WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, April 29, 2012


Neno Fupi La Usiku Huu: Mauaji Ya Usa River Na Kisa Cha Mtego Wa Panya 


Ndugu zangu, 

Kuna kisa cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya.
Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya uliowekwa uvunguni  mwa kitanda na mwenye nyumba.

Panya yule akamwendea jogoo  wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa  uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote".

Jogoo akajibu; " Ondoka zako, mie mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda!"

Panya yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua kabla haujatudhuru sote".

Mbuzi akajibu; " Hivi tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya haunihusu mie mbuzi".

Panya akaenda hadi kwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe ng'ombe wa bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara"

Ngombe akajibu akionyesha mshangao; 
" Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu."

Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba. Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda,  mkia wa nyoka ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika

Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa. Hapana, ni nyoka aliyenaswa mkia. Na ni mwenye hasira pia. Akamng'ata mguu mwenye nyumba. Sumu kali akamwachia. Mwenye nyumba akafa.

Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu walikuwa wachache. Wakahitaji kitoweo . Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba  achinjwe.

Siku ya pili watu wakaongezeka. Kilihitajika kitoweo pia. Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba ili achinjwe.

Na siku ya maziko watu wakawa wengi  zaidi. Akakamatwa  ng'ombe wa mwenye nyumba ili achinjwe.

Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya  yasingewahusu wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya!


Naam, Watanzania tunazidi kupokea habari mbaya za matukio ya mauaji ya kutisha. Vuguvugu la mapambano ya kisiasa linasemwa kuwa ni moja ya sababu za matukio ya mauaji na hata watu kujeruhiwa kwa mapanga. 

Na vuguvugu la mapambano ya kisiasa halipawi kuandamama na vitendo vya mauaji au kujeruhiana kwa mapanga, bali, liwe ni vuguvugu la mapambano ya hoja.

Kule Nyamagana tumeshuhudia wabunge wamepigwa mapanga. Na jana  kiongozi wa Chadema pale Usa River amechinjwa kama  kuku.

Inasikitisha sana kuona vitendo hivi vya kinyama vinazidi kuongezeka.  Inasikitisha pia kuwa polisi wanashindwa kwa haraka kuwatia nguvuni wahusika wa mauaji na kuwafikisha mahakamani.  Labda idara za upelelezi wa kipolisi zinahitaji kuimarishwa zaidi.

Na huu ni wakati, kwa Watanzania, bila kujali tofauti zetu za  kiitikadi, kidini au rangi, tukemee kwa sauti moja vitendo hivi viovu.  Kamwe tusikubali ikawa ni vitu vya kawaida.

Ni wakati  sasa kwa wananchi wakiongozwa na viongozi waandamizi wa vyama vya siasa. Viongozi wa kidini na  wanaharakati wa haki za kibinadamu, kusimama kwa pamoja, na kwa kauli na vitendo,  kulaaani  maovu haya na mengineyo yenye hata kupelekea roho za wanadamu wenzetu kutoweka.

Hakika, kama mtego ule wa panya, tutafanya makosa makubwa kama kuna watakaodhani,  kuwa haya ya watu kuchinjwa na kujeruhiwa na mapanga yatawakuta watu wa kundi fulani tu. Tukiacha yaendelee, basi, yeyote yule, bila kujali dini, rangi,  itikadi au hata wadhifa wake, anaweza kuwa mhanga wa maovu haya. Kama taifa,  kwa pamoja tuwalaani wauaji hawa.

Na hilo ni Neno Fupi la Usiku Huu.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
Habari kwa hisani ya mjengwa blog

Saturday, April 28, 2012

UADILIFU NA UWAJIBIKAJI NI SILAHA PEKEE YA AMANI YETU



Kikwazo kukubwa sana cha uadilifu na uwajibikaji ni matumizi mabaya ya ofisi kwa masilahi ambayo hayagusi maisha ya wananchi, rushwa na matumizi mabaya ya pesa ni miongoni mwa malalamiko makubwa katika hoja hii.



Rushwa ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili dunia nzima kwa ujumla. Mataifa mengi yamekuwa yakipambana na tatizo la rushwa ingawa nchi zinatofautiana katika viwango vya rushwa. Tatizo la rushwa linaigusa jamii katika viwango tofauti na katika mazingira tofauti. Rushwa na matumizi mabaya ya ofisi yako katika viwango vyote vya maisha ya binadamu. Kwa sasa taifa letu linaangalia sana rushwa katika ngazi ya viongozi wakubwa na waandamizi wa serikali ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanaoongoza na kutegemewa sana kwa kuwaletea wananchi maisha bora.

Serikali ya Tanzania  imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kupambana na hali hii mara baada ya Uhuru mwaka 1961 ni:- Mwaka 1966 Serikali iliunda Tume ya Kudumu ya Uchunguzi ikiwa na lengo la kuhakikisha viongozi wa Serikali hawatumii vibaya madaraka waliyokabidhiwa na umma kwa manufaa yao binafsi. Mwaka 1971, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16/1971. Kutungwa kwa sheria hii kulifuatiwa na kuundwa kwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa mwaka 1975, ili kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya rushwa, Bunge iliifanyia marekebisho Sheria ya Kuzuia Rushwa Na. 16 ya 1971, mwaka 1991 ikaundwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa kwa lengo la kuzuia vitendo vya rushwa. Mwaka 2007 baada ya kutungwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007 na kufutwa Sheria ya Kuzuia Rushwa Na. 16/1971 jina la taasisi lilibadilika na kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Hivyo TAKUKURU ilianzishwa rasmi Julai, 2007 na kurithi kazi zilizokuwa zinafanywa na chombo hiki kwa majina ya awali.”




Pamoja na upango huu mzuri wa serikali katika maandishi na katika kimantiki tatizo liko wapi kwa vilio vya wananchi kuhusu matumizi mabaya ya ofisi za viongozi wetu waandamizi? Je mazingira haya mazuri ya sheria ya kumlinda mwananchi na mali zake ni sawa na uamuzi ambao hauna usiammiaji mzuri?

Je tatizo ni serikali au usimamiaji wa sheria husika? 

Je ofisi husika hazina meno ya kutosha kutenda kazi?

Au ni tatizo la kulindana sana kwa masilahi binafsi?

Tatizo ni watu  au mfumo uliopo ambao unatoa fursa kwa viongozi na watendaji kuwajibika kwa waliowateua


Watanzania wengi leo hii wanajiuliza hivi taifa hili sasa linao viongozi wanaojua wanatakiwa kufanya nini?

Au vyeo ambavyo watu wanavyo wamepeana tu kwa “ MUHALI” na kwa msingi huu haiwasumbui nini kinachoendelea  hivyo hawawajibiki  kwenye nafasi katika kuwasaidia Watanzania.

Hoja na matukio ya kujikanganya kutoka watendaji serikali waandamizi mawaziri na manaibu mawaziri pamoja na repoti ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali  kama waandishi wengine walivyowahi andika na kuelezea huko nyuma linalifikisha taifa katika ombwe la uongozi.

Ukiwa na chombo baharini kinapita katika dhoruba kali, halafu nahodha na mabaharia wanajshughulisha na mambo mengine lile la hatari lililoko mbele yao hawalijali, chombo hicho ni lazima kiseree na kupotelea majini”.


Viongozi wetu wanapaswa kujifunza  katika nchi za wenzetu kasoro zinapojitokeza katika wizara yako kama tuhuma hizo ni za kweli au la wajibika kwanza kupisha uchunguzi huru wa tuhuma hizo kwa vile wewe mwenyewe umeshindwa kuwajibika na umekaribisha zengwe hivyo wajibika.

Uwajibikaji wa viongozi wetu ni tatizo nakumbua Raisi Mstaafu Mkapa aliwahi waita mawaziri ni sawa na "askari wa miavuli"; siamini mawaziri wetu ni askari wa miavuli hawaziwezi dhoruma za angani pengine hawana ustadi wa kuruka kwa kutumia miavuli wao; askari wa miavuli lazima ajue utaratibu mzima wa kutumia huo mwavuli ukikosea tu unakupeleka ndiko siko wengi wnaishia huko.

Nafikiri zile kongamano ambazo serikali imekuwa ikiwafanyia kuwanoa ubongo hazijawa effective kwa mawaziri wote kwani wengi wanalalamikiwa kwa utendaji wa uwajibikaji wa chini ya kiwango.

Kipimo kimoja kikubwa cha uongozi bora ni uwezo wa kusimamia rasilimali za wananchi, uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na kumcha Mungu; kiongozi akiwa na vitu hivi huzaa hekima ua uwajibikaji wa kweli na uzalendo wa kupenda nchi yako na kusimamia rasilimali zake kwa faida ya Taifa.
Inaoneka kuwa  baadhi ya viongozi wetu kutumia nguvu zao  sio kuondoa umasikini bali kuongeza umasikini kwa mtanzania wa kawaida.

Kweli naamini madaraka matamu, watu wanayatafuta kwa gharama pengine ili kukizi masilahi binafsi, ndio yanafuata masilahi ya taifa.

Amani yetu ambayo tunamshukuru Mungu kwa zawadi hii pekee kwa ambayo watanzania wamejaliwa kwa misingi mizuri ya waasisi wetu Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Maheremu Mzee wetu Abeid Aman Karume kwa uadilifu wao na mapenzi yao kwa taifa la Tanzania, tusipikuwa makini tuaipoteza kutoka na baadhi ya viongozi wa sasa ambao wanatumia vyeo na madaraka kwa masilahi binafsi ambayo inajenga chuki miongoni mwa wananchi.


Changamoto ya amani yetu ni kwa watendaji wote wa serikali hasa 
watendaji waandamizi kuwa wakweli ili waweze kusikia  sauti ya wanyonge,  na kupitia rasilimali za taifa wasaidie katika kujenga jamii inayozingatia na kuheshimu haki msingi za binadamu. Kashafa ufisadi, rushwa, uzembe na kutowajibika mesomo hii tuweze kuipunguza katika midomo ya wananchi na katika maandiko yetu. Hilo linawezekana kama viongozi wetu watakuwa wakweli  kulingana na viapo vyao kabla ya kuingia katika ofisi husika. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuondoa ombwe la uongozi.

Monday, April 23, 2012

Tafadhali Usininukuu; Afrika Uwaziri Mkuu Ni Cheo Cha Lawama!





Ndugu zangu, 

Nimepata kusimulia haya. Kuwa Mwalimu Nyerere alipong'atuka alipata kumwelezea rafiki yake  Rashid Kawawa. Alitamka; " Huyu Rashid huyu sidhani kama kuna mtu mwingine anayeweza kufanana naye."

Mwalimu alimmwagia sifa nyingi Rashid Kawawa ikiwemo moja kubwa ya uvumilivu.  Rashid Kawawa, ama maarufu kama ' Simba wa Vita' alipata kuwa Waziri Mkuu wakati wa uongozi wa Mwalimu.

Na Afrika cheo cha Uwaziri Mkuu ni sawa na binadamu kugeuzwa ' Tingatinga', tena lenye mabawa. Kazi ya tingatinga ni kutangulia mbele kusafisha njia.   Waziri Mkuu hutangulia mbele. Atakayofanya Waziri Mkuu, kama  yakiwa mema, basi,  hachelewi kutamka; " Jamani haya yote yanatokana na hekima na busara za Kiongozi Mkuu" - Na Afrika hakuna anachofanya Waziri Mkuu bila Kiongozi Mkuu kujua,  na zaidi,  kutoa baraka zake.

Na mambo yakienda  kombo

Waziri Mkuu anapaswa  kuyakabili madongo na mawe yote yatakayorushwa. Ahakikishe,  kuwa Kiongozi Mkuu haguswi hata na changarawe. Afrika ukiona mawe yanarushwa na yanamgusa Kiongozi Mkuu, basi, ujue kuwa Waziri Mkuu hafanyi kazi yake inavyopaswa iwe. Huyo atakuwa amekalia kuti kavu. Maana, cheo cha Uwaziri Mkuu ni cha kujitoa muhanga au kutolewa kutolewa kafara.  Ndio, punda afe, mzigo wa bwana ufike! Afrika Waziri Mkuu ikibidi kufa na afe ( ajiuzuru) ili mradi kufanya hivyo kutahakikisha Serikali inayoongozwa na Kiongozi Mkuu inabaki hai na salama.  

Hivyo basi, Waziri Mkuu pia ni Mshauri Mkuu kwa Kiongozi Mkuu. Afrika ukiona katika nchi mambo yanaharibika na mpaka Kiongozi Mkuu anaguswa na madongo na mawe yanayorushwa, basi, kuna mawili,  ama, Waziri Mkuu hana ushauri mzuri kwa Kiongozi Mkuu, au Kiongozi Mkuu hashauriki. 

Na ilikuwaje kisa cha  Julius na Rashid?

Hawa walikuwa ni marafiki wawili. Katika vyeo mbali mbali alivyopata kumpa Kawawa, Julius Nyerere alimpa rafiki yake  Rashid cheo cha Uwaziri Mkuu. Si kwa sababu ya urafiki wao, ni kwa sababu Rashid alikuwa hodari na mchapakazi. 

Na kwenye kutekeleza mambo ya Serikali, Rashid alikuwa tingatinga kweli kweli. Watanzania tunakumbuka  alivyosimamia operesheni ya maduka ya ushirika. Kila alipokwenda Rashid alitoa maagizo maduka binafsi yafungwe na yaanzishwe maduka ya ushirika. 

WaTanzania wa vijijini na hata mijini hawakuwa na uzoefu wa biashara ya maduka. Hali ikawa mbaya. Maduka ya ushirika hayakuwa na ufanisi .  Wananchi wakalalamika sana. Aliyekuwa akitupiwa lawama ni Rashid Kawawa kana kwamba ule ulikuwa ni mpango wa Kawawa. Na Julius akapima upepo. Akabaini, kuwa tingatinga lake ( Rashid) limekwama porini.

Nyerere hadharani akaikosoa operesheni ile na hata kuonyesha kumshangaa Rashid. Na akamvua rafiki yake cheo cha Uwaziri Mkuu. Tena akamwita na kumwomba ushauri Rashid wa nani anafikiri anafaa kuchukua nafasi yake.

Mpaka anakufa, Rashid hakuwahi kumlaumu Julius  kwa maagizo yaliyoufanya umma umwite Rashid majina kadhaa ya kejeli ikiwamo moja la gea ya gari  aina ya Landrover. Naam, Afrika Uwaziri Mkuu ni cheo cha lawama. Tafadhali usininukuu!

Habari kwa hisani ya Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

Saturday, April 21, 2012

JE WATANZANIA TUMEKUWA NI WATU WA KUOGOPA MABADILIKO?


Maggig Mjengwa aliwahi andika huko nyuma kuwa “Watanzania leo tumekuwa ni watu wa kulalamika tu hata kwa yale ambayo kimsingi ni wajibu wetu wananchi kuyafanya. Kwa tunavyoenenda, hata aje malaika kutuongoza, bado naye atapatwa na  wakati mgumu”.
Ninapata wakati mgumu sana kutafakari na kuielewa dhana hii, je tumeingiliwa na mdudu wa aina gani katika fikara zetu na katika maisha yetu ya kila siku? Kama ni kweli hii ina maana kuwa tunatawaliwa na maisha ambayo hayana matumaini.
Swali ambalo je woga huu wa mabadiliko ni kwa watanzania wa kawaida tu au hata viongozi wetu? Je ndugu yangu mjengwa alikuwa ameyaongelea mabadiliko gani? Ilinifikirisha zaidi pale aliposema hivi “Tumekuwa kama watu wa taifa la kusadikika ... “Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka… Tumekwisha umwa na nyoka wa  matendo yetu mabaya ya zamani”.

Kumbe woga wetu wa mabadiliko unatokana na kutokujiamini kwetu kwa sababu ya matendo yetu mabaya. Ni matendo gani ambayo yanatupa sisi wananchi wa Tanzania wakati  mgumu wa kuamua kubadilika?
Jambo hili la mabadiliko ya matendo yetu nakubaliana nawe kuwa kwa kweli lazima itamfanya mtu kuogopa mabadiliko kwa kufikiria masilahi binafisi kwani akifanya mabadiliko yanaweza kumweka katika wakati mgumu. Mara nyingi maba

Uadilifu na uaminifu. Kwamba mtu ukiamua kuisimamia “ndiyo”, basi aisimamie bila kutetereka, na akiamua kuisimamia “siyo” vile vile aisimamie bila kuyumba. Na kwamba mtu akiisimamia “ndiyo” ukijua kwamba ni “siyo” ni unafiki na uovu. Vilevile akiisimamia “siyo” ukijua kwamba ni “ndiyo” ni unafiki na uovu!
Mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu daima anakuwa mbali na unafiki na uovu. maana ina msingi chanya wa kuendesha maisha katika jamii yoyote ile.

Jamii fulani na kuishi akizungukwa na historia, utamaduni na desturi za watu wake. Privatusi karugendo aliwahi kuandika katika moja ya makala zake kuwa “Katika familia zetu, katika jamii zetu na katika taifa letu, tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Hatuwezi kujenga familia, jamii na taifa imara bila kuwa mbali na unafiki na uovu. Bila kujenga utamaduni wa “ndiyo” kuwa ni “ndiyo na “siyo”  kuwa ni “siyo”, hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo bila kuizingatia falsafa hii”. Kwa msingi huu kuwa ni kweli kuwa bado tunakazi kubwa kuyakubali mabadiliko kutokana na ualisia wa maisha yetu na jamii inayotuzunguka.



Je woga wa kuogopa mabadiliko unatokana na sisi kama taifa kuwa waoga wa kufikiri? Au ni uvivu wa kusoma na kujua nini kinaendelea ndani ja jamii yetu. Lakini katika hili la kutokukubali mabadiliko linanipa wakati mgumu sana pale ninapoona na kuelewa kuwa hata waandishi wetu wa habari “ media crew” pale wanaposhindwa kuhimili wimbi hili ukizingatia kuwa wao ndio walitakiwa kuwa viongozi wa kuwaelimisha watu kuhusu namna na mbinu za kuyakubali mabadiliko,

Katika siku za karibuni kumekuwa na malalamiko ya wanahabari kuegemea jamii Fulani na kuisaidia iendelee kuogopa mabadiliko; lazima tufike mahali tuweze kuiambia jamii yetu kuwa umesahau kuvaa nguo.Kutokana na jamii inayotuzunguka hakuna mtoto mwenye ujasili ambaye atamwambia mama yake leo “ mama angalia mfalme hajevaa nguo” kwani hata watoto wetu wadogo wameshaambukizwa woga wa kuogoma mbabadiliko;

Tatizo hata wasomi wetu katika hoja zao hata kwenye forum zinaonyesha kuwa  “wakati mwingine” zinaogopa mabadiliko hivyo wataendelea kungangania au kushabikia hoja Fulani za mtu au kikundi Fulani cha watu hata kama mwisho wa siku hazina mwelekeo wa mabadiliko ambayo yatalisaida taifa katika mabadiliko na maendeleo ya jamii.
Kama mwandishi mmoja alivyowahi kuandika kuwa             “jamii imeshatambua kwamba mito,maziwa,bahari,mabwawa,madini, ardhi ni vyanzo vya kuletea maendeleo kwa jamii yao lakini jamii hiyo haitumii rasirimali hizo kujiletea maendeleo, basi tatizo ni udhaifu wa kufikiri uliomo kwenye jamii husika”.



Taifa letu kwa sasa kiuhalisia liko kwenye mtikisiko mkubwa sana kuanzia kwenye maadili ya kijamii hadi kwenye nyanja kuu ya siasa. Mtikisiko huu kwa kiasi kikubwa unasababishwa na kukosekana kwa misingi sahihi ya wapi jamii yetu inaelekea. Pamoja na hilo hata watendaji wetu katika nyadhifa mbalimbali wamekuwa na ufinyu na mwelekeo wa ubinafsi zaidi na utumiaji wa madaraka kwa manufaa binafsi na hawako tayari kuwajibika na kukiri kuwa wamekosea. Daima wanajiona nje ya mzingo wa matatizo haya yanayoikabili jamii yetu,hivyo wanafanya hujuma kwa kudhani wao wako sehemu salama,Lakini hali halisi inaonesha wanajidangaya. Wanasafiria katika chombo kwa nje wao wenyewe wanakiona kuwa ni salama sana lakini wamesahau kuwa “Taifa ni kama chombo cha safari baharini,kikizama hakuna kinachosalia, wakati mwingine hata waogeleaji hodari na mahiri hunaswa na wadudu bahari”.

Taifa letu kwa hivi sasa limekumbwa na tatizo na  viongozi wetu ambao wamepewa dhamana ya kuongoza idara za serikali kwa kushindwa kuishi kulingana na viapo vyao vya kazi na kuishia kuwa ni sehemu ya Ufisadi amboo unatafuna nchi yetu. Katika mjadala huu mkuu na mzito ambao baadhi ya wabunge wamekasirishwa na tabia hizi za hawa watendaji wakuu na kuwataka wajiudhuru, kwa kukiuka maadili ya uongozi “matumizi mbaya ya pesa za walipa kodi” kama mbunge wa Njombe alivyosema Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza na kusikitisha kuwa nchi inatafunwa. Wanaofanya haya ni mawaziri wetu. Nchi inakufa na tuelewe kuwa Tanzania sio mali ya CCM, ni ya Watanzania wote.“Mawaziri wetu wamekuwa mchwa, wanaangamiza nchi na leo nitamtaja waziri anayeongoza kwa kutafuta fedha za Watanzania. Ni Waziri wetu wa Fedha, Mustafa Mkulo. Ameuza viwanja, amelidanganya Bunge baada ya kuivunja CHC,”- Deo Filikunjombe ( CCM)



Hili likifanikiwa tutakuwa tumeanza kuondoa woga wa mabadiliko, kama mawaziri watajitafakari kuwa ni mchwa na wamekosa maadili yamekumbwa na wimbi la rushwa basin a wakaamua kujiuzuru hata kama wataona wanaonewa lakini wakaamua kukaa pembeni ili uchunguzi ufanyiki itakuwa ni dalili njema ya mabadiliko.
Wasipowajibika bunge linataka kumuwajibisha Mtoto wa Mkulima “ waziri Mkuu Mheshimiwa  Pinda atawajibishwa na bunge kama taratibu zitatimia.  

Je kweli tatizo ni Waziri Mkuu? Au Tatizo ni jamii ambayo imetulea? Je tatizo kulipa fadhila baadaya uchaguzi kwa wale waliotoa msaada? Au tatizo na ukosekanaji wa Maadili ya uongozi kwa watendaji wetu? Au tatizo ni viongozi wetu kuto mwanini Mungu hivyo kukosa kabisa ubinadamu? Je tatizo ni umasikini wa viongozi wetu kabla ya kuingia madarakani hatima ya uroho na ulafi wanaishi kuwa mafisadi?

Nini hasa tatizo letu na kuogopa mabadiliko? Chama kingine kikishika madaraka nitafungwa au kunyogwa? Je jibu la maswali haya ni lipi?


Nafikiri ujasiri utatusaidia sisi kuweza kufanya maamuzi sahihi ya mabadiliko; hivyo tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa MKALI katika utendaji wake na kama mheshimiwa Pinda  atapigiwa kura naungana na Maggig Mjengwa kuwa “kupigiwa kura ya wabunge kukosa imani nae ina maana pia kuwa wabunge hawana imani na bwana mkubwa aliyemteua Pinda”.

Friday, April 20, 2012

Zitto Kabwe Na Saini 70 Za Kumg'oa Pinda- Tafsiri Yangu


Ndugu zangu,

Leo asubuhi wakati nikifanya ' jogging' kwenye mitaa ya Dar es Salaam niliwasikia watu wa kawaida kabisa wakijiuliza na kujadili; " inakuwaje Serikali iwalipe marehemu mishahara huku sisi tulio hai hatuna hata uhakika wa milo miwili ya siku?" Wanauliza watu wa mitaani.
 

Naam, nchi yetu imekumbwa na mafuriko ya habari. Kule bungeni Dodoma kuna moto unawaka. Zimeitishwa sanini 70 ili Jumatatu ipigwe kura ya kukosa imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Ndio, kuna wanaotaka Pinda ang'oke, na labda kutolewa kafara, maana, siamini kama tatizo la msingi ni Pinda, bali ni la kimfumo zaidi. Na jana kuna mbunge wa CCM kayasema makali yafuatayo;
 

“Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza na kusikitisha kuwa nchi inatafunwa. Wanaofanya haya ni mawaziri wetu. Nchi inakufa na tuelewe kuwa Tanzania sio mali ya CCM, ni ya Watanzania wote.“Mawaziri wetu wamekuwa mchwa, wanaangamiza nchi na leo nitamtaja waziri anayeongoza kwa kutafuta fedha za Watanzania. Ni Waziri wetu wa Fedha, Mustafa Mkulo. Ameuza viwanja, amelidanganya Bunge baada ya kuivunja CHC,”- Deo Filikunjombe ( CCM) Bungeni jana.
 

Lakini ya jana yalitanguliwa na ya juzi; Mbunge mwanadamizi wa CCM Godfrey Zambi aliyasema makali haya;
 

" CCM inaweza kung'olewa madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2015 endapo kasi ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma itaendelea kama ilivyo sasa"- Godfrey Zambi ( CCM, Mbozi Mashariki).
 

Kauli za wabunge hao wawili wa CCM zinatoa tafsiri ya kilio cha wabunge wa CCM kuomba msaada kwa anayeweza kuwasaidia. Inatoa tafsiri pia kuwa hicho ni kilio cha wabunge wengi wa CCM. Kwamba hayo ndiyo wanayaongea hata chini chini. 


Ndio, wananung'unika na wameanza kuiona adhabu wanayokwenda kuipata kutoka kwa wananchi ifikapo 2015. Wanaona pia, kuwa ' kisungura' hiki kidogo kinachopatikana kila mwaka kinavyoliwa na wajanja na wengine kuachiwa mifupa. 


Wabunge wa CCM na wengine wanaona jinsi baadhi ya mawaziri wa kutoka chama chao wanavyojiangalia wenyewe kwa kujikatia zaidi kasungura hako kadogo na hata minofu mingine kuikimbizia kwenye majimbo yao badala ya kuangalia majimbo mengine pia. Hakika, Wabunge wa CCM sasa wanatoa kilio cha kuomba msaada na kilichochanganyika na hasira na hofu ya kupoteza mamlaka ya kuongoza dola ifikapo mwaka 2015. Ndio, kuna wanaokiona chama chao kikielekea kwenye kuzama 2015. Kelele wanazopiga bungeni zimegeuka kama kelele za nyikani, hazisikiki. Wameanza sasa kuwa na ujasiri wa kuzomeana wazi wazi kwenye vikao vyao badala ya kusubiri kuzomewa na wananchi hadharani. Naam, CCM ya sasa inapata tabu hata kwenye kujua namna ya kuitumia misamiati mipya ya kisiasa, maana, kuna wanaojivua gamba, wanaovuliwa magamba na sasa kuna ' wanaojinyambua' magamba wakiwa ndani ya chama- 'Political evolution' ya namna fulani.
 

Na Mtego wa Zitto Kabwe kwa CCM?
 

Jana Mbunge Zitto Kabwe ameitega CCM. Ni mtego wa hatari. Saini zile 70 zina maana hii;
 
- Kama wabunge wa CCM hawatachangamkia kutia sahihi zao zikavuka hata mia na hamsini, basi, kuna ujumbe unaopelekwa kwa umma. Kuwa wabunge wa CCM ni maneno tu, hawana dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi. Wabunge wengi wa CCM hawataiepuka adhabu ya umma inaweza kuwa inawasubiri 2015.
- Kwa wabunge wa CCM kutia sahihi zao na hata Pinda kupigiwa kura ya wabunge kukosa imani nae ina maana pia kuwa wabunge hawana imani na bwana mkubwa aliyemteua Pinda. Busara haiwataki wabunge wa CCM kufikia hapo. Hilo halina maslahi kwa taifa.

Nini kitakachotokea?
 

Kuna matatu;
 
Mosi, Mawaziri wale watano wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma wanaweza kuepusha aibu kwa Serikali kwa wao wenyewe kutangaza kujiuzulu. Ingawa hili ni gumu kufanyika katika nchi hii, lakini, wakati mwingine kuna lazima ya kufanyika- maana, hapo watakuwa wamemnusuru Waziri Mkuu na aliyemteua.

Pili- Likishindikana la kwanza, basi, kabla ya Jumatatu, Waziri Mkuu Pinda awe ameshajiandaa kufanya maamuzi magumu. Kujiuzulu na kulinda heshima yake na ya aliyemteua. Au kutolewe ' Tamko la Serikali' litakalobadili upepo unaovuma sasa bungeni.
 

Tatu: La kwanza na la pili yaweza yasifanyike, na badala yake. Rais anaweza kuyaona yanayotokea sasa bungeni kama fursa ya kufanya mabadiliko makubwa Serikalini mara akitua Dar kutoka ziara ya Brazil.
 

Naam, yumkini pale Diamond Jubilee, kabla ya Jumatatu, kuna watakaopewa kazi ya kusafisha ukumbi na kupanga viti tayari kwa Mkuu wa Nchi kusema jambo kubwa kwa taifa kupitia kwa ' Wazee wa Darisalama'. 


Na tusubiri tuone


Maggid Mjengwa,
 
0788 111 765

Sunday, April 15, 2012

KUMBUKUMBU YA HAYATI SOKOINE

Siku Nilipomsikia Nyerere Akilitangaza Taifa Kifo Cha Edward Moringe Sokoine




( Pichani juu niliposimama  Wami- Dakawa, Julai 15, 2007)

Ndugu zangu,

KUNA wengi  tunaokumbuka tulikuwa wapi siku ile ya tarehe 12 Aprili, 1984 wakati Mwalimu Nyerere alipolitangazia taifa kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine kilichotokana na ajali ya gari eneo la Wami-Dakawa  akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar.

Kwa bahati mbaya, vijana wengi waliozaliwa baada ya 1984 hawajui sana habari za Edward Moringe Sokoine . Mimi nilikuwa Kidato cha Pili tu pale Sekondari ya Tambaza. Nakumbua ilikuwa majira ya saa kumi jioni.  Nilikuwa natembea kwa miguu kutoka Kinondoni ’ A’ kuelekea nyumbani Kinondoni Biafra. Nilipofika maeneo ya jirani na Msikiti wa Mtambani nikasikia wimbo wa taifa unapigwa.

Nilihisi haraka kuna jambo kubwa la kitaifa limetokea. Nikasogea kwenye duka la jirani. Wapita njia wengine nao walisogea mahali hapo. Wimbo wa Taifa ulipomalizika, nikamsikia Mwalimu akianza kutamka kwa sauti ya huzuni; ” Ndugu Wananchi, leo hii…” Kilichofuata ni historia ambayo hapa nashiriki kuiandika.

Naam, Sokoine alikuwa kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma. Ni Sokoine aliyetufanya hata tuliokuwa sekondari  wakati huo, tuwe na imani na uongozi wa nchi. Tuwe na matumaini ya maisha bora kwa siku za baadae.

Ndio, ukitoka kwa Mwalimu, ni Sokoine pia aliyechangia katika kutufanya watoto wa wakati huo, tuamini na tuipende siasa. Alikuwa mfano wa kuigwa. Alishi kama alivyohubiri. Siyo tu hakujilimbikizia mali, halipunguza hata mali zake ili apate nafasi zaidi ya kututumikia Watanzania.
Itakumbukuwa, kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Aprili, 1984, Sokoine alikabiliana n ahoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu yao. Sokoine alitamka;

”  Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea wabunge posho ya chakula chao, lakini kamwe sitakuwa tayari kuwaongezea mishahara na marupurupu mengine.” Mwisho wa kunukuu. Huyo ndiye Edward Moringe Sokoine.  Alikuwa kiongozi wa kanuni na mwenye msimamo usioyumba.

Sokoine alielewa, kuwa ukiwalinganisha na wananchi walio wengi, wabunge walikuwa na hali bora zaidi kimaisha. Alikuwa tayari kuchukiwa na wabunge kwa kutetea maslahi ya wanyonge, kuliko kupendwa na wabunge kwa kujali zaidi maslahi yao. 

Baada ya kikao kile cha Bunge, Edward Sokoine, badala ya kupanda ndege ya Serikali kumrudisha Dar es Salaam, aliamua kurudi Dar Es Salaam kwa njia ya barabara, afanye hivyo ili mle anamopita apate nafasi ya kuona shughuli za maendeleo zifanywazo na wananchi. Sokoine hakufika Dar Es Salaam, mauti yakamchukua kwa ajali ya gari pale Wami- Dakawa, Morogoro.
Leo tuna viongozi wa wananchi wenye kutanguliza mbele maslahi yao binafsi. Viongozi wasiotosheka na posho ya elfu sabini ya kikao. Viongozi wenye kufikiria tu ’ kamuhogo kao’. Wanafikiri magari na marupurupu yao badala ya masuala yenye kuwahusu  wananchi wa kawaida.

Je, Sokoine angefufuka leo ingekuwaje?
Bila shaka angefufuka na kufa tena ndani ya siku saba. Maana, Sokoine angeshangaa kuwaona wabunge wa leo wakichukua posho  ya kikao cha siku moja sawa na mshahara wa miezi miwili au mitatu kwa Watanzania walio wengi.  

Sokoine angeshangaa kuona wabunge hawatembelei tena Landrover za bei nafuu bali magari ya kifahari huku wananchi walio wengi bado wanaishi kwenye nyumba za udongo na nyasi. Kwamba bado kuna wanyonge wengi wasio na hakika ya kula yao ya leo na kesho huku wananchi wakiambiwa, tena na Spika wa Bunge, kuwa Bunge ni eneo la umasikini!

 Sokoine angeshangaa kusikia kuwa uongozi siku hizi unanunuliwa, na hata yeye akijaribu tena kuingia Bungeni atalazimika agawe ’ Vimuhogo’ kwa watakaompitisha kwenye kura za maoni.  Sokoine angeshangazwa pia kusikia, kuwa kuna mawaziri na watendaji wakuu serikalini wanaokaa mahotelini kwa kukosa nyumba za serikali kwa vile umepitishwa uamuzi wa kuziuza, kisha kujenga nyingine na kuziuza tena! 

Lakini, Sokoine angeshangaa zaidi kuona Watanzania aliowaacha mwaka 1984 wamechelewa sana kuamka na kupambana kuibadili hali iliyopo. 

Naam, Sokoine angefufuka leo, angesononeka sana kuona pengo pana  lililopo kati ya wenye nacho na wasio nacho. Kati ya viongozi na wananchi. 

Edward Moringe Sokoine, Daima Tutakukumbuka.

Maggid Mjengwa,
Iringa
HABARI KWA HISANI YA MJENGWA BLOG

Saturday, April 14, 2012

JAJI MSTAAFU JOSEPH SINDE WORIOBA NA JAHAZI HILI UTALIVUSHA SALAMA?


TUME YA KURATIBU KATIBA MPYA YAAPISHWA RASMI NA MHESHIMIWA Dr. JAKAYA MRISHO KIKWETE.


Safari ya mchakato wa katiba mpya yanazidi kuendelea vizuri, baada ya tume ambayo ilikuwa imetangazwa na Rais wa Jamuhuri ya Tanzania kukamilisha viapo vyao na kukabidhiwa dhana rasmi za kazi zao.

Kama ilivyowekwa bayana na Rais Jakaya Kikwete akiunda Tume ya Katiba ambayo ndiyo itakayoratibu maoni ya wananchi kasha kuyapeleka kwenye Bunge la Katiba.


Wajumbe hao wa tume ya mabadiliko ya Katiba walioapishwa na Rais Kikwete ni pamoja na Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Augustino Ramkadhani pamoja na wajumbe wake ambao ni Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk. Sengodo Mvungi, Richard Lyimo , John Nkolo, Alhaj Said EL- Maamry, Jesca Mkuchu, na Profesa Palamagamba Kabudi. Wengine ni Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kasonda, Al-Shaymaa Kwegyir na Mwantumu Malale pamoja na Joseph Butiku.

Wengine ni Dk.Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulid, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohamed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali, Ally Abdullah Ally Saleh. Pamoja na Katibu wa tume hiyo Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu wake Casmir Sumba Kyuki.


Macho ya watanzania kwa sasa yanaelekezwa kwao, katika kuivusha salama Tanzania katika kulipatia taifa katiba Bora itakoyoweza kudumu kwa kipindi kirefu bila malalamiko, kwa msingi huu naungana na wanahabari wengine walio wahi kuandika kuwa “Sina shaka na Jaji Warioba hasa kutokana na uzoefu wake katika masuala ya sheria na utendaji wake katika tume kama hizo”.
Kama mheshimiwa Rais Kikwete, alivyosema “pamoja na kazi hiyo wamewataka Watanzania kutambua kuwa kazi ya tume hiyo ni kuratibu maoni ya Katiba mpya, na sio ya kujadili kuwepo au kutokuwepo Muungano ila ni mchakato wa kupata katiba bora itakayoendesha Taifa la Tanzania. Itafanya kazi ya kukusanya maoni kuhusu katiba na maslahi ya Wananchi wa pande mbili zinazounda muungano”.

  • “Kuzinduliwa rasmi kwa tume hii ya kuratibu maoni ya kupata katiba mpya ya nchi ni ishara tosha ya Taifa letu kuingilia katika historia iliyotukuka kwa kuanza safari mpya ya kuelekea kuzaliwa kwa Katiba mpya itakayotokana na maoni ya Watanzania wenyewe”.


  • “Mwalimu Julius K. Nyerere, alisema mawazo hayapingwi kwa rungu bali hujibiwa kwa mawazon yaliyobora zaidi. Ni vema mtambue kuhamaki si jibu ila jambo jema ni kutoa mawazo yako yaliyobora zaidi. Kama Watanzania tutaifanya kazi hii kwa moyo tutafanikiwa kupata katiba iliyo bora itakalolilea Taifa letu katika miaka 50 ijayo,”


JUKUMU LA WANANISHI NI LIPI?

  • Kuhakikisha kuwa kila mmoja kwa uwingi wetu tuhakikishe tunatoa maoni kwa faida ya vizazi vyetu;


  • Huu sio wakati wa kununuliwa na wana siasa katika ushawishi usio na faida kwa jamii ya Mtanzania


  • Tuhakikishe kuwa maoni yetu yanasikika na yanatekelezwa Kama tume haitafanikiwa kuwafikia huko mliko msibweteke tafuteni njia mbadala wa kuhakikisha kuwa maoni yenu yanasikia.


KAZI YA TUME  NI IPI

  • Kazi ya tume ni moja tu kufanya kazi hii katika maadili ya kweli bila upendeleo wa chama Fulani cha siasa au kikundi Fulani chenye uwezo au matakwa ya dini Fulani; tume iwatumikie wananchi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


JUKUMU LA VYAMA VYA SIASA

  • Wakati huu wa mchakato wa kuratibu maoni vyama vya siasa vijitahidi kuacha kuwachanganya wananchi kwa kuwachakachua kimawazo ili kuhari au kudhoofisha nia njema ambayo iko ndani ya utaratibu mzima;


  • Vyama vya siasa viwahamasihe wanachama wao katika kujumuika kutoa maoni na kuwaelimisha zaidi umuhimu wa kuchangia katika kutoa maoni.


  • Ni matumaini yangu kuwa tume itaweza kukusanya maoni kwa kwa mapana na kwa uwezo wa hali ya juu kutoka na jinsi tume hiyo ilivyoundwa na umahili na uzoefu wa wajumbe wa tume hiyo.


MUNGU IBARIKI TANZANIA NA IWEZESHE KUPATA KATIBA BORA KWA MAENDELEO YA WANANCHI WAKE