WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 29, 2014

SOMA KWA MAKINI MAELEZO NA UFAFANUZI WA YA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA KATIKA AKAUNTI YA “ESCROW” YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL YALIYOWASILISHWA BUNGENI NA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI PROFESA SOSPETER MHONGO


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mhongo
---
 MAELEZO YA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA KATIKA AKAUNTI YA “ESCROW” YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL

1.  Historia ya Mradi
Mheshimiwa SpikaKatika miaka ya tisini (1990s), Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hali iliyopelekea kuwepo kwa upungufu wa umeme na kuathiri shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilichukua hatua za dharura za kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha Megawati (MW) 100.
2.  Upatikanaji wa IPTL
Mheshimiwa SpikaMwaka 1994 Serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni za VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania iliyokuwa na Asilimia 30 na MECHMAR Corporation ya Malaysia(MECHMAR) iliyokuwa na Asilimia 70. Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) Mtambo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 100 kwa kutumia mafuta mazito eneo la Tegeta-Salasala, Dar es Salaam.
Katika Ukurasa wa 52 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, Kamati imependekeza Mtambo huo utaifishwe.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Mkataba wa PPA kati ya TANESCO na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha Mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika Mkataba wa PPA wa tarehe 26 Mei 1995, ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha utaifishaji wa miradi ya uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji binafsi.
Mheshimiwa SpikaTarehe 26 Mei, 1995, TANESCO na IPTL walisaini Mkataba wa PPA kwa muda wa miaka ishirini (20), kwa ajili ya kununua umeme utakaozalishwa na IPTL. 


 Kwa mujibu wa Mkataba huo, IPTL ilitakiwa kuiuzia TANESCO umeme usiopungua Asilimia 85 ya uwezo wa Mtambo (minimum off take). Hata hivyo, uzalishaji wa umeme haukuanza mara moja kutokana na mgogoro uliotokea kati ya TANESCO na IPTL kuhusu gharama halisi za uwekezaji na namna ya kukokotoa Capacity Charges. Hivyo, IPTL ilianza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002. Kutokana na hali hiyo muda wa miaka 20 ya Mkataba ulianza kuhesabiwa tarehe 15 Januari, 2002 baada ya kuanza uzalishaji (Commercial Operation Date).
Mheshimiwa SpikaPamoja na mambo mengine muhimu yaliyokuwemo katika PPA, Kifungu Na. 6 cha Mkataba huo kinaipa TANESCO wajibu wa kulipa malipo yaliyotajwa hapo juu na kwamba endapo kutakuwa na mgogoro wowote kuhusiana na malipo hayo (Disputed Amount), itafunguliwa Akaunti maalum (Escrow Account) ya kuhifadhi fedha hizo hadi pale pande mbili zitakapokubaliana juu ya uhalali wa malipo yanayobishaniwa. Aidha chini ya PPA, migogoro yote kuhusiana na masuala ya utekelezaji wa Mkataba huo ilitakiwa kuwasilishwa na kuamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ya London. Hivyo, ilikuwa ni jukumu la kila mhusika katika Mkataba huu kuwasilisha malalamiko yake ICSID yanapotokea.

Katika Ukurasa wa 8 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa mwaka 2004 TANESCO ilifungua shauri la ICSID 2 kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa SpikaTaarifa hiyo siyo kweli kwani TANESCO haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au Mahakama yo yote dhidi ya Standard Charterd Bank kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa katika Taarifa ya PAC. Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa tarehe 31 Oktoba 2010 na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL.  Wahusika katika Shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na TANESCO na wala siyo TANESCO na IPTL.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Februari, 2014 ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana na Shauri la SCBHK na TANESCO na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na Mkataba wa kibiashara baina yao. Vile vile, kupitia Shauri la Madai Na. 60/2014, lililofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na IPTL tarehe 4 Aprili, 2014 ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo.
3.  Mgogoro kati ya IPTL na TANESCO
Mheshimiwa SpikaMigogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza muda mfupi baada ya PPA kusainiwa tarehe 26 Mei 1995. IPTL waliitaka TANESCO wakubaliane bei za kununua umeme kwa kuzingatia gharama za uwekezaji. Pande hizo mbili zilishindwa kukubaliana gharama za Capacity Charge kwa vile TANESCO walidai kuwa gharama zilizoainishwa na IPTL ni kubwa kuliko gharama halisi za uwekezaji. Mwaka 1998, TANESCO iliajiri Kampuni ya Mawakili ya Mkono & Co Advocates kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani. Kutokana na tofauti za gharama za Uwekezaji, Mawakili hawa waliishauri TANESCO ifungue Kesi ICSID nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.
Mheshimiwa SpikaKwa kuzingatia ushauri huo wa Mawakili, TANESCO ilifungua Kesi Na.ARB/98/8 ya mwezi Agosti, 1998 ikidai kuwa gharama halisi za uwekezaji ni Dola za Marekani milioni 90 na siyo milioni 163.53 kama ilivyodaiwa na IPTL. Aidha, IPTL ilidai kuwa kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ni Asilimia 23.10 ambacho pia kilipingwa na TANESCO.
Mheshimiwa SpikaTarehe 12 Julai, 2001, ICSID ilitoa uamuzi wa Kesi hiyo pamoja na mambo mengine kwamba:-
i.     Gharama halisi za uwekezaji zikiwemo Mtambo na nyumba za wafanyakazi wa IPTL zilizoainishwa katika hesabu ya IPTL zilikuwa ni Dola za Marekani milioni 163.53 lakini ICSID iliona kuwa gharama halisi ni Dola za Marekani milioni 127.20;
ii.     Kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ilikuwa Asilimia 22.31 badala ya Asilimia 23.10 iliyodaiwa na IPTL; na
iii.  TANESCO na IPTL wakubaliane mfumo wa malipo ya kununua umeme ukizingatia gharama halisi za uwekezaji na kiwango cha marejesho ya uwekezaji (IRR) cha Asilimia 22.31 kwa kutumia financial modeliliyokubalika na ICSID.
Katika Ukurasa wa 11 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa mtaji wa uwekezaji katika Mtambo wa IPTL ni Shilingi 50,000/= na kwamba huo ndio ungetumika kukokotoa Capacity Charges ili kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Maelezo hayo siyo sahihi. Ukweli ni kwamba kutokana na maamuzi ya ICSID 1 ya tarehe 12 Julai, 2001, gharama za ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.20 kama ilivyoelezwa katika Ukurasa wa 47Aya ya 4 ya Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika Taarifa hiyo, pia imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30. Hii ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani milioni 89.04 na mtaji ni Dola za Marekani milioni 38.16. Uamuzi huo haujabadilishwa na Mahakama yo yote au mtu ye yote.
Mheshimiwa Spika, Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokelewa kutoka Mabenki ya Ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani milioni 85.86 ambazo kati ya Dola za Marekani milioni 105 zilizokuwa zimeidhinishwa. Swali la kujiuliza, je Mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 85.86, huku gharama halisi ya ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani milioni 127.20?
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 38.16 ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji. Taarifa ya Kamati ya PAC haikuonesha fedha hiyo kuwa sehemu ya uwekezaji.
                                        
Mheshimiwa SpikaTarehe 30 Juni, 2004, Kampuni ya Mawakili iliyokuwa ikiiwakilisha TANESCO katika kesi ya kwanza ya usuluhishi, Kampuni ya Mkono & Co Advocates, iliishauri TANESCO iendelee kupinga kiwango cha malipo ya Capacity Charge kilichokuwa kimeafikiwa tarehe 12 Julai, 2001 na pande hizi mbili katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) ya London. Hii ilikuwa ni miaka miwili tu baada ya usuluhishi uliochukua miaka minne kukamilika na Mtambo kuanza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002.
Mheshimiwa SpikaHata hivyo, baada ya ushauri huu, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates) hawakuishauri TANESCO ifungue kesi katika Mahakama za Tanzania wala katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICSID) ya London.
Mheshimiwa SpikaHadi kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 wakati Mheshimiwa Jaji Utamwa anatoa hukumu yake juu ya mgogoro wa Wanahisa wa IPTL hapakuwepo na kesi yo yote kwenye Mahakama yo yote ya kupinga gharama za Capacity Charge kati ya TANESCO na IPTL, iwe katika Mahakama za ndani au za nje. Kwa kutokuwepo Msuluhishi (Broker) katika suala hili, madai yo yote ya TANESCO yanakuwa ni madai ya upande mmoja ambayo kisheria hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo madai halisi.  Kwa sababu hiyo haikuwepoformula rasmi ya kuutatua mgogoro huozaidi ya majadiliano na maafikiano kati ya pande mbili (TANESCO na IPTL).
4.  Uuzaji wa Hisa za VIP
Mheshimiwa SpikaKutokana na VIP Engineering and Marketing Limited (VIP) kuona kuwa hainufaiki na ubia wake katika IPTL, ilikusudia kuuza Hisa zake kwa MECHMAR. Hata hivyo, MECHMAR haikuweza kununua Hisa hizo kwa sababu ilitaka thamani ya Hisa za VIP zitokane na ripoti ya ukaguzi ya mwaka (Audited Financial Report) na taratibu za kihasibu za kimataifa (International Accounting Rules), VIP haikukubaliana na utaratibu huo.
Mheshimiwa SpikaKutokana na kutokubaliana, MECHMAR iliishauri VIP ifungue Shauri la madai hayo kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Uingereza (LCIA) kulingana na Mkataba wa Wanahisa wa IPTL. Hata hivyo, VIP haikufungua Shauri katika Mahakama ya usuluhishi kama ilivyoshauriwa na MECHMAR badala yake tarehe 25 Februari, 2002 VIP ikafungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Miscellaneous Civil Application No. 49/2002) ikiomba Kampuni ya IPTL ifilisiwe ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuanza uzalishaji.
5.  Uamuzi kuhusu Ufilisi wa IPTL
Mheshimiwa SpikaShauri lililofunguliwa na VIP tarehe 25 Februari, 2002 liliendelea kuwa Mahakamani hadi ilipofika tarehe 16 Desemba, 2008. Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jaji Oriyo, J ilitoa uamuzi wa kuiweka IPTL katika Ufilisi wa Muda (Provisional Liquidation) chini ya Kabidhi Wasii Mkuu (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini - RITA). Mfilisi wa Muda alipewa majukumu maalum yafuatayo:
            i.      Kulinda mali zote za IPTL katika kipindi chote cha Ufilisi wa Muda; na
          ii.      Kufanya uchunguzi wa tuhuma zote zilizotolewa na VIP dhidi ya MECHMAR na kutoa ripoti za uchunguzi huo ili Mahakama iweze kutoa uamuzi.
Mheshimiwa SpikaTarehe 15 Julai, 2011, Mahakama Kuu ya Tanzania (Kaijage, J) ilitoa uamuzi kwamba, IPTL iwekwe kwenye Ufilisi Kamili (Full Liquidation) na RITA ilithibitishwa kuwa Mfilisi wa IPTL.
Mheshimiwa SpikaKutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK) iliyokuwa imenunua deni la IPTL kutoka kwa DANHARTA, ilipinga na kuiomba Mahakama ya Rufaa ifanye mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu (Application for Revision – Civil Revision No. 1/2012) ikiainisha dosari katika uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru kufilisiwa kwa IPTL. SCBHK ilibainisha dosari za maombi ya kutaka IPTL kufilisiwa kwa kuwa maombi ya SCBHK ya kutaka Mahakama iteue msimamizi (Administrator) wa kuisimamia IPTL (kwa niaba ya SCBHK) yalikuwa hayajasikilizwa.
Mheshimiwa SpikaMahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubaliana na hoja za SCBHK na hivyo kuamuru shauri hilo lirejeshwe Mahakama Kuu ili IPTL irudi mikononi mwa Mfilisi wa Muda (Provisional Liquidator) ambaye alipewa majukumu yafuatayo:-
                      i.        Kukusanya mali na madeni yote ya IPTL;
                    ii.        Kupokea na kusajili madeni yote dhidi ya IPTL;
                  iii.        Kusuluhisha migogoro kati ya wanahisa wa IPTL; na
                   iv.        Kusimamia na kuendesha Mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL kwa niaba ya IPTL.
Mheshimiwa SpikaBaada ya kuteuliwa, Mfilisi wa Muda (Provisional Liquidator) alifanya juhudi ya kumaliza mgogoro huo wa IPTL nje ya Mahakama kwa kushirikisha wadau mbalimbali (Stakeholders) wa IPTL kupitia kikao chake cha tarehe 9 Novemba, 2011. (Kiambatisho Na.1). Juhudi hizo hazikufanikiwa na ikalazimu shauri liendelee Mahakamani.
6.  Uhalali wa uhamishwaji wa Asilimia 70 za
   Hisa za MECHMAR kwenda PAP
Mheshimiwa SpikaSuala la uhalali wa umiliki wa Hisa katika Kampuni hizi linahusu wanahisa wa Kampuni wenyewe. Serikali haiwajibiki kuingilia mahusiano ya kibiashara ya wanahisa katikaKampuni Binafsi. Hata hivyo, kulingana na Sheria za nchi ikiwa ni pamoja na Kifungu cha 172 cha Sheria ya Makampuni (Sura 212), mauziano ya Hisa yaliyofanyika nje ya nchi yatatambuliwa tu, endapo usajili wa Hisa hizo utafanyika hapa nchini. Kwa mujibu wa taarifa za BRELA za tarehe 31 Desemba, 2013, zinaonesha kuwa uhamishaji wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki wa Asilimia 70 za IPTL.
Katika ukurasa wa 44 Aya ya 1 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa PAP siyo mmiliki halali wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Katika maelezo ya Kamati ukurasa wa 30, Kamati imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya MECHMAR na Piper Link zilipokelewa na Harbinder Singh Sethi ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP. Kwa uthibitisho huo, Kamati inakubali kuwa Hisa za MECHMAR katika IPTL zinamilikiwa na PAP. 
Katika Ukurasa wa 25 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa hakuna ushahidi wa PAP kumiliki Asilimia 70 ya Hisa zilizokuwa zikimilikiwa na MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa umiliki wa Hisa 7 za IPTL unatambuliwa hata na SCBHK ambayo ilisaini makubaliano tarehe 25 Novemba 2011 na PAP ya kulipwa deni la mkopo wa fedha za kununua deni la ujenzi wa Mtambo wa Tegeta. Kiambatisho Na 2.
7.  Majadiliano ya mikopo ya IPTL na Wadai
Mheshimiwa SpikaKutokana na Hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa tarehe 5 Septemba 2013, Kampuni ya PAP ilijadiliana na wadai halali wa mikopo ya IPTL na kuingia Mkataba wa kuwalipa wadai wote wa IPTL. SCBHK inayodai kuidai IPTL mikopo katika ujenzi wa Mtambo wa Tegeta haikuwasilisha madai ya aina yo yote ili iweze kulipwa.
Mheshimiwa SpikaUkweli ni kwamba, SCBHK iliyokuwa ikiidai IPTL fedha ilizotumia kununua deni lililotokana na kufilisiwa kwa MECHMAR kule Malaysia (siyo Tanzania) haijawahi kujadiliana na IPTL kuhusu malipo ya mkopo wake kama upo. Mvutano huu unaendelea ICSID kati ya TANESCO na SCBHK, ukiitaka TANESCO ilipe gharama za kununua umeme ikijumuisha deni la IPTL. Madai ya SCBHK dhidi ya TANESCO yanatokana na madai ya kuwepo kwa Deed of Assignment ya MECHMAR kuhusiana na Mkopo wa IPTL ambapo Mtambo wa IPTL uliwekwa kama dhamana ya Mkopo.
Mheshimiwa SpikaHata hivyo Deedof Assignment hiyo haikuwahi kusajiliwa hapa nchini kama inavyotakiwa katika Kifungu Na. 172 cha Sheria za Makampuni Sura. 212 zinavyoelekeza. Kutokana na kutokusajili Assignment DeedhiyoSCBHK ilikosa sifa za kufungua madai yake hapa nchini badala yake ilifungua madai haya ICSID nchini Uingereza. Kitendo hicho kinaonesha kudharau Mahakama zetu na PAC inataka tuziamini Mahakama za nje kuliko za kwetu.
8.  Jitihada za Makampuni mbali mbali kununua Hisa za VIP
Mheshimiwa SpikaKutokana na tofauti zilizokuwepo kati ya MECHMAR na VIP kuanzia mwanzo wa mradi, VIP iliamua kuuza Hisa zake zilizoko IPTL kwa makampuni mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwemo MECHMAR kama mwanahisa mwenzake,  NSSF, Camel Oil, Great White Shark Opportunity Fund pamoja na SYMBION lakini haikuwezekana kutokana na kutoafikiana katika bei.
Mheshimiwa SpikaBaadaye VIP chini ya usuluhishi ya RITA, iliuza Hisa zake kwa PAP kwa thamani ya Dola za Marekani milioni sabini na tano (US$ 75,000,000/=). Ununuzi wa Hisa Asilimia 30 za VIP uliofanywa na PAP ndiyo uliyomaliza mgogoro wa Wanahisa uliyokuwa Mahakamani na kuufanya Mtambo wa IPTL kumilikiwa na PAP kwa kuwa ndiyo iliyomiliki Hisa zote Asilimia 100 za IPTL.
Taarifa ya PAC: Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekuwa Dalali Mkuu aliyewakutanisha Bw Harbinder Sethi na Bw James Rugemalira
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa hii siyo sahihi kwa kuwa tangu tarehe 9 Novemba, 2011, RITA aliitisha mkutano na kuwakutanisha wadau wote wa IPTL. Wakati huo, Waziri wa Nishati na Madini aliyeko sasa alikuwa bado hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
9.  Kufungua ESCROW Akaunti
Mheshimiwa SpikaTarehe 30 Juni 2004, TANESCO kwa ushauri wa Mkono & Co Advocates walitoa hoja kuwa gharama za kununua umeme zilikokotolewa kwa kutumia IRR ya Asilimia 23.10 na makadirio ya gharama za mtaji wa Asilimia 30 ambao ni Dola za Marekani milioni 38.16, wakati mtaji halisi (equity) wa IPTL ni chini ya Dola za Marekani 100. Hivyo, TANESCO walikuwa wakitoa notisi (Dispute Notice) kwa kila Ankara ya malipo kupinga gharama hiyo kulingana na Kifungu Na. 6.8 cha Mkataba wa PPA. Kifungu hicho kinaeleza kuwa ikiwa upande wote haukubaliani na usahihi wa malipo katika Ankara zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ya gharama za umeme wanatakiwa watoe notisi (Invoice Dispute Notice) kwa upande mwingine. Vile vile, Mawakili wa TANESCO (Mkono & Co Advocates) walishauri kwamba kutokana na pingamizi hilo, ifunguliwe Akaunti Maalum(Escrow Account) kwa ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zilitokana na Ankara zilizokuwa zinapingwa.
Mheshimiwa SpikaKutokana na ushauri wa Mkono Co. & Advocates tarehe 5 Julai, 2006, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisaini Mkataba wa kufungua Akaunti Maalum (Escrow Account) kwa ajili ya kuweka fedha zote za Ankara zilizopaswa kulipwa kwa IPTL. 
10.    Mmiliki wa Fedha za Akaunti ya Escrow:
Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 22 imeelezwa kuwa Akaunti ya Escrow ilipaswa kuwa na Shilingi bilioni 306.70 ambazo zingekuwa zimewekwa na TANESCO. Hata hivyo, katika mapendekezo ya Kamati ya PAC ukurasa wa 50, Kamati imeeleza kwamba imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba mchakato mzima wa kutoa fedha katika Akaunti ya Escrow umegubikwa na mchezo mchafu na kwamba Mfumo mzima wa Serikali ulipata ganzi ili kuwezesha zaidi ya Shilingi bilioni 306kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kutakatishwa kupitia benki mbili hapa nchini.
11.                  Tahadhari iliyochukuliwa na Serikali
        wakati wa kutoa fedha kwenye akaunti ya  
        Escrow
Mheshimiwa Spika, Kwa kuelewa kwamba kunaweza kukatokea madai kwa IPTL, na kwa kuwa Serikali ilitoa dhamana kwa TANESCO ya kununua umeme wa IPTL, Serikali ilihakikisha inachukua KINGA (Indemnity) kutoka IPTL katika maeneo yote muhimu. Kwa mujibu wa KINGA hiyo, kama kutajitokeza madai yo yote yale, IPTL yenyewe itawajibika. Ikumbukwe kuwa kabla ya kusaini, KINGA hiyo ilipitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuthibitisha kwamba inakidhi matakwa ya kulinda maslahi ya Taifa. KINGA hii ilitolewa tarehe 27 Oktoba, 2013. Inasema, nanukuu:
“IPTL do hereby agree to INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent (jointly and severally) against all presentand future claims, actions and legal proceedings that may arise in respect of and/or all losses, charges, costs, and expenses the Government and the Escrow Agent may suffer or incur consequent upon the release and payment of the funds in the Tegeta Escrow Account or part thereof to IPTL pursuant to the Agreement for Delivery of Funds”.
Katika Ukurasa wa 48 wa Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai mengine yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya Escrow.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, KINGA iliyochukuliwa inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia athari yo yote ambayo ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha katika Akaunti ya Escrow. Kwa hiyo siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.
12.    Dhana ya Madai ya Shilingi Bilioni 321
Mheshimiwa Spika, Madai ya kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/- kwa wakati huo.Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi bilioni 321Kimsingi hata Vitabu vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havioneshi kuwepo kwa deni hilo.
Mheshimiwa SpikaMadai ya Shilingi bilioni 321 yaliyowasilishwa kwa Mfilisi na Mwanasheria wa TANESCO (Mkono & Co. Advocates) ulihitaji kuhakikiwa kabla ya kukubaliwa na Mfilisi kama madai halali. Hata hivyo, uhakiki huo haukufanyika kwa sababu ya Hukumu ya Mahakama ya Rufaa katika Civil Revision No. 1 ya Mwaka 2012, ambayo ilifuta maamuzi ya Mahakama Kuu ya kuiweka IPTL katika Ufilisi na kuirudisha kwenye Ufilisi wa Muda. Hivyo, madai hayo ya Shilingi bilioni 321 na kiapo chake ambacho hakitambuliwi na Bodi ya TANESCO hayakuwa tena na uhalali wo wote.
Kamati ya PAC: Katika ukurasa wa 47 Aya ya 2 Kamati imejiridhisha kuwa madai ya TANESCO ya Shilingi Billioni 321 yana uhalali japo usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na TANESCO na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Madai ya kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/- kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi bilioni 321Kimsingi hata Vitabu vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havioneshi kuwepo kwa deni hilo.
13.      TANESCO na IPTL kufanya Reconcillation ya fedha iliyokuwa kwenye Akaunti ya Escrow
Mheshimiwa SpikaTANESCO kwa kushirikiana na IPTL ilifanya uhakiki (reconciliation)tarehe 9 Oktoba, 2013 ili kujua madai halali ya IPTL kabla ya kufanya malipo. Takwimu za Mfilisi wa Muda wa IPTL (RITA) wakati akikabidhi mali na madeni ya IPTL, ilionesha kwamba deni lote alilokuwa akidaiwa TANESCO na IPTL kamaCapacity Charges ni Shilingi bilioni 370.70, sawa na Dola za Marekani milioni 224.30. Katika majadiliano kati ya TANESCO na IPTL, gharama zilizokubaliwa kama Capacity Charges zilizokuwa zinadaiwa ni Shilingi bilioni 275.20. Fedha hizi ni pungufu kwa Shilingi bilioni 95.50 ya madai ya IPTL. Hadi kufikia tarehe 25 Novemba 2013, fedha iliyokuwa katika Akaunti ya Escrow ilikuwa jumla ya Dola za Marekani milioni 22.20, sawa naShilingi bilioni 36.72 na Shilingi bilioni 161.39.
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum umeonesha pia kuwa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow wakati wa kuifunga ni Shilingi bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa Shilingi bilioni 123.90 wa madai ya IPTL.
14.      Iwapo Serikali ilistahili kutoa fedha katika Akaunti ya Escrow wakati Shauri la ICSID, London inaendelea
Mheshimiwa SpikaKesi iliyopo ICSID, London ilihusu madai ya Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong yaliyotokana na kununua deni lililotokana na uwekezaji katika Mtambo wa IPTL wa Tegeta. Katika Mkopo huo, Mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Mtambo wa kuzalisha umeme wa Tegeta viliwekwa kama dhamana.
Mheshimiwa SpikaTANESCO haikuhusishwa kwenye majadiliano ya dhamana hiyo. IPTL ilishindwa kumaliza marejesho ya Mkopo huo na hivyo Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong kuanza kuidai TANESCO madeni yaliyotokana na Mkopo huo. Hata hivyo, fedha katika Akaunti ya Escrow ilitokana na Ankara za Capacity Charges zilizokuwa zikibishaniwa kati ya TANESCO na IPTL kuhusu viwango vilivyotumikakukokotoa malipo hayo na siyo mikopo ya IPTL.
Mheshimiwa SpikaHata hivyo, Standard Chartered Bank Hong Kong siyo mhusika (not a party)katika Mkataba wa tarehe 26 Mei, 1995 wa PPA kati ya TANESCO na IPTL. Kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, madai yo yote yaliyotokea nje ya nchi yakihusu uwekezaji ulioko nchini ni lazima yasajiliwe hapa nchini.
Mheshimiwa SpikaKwa mantiki hiyo, Shauri lililoko ICSID, London halihusiani na fedha za Akaunti ya Escrow bali mikopo ya IPTL. Hata hivyo, wadai wa IPTL waliamriwa na Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 5 Septemba, 2013 kuwasilisha madai yao kwa PAP. Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong haijafanya hivyo.
15.    Ulipwaji wa Madai na Madeni
Mheshimiwa SpikaKuhusu madai na madeni dhidi ya IPTL ikiwemo VAT, Serikali na BOT ziliitaka IPTL iweke KINGA (Indemnity)ili kuihakikishia Serikali kuwa endapo kutakuwa na madai au madeni ya aina yo yote, IPTL itawajibika kuyalipa. Tarehe 27 Oktoba, 2013, IPTL ilitoa KINGA hiyo, nanukuu:
“IPTL do hereby agree to INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent (jointly and severally) against all present and future claims, actions and legal proceedings that may arise in respect of and/or all losses, charges, costs, and expenses the Government and the Escrow Agent may suffer or incur consequent upon the release and payment of the funds in the Tegeta Escrow Account or part thereof to IPTL pursuant to the Agreement for Delivery of Funds”.
16.        Gharama za Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams ya Marekani) Katika Kuendesha Kesi za IPTL
Mheshimiwa SpikaHadi Hukumu ya Mheshimiwa Jaji Utamwa inatolewa tarehe 5 Septemba mwaka 2013, TANESCO na Serikali zilikuwa zimewalipa Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) jumla yaShilingi za Tanzania bilioni 62.90 na bado Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wanaidai TANESCO Dola za Marekani milioni 4.50. Katika ushauri wao walikuwa wamependekeza kwa Serikali wapewe kazi nyingine ya kwenda kutetea Guarantee ya Serikali pamoja na kupingaHukumu ya tarehe 12 Februari, 2014 iliyotolewa katika uamuzi wa ICSID-2. Ushauri wao upo katika Memorandum yatarehe 9 Oktoba, 2013 waliyowasilisha TANESCO.
Mheshimiwa Spika,Wakati ambapo hatukujua ni kiasi gani Serikali na TANESCO ingeweza kupata kwa kuendelea kupinga Capacity Charges za IPTL, tunajua fika ni hasara gani tumepatakupitia malipo ya Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) yaani ya Shilingi bilioni 62.9 na bado wanadai Dola za Marekani milioni 4.5.
Mheshimiwa Spikakumalizika kwa mgogoro huu wa IPTL si tu kwamba kumetuondoa kwenye hatari ya kuendelea kukamuliwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) hawa bali pia katika mazungumzo yaliyofanywa kati ya TANESCO na IPTL tumeweza kuokoa takribani Shilingi bilioni 95 katika madai ya awali ya IPTL.
17.      Ushauri wa Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wa TANESCO wa Tarehe 4 Oktoba, 2012
Mheshimiwa Spika, Mawakili wa TANESCO na Serikali yaani Kampuni za Mkono & Co Advocates na Hunton & Williams waliandika ushauri wa pamoja wa tarehe 4 Oktoba 2012 ambapowalifafanua kwa kina juu ya Shauri lililokuwa likiendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) ya London. Katika Ushauri wao walionyesha wazi kwamba TANESCO ilikuwa na nafasi finyu mno ya kushinda katika Kesi iliyokuwa ikiendelea kati ya TANESCO na SCBHK.
Mheshimiwa Spika, Katika ushauri wao walieleza mambo muhimu ambayo ni vema Bunge lako Tukufu likAyaelewa hasa kwa ajili ya watu wanaodhani kwamba ilikuwa ni makosa kwa TANESCO kukaa na IPTL baada ya Hukumu ya Mahakama Kuu ya tarehe 5 Septemba, 2013. Baadhi ya maeneo walioshauri TANESCO ikae na IPTL kujadiliana kwa kile kilichoelezwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) kuwa uwezekano wa kushinda kesi ni mdogo ni pamoja na:-
18.    Ushauri wa Mawakili Unaokinzana
Mheshimiwa Spika, Tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili wetu (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) walitoa ushauri kwamba, kwa kuzingatia utetezi walioutoa kwa TANESCO kwenye kesi hii kule ICSID, London kiasi cha chini kabisa kinachoweza kuidhinishwa na Mahakama ya ICSID, London kama malipo ya Capacity Charges kwa IPTL ni kati ya Dola za Marekani milioni 85 hadi 90 na Mawakili wetu (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams)  wakasema, nanukuu, This could be considered TANESCO’s  Best Case Scenario. Hata hivyo waliendelea kusema “This best Case Scenario is overly optimistic”.
Mheshimiwa Spika,Katika maelezo yao mengine ya tarehe 4 Oktoba 2012, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wanasema, “In these circumstances, SCBHK may recover 100% of itsclaimeddamages of USD 130 milion even if substantially TANESCO prevails on a portion of its equity defense”.
Kwa lugha nyingine Mheshimiwa Spika, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wanasema kiasi cha chini kabisa ambacho TANESCO ingedaiwa na SCBHK kingekuwaDola za Marekani milioni 130 bila kujumuisha gharama nyingine za moja kwa moja kwa IPTL.
Mheshimiwa SpikaKatika majumuisho yao ya tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) waliishauri TANESCO ikae na SCBHK na kukubaliana nje ya Mahakama na kumlipa Dola za Marekani kati ya milioni 75 na milioni 90 na kiasi kitakachobaki kikidaiwa kilipwekwa wadai wengine, wakiwemo IPTL, Law Associates na Kampuni ya Mafuta ya TOTAL.
Mheshimiwa Spika, Kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 kwa mujibu wa Taarifa ya Mfilisi (RITA), ilionesha kuwa Kampuni ya IPTL ilikuwaikiidai TANESCO zaidi ya Dola za Marekani milioni 224.30, sawa naShilingi bilioni 370.70. Majadiliano yaliyofanyika kati ya TANESCO na IPTL tarehe 9 Oktoba, 2013 yaliwezesha kukubaliana kuwa malipo stahiki kwa IPTL ni jumla ya Dola za Marekani milioni 166, sawa na Shilingi bilioni 274.56. Kati ya hizo, Dola za Marekani milioni 121, sawa na Shilingi bilioni 220.13 zilikuwa kwenye Akaunti ya ESCROW na Dola za Marekani milioni 45, sawa na Shilingi bilioni 74.43 zitalipwa kwa kipindi cha muda mrefu usiozidi miaka mitano.
19.    Kama fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ni za Umma
Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow zilikuwa za Serikali.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, Huu si ukweli zipo sababu kuu zinazothibitisha kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali.
1.  TANESCO ilikuwa inapata huduma ya umeme bila kulipa moja kwa moja IPTL, lakini ikawa inapeleka fedha hizo katika Akaunti ya Escrow.
2.  TANESCO ilisimamisha kupeleka malipo kwenye Akaunti ya Escrow na wala kulipa IPTL kuanzia tarehe 30 Oktoba, 2010.
Pamoja na kutokulipa, TANESCO iliendelea kupata huduma ya umeme kwa kadri ilivyohitaji kutoka IPTL.
Mheshimiwa Spika, Katika Ukurasa wa 36 hadi 42 wa Taarifa ya Ukaguzi Maalum ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo tumekabidhiwa inaonesha kiasi ambacho TANESCO inadaiwa na IPTL.
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Taarifa hiyo ukurasa wa 36 hadi42 imeonesha kuwa kiasi ambacho kilipaswa kuwekwa kwenye Escrow Account kwa mujibu wa Ankara za IPTL ni Shilingi bilioni 306.68. hata hivyo, kwa mujibu wa Ukaguzi huo fedha zilizokuwa kwenye Akaunti wakati wa kuifunga ni Shilingi bilioni 182.77 na kuwa na  upungufu wa Shilingi bilioni 123.90 ikiwa ni deni ambalo TANESCO bado wanadaiwa na IPTL.
Mheshimiwa Spika, Kwa msingi huo fedha zote zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ni mali ya IPTL na IPTL kama Wakala wa Kodi anastahili kudaiwa na mwisho kulipa kodi yo yote ambayo hajalipa.
Kwa msingi huo, Taarifa ya PAC haisemi ukweli kuhusu fedha zilizowekwa katika Akaunti ya Escrow kuwa ni fedha za umma.
Mheshimiwa spika, Ili kuthibitisha kwamba fedha hizi siyo za Umma, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wake wa Hesabu za TANESCO wa tarehe 31 Desemba 2012, alielekeza kutoa fedha za Escrow kwenye Vitabu vya Hesabu vya TANESCO na kupunguza deni kwa kiasi hicho hicho kwa maelezo yafuatayo:
“As a result, the deposit balance in Escrow account does not meets the definition of an asset of the Company and therefore an adjustment has been made to de-recognize the asset and related liability to the tune of the amounts available in the Escrow account”.
20.    Iwapo kwa mujibu wa Mkataba wa PPA TANESCO na IPTL walilazimika kutumia Mtaalamu wa Upatanishi (Mediation Expert) katika utatuzi wa mgogoro kabla ya kutolewa fedha zilizopo kwenye Akaunti ya Escrow.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 9, imeeleza kuwa kwa mujibu wa Mkataba wa PPA, TANESCO na IPTL walipaswa kutumia Mtaalam wa Upatanishi katika mgogoro wa Capacity Charge.
Mheshimiwa Spika, Tunapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 18.1 ya Mkataba wa PPA, wahusika wa Mkataba huo ambao ni TANESCO na IPTL wanatakiwa kwanza kumaliza mgogoro baina yao kwa njia ya upatanishi (amicable settlement). Iwapo watashindwa kufikia makubaliano ndipo watalazimika kutumia Mtaalam wa Upatanishi kutatua mgogoro huo. TANESCO na IPTL walimaliza mgogoro baina yao kwa njia upatanishi kwa kufanya uhakiki wa kiasi ambacho kila upande ulikuwa unastahili kulipwa katika Akaunti ya ESCROW kabla ya akaunti hiyo kufungwa. Kwa msingi huo, hapakuwa na sababu ya kutumia Mtaalam wa Usuluhishi kama ilivyoelezwa katika Taarifa ya PAC.
21.    Kama muda wote wa Mkataba wa TANESCO na IPTL
hapakuwahi kuwa na Kamati ya Uendeshaji
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya PAC inaeleza kuwa hapakuwahi kuwa na Kamati ya Uendeshaji kwa kipindi chote cha Mkataba wa PPA. Ukweli ni kwamba, Kamati ya Uendeshaji iliundwa kabla ya kuanza uzalishaji wa Mtambo hapo 2002 na imeendelea kuwepo hadi leo. Kamati hiyo ina wajumbe  sita. Wajumbe watatu kati ya hao wanatoka TANESCO. Wajumbe watatu waliobakia wanatoka IPTL. Wajumbe wa TANESCO walikuwa ni kama ifuatavyo:
1.  Mhandisi Masanyiwa Malale;
2.  Mhandisi Christian Msyani; na
3.  Mhandisi James Mtei.
Mheshimiwa Spika, Kwa msingi huo si kweli kwamba Kamati ya Uendeshaji haikuundwa kama ilivyoelezwa na Kamati ya PAC katika ukurasa wa 10.
22.    Wizara kutambua Hati za Hisa za Makampuni
Mheshimiwa Spika, Katika ukurasa wa 27 wa Taarifa ya Kamati ya PAC, Kamati hiyo imeitaka Wizara ya Nishati na Madini kutambua usajili wa Hati za Hisa za Makampuni. Tunaomba ieleweke kuwa siyo majukumu ya Wizara kutambua na wala kujishughulisha na Hati za Hisa za Makampuni Binafsi. Aidha, katika ukurasa wa 45, imeelezwa kwamba “Waziri wa Nishati na Madini ndiyo Mamlaka ya kuthibitisha uhamishaji wa umiliki wa Kampuni katika sekta yake”. Ningependa kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba jukumu hilo pia siyo la Wizara ya Nishati na Madini ni vizuri majukumu ya Wizara yakaangaliwa vizuri na kutoleta mkanganyiko na kuwadanganya wananchi wetu. Hii inaonesha kuwa kamati haikupitia vizuri majukumu ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya PAC, ukurasa wa 30 Aya ya 2, imeelezwa nanukuu “nilishuhudia nyaraka kwamba Piper Link ilinunua Hisa za MECHMAR na katika mauziano hayo Kampuni hiyo iliwakilishwa na Bw. Harbinder Singh Sethi hivyo huyu bwana ndiye Piper Link na ndiye PAP”. Kwa maneno haya ya Kamati ya PAC, aliyekuwa na hati za Piper Link ni Bw. Sethi na aliyenunua Piper Link ni Bw. Sethi anayemiliki PAP. Kwa kuzingatia maelezo haya ya kamati ya PAC, inaonesha kwamba hakuna tatizo la uhamishaji wa Hisa Asilimia 70 kwenda kwa PAP.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na maelezo ya Aya iliyotangulia, bado Kamati ya PAC ukurasa 44 wa taarifa yake, inaonesha kuwa Hisa hizo zinashikiwa na Martha Renju huko BVI lakini Martha Renju amefungua kesi mara mbili Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kutumiwa na SCBHK akiwa na lengo la kutaka kujipatia fedha za Escrow bila uhalali. Hata hivyo, amekuwa akiziondoa kesi hizo mahakamani.
23.    Mikutano ya Bodi ya Wakurugenzi wa
  TANESCO
Mheshimiwa Spika,Katika ukurasa wa 29 wa Taarifa ya PAC, inasema kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilifanya mikutano miwili mfulilizo kati ya tarehe 16 na tarehe 19 Septemba, 2013 na kwamba uharaka huo unatia mashaka kwamba kulikuwa na njama.
Mheshimiwa Spika, Muda wa siku 3 kwa Bodi kukutana si jambo la kutiliwa mashaka kwani Bodi haikutani kwa ajenda moja tu. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa tarehe 16 Septemba, 2013 hapakuwa na kikao cha Bodi isipokuwa kikao cha Bodi kilifanyika tarehe 19 Septemba, 2013. Hivyo si sahihi kusema kuwa Bodi ya TANESCO ilikuwa ina njama katika kushughulikia na kulitolea maamuzi suala la Akaunti ya Escrow na kwamba ilikutana ndani ya siku tatu.
24.    Hoja ya Mwanasheria wa TANESCO
  Kufukuzwa Kazi
Mheshimiwa Spika, Katika ukurasa wa 30 wa Taarifa ya PAC kuna hoja kuwa Mwanasheria wa TANESCO kwa wakati huo Bw. Godwin Ngwilimi aliagizwa na TANESCO kwenda Malaysia kufanya Due Diligence ya Kampuni ya MECHMAR Corporation na kwamba taarifa hiyo ya Due Diligence ilifikishwa katika Bodi na Bodi iliipuuza na kinyume chake Mwanasheria huyo aliachishwa kazi. 
Mheshimiwa Spika, Taarifa hizi si za kweli na ni uongo uliokithiri kwa aliyekuwa Mtumishi wa Umma kuudanganya umma wa Watanzania kwa kiasi cha kutisha na Kamati inatoa taarifa ya uongo ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, Ukweli wa jambo hili ni kama ifuatavyo:
1.  Mwanasheria huyo Bw. Ngwilimi alileta ombi la kusafiri kwenda Malaysia kwa kumdanganya Mwajiri wake kwa kudai kuwa alipewa ushauri wa kwenda Malaysia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika barua ya kuomba ruhusa alisema kuwa alikuwa aende na Mwanasheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliruhusiwa.  Hata hivyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali haikutoa Ofisa huyo na hivyo kuamua kwenda peke yake.
2.  Bw. Ngwilimi hakufukuzwa kazi na Bodi kama ilivyodaiwa katika Taarifa ya kamati ya PAC katika ukurasa wa 30, bali aliomba kuacha kazi mwenyewe kwa kutoa taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa barua ya yenye Kumb na. SEC.215/Conf/2/2014 ya tarehe 27 Februari, 2014 iliyokuwa inasomeka “Notice to Terminate my Service with TANESCO” akitoa notisi ya siku 90 kwa mujibu wa Mkataba wake wa kazi.
3.  Katika ombi lake alidai kuwa anaacha kazi kwa hiari yake mwenyewe kwa kuwa anahitaji kufanya shughuli nyingine na akaushukuru uongozi wa TANESCO kwa ushirikiano kwa kipindi chote alichofanyakazi. Machi 10, 2014 Shirika lilimjibu Bw. Ngwilimi kwa barua yenye Kumb. Na. N.837 kuwa Uongozi na Bodi ya TANESCO wamekubali ombi lake la kuacha kazi.
Mheshimiwa Spika, Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa Bodi haikuwahi kumfukuza na Bodi haikukataa utoaji wa fedha za IPTL katika Akaunti ya Escrow. Badala yake Bodi ilielekeza IPTL ipewe fedha zilizopo kwenye Akaunti ya Escrow tu na kwamba usuluhisho uliyofanyika unakubalika. Aidha, Bwana Ngwilimi aliamua kuacha kazi mwenyewe na kukimbia baada ya kuelewa kuwa angechukuliwa hatua kutokana kumsingizia Mtumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa walitumwa wote na kusafiri wote kwenda kufanya kile alichodai due diligence.

source: haki ngowi blog