WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 18, 2013

Plato, Ubinafsi Na Maadili...( Makala Yangu Raia Mwema)

1 20715
Na Maggid Mjengwa,


WATANZANIA tulifanya kosa kubwa. Ni pale tuliporuhusu mfumo wa vyama vingi bila kufanyia marekebisho makubwa Katiba yetu. Maana, katika nchi zetu hizi, uongozi umekuwa wa awamu.

Kiongozi anaingia madarakani na kukaa kwa  miaka mitano mpaka kumi. Kwa Mwafrika, hapa ina maana ya kuhamia na kuhama kutoka nyumba za mamlaka. Ndio, tumejikuta tunaingiza wapangaji kwenye nyumba zetu bila kuwekeana mikataba. Na kama kuna mkataba, basi umeandikwa na mpangaji mwenyewe. Hapo  utategemea nini?

Katiba tunayokwenda kuiandika itusaidie kwenye kuwadhibiti ‘wapangaji’ wetu kwa maana ya viongozi tuliowapa dhamana za uongozi. Maana, ilivyo sasa, utakumkuta kiongozi anayejigamba hadharani, kuwa ameukwaa uongozi kwa vile ni swahiba wa fulani. Kwamba ana miaka mitano au kumi ya ‘ulaji’. Maana, hata jirani zake watasema ‘jamaa kapata ulaji’. Na magazeti pia yataandika hivyo, kana kwamba uongozi una maana ya ulaji na si utumishi wa umma.

Na Afrika wapangaji waliongia kwenye nyumba (mamlaka) kwa staili hiyo huwa wagumu sana kutoka hata pale wenye nyumba wanapoona wakati umefika wa kuwaondoa. Wameshaonja tamu ya madaraka. Na kama wataondoka, basi, watataka wao waingize wapangaji wapya wa kulinda maslahi yao. Hawataki kazi hiyo ifanywe na wenye nyumba kwa maana ya wananchi wenyewe.

Tatizo ni sisi Waafrika kukosa imani na Waafrika wenzetu  tuliowaweka madarakani. Kikubwa ni kukosekana kwa maadili ya uongozi. Viongozi wengi Afrika wamekuwa ni watu wenye tamaa ya madaraka na mali. Usipokuwa na Katiba yenye kuwadhibiti wanapokuwa kwenye uongozi, basi, nchi wanaigeuza ‘shamba la bibi’.

Kama mbweha, watakula minofu wakifuta damu midomoni. Ndio, watakula wakilindana. Kwa baadhi yao, miaka mitano au kumi kwenye uongozi ina maana ya kujilimbikizia mali, kana kwamba nchi nayo inahama baada ya miaka kumi.  Na siku za kuhama madarakani zikikaribia, itaongezeka, kasi ya kuvuna vilivyobaki kwenye ‘shamba la bibi’

 Swali ni je, Waafrika tuweje? Ni swali la kifalsafa. Inahusu virtue, kwa maana ya maadili na kutenda yalo ya haki. Kutenda yalo mema. Mtu mwenye maadili mema utamwamini, ndivyo pia wasemavyo Waingereza; a virtuous person is someone you can trust.

Mzazi anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kisiasa anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kidini anapaswa kuwa a virtuous person, mwandishi wa habari anapaswa kuwa a virtuous person, vivyo hivyo mwalimu.

Kwa hilo la mwisho, uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi kati ya Mwanafalsafa Socrates na mwanafunzi wake Plato usingepata umaarufu ulionao sasa kama Plato angebaki kuwa ‘mwanafunzi’ tu. Kubaki kuwa  kivuli cha mwalimu wake Socrates. Na Socrates  alitambua, kuwa jukumu la mwalimu ni sawa na la mkunga. Mwalimu ni mkunga.

Katika mijadala ya siku hizi tunaona hata wale wanaojiona ni viongozi wasivyo tayari kukosolewa. Wasivyo tayari kuona upungufu wao. Inasikitisha, kuona baadhi ya viongozi hawa ni vijana sana. Wamekuwa wabinafsi zaidi huku wakijiita ni viongozi. Wanajiita viongozi ilhali, kwa namna nyingi, hawawatendei haki wanaowaongoza, wanatanguliza zaidi tamaa ya mali na mamlaka.

Yumkini, kiongozi mtenda maovu kwa watu wake ni ama mjinga au mgonjwa. Kama ataambiwa bayana, kuwa anatenda maovu, au ana udhaifu wa kiutendaji, basi, huenda tutamsaidia kujirekebisha. Lakini, kamwe usishangae, kama kiongozi huyo atatingisha mabega na kucheka tu. Atacheka na  kutushangaa siye tunaomkosoa.

Katika machapisho yake ya "Republic", yaani , "Jamhuri", Plato anazungumzia kwa kina juu ya ubinafsi na maadili. Je, kuna sababu gani nzuri na za kimsingi za kuwa mtenda haki na si kinyume chake, yaani mtenda maovu?

Glaucon, ndugu wa Plato anajibu; "binadamu wote kwa asili yetu tu wabinafsi, tunajijali sisi wenyewe kila tunapopata nafasi ya kufanya hivyo. Bila kujali kama jambo hilo si la haki kiasi gani kwa wengine. Lakini, kwa bahati mbaya, nasi pia hufikwa na hali kama hiyo kwa kufanyiwa yasiyo haki na wengine. Jambo hilo huwa si la kufurahia," anasema Glaucon.

Katika jibu la Glaucon, Plato anatafuta namna ya kuikabili hali hiyo. Na ubinafsi wa viongozi Afrika huchagizwa na ulevi wa madaraka. Walevi wa madaraka wako dunia nzima. Katika nchi za wenzetu, wao walau wana njia za kuwadhibiti, kupitia Katiba zao. Lakini, Afrika ni bara lenye kuongoza kwa kuwa na walevi  wengi wa madaraka. Katiba zetu tulizorithi kutoka kwa wakoloni zinachangia kuongeza idadi ya walevi hawa wa madaraka. Ulevi wa madaraka Afrika ni sehemu ya jibu la swali; Kwa nini sisi ni masikini?” 

Hivyo basi, ili kuwepo na mazingira ya kuishi kwa amani na usalama ni vema, kwa mujibu wa mwanafalsafa Plato,  kukawepo na taratibu za kuishi kistaarabu. Ndipo hapa dhana ya kuwapo kwa Mkataba wa Kijamii (Social Contract) ikaingia akilini kwa mwanadamu. Ndio chimbuko la Katiba za nchi. Chimbuko la misingi ya utawala bora.

Nasi tuna nafasi sasa ya kuandika Katiba yetu mpya kwa maslahi ya Watanzania wa sasa na hata miaka mia moja ijayo. Inawezekana.

source:

No comments:

Post a Comment