WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 28, 2014

Neno Fupi La Leo: Bunge La Katiba Na Kisa Cha Risasi Ya Mwisho...!

Ndugu zangu,
Jana katika nyakati tofauti nimefuatilia mjadala wa rasimu ya kanuni za Bunge hilo.
Kuna wakati nimejiuliza; hivi wote mle ndani wanajua maana ya dhamana kubwa waliyobeba kwa ajili ya nchi hii, leo na kesho?
Kwamba hawapaswi kuonyesha aibu ile ya kujikita kwenye kujadili mustakabali wa taifa kwa kuvaa miwani ya makundi na vyama vyao vya siasa. Kuingia kwenye ushabiki kama wa Simba na Yanga. Maana, inahusua masuala ya msingi yaliyo mbele ya uhai wa vyama vya siasa.
Katiba ni dira ya nchi. Ni ramani ya kutuongoza Watanzania wa leo na wajao, bila kujali makundi na vyama vya siasa.
Kwa WaTanzania, madai ya kupata Katiba mpya ni madai halali yanayotokana pia na kukosekana kwa Haki, Uwazi na Uwajibikaji, hususan kutoka kwa baadhi ya wenye kupewa dhamana za uongozi.
Watanzania ni kama kisa cha wanakijiji waliokuwa kwenye shida ya njaa ya miaka hamsini. Na katika kuhangaika kwao,na kwa risasi yao ya mwisho waliyobaki nayo kwenye gobore moja na la pekee kijiji kizima, wamekaa kikao na kujadili wafanyeje ili wampate mwenzao atakayekwenda mbugani kuwinda mnyama ili aokoe njaa yao.
Na Jemedari wao, baada ya kutafakari, amewateulia mwenzao anayedhaniwa kuwa makini na mahiri kwa uwindaji. Mwenye uwezo wa kulenga shabaha, na hivyo, kuitumia vema risasi hiyo moja iliyobaki kwenye kumlenga nyati na kumwangusha. Kwamba abebe gobore lenye risasi moja, na aingie nalo msituni kuifanya kazi hiyo.
Aliyekwenda mbugani nyuma amewaacha wengi wenye matumaini ya kuusikia mlio wa gobore utakaoshiria mnyama mkubwa ameangushwa mbugani.
Na hakuna habari mbaya, kama wanakijiji wale watakapousikia mlio huo na kukimbilia mbugani kujionea. Na huko wamkute mwenzao ameitumia risasi ile ya mwisho kwa kumlenga na kumwangusha nyani badala ya nyati waliyemtarajia!
Na kwa mila za wanakijiji wale, nyani haliwi,na ni mwiko.
Na Bunge la Katiba lijione kuwa lina fursa adhimu ya kutimiza ndoto ya Watanzania ya kupata Katiba Bora yenye kukidhi mahitaji ya sasa na hata miaka mia moja ijayo.
Kwa Wabunge wa Bunge la Katiba kwenda Dodoma na kurudi na nyani badala ya nyati, sio tu kutawakatisha tamaa Watanzania, bali, kutawafanya Watanzania wawadharau Wabunge hao na hata kuhoji uzalendo wao kwa nchi yao waliyozaliwa.
Ni Neno Fupi La Leo.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)

Wednesday, February 26, 2014

MWILI WA BALOZI FULGENCE KAZAURA WAAGWA LEO


Jeneza lenye Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marehemu Balozi Fulgence Kazaura likiwa ndani ya Kanisa la Mt. Peter,Osterbay jijini Dar es Salaam tayari kwa Ibada maalum ya kumuombea Marehemu huyo iliyofanyika mchana wa leo kanisani hapo.Picha zote na Othman Michuzi.Viongozi wa Kanisa hilo la Mt. Peter wakiwaongoza waomboleazaji kuaga Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marehemu Balozi Fulgence Kazaura aliefariki Dunia juzi huko nchini India alikokwenda kwa ajili ya Matibabu.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu,Mh. Benjamin Mkapa akiwaongoza waomboleazaji mbali mbali kutoa heshima za mwisho wakati wa kuaga Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marehemu Balozi Fulgence Kazaura aliefariki Dunia juzi huko nchini India alikokwenda kwa ajili ya Matibabu.Ibada hii ya kuaga mwili wa Balozi Kazaura imefanyika mchana wa leo katika Kanisa la Mt. Peter,Osterbay jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mstaafu,Jaji Joseph Warioba akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marehemu Balozi Fulgence Kazaura aliefariki Dunia juzi huko nchini India alikokwenda kwa ajili ya Matibabu.Ibada hii ya kuaga mwili wa Balozi Kazaura imefanyika mchana wa leo katika Kanisa la Mt. Peter,Osterbay jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Prof. Rwekaza Mkandala (mbele) Sir George Kahama,pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,Mzee Phillip Mangula wakitoa heshima zao za Mwisho kwa Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marehemu Balozi Fulgence Kazaura aliefariki Dunia juzi huko nchini India alikokwenda kwa ajili ya Matibabu.Ibada hii ya kuaga mwili wa Balozi Kazaura imefanyika mchana wa leo katika Kanisa la Mt. Peter,Osterbay jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu,Mh. Benjamin Mkapa akimfariji Mjane wa Marehemu pamoja na watoto wakati wa Ibada maalum ya kuaga Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marehemu Balozi Fulgence Kazaura,iliyofanyika kwenye kanisa la Mt. Peter,Osterbay jijini Dar es Salaam leo.
Waziri Mkuu Mstaafu,Jaji Joseph Warioba akiifariji familia ya Marehemu Balozi Fulgence Kazaura.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,Mzee Phillip Mangula akiifariji familia ya Marehemu Balozi Fulgence Kazaura.
Familia ya Marehemu Balozi Fulgence Kazaura ikiwa kanisani hapo sambamba na waombelezaji wengine mbali mbali.
Watoto wa Marehemu Balozi Fulgence Kazaura wakizungumza jambo,pamoja na Mama yao (katikati).
Mtoto Mkubwa wa Marehemu Balozi Fulgence Kazaura,Kamugisha Kazaura akisoma risala fupi ya baba yake wakati wa Ibada Maalum ya kutoa heshima za mwisho,iliyofanyika mchana wa leo kwenye Kanisa la Mt. Peter,Osterbay jijini Dar es Salaam.
Mzee Samuel Tassa ambaye alikuwa ni mtu wa karibu la Marehemu Balozi Fulgence Kazaura,akimzungumzia namna walivyoweza kuishi pamoja katika kipindi chote cha Uhai wake.
Muwakilishi wa Mabalozi wastaafu nchini,Balozi Anthony Nyaki akitoa ujumbe wa Mabalozi wenzake namna walivyoguswa na msiba huo wa Mwenzao,Marehemu Balozi Fulgence Kazaura.
Ibada ikiendelea kanisani hapo.
Mh. Mkapa akilishwa Mkate wa Bwana.
Prof. Mkandala akilishwa Mkate wa Bwana.
Sir George Kahama.
 
source:mjengwa blog

Tuesday, February 25, 2014

Marekani kupitia upya uhusiano wake na Uganda

Uganda_Gays_Leff_16b7f.jpg
 
Na Fadhy Mtanga SERIKALI ya Marekani imeanza mchakato wa kuupitia upya uhusiano wake na Uganda, taifa la Afrika Mashariki baada ya rais wa nchi hiyo kutia saini mswada unaoharamisha vitendo vyote vya kishoga nchini humo.  Hapo jana, jijini Entebbe, rais wa Uganda aliweka saini katika msaada huo ili kuwa sheria rasmi ya Uganda.  Kitendo hicho kimelalamikiwa sana na mataifa ya Marekani na Uingereza kwa madai kinakiuka haki za kibinadamu.
 Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa taarifa kupitia kwa waziri wake, John Kerry ikieleza kuwa serikali ya rais Barack Obama itahakikisha uhusiano wake na Uganda unazingatia sera yake ya kuzuia unyanyasaji wa aina yoyote.
 Katika taarifa hiyo iliyotumwa kwa barua-pepe kwenda kwenye gazeti la Daily Nation la Kenya, Kerry amesema, "Kwa kuwa sasa hii sheria imekwishapitishwa, tunaanza mchakato wa ndani kuhusiana na uhusiano wetu na Serikali ya Uganda ili kuhakikisha namna zote za mahusiano yetu, ikijumuisha misaada ya kimaendeleo zinaakisi dhima yetu ya kuondoa unyanyasaji na ubaguzi."
 Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Marekani amepigia chapuo kufutwa kwa sheria hiyo.  "Hii ni siku ya msiba mkubwa kwa Uganda na wote wanaojali kuhusu haki za kibindamu.  Kimsingi, suluhisho pekee ni kufutwa kwa sheria hii."
 Kuwekwa sahihi kwa sheria hiyo kumewagutua Marekani, Uingereza na jumuiya zingine zinazopigia debe mashoga kupewa haki.  Tayari rais Barack Obama ametoa taarifa kupitia kwa katibu wake kuwa, "rais wa Uganda amefanya kitendo kichachostahili kujutiwa kwa kuwa ameirudisha nchi yake nyuma badala ya kusimamia uhuru na haki sawa kwa watu wake."
 Kerry, katika taarifa yake ameeleza wazi kuwa Marekani imekuwa ikiupinga mswada huo toka ulipofahamika miaka minne iliyopita.  Ameeleza zaidi kuwa sheria hiyo inakinzana na uwepo wa Tume ya Haki za Binadamu ambayo ipo kwa mujibu wa katiba ya Uganda.
 "Kutoka Nigeria hadi Russia na Uganda, tunafanya kazi ulimwengu mzima kuhamasisha na kulinda haki za kibidamu kwa watu wote.  Marekani itaendelea kusimama imara dhidi ya jitihada zozote kuwatenga, kuwaharamisha na kuwaadhibu wahanga wowote wake katika jamii yoyote ile."  Alisema Kerry.
 Kitendo hicho cha Museveni kimeibua hisia kali kutoka kwa baadhi ya taasisi za kimataifa ikiwemo makao makuu Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.  Tayari Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameeleza azma yake ya kulijadili jambo hilo la kupinga ushoga pindi atakapokutana na balozi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa
source: mjengwa blog

Anayeona posho haimtoshi afungashe virago’

bunge_4f64b.jpg
Dodoma. Wizara ya Fedha imepigilia msumari maombi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kutaka waongezewe posho na kusema anayeona ameacha kazi inayomlipa zaidi kwenda bungeni afungashe virago na kuondoka.
Msimamo huo umekuja siku moja tu baada ya gazeti hili kudokeza kuwa madai ya wajumbe wa bunge hilo kutaka waongezewe posho kutoka Sh300,000 za sasa kwa siku, yamegonga mwamba baada ya kamati iliyoteuliwa kuchunguza uhalali wake kusema kiwango hicho kinatosha.
Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Kificho alisema jana bila kutaja viwango, kuwa ripoti ya kamati hiyo imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi.
Madai ya wajumbe kutaka waongezewe posho, yamechafua hali ya hewa ndani na nje ya Bunge, huku baadhi ya wananchi wakipaza sauti zao na kumsihi Rais Kikwete alivunje bunge hilo iwapo wajumbe watashikilia msimamo wa kutaka nyongeza ya posho.
Jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema wanaoshiriki kutunga Katiba ni Watanzania na siyo wataalamu washauri waliokodiwa kutoka nje.
Alisema kwa msingi huo, Serikali ilitarajia kuwaona watu hao wakitanguliza uzalendo zaidi badala ya kudai malipo manono.
"Katika kutengeneza Katiba hii, hatujakodi consultants (wataalamu washauri) kutoka Uingereza, Marekani, Kenya, Uganda wala nchi nyingine yoyote... Hawa ni Watanzania na kazi wanayoifanya ni yao," alisema.
"Wangekuwa wataalamu wa kukodi wangeweza kudai malipo hayo, lakini hapa ni tofauti... wanafanya kazi yao na kila mtu anafanya kazi yake na anapaswa kujivunia kushiriki katika tendo hili la kihistoria kwa kutanguliza uzalendo," alisema.
Nchemba alisema anazielewa hoja za baadhi ya wajumbe walioibua suala la posho, lakini kwa mtazamo wake, hoja hiyo hata kama ingekuwa na mashiko kiasi gani, imewasilishwa wakati usiokuwa mwafaka. Alisema wapo makandarasi na wazabuni waliotoa huduma kwenye taasisi mbalimbali za umma lakini hawajalipwa.
Alisema kwa kawaida, Februari ni mwezi mbaya kwa kuwa baadhi ya wilaya zina historia ya kukumbwa na uhaba wa chakula hivyo kuhitaji fedha nyingi za Serikali ili kuokoa maisha ya watu katika maeneo hayo.
Pia alisema si wakati mwafaka wa kudai nyongeza hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna walimu wapya 30,000 nchini kote ambao hawajapangiwa vituo kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa stahiki zao.
Nchemba alisema mbali na walimu hao wapya kutokupangiwa vituo, walimu wengine wanadai malimbikizo ya fedha zao na kwamba hawajalipwa kutokana na ufinyu wa bajeti serikalini.
"Siku zote ukweli unauma. Nasema kama kuna mjumbe ambaye anaona huko alikokuwa kabla ya kuteuliwa alikuwa anapata pesa zaidi kuliko hii, basi kwa heshima afungashe virago na kuondoka," alisema.
Aibu kwa mjumbe
Akizungumzia suala hilo la posho, Mjumbe wa Bunge hilo, David Kafulila (picha ndogo chini) alisema ni aibu kwa wajumbe ambao wameaminiwa na Watanzania na kupewa jukumu zito la kutunga Katiba, kuanza kujadili nyongeza ya posho.
"Ninachokiona ni tatizo la standard (viwango) vya posho... hakuna standard kwamba posho ilipweje, kwa nani na kwa kiasi gani. Mtu akidai leo kwamba Sh300,000 ni ndogo tunajiuliza ni kwa standard ipi?" alihoji.
Kamati ya Posho
Kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kushughulikia madai ya nyongeza hizo, zinasema imeshauri kuwa kiwango kinacholipwa sasa kinatosha.
Kamati hiyo inaundwa na William Lukuvi, Mohamed Abood Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari na taarifa yake imekwishakabidhiwa kwa Kificho.
Mmoja wa makatibu wa bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alikaririwa juzi akisema suala la posho limetoka mikononi mwa Kificho na mapendekezo yake yameshapelekwa serikalini.
Hoja ya kutaka nyongeza ya posho iliibuliwa na wajumbe wawili ambao pia ni wabunge wa CCM, Richard Ndasa (Sumve) na Suleiman Nchambi (Kishapu).

CHANZO: MWANANCHI

Monday, February 24, 2014

museveni atia sahihi muswada wa sheria ya mapenzi ya jinsia moja

yoweri-museveni-007 33b7d
Hatimae Rais wa Uganda YOWER KAGUTA MUSEVEN mapema leo mchana ametia sain muswada wa sheria ya mapenzi na ndoa za jinsia moja, ambapo sasa raia wa uganda atakae patikana na kosa hilo atatahukumiwa kifungo cha maisha jela. Museveni amesisistiza kwamba ametia sain muswada huo kwa kuzingatia kwamba suala ushoga na usagaji   si udhaifu wa kimaumbile wakuzaliwa nao  bali ni tabia ya kujifunza.(Hudugu)

source: mjengwa blog

Kuhusu Milipuko Ya Mabomu Zanzibar...

Mji wa kitalii wa Zanzibar wa Stone Town ambako raia wawili wa Uingereza wamemwagiwa tindi kali
Ndugu zangu,
Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko habari juu ya matukio ya milipuko ya mabomu mawili ya kutengenezwa nyumbani; moja jirani na kanisa na lingine kwenye mgahawa ambao pia ni maarufu kwa watalii wa kigeni. Hakuna aliyepoteza maisha.
Naungana na ndugu zetu wa Zanzibar kulaani vitendo hivi vya kishenzi na vyenye kutishia uhai wa raia wema na wasio na hatia.
Na hakika, habari hizi hazitoi taswira njema ya Zanzibar na nchi yetu kimataifa. Tayari habari za tukio la mabomu limesharipotiwa kwenye vyombo vya habari kimataifa, http://www.dn.se/nyheter/varlden/bomber-exploderade-pa-zanzibar/,hivyo basi, ni athari mbaya ya moja kwa moja kwa biashara ya utalii ambayo pia ni moja ya mihimili ya uchumi wa Zanzibar.
Ni matumaini yetu, kuwa wahusika na ulipuaji wa mabomu hayo watasakwa popote walipo na kutiwa nguvuni.
Maggid,
Iringa.(P.T)

Sunday, February 23, 2014

Warioba ampa somo Werema

Jaji Warioba 

Dodoma. Siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kusema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wanaweza kubadili chochote, isipokuwa tunu za Taifa, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ameonya kuwa jambo hilo linapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa.
Jaji Warioba alipingana na kauli hiyo ya Jaji Werema na kusisitiza kuwa Katiba ni mali ya wananchi, hivyo mawazo na mapendekezo  yaliyokusanywa na tume yake kupitia Mabaraza ya Katiba “yanapaswa kuheshimiwa”.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo alipotakiwa na gazeti hili kufafanua kile kinachoonekana kama mkanganyiko wa kauli za viongozi hao wakuu kuhusu majukumu ya Bunge la Mabadiliko ya Katiba.
“Katika hili mimi ndiyo msemaji wa mwisho. Kwenye mchakato huu, sisi sote ni washauri  tu, someni vizuri sheria mtajua. Tangu mwanzo, wananchi  ndio waliotoa maoni yao, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikayakusanya na kutengeneza rasimu ya kwanza,” alisema Jaji Warioba na kuendelea: “Baadaye tukairudisha rasimu hiyo kwa wananchi wenyewe, baada ya kuiboresha kupitia mabaraza ya katiba ya wilaya. Wakaibadili wenyewe, kuridhia na hatimaye tukapata Rasimu ya Pili ya Katiba. Hivyo hata hii rasimu itakayojadiliwa bungeni, bado ni mali ya wananchi.”
Jaji Warioba alisema tofauti na nchi nyingine ambako Bunge la Katiba linaruhusiwa kufanya mabadiliko kwenye rasimu, utaratibu tuliouchukua hapa nchini, ni Bunge hilo kuliondolea mamlaka hayo.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba wenzetu Bunge lao linakuwa na uwakilishi wa wananchi  waliochaguliwa kwa ajili ya katiba tu. Kwa maana hiyo ni wananchi wenyewe. Lakini sisi  kwenye Bunge letu tumechanganya wajumbe wa Katiba na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao kimsingi, hawakuchaguliwa kwa kazi hiyo,” alisema. Aliongeza: “Kwa utaratibu huu wa kwetu, wananchi wana mamlaka zaidi juu ya Katiba yao kuliko Bunge. Bunge na sisi wengine wote tunashauri tu, ndiyo maana hata Tume ilipotengeneza rasimu ya kwanza, ilibidi iirudishe tena kwa wananchi.
Jaji Warioba alienda mbali zaidi na kufafanua kazi ya Bunge hilo kuwa ni kuboresha Katiba.
“Ukiangalia kwa undani, huwezi kuboresha bila kubadili, ila unaboresha kwa kiwango gani na mamlaka yako ya kuboresha yainaishia wapi. Ndiyo maana sisi kwenye Tume tulipoboresha maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, tukairudisha kwa wananchi,” alisema.
Alisema kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kuiboresha rasimu hiyo kwa kutoa ushauri na maoni yake ambayo hata hivyo si lazima yakubalike na wananachi ambao ndio wenye Katiba yao.
Alichosema Werema
Akijibu maswali ya wajumbe wa Bunge Maalumu juzi, Jaji Werema alisema Bunge Maalumu linaweza kubadili vifungu mbalimbali vilivyomo katika Rasimu ya Katiba, isipokuwa vilivyotajwa katika kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kama kazi ya Bunge hilo ingekuwa kufanyiwa maboresho kwa vifungu vya rasimu hiyo tu, kusingekuwa na maana ya kuwepo kwake.
“Kwanza idadi ya watu waliotoa maoni ya Katiba Mpya ni Ndogo ikilinganishwa na idadi ya wananchi wote wa nchi hii. Bunge hili halipitishi Katiba na ndiyo maana kuna hatua nyingine ya wananchi kupiga kura. Kama itaonekana kuna kitu kinafaa na kinaweza kuingizwa na kukubalika ni sawa,” alisema na kuongeza:
“Nyinyi kama mngekuwa mnafanya maboresho tu au ukarabati sidhani kama kungekuwa na umuhimu wa kuwa na Bunge hili.” Alisema hata mawazo mazuri ambayo yapo katika nyaraka za makundi mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa yanaweza kujadiliwa katika Bunge hilo.
“Kisichotakiwa ni nyaraka hizo kutoingizwa humu bungeni. Rasimu inayojulikana na kukubalika ni hii iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tu,” alisema.
Mambo yaliyomo katika kifungu hicho ambayo hayatakiwi kubadilishwa ni uwepo wa Jamhuri ya Muungano, uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama, mfumo wa kiutawala na kijamhuri na uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mengine ni umoja wa kitaifa, amani na utulivu, uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalumu, ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu, utu usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria na uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.
“Fanyeni vyote lakini katika kifungu cha tisa hamtaruhusiwa kubadili chochote labda muongeze tu baadhi ya mambo lakini siyo kupunguza,” alisema Werema.

source:mwananchi

Vita ya uenyekiti Bunge la Katiba

Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa kutaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa Bunge la Katiba wakipeana mikono siku za hivi karibuni. 


Dodoma. Kadiri siku zinavyosogelea uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, ndivyo mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unavyozidi, kutokana na kuwapo kwa makundi mawili yanayojipanga kusimamisha wagombea na ambayo yameanza kuendesha kampeni kuchafuana.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa makundi hayo ni yale yanayomsaidia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa kutaka kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, wakati Chenge akiwa hayuko tayari kuthibitisha nia yake hiyo, Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo. Lakini habari zinasema vigogo hao wameshajipanga kwa ajili ya mbio hizo za uchaguzi na sasa wanatafuta watu wa kuwasaidia.
Makundi hayo yalianza wakati wa kikao cha ndani cha CCM kilichofanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, ambako habari zilisema, baada ya chama kumteua Pandu Ameir Kificho kuwania nafasi ya mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho walimpendekeza Chenge kuwa mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo.
“Hapo ndipo mgogoro ulipoanza. Kwanza tulimkubali Kificho ili kupunguza wingu la ushindani kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu. Lakini wajumbe tulimkataa Chenge kwa hoja nzito na mwenyekiti alikubali na kuamua kuwa watu wakagombee bungeni.”
Tuhuma dhidi ya Chenge
Baadhi ya wabunge wa CCM wamesema ni ukweli ulio wazi kwamba Sitta na Chenge ndio wanaofaa kuwania nafasi hiyo, lakini mchuano utakuwa mkali kutokana na kila mmoja kuwa na ushawishi wa aina yake kwa wajumbe ambao ndio watakaopiga kura kumchagua mwenyekiti.
 “Wakati wa kuapa, wajumbe watatakiwa kushika Biblia au Qur’an. Ila tusema ukweli, unawezaje kufanya kiapo cha utii mbele ya mwenyekiti ambaye uadilifu wake unatia shaka? Alihoji mmoja wa wajumbe wanaomuungano mkono Sitta.
Mjumbe mwingine alisema Chenge hazuiwi kugombea, lakini ajiandae kujibu maswali makuu matatu, moja likihoji uadilifu wake wakati kuna mikataba mingi ya wawekezaji kwenye kampuni za madini iliyoshuhudiwa na yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni mibovu.
“Pia tutamtaka aeleze kwa nini alikubali Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri kwa uteuzi wa Spika, wakati kanuni zinasema wenyeviti wachaguliwe na wabunge wenyewe,” alisema mjumbe huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Kauli ya Chenge
Chenge mwenyewe amepuuza tuhuma hizo akisema kuwa ni za watu wasiopenda kuelewa.
“Hayo yote na mengi zaidi nimeyasikia ndiyo maana nimeamua kuondoka Dodoma. Siko Dodoma nitarudi Jumatatu,” alisema Chenge na kuendelea;
“Lakini ndugu yangu, mi naona hakuna haja ya kulumbana na watu ambao hawataki kuelewa. Kama watu wanatuhumu, lakini hawana kielelezo cha kwenda nacho mahakamani, wanaambiwa kwa ushahidi kuwa tuhuma zao hazina msingi na hawataki kusikia, unadhani tutawafanyaje zaidi ya kuwaacha tu?”
Alipotakiwa kuthibitisha kuwa kweli ana mpango wa kugombea nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alijibu;
“Chama kina utaratibu wake na mipango yake. Ni taasisi inayopaswa kuheshimiwa, kwa nini tulumbane leo wakati chenyewe kina msimamo wake juu ya hilo?”
Alipoulizwa tena kueleza namna anavyojiandaa kujibu maswali matatu magumu yanayoandaliwa na wapinzani wake, endapo atasimama kunadi sera zake akitakiwa kugombea nafasi hiyo alijibu;
“…Bwana! Chenge ni huyo huyo, chaguzi ni hizo hizo ambazo ameshinda mara kadhaa na nchi hii ni yetu sote.”
Sitta
Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, lakini mmoja wa wanaomuunga mkono ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema hawana shaka kwamba akisimama na Chenge kwa kura za haki, atapita.
Tayari kumeripotiwa taarifa za rushwa kwenye mbio hizo za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameonya vitendo hivyo na kuzitaka jumuiya za CCM kuwa macho dhidi ya suala hilo.
Pinda alitoa karipio hilo jana alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi mjini Dodoma.
Alisema viongozi wanaopatikana kwa njia ya rushwa siyo viongozi bora na kuhoji, “Hivi mtu anayetumia fedha kuingia madarakani akipata madaraka fedha hizo atazirudishaje?”
Pinda ametaka jumuiya hiyo kuwa mstari wa mbele kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndani ya chama kwa misingi ya maadili, kwani wanaomwaga fedha ili kupata uongozi ndani ya chama wanawavuruga na hiyo siyo njia ya kukijenga chama.
Pinda aliwaasa wanachama wa CCM waache kupanga nani agombee na nani asigombee na kufafanua kuwa hali hiyo hujenga makundi ndani ya chama hicho.
“Tunahitaji kupata viongozi kwa kuzingatia umoja wetu na mshikamano miongoni mwa wanachama. CCM ikiwa imara itaunda Serikali imara. Chama kikiwa dhaifu ni wazi kuwa hata Serikali yake nayo itakuwa dhaifu,” alisema.

source: mwananchi