WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, June 30, 2012

DR. Ulimboka Ana Siri Nzito




ASEMA ATAANIKA KILA KITU BAADAYE, ASEMA ACHWE APUMZIKE, MKUU WA JOPO LA MADAKTARI WANAOMTIBU ASEMA ALING'OLEWA KUCHA, MENO MAWILI NA KUPATA MTIKISIKO WA UBONGO.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya usiku wa kumkia juzi, kisha kutupwa Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe auguze maumivu makali yanayomkabili.

Dk Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na watu waliokuwa na silaha akiwa katika Viwanja vya Klabu ya Leaders, Kinondoni.

Jana, Dk Ulimboka ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikiwa haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu makali anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.

Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.
Hata hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka kujua nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado limetanda.

Siri nzito
Akisimulia mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema, akiwa katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku nyingine na kuongeza; "Yaani sikuwa na amani."

Alisema, "Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk Ulimboka)," alieleza na kuongeza:

"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."

Hata hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala yake alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali kuhusu hali yake na tukio hilo, baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.

Daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).

"Kidogo najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina maumivu makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu yeyote anayetaka kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa ni vizuri nipumzike," ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.

Lakini, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka, kuna ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela siyo tu kwa sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu ovyo.

Madaktari wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu tunamlinda wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani, na hilo tutahakikisha sisi wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa madaktari hao.

Kiongozi jopo la madaktari

Katika hatua nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk Ulimboka, Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Ulimboka ana majeraha mwili mzima.

“Ingawa kwa sasa anaendelea vizuri, Dk Ulimboka ameumia sana, kwani mwili wake mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji hao,”alisema Profesa Kahamba na kuongeza:

“Aliumia mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha za vidole na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa meno mawili,”alisema.

Alifafanua kwamba, kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo la mtikisiko wa ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari bingwa wanaendelea na harakati za kuokoa maisha yake.

Uongozi wa Moi watoa neno

Uongozi wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi hiyo.

Msemaji wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali yake kuendelea vizuri, lakini haingewezekana kwa waandishi wa habari kuingia ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.

“Mgonjwa anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua watu wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi imeshindikana kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu wake,”alisema Jumaa.

Jumaa aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia wodini analazimika kuvaa vazi maalumu na mavazi yaliyopo, yasingetosha, lakini pia wapo watu wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.

Tamko la Jumuiya ya Madaktari

Wakati hali ya Dk Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai mazingira ya tukio hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa wangependa kuundwa kwa tume huru itakayofanya kazi ya kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma.

“Madaktari kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa nyara,kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa sababu mazingira ya tukio hayaondoi kuhusika ama kutohusika kwa jeshi hilo,”alisema Dk Chitage.

Chitage alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku akionya Serikali kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.

“Kumekuwa na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara moja na itambue kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine yoyote bali ni kwa Serikali kutekeleza madai ya madaktari,”alisema Chitega na kuongeza:

“Sisi madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia Watanzania wakipoteza maisha kwa magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya kazi katika mazingira magumu huku kukiwa hakuna mipango ya kuboresha mazingira ya kazi, kukosekana kwa dawa na vifaa tiba.”

Mgomo huo wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na mwenyekiti huyo kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita. 

Chanzo:   http://www.mwananchi.co.tz

Friday, June 29, 2012

HEBU TUJIKUMBUSHE HII NA MGOMO WA MADAKTARI NA MATUKIO YANAYOENDELEA SASA;


MIGOMO NA KUKOSEKANA KWA EFFECTIVE COMMUNICATIONS


KWA NINI SWALA LA MIGOMO LINACHUKUA MUDA MREFU KUPATA UFUMBUZI?

Kama wataalamu wengi walivyowahi kusema huku nyuma kuwa chanzo cha migomo mingi kutokea na kuchukua sura mpya inatokana na  kupungua kwa mawasiliano miongoni mwa  pande mbili ambazo zinatofautiana au kama kuna mawasiliano mawasiliano hayo yanakuwa hayakubaliki kwa upande mmoja au kutohusishwa moja kwa moja katika majadiliano husika katika  kututua tatizo husika. 

Tatizo wakati mwingine wakati wa majadiliano mhusika mkuu mara nyingi Serikali  anachokizungumza pengine kinatia mashaka ya ukweli wa suluhu;  Baba Wa Taifa akikuwa akisuluhisha Mgomo  wengi walikuwa wakijenga imani  kwani  alichokuwa akikiongea unaona kabisa anachosema ndio anachomaanisha. Tofauti na viongozi wetu wa sasa mara nyingi wanachoongea na hali halisi ni tofauti kwani wanachukua mno hali ya kujilinda zaidi  na mbaya zaidi wanakimbilia kutupa taarifa ambazo zinaongeza wasiwasi baada ya kutatua tatizo.

Nafikiri katika hali yeyote ile serikali kama msimamizi wa sera na  taratibu za maisha ya watanzania katika hali ya migomo  ambayo imeendelea kujitokeza katika taifa letu, tunahitaji uthubutu katika kutatua tatizo hili;

Katika sakata la mgomo wa serikali na  madaktari ambao umedumu kwa takribani wiki tatu sasa;

  • Swali ambalo tunahitaji kujuuliza leo ni hili  Hivi serikali imeonyesha nia ya kumaliza mgogoro huo katika meza ya majadiliano mapema?

  • Je madaktari  wanajisikia vipi wakiona ndugu zao marafiki au watanzania wakipoteza maisha kwa kukosa hudumu muhimu ya afya ikiwa ni  sehemu haki ya wananchi kikatiba?

  • Nafikiri Majadiliano na maelewano ni sehemu muhimu katika kufikia muafaka wa migogoro

Hii ni vita ya mafahari wawili na wanaoumia kwa kiasi kukubwa ni wananchi ambao hawana kosa pamoja na mchango mkubwa mkubwa wa kodi zao wameishaia kupoteza maisha na kwa mvutano unaoendelea;

 Ni kweli kuwa Ikumbukwe kuwa, serikali ikitenda wajibu wake na  na kutoa haki kwa wahusiaka bila upendeleo  kwa wakati  sahihi kwa kila jamii ambayo inahusika kulingana na tatizo linalosababisha mgomo. Migomo mingi ambayo inajitokeza katika taifa letu inahusiana na tatizo la uwiano wa masilahi (mishahara) katika jamii pale panapotokea  tofauti ya mishahara iliyowekwa kwa makusudi ya kuwapa nafuu wafanyakazi wa kundi moja ndiyo inayotumiwa katika kudai nafuu ya wajibu na haki kwa kundi lingine.

Pengine hata swala la mgomo huu wa madaktari katika kipindi hiki unaweza kusababisha na mvutano wa posha za viongozi wetu watunga sheria (wabunge) ambao walitaka walipwe posho ya shilling 200,000 kutoka elfu sabini;(70,000) hii ni assumption moja ambayo imekuwa kichocheo cha mgomo;

Kama ni kweli kwa nini  wanasiasa  wanajifikira sana wao wenyewe na kujijengea hoja na kubeza hoja za wananchi  au makundi mengine ndani ya jamii hasa wanapozungumzia masilahi;  ni ukweli ambao haufichi kuwa wanasiasa ambao ni watawala amabo tumewapa dhamana ya kutuongoza  mara nyingi wanajitengenezea masilahi bora, posho  nono na marupurupu mengine yanayowafanya waishi maisha bora na pale wanapoumwa na familia zao wanatibiwa nje ya nchi. 

 Mwalimu Nyererealiwahi sema kuwa , “leo ukigoma unamgomea nani; tafakari matokeo!”  Jibu ni rahisi kada zinagoma kwa kukosa majibu sahihi ya maswali yao, na kukosekana kwa effective communication ya madaia husika.

Mwalimu Nyerere kwenye alitukumbusha kuwa , “Wafanyakazi wa Tanzania wanayo haki ya kuheshimiwa na wafanyakazi wengine na wananchi wote. Lakini kwa heshima yao wanayoipata, lazima wafanyakazi wote wakubali kufanya kazi kwa bidii. Ndiyo kusema kwamba kila mfanyakazi lazima afuate masharti ya kazi anayopewa. Kama kwa sababu fulani hayapendi masharti hayo, anaweza kupeleka shauri hilo katika kikao kwa utaratibu uliokubaliwa. Lakini kwa sasa lazima atafuata masharti yaliyopo.”

Tatizo la wakati wetu tabaka la masilahi bora linaongezeka na kusababisha  migomo  miongoni mwa jamii; kwa viongozi wetu na wanansiasa wetu nafikiri ni wakati mwafaka wa kuitafakari hali hii na kuijengea mikakati ya kuhakikisha kuwa migomo inatokomea kabisa ndani ya jamii zetu; Hakuna lisikowezekana; Pamoja tukisima tutaendelea kwa faida ya wote

Thursday, June 28, 2012

Mgogoro Wa Madaktari Na Serikali Ni Balaa Kwa Taifa


 

Ndugu zangu,

Nimepitia nilichoandika Februari 4, 2012 juu ya mgogoro wa madaktari na Serikali nikaona ni vema niyarushe tena maandiko yangu yale kama yalivyokuwa, bila kuongeza au kupunguza neno. Maana, kuna ambacho wahusika wanaweza hawakukiona wakati ule, lakini wakakiona sasa. Soma nilichoandika...


Ndugu zangu, 


Mgomo wa madaktari wetu ni habari kubwa. Umeingia sasa kwenye wiki ya pili. Hata kama ungekuwa ni wa siku mbili, bado ungesababisha madhara makubwa kwa nchi. Kwamba sasa una zaidi ya siku kumi na nne ni balaa kubwa kwa nchi yetu.
 

Tafsiri yangu;
 

Uliopo ni mgogoro kati ya madaktari na Serikali. Na kwenye mgogoro kama huu, siku zote, wenye kuathirika zaidi ni wananchi walio wengi.
 

Ni ukweli, kuwa karibu kila Mtanzania anayeamka asubuhi, ama ni mgonjwa au ana ndugu, jamaa au rafiki aliye mgonjwa.
 

Hivyo basi, kuna mamilioni ya Watanzania wenye kutaabika kila siku na maradhi ya aina mbali mbali. Ni Watanzania wenye kutegemea sana huduma ya tiba inayotolewa na madaktari wetu. Na katika nchizetu hizi, daktari ni rafiki muhimu sana wa mwananchi.
 

Ni jambo baya sana, pale Serikali inapoingia kwenye mgogoro na madaktari. Inapoingia kwenye mgogoro na marafiki wa wananchi. Hakuna mahali popote duniani wananchiwakatokea kuwachukia madaktari.
 

Hivyo basi, ni balaa pia pale Serikali inaposhindwa kumaliza tofauti zake na madaktari wa wananchi kwa njia ya mazungumzo na hata kufikia hatua ya madaktari kugoma.
 

Katika nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha za walipa kodi na kwa miaka mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika sana. Na hata kama angelikuwapo Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba , naye angehitajika sana. Vivyo hivyo kwa wakunga wakuu na wasaidizi, wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao anahitajika sana.
 

Na katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua ya kuwatisha na hata kuwafukuza kazi madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo njia nyingine zote za kumaliza tofauti na kusuluhisha migogoro na madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Na kwanini ishindakane?
 

Tufanye nini sasa?
Taarifa kwamba Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya huduma za jamii imepanga kukutana na madaktari wetu ni hatua njema na ya busara. Maana, katika mgogoro huu taarifa zimekuwa zaidi za upande mmoja; upande wa Serikali. Ni wakati sasa pande zote mbili zikasikilizwa na Kamati hiyo ya Bunge. Ndio, ni wakati pia hata madaktari wetu wakapewa nafasi tuwasikie.
 

Huu si wakati wa kufanya "propaganda" za kisiasa kwenye masuala ya afya za wananchi. Na hata pale Waziri wa Afya alipokaririwa jana Bungeni akitamka kuwa hali ya huduma za mahospitalini zimerejea katika hali yake ya kawaida ni mfano wa ’ Propaganda’ za kisiasa ambazo Watanzania hatuzihitaji kwa sasa. 


Hivi ni hali gani hiyo iliyorejea kwenye kawaida yake kwenye hospitali zetu baada ya mgomo huu wa madaktari unaoendelea sasa? Kwamba askari wetu wa Jeshi la Wananchi wamelazimika kwenda kutibu wagonjwa Muhimbili hiyo haiwezi kuwa ni ’ Hali ya kawaida’. Kwamba madaktari wameripoti lakini hawaonekani mawodini hiyo haiwezi kuwa ’ hali ya kawaida’. Na kama ni kawaida, hivi ni nini tafsiri ya ’ kawaida’?
 

Hapa kuna ukweli unaopaswa kusemwa, na si kitu kingine bali ni ukweli. Watanzania tunataka kujua; ni kwanini watendaji wa Wizara husika wameshindwa kulitatua suala la madaktari wetu na hata kutufikisha hapa tulipo? 


Yumkini, kulikuwa na hali ya kuyapuuzia madai ya madaktari katika hatua za awali. Yawezekana pia watendaji wa Wizara hawakuwa karibu na wawakilishi wa madaktari hao ili kutoa fursa ya kuongea na kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda ndio maana tumefika mahali sasa mgogoro umekomaa na wahusika kuonyesha hali ya kutunishiana misuli. 


Kuna mahali kosa limefanyika. Ni wapi?
 

Ndio hapa, kuwa hata kama Kamati ya Bunge itafaulu kusuluhisha mgogoro huu, bado Watanzania tutahitaji iundwe Tume huru itakayochunguza namna watendaji wa wizara husika walivyolishughulikia suala hili kwa upande wao.
 

Tume hiyo itusaidie kuupata ukweli mzima ili kama taifa, tujifunze. Na wakati tume kama hiyo itakapokuwa ikifanya kazi yake, itakuwa ni busara, kwa watendaji wakuu wa wizara husika wajiweke pembeni kwa maana ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huo. 


Kama Tume itabaini kuwa hakukuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wao na hususan walivyolishughulikia suala
 
hili la mgogoro na madaktari, basi, itajulikana hivyo, na wana nafasi ya kurudi tena kwenye nafasi za utendaji Serikalini. Inahusu umma kurudisha imani yake kwa Serikali yao. Ndio maana ya umuhimu wa wahusika kupisha pembeni kuruhusu uchunguzi ufanyike. Maana, haitakuwa busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali limegharimu maisha ya Watanzania.

Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea kufanyika sasa, sote, kama taifa, tumeshindwa.
 

Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi. 


Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika. 


Maggid Mjengwa,
 

Dar es Salaam,
 
Jumamosi, Februari 4, 2012

Wednesday, June 27, 2012

Kamamnda Kova Azungumzia Tukio La Kutekwa Dr. Ulimboka...!





Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamanda Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la utekaji nyara na kujeruhi lililompata kiongozi mgomo wa Madaktari Steven Ulimboka anayedaiwa kutekwa na watu watano wakati akipata kinwaji katika klabu ya Leaders Kiondoni jijini Dar es salaam.

Kamanda Kova amesema Ulimboka aliokotwa na msamaria mwema ambaye hakutaka kumtaja jina lake kiusalama na kutoharibu upelelezo kuwa msamaria mwema huyo alimuokota Ulimboka katika msitu wa Mabwepande na kutoa taarifa kituo cha polisi cha Bunju, ambapo polisi aliyekuwa zamu alichukua maelezo yake na baadae Steven Ulimboka kuletwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Kamanda Kova amesema jeshi la Polisi Kanda Maalum limeunda jopo maalum kwa ajili ya uchunguzi na upelelezi wa tukio hilo la utekaji nyara, kwani ni tukio la kwanza kutoke nchini, ameongeza kwamba wahusika wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo wachukuliwa hatua za kisheria na sheria itafuata mkondo wake ili kukomesha matukio mengine kama hayo

 

Waandishi wa habari waimsikilza kamanda Suleiman Kova katika kituo kikuu cha polisi Kati jijini Dar es salaam leo mchana.

Tuesday, June 26, 2012

Wakosoa Matumizi Ya Kiingereza, Uzungu Kwenye Filamu Za Kitanzania





Na Mwandishi Wetu

Wadau wa Sanaa wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia kiingereza kwenye majina ya filamu zao huku wakishangazwa na kazi hizo kubeba maudhui ya kizungu zaidi.

Wakizungumza wiki hii kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa, wadau hao walishangazwa kitendo cha filamu hizo kutumia majina ya kizungu wakati hapa kwetu kuna filamu nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za kihindi, kichina, kifaransa na zinafanya vizuri.

“Hoja kwamba, wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni ya kitoto, mbona hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi na kichina zinanunuliwa kwa wingi? Hapa kuna udhaifu katika kutengeneza filamu zenye ubora tujikite huko”alisema Mzee Nkwama Bhallanga.

Kwa mujibu wa wadau wengi waliozungumza, filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu.

“Maneno kwenye filamu si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na picha zaidi, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea” alisema Godfrey Lebejo ambaye ni Murugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na habari, BASATA.

Aliongeza kuwa, kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana kwa weledi na uhalisia wa tamaduni zetu kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili na utamaduni wetu.

“Inawezekana vipi utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto hawawezi kukaa pamoja kuitazama? Tufike mahali tuseme mambo haya ya kipuuzi basi kwenye filamu zetu” alionya Lebejo.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Filamu, wasanii na haja ya kujiendeleza kielimu, Msanii wa filamu Emmanuel Myamba maarufu kam Pastor Myamba alisema kuwa, tasnia ya filamu inakosa weledi hivyo kuhitaji mabadiliko.

“Ni wazi ukiangalia filamu zetu zinakosa weledi katika uandishi wa miswada, uongozaji, uhariri na hata uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali udhaifu huu turekebishe” alisema Myamba ambaye kwa sasa amefungua kituo cha mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film Training Centre (TFTC) kilichoko Ubungo.

Monday, June 25, 2012

JE BUNGE LETU LINA VIONGOZI WENYE SURA MBILI?



Kuna mwanasiasa mmoja mkongwe aliwahi sema katika moja ya mikutano yake kuwa; “Msishangae, tuna viongozi wenye sura mbili, wapo wanaofikiri kwa kutumia matumbo yao jinsi ambavyo wataneemeka na kujinufaisha wenyewe, hawa ni wale wabinafsi lakini wapo viongozi ambao wanatumia ubongo katika kufikiri jinsi ambavyo watatumia uwezo wao wote katika kuwatumikia wananchi, mimi ni miongoni mwa hawa,” 

Mwannasiasa mwingine naye aliwahi sema kuwa “Mawaziri ni lazima wajenge umoja na wakubali uwajibikaji wa pamoja. Katika uwajibikaji wa pamoja, hakuna wa kuwaruka wenzake.”

Na aliendelea kusisitiza kuwa “uadilifu si usomi, bali ni tabia akisema hivi sasa bungeni kuna vijana wengi tu waliosoma kuliko enzi zao, lakini linazidi kupoteza hadhi yake. Alisema viongozi wanaochaguliwa wanapaswa waache baadhi ya mambo ili kulinda hadhi yao...Huwezi kuwa mbunge au jaji halafu unakwenda baa unalewa hadi unaning’iniza miguu juu.”

Naungana na mheshimiwa mmoja mabaye aliwapa rai wabuge au wanasiasa wenzake kuwa “Lazima wanasiasa wa Tanzania tubadilike, kulaumiana na kunung’unika tu hakutusaidii. Leo wananchi wananung’unika na viongozi wananung’unika, kinachotakiwa ni kutafuta majibu.”

Lakini tukiangalia mbali kwa faida ya Taifa letu a tukiangalia utendaji wa wanasiasa wetu hasa wakiwa bungeni, kuzomeana, kulaumiana, kunyosheana vidole, hakutatuvusha katika maisha bora tunayoyafikiria kwa faida ya Taifa letu, nafikiri itastusaidia sana kama tafakari ya maisha bora itaanzia kwa waheshimiwa wabunge ambao wanabeba dhamana kubwa ya maisha ya watanzania;

Katika maisha ya kawaida ya binadamu na wabunge wetu wakiwa ni sehemu ya binadamu hawa ni ukweli ambao haufichiki kuwa hata waheshimiwa wabunge wana vibanzi au mapungufu ambayo wanayaona kwa wenzao na sio kwao, tukifanya tathimini ya kichama; na kujihesabu wao kama chama wako safi na wana hoja ambazo zinakidhi haja na wenzao wananamapungufu kihoja au katika kuleta utatuzi wa tatizo; matokeo yake mchango wa mbunge mwingine hugeuka kichekesho kebei na hatimaye kuhatarisha mwenendo wa mjadala.

Bunge imara linajengwa katika msingi wa uwazi kwa kukosoana na kuheshimiana kihoja; ushindani na uchambuzi wa hoja ni sehemu muhimu sana katika kusaidia Taifa kusonga mbele; wabunge wote hawawezi kamwe kuwa na mtazamo wa pamoja; Mwenyezi Mungu ametujalia vipaji tofauti katika kufikiri na katika kutatua matatizo; Waheshimiwa wabunge wetu  ni lazima wajifunze kujenga bunge lenye ushindani wa hoja kama sehemu ya  kutatua matatizo mbalimbali. Tutaweza kushinda tu kama tutafanikiwa kujenge jamii inayotafakari na si jamii ya kulalamika kila wakati na kuishia kutukanana bila aibu.

Tunafahamu kuwa Bunge ndicho chombo cha kutunga sheria na muhimili mkuu sana wa uchumi kutokana na michango yao bungeni hasa wakati huu wa bunge la Bajeti. Bunge linatakiwa liwe na uwezo wa kuchangia na kuandaa mazingira yanayofaa kwa maendeleo yetu. Lakini Kama Bunge halina   uwezo wa kuyaangalia matatizo ya nchi hii na kuyatafutia ufumbuzi, basi, kuna tatizo kubwa katika jamii yetu, kuna tatizo kubwa ambalo kama tukibweteka, litatutafuna sisi na vizazi vijavyo.

  • Je ni kweli kuwa wabunge wa chama tawala wanatanguliza maslahi ya chama chao kabla ya kuangalia na kuwakilisha matatizo na hoja za wananchi waliowapigia kura?


  • Je ni kweli kuwa wabunge wa upinzani ndio wabunge wanafanya jitihada kubwa za kuleta hoja za maendeleo bungeni?


  • Au wote kwa pamoja na wabunge wetu  wanaamini kuwa wao wanaostahili kula kwanza kisha wananchi wale baadaye?


  • Je  kama hivi ndivyo  baadaye hiyo ikifika kunakuwa hakuna zaidi ya makombo na ukoko uliobakia?


Nafikiri linalowezekana leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina ya Muumba wetu tu;

Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa “Kupanga ni kuchagua”. Je wabunge wetu wanapanga nini kwa maasilahi ya jamii? inatupasa kuwakumbusha waheshimiwa wabunge  watambue kwamba chochote wanachokipanga na kukitekeleza ambacho hakiongezi uhuru na umoja wetu wala hakina manufaa kwa walio wengi sio kitendo cha maendeleo.

Kwa nini kila kikao cha bunge Bunge kinachofanyika tunaendelea kuona kuwa Bunge letu Tukufu  linakuwa ni jepesi mno katika kuwapigania wananchi? Hoja nyingi zinazotolewa hazilengi sana katika kumnufahisha mwananchi kumwondoa katika tope alilonaswa la umasikini? 

Je tunafaidika nini kama waheshimiwa wabunge baada ya kujadili hoja kwa kumletea maendeleo mwananchi wa kawaida wanajadili hoja namana ya kukomoana wao wenyewe;  kama bunge letu litaendelea hivyo basi itatupasa kuamini kuwa baadhi ya mambo yanayofanywa na Bunge hili hayana tija kwa maendeleo ya Taifa letu. Wabunge Wasisahau kuwa Wabunge wanapokuwa bungeni wanatumia fedha za walipa kodi. Je hilo linawauma na wanaojiona wanafiki na waongo pale wanaposhindwa akutimiza wajibu wao? Kama inawauma na kuwakereketa ni vyema basi kila wakiwa bungeni lazima watumie kwa tija pesa ya mlipa kodi mnyonge ambaye hakwepi kodi ili kumnufaisha huyu anayewakilishwa na kumfanya aweze kuishi vizuri huko bungeni wakati wote wa kikao cha Bunge.

Nafikiri kama wabunge Kuna haja ya kuweka mbele mjadala wa  maslahi ya taifa letu. Tumeshaona na kusikia tabia mbaya wa baadhi ya mabunge ya wenzetu kupigana bungeni, kutukanan lakini hapa kwetu kwa waheshimiwa wabunge kuiga tabia hii nafikiri sio jambo njem; majadiliano ya amani kuhusu hoja mbalimbali za kumkomboa Mtanzania sitasaidia zaidi katika kuleta umoja wa kitaifa na itatusaidia kama taifa kuweka  maslahi ya taifa letu.

Inafurahisha pale tunapowaona waheshimiwa wabunge bila kujali chama wakikubaliana hoja za msingi ambazo zinasaidia kujenga uzalendo wa kutetea maslahi ya  ya watanzania  ambayo hayafungamani na chama chochote cha siasa wala dini. Bunge letu likiweza kufanya kazi yake katika msingi huu kuondoa taswira ya BUNGE LENYE SURA MBILI NA MBAYA ZAIDI LINALOANGALIA MASALAHI BINAFSI YAKUWANUFAISHA WAO NA KUTOKUMJALI MTANZANIA WA KAWAIDA AMBAYE NDIYE AMEWACHAGUA NA UNASALITIWA.


MUNGU IBARIKI TANZANIA

Sunday, June 24, 2012

Waraka Wa Kwanza Wa Mnyika Kwa Wananchi,Ukweli Ni Uhuru






Waraka wa kwanza mwaka 2012 wa Mbunge kwa Wananchi- “Ukweli ni Uhuru”


Waheshimiwa Wananchi wenzangu,
Amani iwe kwenu,
Kwa kipindi cha wiki nzima kumekuwepo na mjadala mkali bungeni, kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na katika taifa kwa ujumla juu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13 sanjari na yaliyojiri kutokana na kauli niliyotoa bungeni juu ya udhaifu wa Rais katika usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti pamoja na mipango muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.


Aidha, kupitishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 bila marekebisho yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa kumedhihirisha kile nilicho tahadharisha tangu awali kwamba; kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na uendeshaji wa nchi, udhaifu wa Rais una athiri maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.


Katika mazingira haya, udhaifu wa rais na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na serikali kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea pia migomo baridi ya watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kutokana pia na madai yao ya muda mrefu kutokuzingatiwa kwenye bajeti.
Ukweli ni Uhuru!.
Kadhalika udhaifu wa kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia tu mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya serikali. Ukweli ni Uhuru!.


Pia, katiba imempa mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge likikataa bajeti ya serikali kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja bunge suala ambalo huwapa hofu wabunge wengi hususani wa chama kinachotawala na kuwafanya wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika.


Hivyo, udhaifu wa bunge unachangiwa na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais katika kuvunja bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo wabunge hawana uwezo wa kubadilisha na wakati huo huo wakikataa bunge linavunjwa, katika mazingira haya udhaifu wa Rais wa kushindwa kutumia nguvu hizo za kikatiba una madhara makubwa sana kwa nchi na maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.


Kwa mantiki hiyo, katika mchakato wa katiba mpya ni muhimu kwa wananchi kutoa maoni ya kuwezesha ukuu na uhuru wa bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. Wakati katiba mpya ikisubiriwa, ni muhimu kwa marekebisho ya haraka kufanyika katika kanuni za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka kanuni ya 107 ili kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa. Katika muktadha huo, nimeanza kufanya uchambuzi ili kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni. Ukweli ni Uhuru!.


Hata hivyo, hata kwa kanuni zilizopo sasa udhaifu wa bunge unaongezeka kutokana na maamuzi ya kizembe mathalani ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge, mfano Kanuni ya 94 inalitaka bunge ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano wake wa mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, kanuni ambayo toka niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa wakati hata mara moja pamoja na kuwakumbusha wanaohusika kusimamia kanuni. Ukweli ni Uhuru!.


Mwaka huu udhaifu umekuwa mkubwa zaidi kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sanjari na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni 2012 hali ambayo imechangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilfu mpango wa taifa wa miaka mitano. Ukweli ni Uhuru!.


Nashukuru kwamba Spika wa Bunge Anna Makinda amekiri bungeni tarehe 20 Juni 2012 kwamba kulikuwa na udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge kukamilisha kazi ya kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha serikali kuongeza vyanzo vya mapato kama wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na pendekezo hilo kurudiwa tena na kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni 2012. Ukweli ni Uhuru!.


Izingatiwe kuwa iwapo sheria ya fedha ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012 kama ilivyokuwa imepangwa awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia sehemu kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye bunge na waziri. Hivyo, michango na mapendekezo ya wabunge bila Rais mwenyewe kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa mapato kwa kuwa kwa kuwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) udhaifu wa bunge ni pamoja na kukatazwa kutoza kodi au kuongeza kodi. Ukweli ni Uhuru!.


Hivyo, Kamati ya Fedha na Uchumi itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3) kurejea maoni yake, ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne wa Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 na kufanya marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri Waziri. Ukweli ni Uhuru!.


Aidha, ili kuondoa udhaifu uliopo Rais Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu rasmi za bunge (Hansard) za tarehe 18 Juni mpaka 22 Juni 2012 na kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha Waziri wa Fedha ya 86 (10) kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika bidhaa zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni Uhuru!.

Izingatiwe kuwa nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa ufupi nilichosema bungeni na nilichotarajia kusema na kuahidi kwamba nitatoa tamko kamili baadaye; baada ya kujipa muda wa kutafakari nimefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati bunge litakapoelekea kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013; ambapo pamoja na masuala mengine nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa kwa watanzania kuweza kutekelezwa na serikali. Ukweli ni Uhuru!.


Kwa sasa niwashukuru wananchi wa Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na watanzania kwa ujumla walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni yao kwenye mitandao ya kijamii, simu za mkononi na katika vyombo vya habari. Nawashukuru pia viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya taifa. Ukweli ni Uhuru!.


Nashukuru pia kwa mchango wa walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli niliyotoa juu ya udhaifu wa Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana na jazba na wengine wameeleza kuwa ningetumia lugha ya diplomasia kufikisha ujumbe ili kutodhalilisha taasisi ya urais na kwa kuzingatia utamaduni wetu wa heshima kwa wakubwa na wapo wachache waliosema kwamba ni matusi kutamka ‘udhaifu wa Rais’. Ukweli ni Uhuru!.
Wakati mjadala huu ukiendelea ni rai yangu kwamba rejea ifanyike katika mchango wangu wa tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili pia ifanyike kwenye mchango wangu wa tarehe 19 Juni 201; na ieleweke kwamba naheshimu taasisi ya urais na umri, naamini katika matumizi ya lugha ya kidiplomasia, hata hivyo nilitafakari na kuamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka zote zinazohusika na wauchukulie kwa uzito tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita. Ukweli ni uhuru!.


Niliamini, naamini na nitaendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka; hata hivyo kwa kuwa pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa chanzo cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni wa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa; nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli ni uhuru!.


Katiba ya Nchi ambayo niliapishwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”. Toka nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010 kwa nyakati na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wa kawaida wakilalamika kuhusu udhaifu wa Rais na kutaka atumie nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti serikali kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayolikabili taifa; niliamua kuendelea kusema bungeni kwa mara nyingine ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Ukweli ni Uhuru!.


Tarehe 19 Juni 2012 nilieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti na tarehe 22 Juni 2012 nilipiga kura ya hapana ya kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa ajili ya miradi ya barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais Kikwete na kuingizwa kwenye jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande wa miradi ya maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika bajeti ya 2012/2013.
Ukweli ni Uhuru!.
Pamoja na utetezi uliotolewa na Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri kati ya kiingereza na Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua kuikataa bajeti kwa kuwa ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao uliwasilishwa na Rais Kikwete na ukapitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo kama zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli ni Uhuru!.


Naamini Rais Kikwete anayofursa ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake katika muswada wa sheria ya fedha kupanua wigo wa mapato na hatimaye kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 107 mapendekezo ya matumizi ya nyongeza ya fedha za serikali yenye kulenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo.


 Kwa upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam, serikali kwenye bajeti ya nyongeza inayopaswa kuwasilishwa iongeze fedha za miradi ya Maji kwa upande wa Ruvu Juu ikiwemo kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa Bwawa la Kidunda, kwa upande wa Barabara iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za pembezoni za mchujo na za mzunguko za kupunguza msongamano wa magari, na fidia ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la Mloganzila.
Ukweli ni Uhuru!.
Kwa Wasemaji wa CCM waliodai kwamba nimetoa lugha ya matusi dhidi ya Rais na mwenyekiti wa chama chao wasome Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania cha mmoja wa waasisi wa TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere ambapo wakati huo taifa likiwa katika mtanziko alimueleza Rais wa wakati huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’ katika ukurasa wa 50 na kuendelea kusema katika Ukurasa wa 51 na namnukuu “Kwa sababu ya minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake salama” . Ukweli ni Uhuru!
Naamini Mwalimu Nyerere hakumtukana Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu nimetukana ni kumtuhumu pia Marehemu Baba wa Taifa; narudia tena kusisitiza kuwa udhaifu uliojitokeza ni kutokana na Rais kutokutumia kwa uthabiti nguvu na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ibara za 33, 34, 35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji wa serikali na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni Uhuru!.


Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “ Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni ubinafsi.
 Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho wa kunukuu: Ukweli ni uhuru.


Wenu katika utumishi wa umma, 


John Mnyika
22 Juni 2012
Bungeni-Dodoma
                   Chanzo:   http://mnyika.blogspot.com

Udhaifu Wa JK; Tafsiri Yangu








“ OUR President is important; but, he is not Tanzania. All of our people organaized together are Tanzania”- (Julius Nyerere, Julai  29, 1985)

Ndugu zangu,
Watanzania wengi hatuna mazoea ya kusoma, hata makala za magazetini ukiachilia mbali vitabu vya taarifa na hadithi. Ndio, tu wavivu wa kusoma.

Kigong’onda ni aina ya ndege.  Ndege huyu  ana mdomo mrefu na anapenda sana kugongagonga mti kwa mdomo wake. Ndivyo anavyojipatia ridhiki yake. 

Lakini, kwa hulka yake ya kugong’onda kila kilicho mbele yake, basi, hata ukimwekea mti wa chuma porini, kigong’onda atahangaika nao mpaka damu zimtoke mdomoni. Ni hulka yake.  Kiongozi hapaswi kuwa kama kigong’onda.

Kuna hoja mezani juu ya udhaifu wa JK, imetokea Bungeni.  Yumkini, kama mwanadamu, JK ana mapungufu na udhaifu wake, nani asiye na mapungufu na udhaifu? Lakini, tukimzungumzia JK kama taasisi ya ’ Urais’, namwona Rais anayejipambanua na waliomtangulia. Ni  kwa kujitahidi kufanya yale yalo nafuu na yenye manufaa kwa nchi yetu  kwenye mfumo dhaifu uliopo.  

 Wanadamu tunapaswa kuhukumu dhamira ya mtu na si matokeo. Bado namwona JK kama kiongozi mwenye dhamira njema kwa nchi yetu. Nauona ujasiri ndani ya JK. Ni ujasiri wa kufanya yale ambayo, hata ndani ya chama chake hayakuwezekana kufanywa na Mwenyekiti wa chama huko nyuma. Na bila shaka, kuna wahafidhina ndani ya chama chake wanaomwona JK kuwa ni dhaifu kwa mantiki hiyo. Kuna wanaoamini, ndani ya CCM, kuwa Rais wa chama tawala anayekaa na kuongea na wapinzani Ikulu ni Rais dhaifu!

Na hata haya tunayoyashuhudia sasa, yumkini ni matokeo ya dhamira njema ya JK. Naamini, kwa tunavyoenenda sasa, Tanzania atakayoiacha  JK haiwezi tena kurudi kuwa kama ilivyokuwa kwa Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. JK amepanua uhuru wa Watanzania kuchangia fikra zao bila hofu. Siku zote, hofu haijengi nchi.

Maana, tumefika hapa kutokana na mfumo dhaifu unaozaa Serikali dhaifu, unaozaa Bunge dhaifu na unaopelekea pia kuzaa vyama dhaifu vya siasa ikiwamo chama tawala. Na chimbuko lake ni Katiba ya Nchi iliyo DHAIFU. Ndio, tatizo la nchi yetu ni tatizo la kimfumo.

Ni tatizo lililoasisiwa tangu Awamu ya kwanza ya Urais.  Angalia, Katiba yetu inampa nguvu nyingi sana Rais. Tuna bahati tu hajatokea Rais anayeamua kuzitumia ipasavyo nguvu hizo.

Nimeona katuni ya ndugu yangu Masoud Kipanya kwenye gazeti la Mwananchi la jana, Juni 23, 2012.  Kipanya alionyesha foleni ndefu ya wapiga kura Watanzania walio tayari kumpigia kura Rais Dikteta.   

Niliogopeshwa na michango ya  maoni ya Watanzania juu ya katuni ile. Wengi walionekana kuikubali hali hiyo. Kuwa kwao kwa hali ilivyo sasa ni heri kutawaliwa na dikteta kuliko Rais dhaifu!

Inasikitisha na inaogopesha kuona kuwa tumefika hapa. Naamini mimi na wengine wengi tuliokulia enzi za chama kimoja  na Rais mmoja ambaye ni kila kitu, tusingependa kurudi huko tulikotoka. Nikayasoma jukwaa moja maoni ya Mtanzania Ludovic Mwijage aliyejaribu kuonyesha ubaya wa udikteta. Hapo chini nimeweka kitabu cha Mwijage kilicho kwenye maktaba yangu. Kwa mimi niliyesoma kitabu chake, ningeshangaa kama Mwijage angeunga mkono hoja ya kumwona JK dhaifu na kutamani Rais Dikteta.

Ukweli, sisi wa ’ Kizazi Cha Azimio’ tuliwaona wazazi wetu wakiishi katika hali ya hofu na mashaka. Waliishia kunong’ona tu pale walipotaka kuishutumu Serikali na Rais aliye madarakani.

Mjumbe wa nyumba kumi alikuwa ni mtu aliyeogopewa sana.  Huyu  alikuwa ni wakala wa Chama tawala na Serikali. Moja ya majukumu yake ilikuwa ni kuwatambua, katika nyumba zake kumi, wale wote waliokuwa na mitazamo tofauti na ya Serikali na Mkuu wa Nchi. Ni wale walioitwa ’ Wapinga Maendeleo!’. Kuna waliosekwa rumande, kuna waliofungwa magerezani.

Enzi zile viongozi watu wazima walisimama majukwaani na kusema; ” We have a One Party Democracy!” Katika dunia hii hakuna ‘ One Party Democracy’ bali ‘ One Party Dictatorship’. Hata kwenye nyumba mwanamme ukishaoa huwezi tena kutamka juu ya ‘ One Man Family!’- Na watoto wakiingia kwenye familia , nao pia wanatakiwa wawe na sauti.

Afrika Rais anategemea sana wasaidizi wake katika kuifanya kazi yake. Hivyo, mfumo dhaifu huzaa wasaidizi dhaifu pia. Mfano, pale Bungeni hakukuwa na haja yoyote ya mbunge kutolewa nje kwa kutamka ‘ JK ni Dhaifu’.   

Badala yake, ilikuwa fursa kwa wasaidizi wa JK kujenga hoja za kubomoa hoja za mbunge huyo.
Kumtoa Mbunge nje kumemsaidia zaidi kuwasilisha ujumbe wake na hata ukaaminiwa na wengi. Maana, swali la hata wasiofutilia vipindi vya Bunge ni ‘ Kwani huyo Mnyika amesema nini?” Ni yale yale ya Zitto Kabwe kutolewa Bungeni kwa hoja ya Buzwagi. Nakumbuka kumsikia Mzee Malecela akisimama Bungeni na kutamka, kuwa dawa ya kidole chenye kansa ni kukikata!

Malecela na wengine katika CCM walisaidia, kwa kasi ya ajabu, kumtangaza na kumpa umaarufu Zitto Kabwe. Maana, wengi mitaani walitaka kukiona kidole hicho chenye kansa kinachokisumbua chama tawala na kikongwe hapa nchini, CCM.  

 Na mpaka hii leo, CCM wanarudia makosa yale yale ya jana. Na kwanini wanarudia? Ni kwa baadhi ya watendaji, kuingiwa hofu na wimbi hili la mabadiliko, hivyo kutojiamini na hata kufanya yale wanayodhani yatamfurahisha aliyewateua, kumbe, wanamharibia, na wanazidi kukipaka matope chapa chao.
Naam, tunaweza kuondokana na mfumo dhaifu kupitia Katiba mpya ijayo. Inawezekana.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765