine kwa watendaji wabovu ambao wanajali sana masilahi yao na sio ya taifa?,

Kama wengi ambavyo wameseama kuwa kitendo chochote cha kupunguza matumizi yasiyo na lazima, na kutumia fedha kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania lazima kiungwe mkono kwa hali na mali.  Waziri Mkuu Majaliwa anastahili sifa kwa hilo na tumwombee Mungu amlinde ampe nguvu na aweze kutuletea mabadiliko ya kweli. 

Kwangu mimi leo kauli ya “nimekuja kujifunza” ina maana kubwa sana sisi kama taifa tunao wajibu wa kujikomboa kimawazo ili tuweze kufikiri sisi wenyewe, katika kuyapa thamani maamuzi yetu ya utendaji badala ya kusubiri ziara za ghafla za viongozi wetu ili watufundishe jinsi ya kutumia nyazifa zetu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Haiingia akili kwa watendaji wa mashirika ya umma pamoja na bozi zake kutumia pesa nyingi ili walipane mishahara na malupulupu binafsi na kuliona shirika linaendelea kudidimia na wafanyakaza na likishindwa kujiendesha. Tuwe na vichwa timamu vya kutuwezesha kuyatafakari masuala sisi wenyewe. Tunapaswa tujijengee huu msingi ili tuweze kuitathmini dhana ya maendeleo, tuweze kujiuliza maendeleo ni nini?

Katika kufanya hivyo, tunapaswa kuchukua jukumu na wajibu wa kujitungia vigezo vyetu na kuvitumia. Lazima tujenge utashi wa kujiamini na kujiamulia mambo yetu wenyewe kwa manufaa  ya taifa letu.  Ni uongo kudhani kuwa hakuna nchi ambayo imesimama tu na haibadiliki. Kosa tunalofanya ni kutozingtia ukweli huo na badala yake kuziona nchi za Ulaya na Marekani kama nchi zilizoendelea na sisi kutumia rasilimali zetu vibaya tukiendelea kusaidiwa na nchi hizo kama sisi ni mataira wa kufikira na hatujui kutenda kazi ipasavyo isipookuwa ni kufikira kuiba tu . Kwa mtindo tulio nao sasa tutabaki na hii dhana ya kujidunisha, na watu wetu kuendelea kuwa masikini miaka yote. Kwa kweli tunatakiwa Kujifunza ili tuweze badilisha huu msimamo tegemezi.

Mheshimiwa Majaliwa anatuonyesha kuwa tuna takiwakuwajibika kujikomboa kifikra, tuweze kujiwekea vigezo vyetu wenyewe. Pasipo kuwa na vigezo vinavyozingatia haki ya  uwajibikaji. Uadilifu na kumwogopa Mungu dhana ya mabadiliko na maendeleo itaendelea kuwa ndoto. Asante awamu ya Tano sasa mmeanza  

kutoondolea dhana hii. Inatubidi tubadili fikra; tukatae huu mkondo uliopo sasa wa kuitwa au kujiita sisi ni masikini wakati watu wachache ambao wamepata nafasi serikalini katika mashirika ya umma kwa sababu zao binafsi wanarudisha maendeleo yetu nyuma.

Dhana ya Maendeleo ni mabadiliko katika kitu au hali yoyote, katika nyanja mbali mbali za maisha, mabadiliko ya manufaa kwa mujibu wa mazingira husika. Katika jamii au nchi, maendeleo yanaboresha maisha ya binadamu, yanahifadhi au kuboresha mazingira, na yanaendana na heshima, utu, na haki. Maendeleo yanatokana na msukumo wa jamii au nchi husika, kwa mujibu wa mahitaji yake halisi, na kwa mujibu wa maamuzi na matakwa ya jamii hiyo, maamuzi yatokanayo na fikra huru na tambuzi, zenye mwelekeo wauwajibikaji na uadilifu. Maendeleo hayatakiwi yalete matabaka miongoni watanzania.

KWA KWELI NIMEKUJA KUJIFUNZA mimi imenifundisha kuwa tukitaka kufanikiwa katika hii safari ya kuondoa umasikini wa Taifa letu tunatakiwa kuendelea kuitekeleza kauli mbiu ya Ya Hapa Kazi Tu kwa vitendo katiaka kujiletea  maendeleo yetu na sisi kama wazalendo wa taifa hili lazima kwa umoja wetu tusiwaonee haya mafisadi, wla rushwa wazembe katika kusukuma gurudumu la nchi yetu mbele , na tuondoe dhana ya kungojea misaada kutoka nchi za nje hii haiwezi kusaidia maendeleo bali inatufanya tuendelee kuwa tegemezi zaidi .

Tunaona mfano wa nchi kama CUBA ile haifuati njia za uchumi kama nchi nyingi duniani ina uchumi wake unaokuwa kila siku , angalia uchina na mipango yao na mao ni serikali ya kikomunisti ndio lakini walikuwa na malengo ikazaa mikakati hii tunayoiona sasa hivi ni dira ya china na kufikia mwaka 2030 iwe super power; au tuangalie nini walifanya south Korea  iaka ile ya 1960s.  
Kwahiyo tuwekeze katika rasilimali ambayo tunajua inaweza kututoa hapa tulipo kwenda hatua mbili au 3 zaidi mbele bila kutegemea msaada kutoka nje. ,

Tunaweza kuendeleza mawazo ma-pya, na kuyakusanya, kuyachuja, kuyaangalia na kuyaunganisha. Hivyo, maendeleo ni hatua ambayo husonga mbele na yenye mabadiliko. Maendeleo yanajumu-isha utendaji ufuatao malengo.  Viongozi wetu wengi wanajiona wao pekee ndio wenye wajibu wa kufaidi utajiri wa nchiyetu, kupitia hulka zao za RUSHWA NA UFISADI.

Sisi kama wananchi wazalendo wa taifa letu tuko tayari kushirikiana na viongozi wa awamu ya tano katika kuyachoma magugu ambayo mengine yalikuwa yameota sugu na kuwa msitu mkubwa ambao umekuwa tishio kwa wachomaji na walulima ambao wako tayari kulisafisha pori hili. Tumeamua kuwaunga Mkono Mheshimiwa Dr. Magufuli Rais wetu na Mama Samia Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Majaliwa msitoke jasho peke yenu katika kufyeka msitu huu. Nasi tjuko tayari kutoa ili shamba letu liweze kutoa mazao bora na sio tene kuitwa shamb la BiBi. Tunafahamu kuwa Shamba la Bibi ni letu sote kila mtu anamchango wa kulifanya listawi na kutoa mazao bora kwa faida ya wajukuu na watoto wote wa Bibi.

 
Kwa kweli nimekuja kujifunza na kugundua kuwa UFISADI NA RUSHWA unatengeneza kikundi cha watu...wenye kusimamia maslahi yao kwa faida yao UFISADI NA RUSHWA Inaunda uwepo wa vikundi visivyo rasimi kisheria kwa ajili ya kupinga/kuzuia/kufanya lobbing na kufanikisha mambo ambayo wao walio kwenye kundi husika Watafaidika nayo;

UFISADI NA RUSHWA Inapanua wigo wa Rushwa kwenye jamii na kufanya baadhi ya watu kwenye jami wasiweze kuguswa na sheria kwa sababu ya uwezo wao kwenye fedha. UFISADI NA RUSHWA Inaleta usumbufu kwenye utendaji wa Serikali kwa kuwa baadhi ya raia wanakuwa na nguvu ya fedha hivyo umma wa raia wa kawaida unatengeneza hofu ya kuogopa watu wao wenye ukwasi.

UFISADI NA RUSHWA Inavunja na kuharibu mfumo wa HAKI kwa kuwa wenye UKWASI huo wa kifisadi wanatumia ukwasi huo kuvulugu HAKI inapotafutwa. UFISADI NA RUSHWA Uzalisha kiburi/Jeuri za watu wenye ukwasi dhidi ya Watumishi wa Umma na kuwafanya waonekane si kitu mbele ya sura za jamii UFISADI NA RUSHWA Uchochea kwa kasi kubwa ongezeko la kukosekana kwa maadili ya umma na maadili ya Viongozi wa umma.Hivyo kuongeza mpasuko wa kuwa Taifa lina mmomonyoko wa maadili.

UFISADI NA RUSHWA Usababisha woga wa kitaifa hata uwezo wa kitaifa kukemea mambo yasiyostahiki utegemea ujasili wa mkemeaji. UFISADI NA RUSHWA Pia utengeneza ushawishi wa wageni kuona sehemu za kupenyeza mambo yao kwa kuwa utafuta milango ya kuingia kwa namna ambayo wao wanaona kuna njia ama upenyo. UFISADI NA RUSHWA Uchafua pia mfumo wa uendeshaji wa siasa na Serikali kwa kujalibu kuweka mapandikizi yake. 

MUNGU IBARIKI TANZANIA KATIKA AWAMU HII YA TANO HAPA KAZI TU 



Wednesday, December 2, 2015

UTHUBUTU WA RAISI MAGUFULI NA UTUMBUAJI MAJIPU



Katika kipindi chote cha Kampeni Mheshimiwa Dr. Magufuli daima alionyesha upendo, maumivu  na haja ya kuibadilisha Tanzania kuwa kweli ya watanznaia na sio Tanzania ya wachache katika kufurahia matunda yatokanayo na rasilimali la taifa letu. Mfuatiliaji mzuri aliweza kugundua kuwa Magufuli aliamua kwa hiari yake kuwatumikia watanzania kuwa kiongozi mzuri kufuatia kwa ajili ya watanzania wote bila ubaguzi wowote.

Rekodi zake za utendaji kwa falfasa ya kuwa atakuwa kiongozi ambaye  hataficha chochote kwa wananchi; hatasema uongo,  na atafichua uongo kila unapoibuka. hatakuwa mtu wa kuficha matatizo, makosa, mapungufu na kushindwa kuyatafutia suluhu na kamwe sio mtu wa makundi au wa kujijengea sifa nyepesi nyepes binafsi.

Mchakamchaka ambao anaendlea kuufanya Magufuli sasa ndicho haswa kinachotakiwa kufanyika katika kipindi kirefu nyuma. Kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha wazi kuwa anajua matatizo na mapungufu yaliyopo na badala ya kuyafunika na kuyapaka rangi anayaweka wazi kwa maendeleo ya watanzania wote. Bahati nzuri Magufuli amekuwa akielezea namna atakavyoshughulikia hayo matatizo na mapungufu. Bahati nzuri tabia hii ya Magufuli siyo mpya. Watanzania watakumbuka kuwa hulka hii ya Magufuli ilijionyesha wakati hata alipokuwa waziri chini ya Rais Benjamin Mkapa alipoikosoa Ofisi yake hadharani kwa baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo kujimilikishia magari ya umma isivyo halali. Tukumbuke hata Katika kipindi cha kampeni, Magufuli amekuwa akitoa mapungufu ya serikali hata pale ambapo Rais Kikwete yupo.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuandika kitabu mwaka 1962 kiitwacho "Tujisahihishe" akitaka Watanzania na hasa viongozi wawe tayari muda wote kujisahihisha. Katika kitabu hicho Baba wa Taifa, alisema kuwa “makosa ni makosa bila kujali ni nani ameyafanya. Muhimu ni kuyajua makosa hayo na kujisahihisha.” Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere aliendelea kusema;

“Kujielimisha ni kujua ukweli wa mambo na kuwa na ujuzi wa sababu mbalimbali za mambo; na kama mambo hayo ni mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama ni mema, jinsi ya kuyadumisha. Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na kushauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo na jinsi ya kuyaondoa(Nyerere, 1962, 5).”

Kwa maelezo hayo ya Baba wa Taifa, ni wazi kuwa Magufuli ameamua kuwa mkweli katika utendaji wake kama Rais wa wamu ya tano na ameepuka kuwa mpumbavu kama alivyobainisha Baba wa Taifa. Magufuli anaamini dhana hii kiongozi mkweli na aliye na uthubutu wa kujikosoa anaonyesha kuwa ana uwezo wa kutafuta suluhisho la kweli la matatizo yaliyopo, na tumejionea katika kipindi kifupi sana akiwa ameanza kutumbua majipu kama alivyohaidi.



kama mwandishi Maggid alivyowahi andika kuwa Sehemu kubwa ya matatizo ya nchi zetu hizi yanatokana na ubinafsi huo. Na bahati mbaya kabisa, baadhi ya viongozi tuliowapa dhamana za uongozi ndio wenye kuongoza kwa matendo yenye kutanguliza maslahi yao binafsi. Kwetu sisi Watanzania hali yetu ya kiuchumi bado duni mno. Ufisadi unalitafuna taifa letu. Tuna lazima ya kukumbushana ukweli huu, maana, tukifanya masihara taifa letu liko katika hatari ya kuingia katika hali ya machafuko makubwa. Ili kuunusuru uchumi wetu usiyumbe zaidi tuna lazima ya kutumia fedha na rasilimali zetu kwa busara kubwa. Kuna busara ya kutomuiga tembo kwa lolote lile

Sokoine alionyesha moyo wa kujitoa kuwatumikia wananchi mara tu baada ya kuteuliwa katika wadhifa wa waziri mkuu wakati huo akiwa mbunge wa Monduli mkoani Arusha. Katika utawala wake, kama waziri mkuu, aliendesha na kusimamia mwenyewe vita dhidi ya dhuluma iliyokuwa inaendeshwa na wachache wenye nacho dhidi ya wengi wasionacho. Vita dhidi ya walanguzi na wahujumu uchumi ni miongoni mwa mambo ambayo yaliinua jina la Sokoine kila pembe ya nchi hii na katika medani za kisiasa.


Sokoine alipenda haki, aliona ni kitu cha kushangaza kwamba wananchi walio wengi walikuwa wanaishi maisha ya dhiki, hawakusikilizwa na watendaji. Alishangaa kuona kwamba urasimu umezama kwenye rushwa za nipe-nikupe na kuporomoka kwa maadili hasa upungufu mkubwa katika kutoa huduma na haki. Sokoine alitumia uwezo kama waziri mkuu kujaribu kurejesha nidhamu katika sekta ya utawala kwa kuwajibisha viongozi na watendaji wabovu. Kwa upande mwingine, alijitahidi kuvunja ushirikiano kati ya viongozi warasimu na wafanyabiashara ambao kwa pamoja waligeuza sekta ya umma kama shamba la bibi. Hili ndilo analolifanya Magufuli na watendaji wake katika mwezi huu wa kwanza wa awamu yake ya Tano ya kuliongoza Taifa hili.

Dr. Magufuli tuko alipopendekezwa na chama chake cha mapinduzi kupeperusha bendera ya kuwania urais wa awamu ya tano alisema wazi kabisa kuwa wananchi wategemee  utumishi uliotukuka toka kwake, watarajie uadilifu wa khali ya juu,watarajie uchapakazi, watarajie serikali itakayo kuwa imara: itakayo simamia maslahi ya uma; na wategemee nidhamu sio tu kwa watumishi wa serikali bali kwa watanzania wote; wasitegemee propaganda za ujanja ujanja; balo ukweli wakati wote; na alihaidi kufuatilia mambo mengi kwa kina mimi  mwenyewe; wasitarajie sherehe na hafla nyingi toka kwangu. Na watarajie kuwa nitalinda umoja amani na usalama wan chi yetu kwa nguvu yetu zote. Nitakuwa kiongozi wa wote bila kubagua mkoa kanda dini kabila wala vyama.

Kama mwandishi Mmoja alivyowahi andika “Dr John Pombe Magufuli raisi wa awamu ya tano anataka kuwaonyesha watanzania kwa ujumla wake kuwa atakaye aliyethubutu kuchezea shilingi ya Serikali atajitutia yeye mwenyewe; ni kweli ilikuwa inasikitisha kila siku kusoma magazeti yenye vichwa vya habari, Mamilioni yametafunwa yayeyuka na kuunda kamati ambazo zilikuwa vile vile zikitumia pesa katika kutafuta suluhu na suluhu haipatikani. Kama mwandishi Maggid alivyowahi andika  Maana, kuna walioishi wakiamini, kuwa ng'ombe wa Serikali huzikwa na ngozi yake. Ni nani anayejali? Maana, kama ng'ombe ni wa mtu binafsi, basi, akifa, atahakikisha walau anachuna ngozi yake, ili walau aambulie senti kidogo! Utamaduni huu wa kudhibiti mapato ya hazina ni utamaduni mwema utakaomsaidia mwananchi wa kawaida”.


Hatua ambazo ampaka sasa rais Dr Magufuli, ameshchukua ni funzo tosha kwa watu wengine; tunafahamu kuwa kuteuliwa na hatimaye kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa awamu ya tono kulitokana sana na record yake ya uchapakazi, uadilifu, kutoyumbishwa hovyo hovyo kwa sababu ya kusimamia kile anachokiamini kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla, Hiyo imejidhihirisha zaidi katika wizara zote alizowahi kuziongoza mfano Ujenzi na Miundombinu pamoja na Kilimo na ufugaji. Ni kweli kuwa fundisho tunalopata hapa ni kwamba usingoje mpaka upewe nafasi kubwa ya utumishi ndio uanze kuonyesha namna ya kuwatumikia wananchi.


Dr Magufuli ni visionary leader ambaye anaamini katika jambo moja kuwa mabadiliko ya maisha bora yanawezekana  katika Tanzania yetu. Tatizo ambalo analijua linalokwamisha maisha bora kwa watanzania ni Usimamizi mbovu sekta zote kutokana na ubinafsi, udugu, rushwa. Katika kampeni yake alipotembelea kaburi la hayati sokoine alisifu weledi wa hayati sokoine ambaye alikuwa mkweli, mchukia rushwa, na alikuwa na uthubutu bila kumwogopa kiongozi yeyote Edward Moringe Sokoine alikuwa kiongozi mwenye uthubutu wa dhahiri katika kupigania na hata kufia maslahi ya raia, hasa maskini. Tunamkumbuka Moringe alivyowasha moto  bungeni kabla ya kuondoka, hasa alipozungumza kuhusu kubana matumizi ya serikali, ambako kuliambatana na hoja juu ya ukubwa wa serikali na hasa mantiki ya kuwa na mawaziri wasiokuwa na wizara maalum, lakini wakipatiwa haki zote sawa na mawaziri wenye wizara. Nyota yake ilizidi kung'ara na kuwa chachu ya kupendwa miongoni mwa walio wengi; akaonekana mwiba kwa walafi na wadokozi wa keki ya taifa.  

Ingawa kwa upande mmoja Sokoine alionyesha kupata mafanikio kwa kuungwa mkono na wananchi, kwa upande mwingine alijikuta akipoteza marafiki na kujijengea maadui lukuki kutokana na mfumo wa utendaji uliokuwepo kabla yake. Katika utendaji wake mara zote, Sokoine aliamini katika siasa za uwazi. Alizungumza kile alichoamini ndicho na alisimamia na alionyesha mfano katika utekelezaji wa kila jambo alilotaka lifanyike. Mambo mengi aliyojaribu kufanya Sokoine yalitokana na uthubutu wake binafsi. Alitumia mfano wake kama kiongozi ambaye alikuwa na uadilifu mkubwa na hakuwa na ubinafsi.

Rekodi ya utendaji kazi wa kiongozi huyu ambaye alibahatika kushika wadhifa wa waziri mkuu katika vipindi viwili tofauti, haijafikiwa na kiongozi yeyote katika ngazi hiyo, miongo mitatu tangu kifo chake. Inasemekana ni katika kipindi chake cha uongozi, Mwalimu Nyerere alipata ahueni, alinenepa. 



Na katika awamu hii ya Magufuli watanzania wanyonge ni zamu yao kunenepa; na kuanza kufurahia matunda ya nchi yao tumejionea wenyewe muhimbili wagonjwa wakiwa wamelala katika vitanda na sio katika sakafu.



Kama ilivyokuwa kwa marehemu  Sokoine Mheshimiwa Dr. Magufuli ameanza kuonyesha kuwa atakuwa kiongozi mkuu ambaye ataweza kuisimamia kusimamia serikali kwani ameonyesha kwa moyo mkunjufu kuwa anamainisha kila ambacho anakiongelea na kukiishi. Tunafahamu kuwa viongozi wa aina ya Mwalimu Nyerere na Sokoine hawazaliwi kila mara. Kama taifa tumepata bahati ya ajabu kwani sasa tumempata kiongozi wa aina hii ndio mheshimiwa Dr.John Pombe Joseph Magufuli. Amekuwa kiongozi mwenye ujasiri wa kuchukua maamuzi katika mazingira magumu ambayo yanawagusa hata vigogo wa serikali ili nguvu kubwa zielekezwe kuwasaidia maskini,.


Dr. Magufuri ameonyesha awajibike wa ukweli, kuwa muwazi katika utendaji wake kubana matumizia ya serikali.

Maswali ambayo najiuliza leo

  • Uwajibikaji ulipotelea wapi kwa viongozi wetu?


  • Nini maana ya kuwa kiongozi wa umma?


  •  Je wengi wa viongozi wetu wanaelewa dhana hii nzima ya kuutumikia umma au jamii?


  • Je walioko madarakani na wanaoongozwa wanaonyesha na kufahamu wajibu wao kwa jamii na kuwa viongozi bora wa kuigwa na kizazi chetu cha baadae?


Ninachofurahia mimi katika awamu hii ya tano, misamiati kama kula nchi kwa watendaji wa serikali na mashirika ya umma; dhana ya umungu mtu kwa watendaji wengi sasa inapotea katika kamusi ya utumishi wa umma.


Ni wakati umefika sasa kwa watendaji wetu kujua nini maana ya uongozi; na wakumbuke kuwa uongozi sio maana yake kulindana katika utendaji wa maovu. Imefika wakati wa kuwaambia viongozi wote wabovu umekosea ondoka:  Mheshimiwa Magufuli ameweza kuonyesha hili katika kipindi kifupi sasa cha uongozi wake kama Rais Magufuli ameonyesha kwa dhati Moyo wa kuwatumikia hao waliomchagua na sio kujali maisha yake na familia yake tu kama ambavyo hali ilivyo sasa. Hivi sasa Dr. Magufuli anaifufua dhana yaw a kuwatumikia wanachi ambayo ilikuwa imeshakufa na kupitwa na wakati. Hapa nchini kwetu kila aingiaye madarakani anafikiria kujinufaisha binafsi na waliomzunguka.

Uongozi na kuwa kiongozi Tanzania ilikuwa ni mradi wa kutajirika na wala hakuna anaeuliza mara baada ya kiongozi kuwa madarakani maisha yake kwa ujumla yanabadilika na kuwa ni mtu wa juu kupita wote ndani ya jamii husika. Inashangaza lakini hii ndio hali halisi kwa Tanzania yetu.  Hatukatai mabadiliko lakini hali iliyoko sasa inakatisha tamaa kwa wanaojua maana ya kuwa kiongozi wa umma.

Nimefurahi kwa ujasili wa Dr. Magufuli wa kuondoa  utamaduni uliojengeka wa kusifia makosa na pale mmoja miongoni mwetu anapotaka kusema ukweli huambiwa ni msaliti wakati anachotaka kukisema au alichosema ni cha haki na ukweli kabisa. Asante Mheshimiwa Magufuli kwa kuanza kuibadili dhana hii na kuwabadili na wananchi kwa ujumla huu sio wakati tena wa kuwaachia watu wachache wakitupeleka peleka katika lindi la umasikini na matatizo kutokana na ubinafsi na ulafi wao tu.

Mheshimiwa Magufuli amesema kuwa kazi  iliyo mbele yake ni kubwa na ngumu lakini amekubali kuwa yeye ndiye atakuwa anatumbua haya majipu; hivyo Kama Mwandishi mmoja aliandika kuwa “ Uzalendo wetu kama Watanzania tunaoipenda nchi hii ni kubainisha yale machafu ya viongozi na sio kuwa wanafiki. Ilishasemwa zamani kuwa Ukweli ni mchungu, hatuna budi kuusema japo unauma tuseme ukweli bila ya hivyo matatizo yetu hayawezi kwisha kwa kutegemea wanafiki na walioingia madarakani kwa maslahi binafsi”

Maendeleo ya kweli ya watanzania yatatoka na watanzania wenyewe; Hata siku moja hatotokea mtu toka nje ya nchii hii kuja kutuletea maendeleo ila ni sisi wenyewe tunapaswa kujiletea hayo maendeleo, nayo ni kuwajibika kutokana na dhamana tulizopewa na sio kuipelekea kuzimu nchi yetu kama hali ilivyo sasa. Mfano mdogo tu hebu angalia uozo wa Bandari na TRA na hasara ambayo Taifa limepata.


Mheshimiwa Rais Magufuli ameliona wazi kuwa Kiongozi wa umma anawajibika kwa umma uliomuweka madarakani na sio kufanya safari nyingi za nje na kusema kuwa hana nafasi  na kwenda vivijini kuona shida za watanzania Hongera Dr. Magufuli kwa kuliona hilo. Uamuzi wa hivi karibuni wa  kufuta safari za nje ni wa kishujaa na utapunguza matumizi makubwa ya pesa za wananchi.  Hii inaonyesha jinsi ya ukubwa wa tatizo la viongozi kutowajibika kutokana na nafasi zao ndani ya nchi hii lilivyo.

Ni wakati umefika sasa wa kuanza upya kuanza kujitawala tukaanza kujenga Taifa la viongozi na wananchi wanaowajibika kutokana na nafasi zao kwa maendeleo ya Taifa hili kama ilivyokuwa kwa viongozi waadilifu kama Mwalimu Nyerere na Edward Moringe Sokoine; Unapowajibika kutokana na nafasi ya uongozi inaonesha ni jinsi gani ulivyokuwa kimaadili na kuwa tayari kulitumikia Taifa la wanyonge.




Tukumbuke kuwa zao la viongozi wabovu limezalisha taifa la Watanzania walio wengi sasa wamejikita katika mazingira ya udanganyifu, rushwa na uzembe.  Tukumbuke kuwa Watumishi wa umma wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji, weledi na ushirikiano ili kuuiwezesha Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake na taifa  kwa ujumla. 

MHESHIMIWA RAIS DR. JOHN POMBE MAGUFULI WATANZANIA TUNAKUOMBEA KATIKA SAFARI HII YA UTUMBUAJI MAJIPU KWA AJILI YA MAENDELEO YA WANYONGE: TANZANIA SIO MASIKINI ILA VIONGOZI WACHACHE AMBAO TULIWAKABIDHI NAFASI MBALIMBALI WALIKIUKA MAADILI YA UONGOZI NA KULILETEA TAIFA HASARA KUBWA.

MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU MBARIKI RAIS WETU MAGUFULI AENDELEE KUWAHUDUMIA WANYONGE NA MASIKINI -TANZANIA







Monday, November 23, 2015

RAISI DR.MAGUFULI AKIELEZEA MWELEKEO WA SERIKALI YAKE 2015-2020


Hotuba ya Dkt John Magufuli alipofungua rasmi Bunge- NOVEMBER 2015


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,
20 NOVEMBA 2015

Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi huu.

Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.

Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu mbili:


·          Kwanza, ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
·          Pili, nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka Wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani pia watafanya hivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na utulivu mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga kura. Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa, na hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.
Wale waliotarajia kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara nyingine tena tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa cha Amani katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya nchi yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.
Aidha, napenda niungane na ninyi pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa pamoja na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi. 
Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua za awali za kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa Spika;
          Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu wa nchi yetu walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi yetu. Natambua mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga misingi imara wa umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na kuijenga misingi yake. Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua na kuimarisha misingi ya uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao. Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.
Mhishimiwa Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja, tumeshindana katika kampeni tukiwa wamoja, na tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi za Umoja na Amani. Hatutakuwa na simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga umoja na amani yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila, vyama au ukanda.
Mheshimiwa Spika;
       Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza kwa kulalamikiwa sana na wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni pamoja na:
·          Rushwa - Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa wananchi.
·          TAMISEMI - Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k.;
·          Ardhi – Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;
·          Bandari - Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;
·          Maji – Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji kupatikana mbali na makazi, n.k.;
·          TRA - Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara wakubwa;
·          TANESCO - Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;
·          Maliasili na Utalii - Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;
·          Huduma za Afya (Hospitali) - Huduma kuwa mbali na wahitaji, Ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, n.k.;
·          Uhamiaji na Ajira - Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi nchini kwa wageni, Kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, n.k.;
·          Elimu - Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;
·          Polisi - Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari, Ukosefu wa nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;
·          Zimamoto – Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea kazi kama maji, n.k.;
·          Mizani – kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;
·          Mahakama - Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa kesi. Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.
·          Madini – Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia, n.k;
·          Kilimo na Mifugo – Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la masoko, Kukopwa mazao ya wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa Maghala, Mabwawa, Malambo, Majosho, n.k.;
·          Uvuvi – Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi hususan viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa bahari;
·          Reli – Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa reli, upungufu wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara, n.k.;
·          ATC – Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa mishahara ila ndege ni moja (1);
·          Makundi Maalum – Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa;
·          Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo – Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, Haki na maslahi yao, n.k.;
Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue na mshirikiane na Serikali na wadau wengine tuzitatue haraka.
Pamoja na kero hizo tutashughulikia pia mambo yafuatayo.
Kuimarisha Muungano
Mheshimiwa Spika;
Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani. Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu.
Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.
Serikali nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuendelea kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.



Kuimarisha Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaheshimu na kuendeleza utamaduni mzuri uliojengeka nchini wa kuheshimu mihimili ya dola. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata fedha za kutosha kuendesha shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Kwa upande wa Bunge, tutahakikisha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinapatikana kwa wakati ili Waheshimiwa Wabunge mkashirikiane na wananchi wenu kusukuma maendeleo. Kwa upande wa Mahakama, tutalipa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa Mahakama kwa kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, kuongeza kasi ya utoaji haki na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama zetu.


Mchakato wa Katiba
Mheshimiwa Spika;
Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba. 
Uchumi na Matarajio ya Wananchi
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kukiwa na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika Awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na kukua wastani wa asilimia 7. Katika kipindi hicho fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa. Hii ni kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali za Awamu zilizopita za kujenga miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, uimarishaji wa bandari, uimarishaji wa reli, na ukuzaji wa sekta za mawasiliano ya simu na mitandao, ukuzaji na uongezaji wa uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme.
Napenda kuwahakikishia kuwa tutaendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu mipya na kuiimarisha iliyopo ili kuvutia na kushawishi wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mheshimiwa Spika;
Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa ahadi tulizowaahidi Watanzania ni kuendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya; barabara ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na upanuaji wa barabara za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga flyovers, barabara za pete (ring roads), n.k. Uboreshaji wa barabara na njia nyingine za uchukuzi na usafirishaji kuingia na kutoka Dar es Salaam ni muhimu sana kwa sababu bandari ya Dar es salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika;
Katika jitihada hizo hizo za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi Serikali ya Awamu ya Tano, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge). Reli ambazo tunakusudia zianze kujengwa ni:
·          Dar es Salaam – Tabora – Kigoma/Mwanza
·          Uvinza – Msongati (Burundi) na Isaka – Kigali (Rwanda)
·          Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga;
·          Tanga – Arusha – Musoma
·          Kaliua – Mpanda – Karema
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu pia imejaliwa kuwa na madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi asilia umeongeza matumaini ya watu wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi katika miaka ijayo. Serikali itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo. Aidha, napenda kuipongeza kwa dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Bunge la 10 kwa kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi yaani The Oil and Gas Revenues Management Act, 2015. Serikali yangu itasimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini mkubwa.




Ujenzi wa Viwanda
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda. Natambua kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Hatuna njia nyingine kama kweli tunataka kujenga msingi wa uchumi endelevu katika nchi yetu utakaopaisha uchumi na maisha ya watu wetu. Dira ya Maendeleo ya 2025 inatutaka tuwe nchi ya watu wenye kipato cha kati. Tunaweza tukafika huko, na dalili zipo, lakini pia tunaweza tukafika huko kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia wa mambo ni tofauti. Utofauti ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha kwamba sisi ni nchi ya kipato cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha ya watu wengi hazifanani na takwimu hizo. Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda.
Mheshimiwa Spika;
Tutahakikisha suala la viwanda linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa. Matarajio yangu ni kuwa Bunge lako Tukufu litatuunga mkono mimi na Serikali nitakayoiunda katika kufikia lengo hili.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema wakati wa Kampeni, na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda vilivyopo na kuhakikisha vinafanya kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa viwanda vilivyokuwa vya umma kwa makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka wafanye hivyo mapema. Na hapa nataka nisisitize wito wangu huo kwao. Najua huko nyuma ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya aina hiyo umekuwa ukilegalega na watu wamejifanyia mambo watakavyo. Wapo walioacha kabisa uzalishaji na kufumua hata mitambo ya uzalishaji. Mimi niliahidi, na nataka niseme hapa kwa wazi kabisa, kwamba wale waliobinafsishiwa viwanda hivyo waanze kazi, waanze kazi mara moja. Wakishindwa basi tutavitwaa viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na kuwapa watu wengine wenye nia ya kuviendeleza. Hatuwezi kuwa na watu wanajiita wawekezaji tunawapa viwanda vyetu halafu wanaviatamia tu. Mimi hilo sitalikubali na wala sitalivumilia. Nimeielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanza kushughulikia suala hili mara moja. Naomba Bunge lako lituunge mkono.
Mheshimiwa Spika;
Njia ya pili ya kuendeleza viwanda ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu ya kufanya hivyo tayari ipo na baada ya muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo watu wanaotaka kuwekeza Tanzania sasa, katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka ya nyuma kidogo, lakini wakati mwingine sisi humu humu – tukiwemo sisi viongozi kwa kushirikiana na wafanyabiashara matapeli na laghai – tumehujumu mipango na shauku ya wawekezaji wa nanma hiyo. Pamoja na shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea vikwazo na kuwapiga vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi jirani. Sisi katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa usumbufu na urasimu wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji wa Serikali watakaokwamisha jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda hapa nchini hatutawavumilia.   
Mheshimiwa Spika;
Ni viwanda vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura ya kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani, hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini – na maliasili nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana. Viwanda vya aina hii vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja, na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) – yaani bidhaa kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi vitakuwa na uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. Viwanda hivi vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje. Yote mawili yakitokea, yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje, itatuongezea akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na kuendeleza mipango mingine kwa ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura ya tatu ya viwanda tunavyovikusudia ni kuzalisha ajira nyingi. Shabaha yetu ni kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda ifikieasilimia 40 ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.

Mheshimiwa Spika;
Nimeamua kulisema hili kwa kirefu sana kwa sababu ili tufanikiwe lazima tuelewane na tusaidiane kulisukuma kwa pamoja jambo hili. 
Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Sekta nyingine ambazo lazima tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza ni kilimo, mifugo na uvuvi. Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani mazao yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi kikubwa ni nchi ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia 75 wanaishi vijijini na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao na wanazalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula chote kinacholiwa hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25 kwenye pato la taifa yaani GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu ya fedha za kigeni. Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa sekta ya kilimo, mifugo  na uvuvi katika uchumi wetu na maisha yetu ni mkubwa sana. Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika maisha yetu na uchumi wa nchi yetu. Nataka kuahidi kwao sitawaangusha.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu wakulima, wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni watu maskini. Mapato yao yako chini na wanaishi maisha duni. Lengo letu ni kuuimarisha sekta hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi lakini pia ziweze kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadili maisha yao. Tukiweza kuboresha sekta hizi vijana wengi zaidi watavutiwa kujiunga nazo na hivyo kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira. Nataka niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao tutahakikisha zinatekelezwa. Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia kwa dhati ahadi hizo ili kuhakikisha kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa zaidi na wenye tija. Baadhi ya mambo tuliyowaahidi kuyatekeleza ni pamoja na haya yafuatayo:
1.    Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa ikiwa pamoja na ufugaji wa samaki,
2.    Kuwapatia pembejeo,
3.    Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,
4.    Kuwapatia wataalamu wa ugani,
5.    Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,
6.    Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana kufikia lengo hili,
7.    Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa, kule Kagera ina kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda ambako bei iko juu, tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili wakulima wapate bei nzuri. Tutafanya hivyo pia  kwa mazao mengine kama mahindi, chai, pamba, korosho, mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki, n.k.),
8.    Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa wao kuondolewa kwenye ardhi zao kupisha  wawekezaji,
9.    Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya migogoro hiyo tunaviondosha haraka,
10.      Kuhakikisha kwamba tatizo la wavuvi kuvamiwa   na majambazi na uvuvi haramu linashughulikiwa kikamilifu.
Tatizo la Umaskini na Ajira
Mheshimiwa Spika;
Nimezungumzia umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ya matatizo makubwa mawili yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo la UMASIKINI na pili ni tatizo la AJIRA. Ni kweli uchumi wetu umekuwa ukikua kwa kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana na kasi ya kuondoa umasikini na uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana wetu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 28.2 ya Watanzania ni maskini. Na kwamba kwa namna na kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo baina ya matajiri (walionacho) na maskini (wasionacho) linazidi kukua. Tukiendelea hivi tunavyoendelea sasa hatutakuwa tunaitakia mema nchi yetu kwa sababu mgawanyiko mkubwa wa kimapato na tofauti kubwa za kimaisha baina ya matajiri na maskini ukiachiwa uendelee na kuzidi kukua utachochea chuki na uhasama baina ya walionacho na wasionacho. Lazima tujizatiti na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na kuibadilisha hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa watu wetu. Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni uendelezaji wa sekta ya viwanda na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA. Kama nilivyokwisha kugusia, ukuaji wa uchumi wetu haujaenda sambamba na kasi ya watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Tatizo la ajira ni kwa vijana wote waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na ujuzi. Hii inamaana kwamba sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu sizo zinazozalisha ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka msisitizo kwenye sekta ya viwanda hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo ambavyo ndio mwajiri mkubwa hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuweka msisitizo katika Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi kuwawezesha vijana wetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango mbalimbali. Ili hili liwezekane, na sisi tutalifanya, linahitaji mambo mawili makubwa.
Kwanza, kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi. Hatuna budi kuweka mkazo katika viwango vya ubora vya elimu na stadi za kazi wanazopata vijana wetu. Nalisema hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia uendelezaji wa viwanda ikiwa hatujaandaa vijana wenye uwezo, ujuzi, na stadi za kufanya kazi hizo kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu; hatuwezi kutaka kuwekeza katika viwanda vya nguo au samani ikiwa hatuna wahandisi wa mitambo wazuri, wabunifu  wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa na kukubalika. Aidha hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha shughuli za uzalishaji kama hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi na kuiendeleza. Kwa hivyo tutaelekeza nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa shule na vyuo vyetu katika ngazi mbalimbali vinafundisha na kutoa vijana wenye viwango vya hali ya juu vya elimu, maarifa, ujuzi na ufundi.
Mheshimiwa Spika;
Pili, ni suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka kujiajiri. Katika kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua na kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo:
·          Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na fani walizosomea;
·          Kuwawezesha vijana kuanzisha  SACCOS zao na kupitia SACCOS hizo kuwawezesha kupata mikopo;
·          Kuwawezesha vijana wajasiriamali kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na mafao mengine katika mifuko hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Tatu, ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha shughuli za kina Mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda na Maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k. Shughuli za makundi haya zinatusaidia sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa tu na kuzurura zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo wetu wa kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha. Niliahidi, na nataka nirudie hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri zetu, pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na rafiki kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao na shughuli nilizozitaja tutauondoa. Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato, na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali mabilioni ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana mitaani. Viongozi na watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.
Afya
Mheshimiwa Spika;
Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:
·          Kwanza, kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo. Lengo ni kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali ya Rufaa.
·          Pili, tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika Nyanja za afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.
·          Tatu, tutaongeza bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha, tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.




Elimu
Mheshimiwa Spika;
          Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.  Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.  Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.  Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati.  Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi.
Maji
Mheshimiwa Spika;
          Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi sana ya ukosefu wa maji. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanzisha miradi mipya mikubwa na midogo ya maji kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya uhakika vya maji  ikiwa  pamoja na kuvuna maji ya mvua. Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.



Umeme
Mheshimiwa Spika;
          Suala la upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo katika nchi yetu pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita. Hatuwezi kuzungumzia suala la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi. Serikali yangu itahakikisha kwamba umeme unapatikana wa kutosha na wa uhakika. Tutakamilisha miradi ya umeme iliyopo na kujenga mingine mingi mipya ili wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati ya umeme na viwanda vingi zaidi vidogo vidogo, vya kati na vikubwa vianzishwe.
Madawa ya Kulevya
Mheshimiwa Spika;
          Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike. Familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya taifa imepotea.  Tutaushughulikia mtandao huo hususan wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila ajizi.
Mheshimiwa Spika;
Masuala mengine tutakayoyawekea mkazo katika utawala wa Awamu ya Tano ambayo ninaamini yatasaidia katika kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya Utalii, Mawasiliano, Madini, Ardhi na Makazi, Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara, Ulinzi na Usalama, utunzaji wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Ualbino, Wazee, Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari, wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa masuala haya umefafanuliwa vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Tutayatekeleza ipasavyo.


Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa Spika;
Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.
Mheshimiwa Spika;
Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.

Mheshimiwa Spika;
Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa na ufisadi. Ndio maana moja ya Imani kuu za CCM ni ile isemayo: “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa
Kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kuifananisha rushwa na ufisadi‘Kama Adui Mkubwa wa Watu’.  Akiongea Bungeni Mei 1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
Rushwa [na ufisadi] havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”
Mheshimiwa Spika;
Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri, wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako tayari kuvumilia upuuzi wa serikali itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.
Mheshimiwa Spika;
Ninafahamu ugumu wa vita niliyoamua kuipigana. Nasema nafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha na rushwa sio watu wadogo wadogo. Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi yetu hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi na utumishi ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu.  Kwa hivyo ili niweze kufanikiwa lazima nipate ushirikiano mkubwa toka kwa Bunge lako tukufu na vyombo vingine vilivyopo na vyenye majukumu ya kupambana na vitendo hivi.
Aidha, tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina mashaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Katika kushugulikia tatizo hili nimeahidi kuunda mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili havitanikwamisha.
Aidha, nataka niahidi mbele ya Bunge lako tukufu kwamba, kiongozi yeyote wa kuteuliwa, ambaye mimi nitakuwa nimemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na ninayo mamlaka ya kumwajibisha, pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya mimi kuchukua hatua hizo hatua na taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Mheshimiwa Spika;
Ninachotaka kusema ni kuwa Serikali yangu itafuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi na watendaji wake ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi. Na tukishajiridhisha hatutasubiri, tutachukua hatua. Ni imani yangu wengine pia katika ngazi mbalimbali mtafanya hivyo. Kwa sababu bila kufanya hivyo rushwa na ufisadi vitazoeleka na kuwa wimbo unaoburudisha badala ya kuudhi na kukera.
Muundo wa Serikali na Utumishi
Mheshimiwa Spika;
Nilipokuwa nazunguka na kuzungumza na wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi, niliahidi kuwa nitaunda serikali ndogo ya wachapa kazi.
Aidha, niliahidi pia kuunda serikali ambayo itawatumikia watu na hasa wananchi wa kawaida. Serikali nitakayounda, nataka iwe inawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu watumishi wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali nitakayoiongoza. Lugha za “hiyo ni changamoto tutaishughulikia”, au “Mchakato unaendeela” hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi Tu. Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza ofisi za umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuwataka watumishi wa Serikali kufanya kazi hatuna budi kuyaangalia na kuboresha mishahara na maslahi yao namazingira yao ya kufanyia kazi kwa kuwapatia vitendea kazi bora na vya kisasaNa jambo moja tutakalolitekeleza ni kuangalia namna ya kupunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi yaaniPAYE.  Pia tutajitahidi kuwatambua na kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.
Kuongeza Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.  Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi. 
Mheshimiwa Spika;
Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo tutayasimamia kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza, safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.
Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
·          Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;
·          Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;
·          Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;
Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.
          Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za walimu ngapi?, madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.
Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.
Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha ambayo kwa kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya Serikali.
Nne, tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba. Ni matarajio yangu kutakapoleta Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono.
Tano, tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu ununuzi wa bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Samani zote kwa ajili ya matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa hapa hapa nchini.
Sita, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu na kuthibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi waandamizi wa Serikali; na
Saba, tutaendelea kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na Taasisi zake zote yasiyo na tija kwa uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa ajili hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia kuiunda vitakuwa ni: kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikalikubana matumizi kwa kupunguza yale ambayo kutokana na hali yetu ya uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika; na kurejesha nidhamu ya  Serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.
          Tutatekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja na mambo mengine kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri; kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha kwamba wale wote wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu ya matumizi ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na waajiri wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kubainisha maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaigharimu Serikali fedha nyingi na kuyadhibiti. Aidha, nitoe wito kwa Watanzania wote kila mmoja wetu afanye kazi iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni, n.k.  Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka kwa Watanzania kutokupenda kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi vijiweni, muda ambao ungetumika kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu yangu ni HAPA KAZI TU!
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kikanda na Kimataifa
Mheshimiwa Spika;
          Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja ya diplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika awamu zilizotangulia za uongozi. Serikali yangu itaendeleza sifa hiyo kwa kujenga juu ya msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa waumini na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu. Tutaendelea kuwa waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na daima tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi wanachama. Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano wetu hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama ambao tunauhusiano wa kihistoria na kidugu. Tutaendelea kuamini katika Umoja wa Afrika (AU) na azma ya ndoto ya waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika. Tutaendelea pia kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na kushirikiana na nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu ya amani, usalama na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.
          Tutaendeleza na kustawisha mahusiano na marafiki zetu wote Magharibi, Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi zetu na watu wetu. Tutapenda kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri kisiasa kukuza mahusiano yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi. Tutafanya hivyo pia kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu na Umoja wa Mataifa (UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), n.k.
Aidha, tutazitaka Balozi zetu zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya fedha tunazowapelekea hususan katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na mchango wao katika ukuzaji wa sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia yetu na Sera yetu ya nje ikijibu changamoto zetu za ndani za ajira, miundombinu, masoko ya mazao ya wakulima, viwanda n.k.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika;
Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Bunge hili linalo nafasi ya kuweka historia ya kuwa kitu kimoja na kuweka masilahi ya Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha za vijembe, mipasho, na ushabiki wa vyama bungeni. Kwanza, tukumbuke wote bila kujali itikadi za vyama vyetu sisi ni kitu kimoja; na pili tumechaguliwa kuwawakilisha wenzetu. Baada ya miaka mitano kila mmoja atarudi kwenye jimbo lake kuomba kura na huko atapimwa kwa maendeleo aliyopeleka. 
Tusimame pamoja, Tanzania ni yetu sote tutangulize masilahi ya nchi mbele, na kwa mara ya kwanza Watanzania waone Bunge tofauti na sio Bunge la kuzomea, kutoka nje, kutukanana, mipasho, n.k. Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge hili Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.
Aidha, napenda kusisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa. Matarajio na matumaini ya Watanzania waliotuchagua na kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni makubwa. Wanachotaka kuona ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na mimi, baada ya miaka mitano toka sasa, tutapimwa kwa namna tutakavyokuwa tumetekeleza mambo ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu. Mimi nina amini kabisa kwa ushirikiano wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu tutaweza kuzitimiza ndoto za Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Spika;
Sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!

Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!

Ahsanteni kwa kunisikiliza.