WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, April 29, 2013

UFUNGUZI WA KIKAO CHA KUMI NA MOJA CHA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI KATIKA PICHA

 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Rais Mpya wa Kenya Uhuru Kenyatta wakiwaaga wajumbe waliohudhuria mkutano wa Wakuu wa  nchi za Jumuiya ya Umoja wa Afrika ya Mashariki uliofanyika katika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha Jana. 
 
 
 Marais wa jumuiya ya Afrika Mashariki wakisimama kwa dakika moja kumkumbuka laiyekuwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Uganda Marehemu Eriya Kategaya wakati wa ufunguzi wa kikao cha kumi na moja cha Jumuiya hiyo jijini Arusha leo mchana. Katika Hoteli ya Ngurdoto.Kutoka kushoto Rais Wa Burundu Pierre Nkurunzinza,Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda,Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Wa Kenya Uhuru Kenyatta.
  Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wakati wa ufunguzi wa kikao cha juu cha kumi na moja cha Wakuu wa nchi wa jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofaniyka jijini Arusha.
 Marais wa jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye kikao cha kumi na moja cha Jumuiya hiyo jijini Arusha leo.
 Baadhi wa ajumbe walioshiriki ufunguzi wa kikao cha Juu cha kumi na moja cha Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki(11th Extraordinary EAC Summit) kilichofanyika jijini Arusha.Picha na Freddy Maro-IKULU

Jaji Warioba: Tutatoa rasimu ya katiba yenye maslahi ya Taifa

9 3bae8
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid
10 38499
Mwenyekiti wa kamati ya uwasilishaji wa mapendekezo ya muundo wa mabaraza ya Katiba kwa jamii ya watu wenye ulemavu, Bw. David Nyendo (kushoto) akiwasilisha maoni yake ya kamati hiyo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika mkutano baina yao uliofanyika ofisi za Tume Jijini Dar es Salaam.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).

Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.

"Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi," amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.

Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.

Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.

Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.
Jaji Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.

"Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote," amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.


Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.

"Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo," amesema Jaji Warioba.
Kuhusu hatua inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji Warioba alisema Tume inaendela kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ya wananchi wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).
Changamoto

Akizungumzia kuhusu changamoto zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini

"Katika baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini," amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya katiba.

"Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya rushwa," alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.
Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba

Katika mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.
Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.

"Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi," alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.

source:Mjengwa blog

Sunday, April 28, 2013

Wanaotaka kujifunza Muungano waje Tanzania



 
Viongozi wa Taifa wakishangilia jambo siku ya kuazimisha kwa miaka 49 ya Muungano wa Tanzania, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam 

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa mfano duniani. Ni dola mbili huru zilizoungana na kuunda nchi moja yenye serikali mbili.

Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9/1961 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa Desemba 14, 1961. Namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1667 (XVI).’ Zanzibar nayo ikapata uhuru wake Desemba 10, 1963 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa Desemba 16, 1963; namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1975 (XIII).’

Ilipofika Aprili 26, 1964, mataifa hayo mawili huru yaliungana na hapo ndipo ilipozaliwa nchi iliyojulikana kwa jina la Tanzania.
Novemba 2, 1964 kupitia Wizara wa Mambo ya Nchi za Nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliuandikia barua Umoja wa Mataifa na kutaka Zanzibar na Tanganyika ziondoshwe katika orodha ya mataifa na iingizwe nchi inayojulikana kwa jina la Tanzania.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni sawa na muungano wa Siria na Misri walioungana mwaka 1958 na ni sawa na muungano wa Yemen ya Kaskazini na Yemen ya Kusini walioungana mwaka 1990. Kwa bahati mbaya muungano wa Siria na Misri ulivunjwa mwaka 1961 (ulidumu kwa miaka 3).

Kwa sasa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umefikia hatua nzuri na ya kupigiwa mfano duniani kwa sababu umedumu kwa miaka 49 sasa.

Hata hivyo pamoja na kuwa muungano huu una muundo wa kipekee na kuwa umedumu kuliko miungano mingi iliyowahi kuwapo Afrika.

Muungano wa kwanza ulikuwa ni ule wa nchi za Afrika Magharibi, mwishoni mwa miaka ya 50 na mwanzoni mwa miaka ya 60, ulioanza na nchi mbili Ghana na Guinea na baadaye Mali ikajiunga nao. Muungano huu ulitokana na vuguvugu la umajimui wa Afrika (Pan Africanism), vinara wake wakiwa Kwame Nkrumah wa Ghana, Sekou Toure wa Guinea na Modibo Keita wa Mali.

Novemba 1958 uliundwa muungano wa Ghana na Guinea mara baada ya mkutano wa watu wa Afrika (All- African Peoples’ Conference). Ghana ilitoa fedha nyingi na kuipa Guinea ili ijitoe haraka kutoka katika utegemezi wa Ufaransa.

Mei 1959 ikatangazwa kuwa umoja huo utatambulika kama Umoja wa Dola za Kiafrika.

Ilipofika Aprili 1961, Mali nayo ilijiunga na umoja huo. Muungano huo ulivunjika mwaka 1962 kutokana na vita baridi, ambapo Guinea ilionekana ikiinyooshea mikono Marekani wakati wenzake walikuwa wakifuata mrengo wa kushoto wa Karl Marx/Lenin
Muungano mwingine wa nchi za Afrika ulifanyika mwaka 1981 baina ya nchi za Senegal na Gambia, uliojulikana kama Senegambia ambao ulikufa mwaka 1989.

Pamoja na kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa kupigiwa mfano, lakini bado si vyema kuacha kusema kuwa una matatizo.

Tatizo kubwa la muungano huu ni ile hali ya upande mmoja kujiona kama unabinywa na upande mwingine wa muungano, nadharia iliyozoeleka ni ‘samaki mkubwa kummeza mdogo.’ Tatizo hilo lilisababisha baadhi ya Wazanzibar kulalamika na kumi katika hao walijitokeza na kwenda mahakamani kudai Hati ya Muungano. Jibu walilopata ni kuwa hakuna Hati ya Muungano (Mkataba).

Mwanasheriaa Mkuu wa Zanzibar alisema hakuna Mkataba wa Muungano kwa kuwa suala la muungano ni kama ardhi kwa sababu muungano ni wa nchi na nchi ni sawa na kuunganisha sehemu mbili za ardhi suala ambalo kisheria linaweza kuhojiwa ndani ya miaka kumi na mbili (12), baada ya hapo huwezi kuhoji, kwa maana hiyo ni halali kwa mujibu wa sheria ukizingatia waliohoji walifanya hivyo mwaka 2004 sawa na miaka 40 tokea nchi ziungane.

Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar umekumbwa na misukosuko mingi ambayo ndiyo hii inayoitwa kero za Muungano ambazo zinatolewa na wananchi wa pande zote mbili.
 
Kutokana na kelele nyingi kuhusu muungano, iliundwa kamati ya kujadili na kujaribu kutatua kero za muungano ikiongozwa na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kamati hiyo iliyo na uwiano sawa wa wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano imepokea kero 11 za muungano na kwa sasa wameshazitatua tisa zimebaki tatu ambazo ziko njiani kutatuliwa kwa hivyo kwa upande wa kero wamefikia hatua nzuri sana.

Miungano mingi duniani inakuwa na kero lakini hutatuliwa kwa ushirikiano kwa pande zote zinazohusika. Kwa mantiki hiyo kero ni vitu vya kawaida katika muungano wowote ule uwe wa nchi, mataifa au hata katika jamii. Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia muungano huu.

Nchi nyingi duniani zilizoungana zimeweza kupata maendeleo ya kasi ya kiuchumi na kiulinzi, tunaweza kuuangalia Umoja wa Nchi za Ulaya kama mfano. Vilevile Umoja wa Falme za Kiarabu ambao msingi wake ni uamuzi wa ulinzi wa uchumi wa falme saba ya kiarabu yanayozalisha mafuta yakiongozwa na Abudhabi.

Hivyo muungano kimsingi pamoja na mambo ya kisiasa na kijamii unakuwa na dhamira ya kuendeleza maendeleo ya nchi husika na kutumia rasilimali zao sambamba na rasilimali watu kuweza kujikomboa kiuchumi na kupandisha uchumi wao.

Na kwa Tanzania kupitia Muungano hilo kwa kiasi fulani limewezekana kwa sababu pamoja na kelele zinazopigwa kuhusu rasilimali lakini kimsingi rasilimali zote zinazopatikana Tanzania ni za Watanzania wote kwa sababu zinaelekezwa katika kujenga miundombinu ya maendeleo ya nchi yetu.

Na hata kwa upande wa ulinzi, si rahisi kuichezea Tanzania kwa sababu ina nguvu ya pamoja ambapo pengine Zanzibar peke yake na udogo wake isingeweza kuilinda vyema mipaka yake hasa kwa sababu ni nchi iliyozungukwa na bahari na ni visiwa vya kinacholengwa kwa stratejia za kiuchumi na hata kiutamaduni.

Waasisi wa Muungano huu, kwa kuamini watakuwa na taifa moja madhubuti lisiloyumba wala kuyumbishwa ndipo kwa moyo mmoja walipokubali kuunganisha nchi mbili na kuwa na taifa moja lenye dhamira moja na kwa pamoja kujifaharisha kuwa sisi ni Watanzania, na Tanzania ndiyo nchi inayotambulika Umoja wa Mataifa, si Tanganyika wala si Zanzibar.

Na bado kama kuna nchi ambazo zinataka kuungana basi zije kusoma Tanzania na watajua nini maana ya muungano wa dhati, nini umuhimu wa kuvumiliana, kuaminiana na kusaidiana. Hapa hasa ndipo penye udugu wa kweli hata kama wanagombana lakini hatimaye husuluhishana na kupatana na maisha kuendelea. Waswahili wanasema ‘ndugu wawili wakigombana, chukua jembe ukalime….’

Rashid Yussuf Mchenga ni mwanasiasa mkongwe/mwanaharakati aliyeko Zanzibar.

+255 773 560243 / 775-560243

SOURCE: MWANANCHI; Na Rashid Yussuf Mchenga

MSIBA WA NDUGU ADOLPH BRIAN/THADEO LWAKAJENDE

Adolph, Brian au Thadeo Lwakajende Enzi ya uhai wake
---
NDUGU WATANZANIA TUNAOISHI MAENEO YA NEW YORK,NEW JERSEY NA VITONGOJI VYA KARIBU TUNAOMBWA KUHUDHURIA KWENYE HARAMBEE YA KUCHANGISHA FEDHA ILI TUWEZE KUKAMILISHA MAZISHI YA MTANZANIA MWENZETU ALIYEANGUKA GHAFLA NA KUFARIKI DUNIA WIKI ILIYOPITA.NDUGU ZANGU WATANZANIA TUJITOKEZE KWA WINGI ILI TUUNUSURU MWILI WA MAREHEMU WETU USICHOMWE MOTO KUTOKANA NA SHERIA  ZA MUDA WA HIFADHI ZA MAITI KATIKA KITONGOJI CHA NEW JERSEY.NDUGU MTANZANIA ADA HII INAWEZA IKAMTOKEA YEYOTE KATIKA SISI NA WAKATI WOWOTE TUJITAHIDI KUONYESHA UMOJA WETU ILI TUFANIKISHE MSIBA HUU.KWA  WALE WATAKAOKUWA NA VITU WAKA PENDA VIPIGWE MNADA TUNAWAOMBA WAJE NAVYO ILI TUWEZE KUMSAIDIA KUMSITIRI MWENZETU.KWA WALIO MBALI YA NEW YORK TUMEFUNGUA ACCOUNT KWAAJILI YA MSIBA UNAWEZA KUTOA MCHANGO WAKO KUPITIA HUKO.MAZISHI TUMEPANGA YAFANYIKE JUMATANO TAREHE 1 MAY 2013,ANWANI ITAFUATIA.

HARAMBEE ITAFANYIKA LEO JUMAPILI 28 APRIL 2013 NYUMBANI KWA  MR.PETER LUANGISA SAA 10:00 JIONI.
374 HAWTHORNE TERRACE
MT.VERNON,NY,10552
                       

MAZISHI YATAFANYIKA JUMATANO 1 MAY 2013 MAHALA NA KWA TARATIBU ZIFUATAZO;

     VIEWING:LEE.O.WOOD FUNERAL HOME
23 EAST 2ND STREET
 MT.VERNON,NY,10552   
 TIME:  10:00 AM/ 4 ASUBUHI

     MAZISHI :MT.PLEASANT CEMETERY 
80 COMMERCE STREET
HAWTHORNE,NY,10532 
 TIME: 1:00PM/7 MCHANA


    ACCOUNT: BANK OF AMERICA/ PETER LUANGISA
 # 483033242384...ROUTING #02100032

KWA MAELEKEZO ZAIDI WASILIANA NA:

   RAHMA ADAM.........617 818 7657
  PETER LUANGISA...917 681 6971
  RASHIDI KAMUGISHA...973 703 4596
  BERNARD KIVUGO.......973 580 7166
  WILLIAM VEDASTO......973 551 2916

TAFADHALI MTAARIFU MTANZANIA MENZAKO UKIPATA UJUMBE HUU.

SOURCE: HAKI NGOWI

RAIS WA KENYA ATUA ARUSHA

   Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Rais wa Kenya Mhe Uhuru Kenyatta katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakati alipowasili  jana  jioni kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki unaofanyika jijini Arusha.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Mkewe Margareth Kenyatta wakifurahia ngoma za utamaduni muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika jijijini Arusha.Picha na Freddy Maro
 
SOURCE: HAKI NGOWI

Saturday, April 27, 2013

Mbowe: Ni kweli Mbunge wetu alidharau mamlaka ya Spika lakini...

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma jana, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akizungumzia kuhusu adhabu za wabunge watano wa chama chake kupewa adhabu kwa utovu wa nidhamu, amekiri kuwa mmoja wa wabunge wa chama chake, walidharau mamlaka ya Spika lakini kanuni zilizotumika hazikustahili na zilikuwa kiini macho.

Alisema Naibu Spika, Job Ndugai, hakustahili kutumia kanuni hizo za kifungu cha 2.2 na 5 za Bunge toleo la mwaka 2013, ambazo zinamtaka Spika atoe uamuzi kuhusu jambo litakalotokea bungeni endapo katika kanuni zilizopo hazina Mwongozo.

“Ukweli ni kwamba vurugu zilizotokea bungeni na kitendo cha mbunge wetu Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Tundu Lissu kinachodaiwa kuwa amedharau mamlaka ya kiti, kanuni zake zipo pamoja na adhabu yake,” alisema.

Alisema katika kanuni hizo za Bunge, vifungu 74 na 76 zimebainisha wazi adhabu zinazotakiwa kutolewa kwa mbunge atakayebainika kudharau mamlaka ya Spika au kuwa chanzo cha vurugu ndani ya Bunge.

“Ni kweli hakuna shaka kabisa Mbunge wetu alidharau mamlaka ya Spika, lakini zipo adhabu stahiki za kushughulikia suala hilo, na kwa namna kanuni hizo zilivyo kama zingetumika vizuri, huenda adhabu ingekuwa kubwa zaidi ya hii iliyotolewa, huku akiongeza kuwa wabunge hao walioadhibiwa hawakupewa haki ya kusikilizwa,” alisisitiza.

Adhabu hizo ni pamoja na Spika kutaja jina la Mbunge husika hadharani kuwa amedharau kiti na kumpeleka mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na Bunge na kwa upande wa fujo zinapotokea ndani ya ukumbi huo wa Bunge, kabla ya kutoa hoja ya nguvu, hutakiwa kwanza kuahirisha Bunge.

“Siku ile kweli vurugu zilitokea na kulikuwepo na vitendo vya kudharau mamlaka ya Spika, lakini Naibu Spika alitakiwa kwanza aahirishe Bunge, ndipo atumie nguvu, sasa badala yake waliingia askari wa kila aina ndani ya ukumbi jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Bunge,” alisisitiza.

Aidha, alisema kuhusu suala la adhabu kwa mbunge anayedharau kiti au kuhusika na vurugu, hutakiwa kwanza Spika amfikishe mbunge husika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ambayo baada ya kushauriana ndipo hutoa adhabu ambayo ni kutohudhuria Bunge vikao 10 iwapo kosa ni la kwanza na vikao 20 iwapo kosa ni la pili.

“Adhabu yoyote inayotolewa bungeni hutolewa kwanza na Azimio la Bunge na si Spika mwenyewe, endapo kanuni zilizopo zingefuatwa, huenda wahusika kama wangethibitika kabisa kuwa wamekosa, wangepata adhabu kali zaidi kama zilivyoainishwa kwenye kanuni,” alisema Mbowe.

Wabunge wa CHADEMA walioadhibiwa kutokana na vurugu zilizotokea bungeni humo hivi karibuni pamoja na Lissu, ni Ezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Peter Msigwa (Iringa Mjini).

---
via HabariLeo

Yanga Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara.




Kwa matokeo haya ya Coastal U 1-1 Azam FC, Yanga anakuwa bingwa kwakuwa Azam ina michezo miwili kama ikishinda itakuwa na 54, pointi ambazo Azam haitaifikia Yanga ambayo inapointi 56 mpaka sasa.
Fuatilia ratiba na msimamo hapa. Tovuti ya kandanda itawaletea takwimu za mechi zote za mshindi wa kwanza na wa pili hapo baadae mwishoni mwa msimu.

Uchambuzi

Hatimaye timu ya soka ya Dar Es Salaam Young African imechukua ubingwa wake wa 24 bila kuingia uwanjani. Hiyo imetokana na wapinzani wake wakubwa kwenye Ubingwa kwa mwaka huu timu ya Azam kutoa sare ya kufungana goli moja kwa moja katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Kwa matokeo hayo Azam imefikisha point 49 na hivyo hata ikishinda mechi zake 2 zilizosalia itafikisha point 55 ambazo tayari zimekwisha pitwa na Yanga yenye point 57. Yanga pia imebakiza michezo miwili yote itapigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam
 
Kimsingi dalili za Yanga kuchukua Ubingwa zilijionyesha tangu awali na tunaweza kusema imepata ubingwa iliyostahili.
Pamoja na kuanza ligi kwa kususasua kwa kutoa sare na Prison ya Mbeya na kufungwa mechi ya pili kwa mabao 3 kwa nunge, Yanga ilibadilika na kuanza kushinda mfululizo na mpaka pale mzunguko wa kwanza ulipokuwa unamalizika, tayari ilikuwa inaongoza kwa pointi 5 mbele ya Azam na kuipoteza kabisa Simba kwa pointi 6 zaidi na kufaulu kuziba pengo la pointi 8 ilizokuwa nazo samba dhidi ya Yanga.

MAPINDUZI
Mafanikio ya Yanga yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi ulioingia baada ya kushinikiza kuondolewa kwa uongozi wa Lord Nchunga aliyeonekana kushindwa kuongoza timu na kupelekea Yanga kumaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 3 nyuma ya Simba waliokuwa mabingwa na Azam iliyoshika nafasi ya 2. Kumaliza nafasi ya 3 ilikuwa matokeo mabaya zaidi kwa Yanga katika miaka ya hivi karibuni lakini kibaya zaidi walifunga dirisha la msimu kwa kupatwa kipigo cha aibu cha magoli 5 kutoka kwa hasimu wake Simba.

UONGOZI BORA
Kiukweli uongozi wa Yanga umekuwa makini sana kuanzia katika mfumo, uendeshaji wa timu, huduma kwa wachezaji na menejimmenti kwa ujumla. Chini ya uongozi wa Yusuph Mehboob Manji, Yanga hawajatetereka na wamekuwa mfano wa kuigwa katika mambo yake kuhusu klabu

USAJILI
Ili timu ifanikiwe ni lazima uwekezaji uanzie kwa kusajili wachezaji wenye kiwango.
 
Katika hilo, Yanga hawakufanya ajizi, walisajili wachezaji wenye kiwango kama akina Mbuyu Twite, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Kelvin Yondani, Ally Mustapha (Barthez) na Simon Msuva na kuwaongezea mikataba wachezaji wengine wenye viwango kama akina Kiiza (Diego) na Niyonzima (Fabregas). Ukiangalia na ukajaribu kuwa makini, utagundua kuwa Yanga ndiyo iliyosajili kwa umakini zaidi labda ikikaribiana na Azam

MAANDALIZI YA TIMU
Hapa pia YANGA walikuwa makini, walimsikiliza kocha kuangalia program zake na kuzifuata. Itakumbukwa kwamba timu ilipata michezo kadhaa ya kujipima nguvu na hata kuweka kambi nje ya nchi (Uturuki) kama ilivyopendekezwa na kocha

ARI YA WACHEZAJI
Ari ya wachezaji wa Yanga kusaka ushindi ilikuwa juu. Hata kama timu ilicheza na kushindwa kupata pointi yeyote katika mchezo mmoja, timu ilijipanga na kupata pointi katika mchezo uliofuata. Kitu kikubwa zaidi, wachezaji walichukulia kila mechi kama fainali kwao na walikuwa na uchu wa kupata pointi kwa mchezo

UMOJA NA MSHIKAMANO
Kulikuwa na umoja na mshikamano baina ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Hii iliwawezesha kuelekeza nguvu zao katika michezo inayowakabili badala ya kushughulikia migogoro isiyokuwa na tija klabuni.

JE AZAM ALISTAHILI KUSHIKA NAFASI YA PILI
Ndiyo na hata ubingwa pia kwani sifa zote zilizotajwa hapo juu pia Azam alikuwa nazo. Kimsingi kama kuna klabu ambayo ilikuwa inawanyima usingizi viongozi wa Yanga, benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla basi ni klabu ya Azam. Walijipanga na wanastahili heshima yao

Hongera Yanga kwa kurejesha Ubingwa wenu mliopokonywa na Simba msimu ulioisha na hongera Azam kwa kushika nafasi ya pili na kupata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa. Safari moja huanzisha nyingine. Wito wangu kwenu (Yanga na Azam) mjiandae vyema ili kuepuka aibu kama iliyowakuta wenzenu Simba

Kwa upande wa mahasimu wa Yanga timu Ya Simba msimu huu haukuwa mzuri sana kwenu. Kimsingi, migogoro na soka havikai pamoja. Nawaomba make chini na kujipanga upya mkisahahihisha yaliyojitokeza ili yasijitokeze tena na kwa kufanya hivyo mtarudisha ushindani uliaonza kupotea

 
Source: mjengwa blog