WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, August 31, 2013

Kingunge Anaangalia Miaka 50 Nyuma, JK Anaangalia Miaka 50 Mbele !

kingunge_bd410.jpg

Ndugu zangu,

Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru ni mmoja wa wanasiasa ninaowaheshimu sana. Nimemsikia Kingunge tangu nikiwa na miaka saba.

Lakini, kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere, hakuwa malaika, Kingunge naye ni mwanadamu kama wengine. Si malaika.

Nimeyasikia mawazo ya Kingunge juu ya Serikali Tatu na hata Uraia wa Nchi Mbili. Ni mawazo yake, nayaheshimu, ingawa, kwa mtazamo wangu, Kingunge hayuko sahihi kwenye yote mawili.

Na hapa nitalizungumzia hili moja tu la mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba juu ya muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Kimsingi haya ni mapendekezo yenye kutokana na maoni Wananchi. Hivyo, Tume imewasilisha tu. Si mapendekezo ya Jaji Warioba au wajumbe wake.
Hii ni tofauti kubwa na mazoea ya ' Ukale' ya Mzee Kingunge ambayo hata sasa anataka yafuatwe; kuwa jambo kubwa la muundo wa Muungano liachiwe Chama Cha Mapinduzi na vikao vyake.

Ni jambo jema kwa mwanadamu kujifunza kutokana na historia, lakini, si jambo jema kwa mwanadamu kuwa mtumwa wa historia. Ni bahati mbaya, kuwa Mzee wetu mpendwa, Kingunge Ngombare Mwiru, anataka tubaki kwenye utumwa wa historia. Hatutaki.

Na hakika Mzee Kingunge anapaswa kuelewa, kuwa nchi hii ni zaidi ya Chama cha Siasa. Na chama cha siasa kilicho madarakani hakiongozi mawe. Na hata kama kingekuwa kinaongoza tumbiri, bado kingekumbwa na changamoto ya uwepo wa tumbiri wenye kutaka mabadiliko, kulingana na mahitaji ya wakati.

Tukubali, kuwa yalifanyika makosa makubwa ya kiuongozi huko nyuma. Ni pale masuala makubwa ya kitaifa kuachwa maamuzi yake kufanywa na kundi dogo la watu kwa kutumia nyadhifa za uongozi wa chama. Kwenye masuala makubwa ya nchi Chama kiliamua juu ya vichwa vya watu bila kushirikisha mawazo ya wananchi wenyewe, iwe kwa kupitia kura za maoni au kukusanya tu maoni ya makundi wakilishi. Huo ni msingi wa manung'uniko mengi ya sasa.

Kwangu mimi, Jakaya Kikwete ni mwanamageuzi wa kweli ambaye, kama kiongozi, ameonyesha ujasiri mkubwa wa kuzipa mgongo fikra za ukale na kuiangalia zaidi nchi na mustakabali wake kwa miaka mingi ijayo. Anafanya hivyo bila kujali nani au chama gani kitakuwa madarakani.

Wakati Mzee Kingunge na wahafidhina ( wasiotaka mabadiliko) wengine ndani ya mfumo uliopo wanatoka mahandakini huku wakihaha kujaribu kuurudisha nyuma mshale wa mabadiliko chanya kwa jamii , Jakaya Kikwete anaonekana, kuwa sio tu amesimama imara katika kuhakikisha mshale wa saa ya mabadiliko chanya kwa nchi unakwenda mbele, bali, unakwenda mbele kwa kasi.

Ni imani yetu, Wananchi walio wengi, kuwa Jakaya Kikwete hatakatishwa tamaa wala kuyumbishwa katika kukamilisha ajenda yake njema ya mabadiliko chanya kwa jamii ya Watanzania kuelekea miaka 50 ijayo.

Mzee Kingunge aelewe pia, kuwa wakati umebadilika. Kuwa ya mwaka 1974 alipojiunga na TANU ni tofauti na ya sasa, mwaka 2013. Huu ni wakati wa kiongozi kuonyesha uwezo wa kusoma alama za nyakati. Hivyo, kujitahidi kuendana na mabadiliko ya nyakati.
Hiyo pia ndio tafsiri ya kuwa ' Kiongozi wa Kisasa na Kimaendeleo'- A modern and progressive leader. Jakaya Kikwete kwa sasa yumo kwenye kundi hilo.

Na wenzake ndani ya CCM wakimsaidia katika kazi yake, basi, ni fursa pia kwa Chama chao kuiteka tena mioyo ya Wananchi wengi, mijini na vijijini. Maana, kati ya ambayo yanawachosha wananchi ni kukosekana kwa mawazo ya usasa na ya kimaendeleo kutoka kwa miongoni mwa viongozi wa CCM. Ni moja ya sababu ya chama hicho kupungukiwa na mvuto hususan kwenye kundi kubwa la vijana.

Na hakika, hata kama hatuoni leo, historia itakuja kumkumbuka Jakaya Kikwete kama mmoja wa viongozi Wana-Mageuzi ndani ya Chama chake CCM, na nchi kwa ujumla.
Maggid.
Iringa.
0754 678 252

Comments!
Thabit Molly Ni kweli japo na mimi napingana na wewe katika suala la uraia wA NCHI MBILI
41 minutes ago · Like · 1

Goddy Semwaiko sijakuelewa Maggid. hujaeleza Kingunge kaongea nini na kwa point zipi wewe unapishana nae. hebu nifafanulie tuweze kuchangia na kujadiliana. naona umetumia muda mwingi kumlaumu, nadhani na yeye ana uhuru wa mawazo na mchango wake. Haya mimi sijamsikia huyu babu kaongea nini, nihadithie
36 minutes ago · Like · 2

Thabit Molly Kama uko Tz fatilia magazeti yote yameongelea alichoongea mzee Kingunge jana@Goddy Semwaiko
29 minutes ago · Edited · Like · 1

Maggid Mjengwa Baada ya kukaa kimya muda mrefu, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingune Ngombale-Mwiru, ameibuka na kuwatupia lawama viongozi wa CCM, kwa kutaka kupenyeza suala la uraia wa nchi mbili ndani ya Katiba Mpya.Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, ...See More
32 minutes ago · Like · 2

Goddy Semwaiko OK. Mimi sioni tatizo na naungana mkono moja kwa moja na huyu mzee. Nakubaliana nae kabisa, kama hoja ya muhimu inajadiliwa na kundi dogo la watu na kutumia fursa yao kutengeneza Kitabu wanachokiita Ufafanuzi wa Rasimu ya Katiba, sidhani kama watu hao wana haki ndani ya kundi kubwa la wanachama. Sasa Maggid wewe unalalamika nini hapo? Kiasi cha kumshambulia huyu mzee???
27 minutes ago · Like

Maggid Mjengwa Goddy, nimejikita kwenye Serikali Tatu. Kingunge hataki Serikali Tatu, anataka tubaki tulikokuwa. Hayuko sahihi. Kwa mtazamo wangu. Hata la Uraia wa nchi mbili napingana nae. Nitalifafanua.
14 minutes ago · Like

Goddy Semwaiko Mimi Naona serikali tatu ni tatizo Kubwa mno, na gharama zisizo na sababu. Kama serikali moja haiwezekani, basi serikali mbili ziangaliwe upya. Ingawa najua upande wa pili hawataki kusikia swala la serikali mbili. Mimi binafsi kwakweli serikali tatu ni kudanganya wenyewe, kwani haiwezi kudumu wala hakutakuwa na la msingi kwa hii serikali ya muungano.
 
Kuhusiana na swala la Uraia wa nchi mbili pia, sioni umuhimu, na swala la fursa na uwekezaji, bado wanaotaka kuwekeza nchini mwao wanaweza tu, mbona kuna wawekezaji ambao si raia wa nchi hii na wanafanya vizuri kibiashara? Iweje raia anaepata fursa huko nje ashindwe kuwekeza hapa, hata kama akiukana uraia wa nchi hii, anaweza kuwekeza kama mgeni, tena atakuwa mgeni mwenye kujua in and out. Swala la uwekezaji kutetea uraia wa nchi mbili nalo naliona halina mashiko....
Leta hoja Maggid...

source: mjengwa blog

Museveni aombwa kumaliza mgogoro Rwanda, Tanzania


 Rais wa Uganda, Yoweri Museveni 

Dodoma. Mgogoro wa kidiplomasia ulioibuka kati ya Rwanda na Tanzania, jana ulitinga bungeni huku Rais Jakaya Kikwete, akimuomba Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa msuluhishi wa mgogoro huo.

Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alionyesha kutoafiki kuombwa kwa Rais Museveni akisema naye yuko katika kundi linaloitenga Tanzania.

Kauli ya kwamba Tanzania kupitia kwa Rais Kikwete imemuomba Rais Museveni kuwa msuluhishi wa mgogoro huo,ilitolewa jana bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la papo kwa hapo aliloulizwa na Mbowe akitaka kupata kauli ya Serikali juu ya kuibuka kwa mgogoro huo wa kidiplomasia na dalili za Tanzania kutengwa.

Katika swali lake la msingi, Mbowe alisema mvutano huo wa kidiplomasia umesababisha Tanzania kutengwa katika shughuli ambazo zilipaswa kuwa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alikiri kuwapo kwa hali ya  kutoelewana na kwamba hata baada ya kauli ya Rais Kikwete kuwa Tanzania haina uhasama na Rwanda, mvutano unaendelea.

“Mimi ninavyojua Rais (Kikwete) amemuomba Rais wa Uganda Yoweri Museveni ajaribu kuona ni namna gani jambo hili linaweza kusuluhishwa na maneno haya yakapungua,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu alisema anaamini busara zitatumika ili kuona jambo hilo linakwisha vizuri lakini kama litaendelea na kuonekana dalili za Tanzania kutengwa busara zaidi itahitajika. Katika swali la nyongeza, Mbowe alisema kinachoonekana, Rwanda wameweza kuwavuta Waganda na Wakenya katika mikakati ya kiuchumi ambao kwa hali ya kawaida ingekuwa ni ya jumuiya

Alisema viongozi wa mataifa hayo wamekutana Kampala na Kenya bila kuwapo kwa Tanzania

source: mwananchi

Viongozi wa CCM wamtibua Kingunge

Mzee Kingunge 

Dar es Salaam. Baada ya kukaa kimya muda mrefu, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingune Ngombale-Mwiru, ameibuka na kuwatupia lawama viongozi wa CCM, kwa kutaka kupenyeza suala la uraia wa nchi mbili ndani ya Katiba Mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam jana, Kingunge alisema baadhi ya ‘wakubwa’ ndani ya chama hicho wanataka kuliingiza suala la uraia wa nchi mbili kwenye Katiba Mpya kwa masilahi yao binafsi, bila kuwashirikisha wanachama.

Alisema anashaanga namna ambavyo suala hilo limeingizwa kwenye kitabu kiitwacho ‘Ufafanuzi wa rasimu ya Katiba Mpya’ kilichoandikwa na chama hicho, kwa kuwa halikuwahi kujadiliwa katika mikutano ya wanachama.

“Lipo jambo limenikera sana, napenda niliseme na lieleweke vizuri linahusu uraia. Nimearifiwa kuwa kwenye kikao cha Kamati Kuu walikuwa wakijadiliana, mimi nastaajabu kweli kwa chama changu kuliingiza suala hili,” alisema Kingunge.

Alisema yeye analipinga kwa sababu lingekuwa kubwa lingejadiliwa na wanachama ambao ni wenye nchi.” Alisema anapinga pendekezo la Watanzania kuruhusiwa kuwa na uraia wa nchi mbili kwa sababu hoja zilizotolewa, hazina nguvu.

“Tunaambiwa eti Watanzania wengi wako Marekani na Ulaya na huko wana fursa nyingi, eti wakipata uraia wa pili watafaidi vizuri fursa hizo. Wanaosema hivyo wana matatizo kidogo, wanataka uraia wa nchi yao na uraia wa nchi nyingine,” alisema.

Akizungumzia rasimu ya Katiba Mpya, Kingunge alisema mapendekezo ya kuwa na Serikali tatu yanaleta mkanganyiko kwa wananchi na kwamba hilo ni tishio tu la kutaka kutoka kwenye Muungano sahihi.
Wakati huohuo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetamba kukusanya maoni ya watu 3,5 milioni kuhusu rasimu ya Katiba Mpya kwenye ngazi mbalimbali ya mabaraza.

Chama hicho kimesema leo kinatarajia kukabidhi rasmi maoni hayo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Willibrod Slaa alitamba kuwa maoni hayo wameyakusanya kwa uwazi kutoka kwa wananchi katika ngazi ya wilaya, majimbo, kata na kwa njia ya simu,

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri ya Chadema, John Mrema, alisema chama chake kinahofia CCM inaweza kuchakachua maoni ya Katiba, hasa kama Bunge la Katiba litakuwa na idadi ya wabunge wa sasa.

Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), limesisitiza kutambulika kwa Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba mpya.

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Bin Simba, alisema licha ya kutuma maoni ya kutaka kuwepo kwa mahakama hiyo wakati wa kukusanya maoni, inashangaza kuona kuwa katika rasimu ya katiba maoni, hayakuwekwa.

“Kwa kuwa ukusanyaji maoni bado unaendelea sikuona sababu ya kususa au kukasirika, mimi na jopo langu tumeandika upya na kupeleka tena kwenye Tume tukilidai hilo,”alisema Simba.

Mufti Simba alitoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazowafanya Waislamu kuidai mahakama hiyo kuwa ni kutaka kusimamia haki zao ikiwemo ya kumiliki makaburi ya Waislamu ambayo sasa yanamilikiwa na manispaa.

“Kwa Waislamu kudhuru makaburi ni ibada na hata katika vitabu vya dini imeandikwa, hivyo sisi kama Waislamu, tunataka kutetea haki zetu ,”alisema Simba.

Imeandaliwa na Goodluck Eliona, Kalunde Jamal na Beatrice Moses

source: Mwananchi

Askofu Kulola afariki dunia


Askofu,Dk Moses Kulola 

Dar es Salaam. Vilio, simanzi na maombi ya kunena kwa lugha vilitawala jana katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Temeke Dar es Salaam wakati waumini na ndugu wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Moses Kulola (83) walipopata taarifa za kifo cha kiongozi huyo.

Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile alisema kuwa Askofu Kulola alifariki dunia jana saa tano asubuhi kwenye Hospitali ya Africa Medical Invesment (AMI), Dar es Salaam.

Mwakipesile alisema afya ya Askofu Kulola ilianza kubadilika Mei mwaka huu akiwa mkoani Mwanza ambako alipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando ambako alibainika kuwa na matatizo ya moyo.

“Kanisa liliamua kuchukua jukumu la kumpeleka Hospitali ya Apollo, India kwa matibabu zaidi na baada ya kuona afya yake inatengemaa aliruhusiwa kurejea nchini, lakini Agosti 16, mwaka huu hali ilibadilika ndipo tukampeleka AMI alikofikwa na mauti,” alisema Mwakipesile.

Alisema kifo hicho kimeacha pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibwa kwa sasa. Hata hivyo, wanafarijika kwa upande mwingine wakiamini kwamba Mungu amemchukua mtumishi wake kwa wakati alioukusudia.

Alisema mwili wa Askofu Kulola utasafirishwa kwenda Mwanza Jumamosi jioni kwa ndege baada ya kuagwa kanisani hapo. Atazikwa kwenye Uwanja wa Kanisa la EAGT Bugando.

Askofu Kulola ni mmoja wa viongozi wa dini waliokuwa na jina kubwa nchini na alifanya kazi za utumishi wa kanisa kwa miaka 53 kwa kuhubiri na kuwaombea wenye matatizo mbalimbali.

Mtoto wa kwanza wa askofu huyo, Goodluck Kulola alisema wamejifunza mambo mengi katika maisha ya baba yao, ikiwamo upendo na unyenyekevu ulioongozwa na uchaji Mungu.

“Baba alikuwa ni asiyependa kabisa migogoro ya kidini, kisiasa yaani ikitokea hali ya uvunjifu wa amani wa namna yoyote ile alikuwa anaumia sana. Alipenda watu kwa ujumla ametufundisha upendo.”

Askofu Kulola ameacha mke wake aitwaye Elizabeth, ambaye alibarikiwa kupata naye watoto 10 na wengine wawili wa kuasili. Hata hivyo, watoto watatu walishafariki dunia. Ameacha wajukuu 44 na vitukuu 10.

Askofu Kulola, ambaye alizaliwa 1928, alianza Shule ya Misheni ya Ligsha Sukuma mwaka 1939, baadaye alijiunga na Shule ya Bwiru kabla ya kusomea Usanifu Majengo huko Israel kisha kuanza kazi ya kumtumikia Mungu mwaka 1950.

Alifuzu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Theolojia katika Chuo Kikuu cha California State Christian Marekani.

Aliwahi kutumika kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) mwaka 1966 mpaka 1991 alipoamua kuanzisha Kanisa la EAGT lenye matawi katika nchi za Zambia, Malawi, Burundi na Msumbiji.
Rais Jakaya Kikwete jana alituma salamu za rambirambi kutonana na kifo cha Askofu Kulola.

source: mwananchi

Wednesday, August 28, 2013

Kumbe! Jeuri , kiburi cha Kagame vinatoka kwa wakubwa!


kagame_48210.jpg

Aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton, hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC.

Kwa muda wa miezi takriban minne kumekuwa na maneno ya kejeli kutoka kwa Serikali ya Rwanda na kwa hakika maneno hayo yanatoka mdomoni mwa Rais Paul Kagame na maofisa wa ngazi za juu katika Serikali yake

Kagame amekuwa mbogo baada ya Rais Jakaya Kikwete kumshauri afanye mazungumzo na wapiganaji wa Kihutu waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari nchini mwake mwaka 1994.

Inakadiriwa kuwa Watutsi na Wahutu 800,000 wenye msimamo wa wastani waliuawa wakati huo, ingawa takwimu hizo zina utata, kwani wako wanaodai kuwa nchi hiyo wakati huo ilikuwa na idadi ndogo ya watu ambao idadi hiyo inasemekana ndio waliouawa.

Pia, wapo wale ambao wanaweza kushangaa kwa nini Kagame amekuwa hivyo na kuikosea heshima Tanzania, nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele kupokea wakimbizi wake toka miaka ya 1960 na kwa nini Rais Kikwete alitoa ushauri huo.

Kagame hakupendezwa na ukweli huo kwani kila mara amekuwa akikataa kuwa hana mkono katika mapigano yanayoendeshwa na vikundi vya msituni vinavyoanzishwa nchini DRC kila inapotokea hali kutulia.

Kikwete amekuwa akijua jambo hili kwa muda mrefu kwani amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kipindi cha miaka kumi na amekuwa akihudhuria mikutano ya kutafuta amani ya DRC bila mafanikio kwa sababu kila kikundi kinapoingizwa katika jeshi la DRC na kudai kuwa kimemaliza vita kinazuka kikundi kingine ambacho nacho kinaanzisha mapambano dhidi ya serikali.

Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) alikuwa mkuu wa shughuli za kijeshi za umoja huo kabla hajapanda cheo na kuwa katibu mkuu wa umoja huo, alipotembelea Rwanda baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, msafara wake ulirushiwa nyanya.

Hiyo ilikuwa ni kama kumpa ujumbe kuwa hakuna alichofanya wakati ule Watutsi walipouawa na Wahutu mwaka 1994.

Masikini! Annan angefanya nini wakati alipokuwa akiyaomba mataifa makubwa kuingilia kati ili kusitisha mauaji kila moja lilikuwa likiangalia maslahi yake na ulikuwepo mpango wa uchelewashaji wa makusudi.

Baadaye Annan alipokuwa akigombea Ukatibu Mkuu wa UN ni Rwanda pekee katika nchi za Afrika ndiyo iliyopinga na hata alipokuwa akiomba kuongezewa muda ni nchi hiyo iliyokuwa kinara wa kumpinga wakati ukweli ni kuwa mambo yote yaliyokuwa yakifanyika wakati huo Kagame alikuwa akiyajua.

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, Meja Jenerali Kayumba Nyamwasa, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa uhamishoni Afrika Kusini akithibitisha kuwa vikundi vyote vimekuwa vikianzishwa na Kagame kwa nia ya kuhakikisha kuwa Wahutu na jeshi la zamani la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa linaundwa na waliokuwa vijana wa Inteharamwe hawapati muda wa kujijenga.

Kwa maneno mengine, Kagame ameifanya ardhi ya DRC kama uwanja wa mapambano kati yake na wapinzani wake ambao wako mashariki mwa nchi hiyo.

Jenerali Nyamwasa, ambaye kabla ya kukimbilia Afrika Kusini alikuwa Balozi wa Rwanda nchini India anasema kuwa Kagame ndiye aliyeamrisha kutunguliwa kwa ndege iliyokuwa imebeba ujumbe wa nchi hiyo pamoja na Rais Juvenal Habyarimana na Cyprian Ntyaramira wa Burundi ambao ulikuwa umetokea Tanzania kwenye mkutano wa kujadili amani ya nchi hiyo.

Baada ya vita kumalizika na hatimaye RPF kuchukua uongozi, Ufaransa, mtawala wa zamani wa Rwanda ilimtuhumu Kagame kwa kusababisha mauaji ya kimbari kwani Wahutu wasingianzisha chinja chinja ya Watutsi kwa wakati huo kwani mazungumzo yale yalikuwa yanaelekea ukingoni na hatua ya mwisho ingekuwa kwa RPF kuwa chama cha kisiasa ambacho kingeshiriki kwenye uchaguzi.

Nia ya Kagame ilikuwa ni kuchukua uongozi Rwanda kwa nguvu kwa sababu kwa mizania ya siasa za nchi hiyo ambazo zimejikita zaidi kwenye ukabila ingekuwa vigumu kwa Watutsi walio wachache kushinda.

Sababu ya pili ambayo ndiyo iliyowafanya RPF wakatae au watumie nguvu ilikuwa ni juhudi ya Marekani ambayo ilikuwa mfadhili mkuu wa RPF kuhakikisha kuwa ushawishi wa Ufaransa katika eneo la Maziwa Makuu unaondoshwa kwa gharama yoyote.
Hii inathibitishwa katika kitabu Global Intelligence; the world's secret services today ambacho kimeandikwa na waliberali, Paul Todd na Jonathan Bloch.

Waandishi hao wanabainisha kuwa wakati huo kulikuwa na vita vya kijasusi baina ya Marekakani na Ufaransa ambavyo baadaye vilibadilika na kuwa ni vita vya kijeshi.

Kagame alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda kabla ya kujiunga na RPF.
Ufaransa ikimsaidia Habyrimana na Marekani ikiwasaidia RPF ambao tayari walikuwa wakisaidiwa na Uganda walijipatia taarifa za kijasusi kutoka kwa Serikali ya Rwanda na wapiganaji wake.

Majasusi wa Marekani ambao walikuwa wakitumia njia za kijasusi za siri za kunasa taarifa za mawasiliano katika eneo la Afrika Mashariki walifanikisha mipango ya RPF katika uwanja wa mapambano.

Marekani ilikiri kuwa kuanzia 1994 ilikuwa ikiwasaidia RPF kwa kuwapatia silaha na Kagame alipewa simu ya satelaiti aina ya Motorola INMARSAT ambayo licha ya kufungwa kitaalam (encryption) ili mawasiliano yake yasinaswe na wapiganaji wa Serikali ya Rwanda au yeyote yule, kwa bahati mbaya shirika la Ujasusi la Kimataifa la Ufaransa, DGSE (Direction Generale de la Securite Exteriure) lilifanikiwa kunasa mawasiliano yale na Ufaransa iliituhumu Marekani kwa kutoa kombora lililoiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana.

Kwa maana nyingine, ni kuwa Kagame hawezi kukwepa mkono wa sheria wakati utakapofika kwani taarifa muhimu za namna mambo yalivyokuwa yakienda katika uwanja wa mapambano, mawasiliano yake yamehifadhiwa na taasisi hiyo ya kijasusi ya Ufaransa.

Waandishi hao wamebainisha kuwa kwa kuwa Rais Mobutu Seseseko wa Zaire (sasa DRC) alikuwa akimsaidia Jonas Savimbi ambaye Wamarekani walikuwa wameishamchoka na walimtaka aache vita ili utulivu urejee Angola, nao wavune madini na mafuta huko wakiwa na sababu ya kumwondoa Mobutu madarakani ili kukata mizizi ya usaidizi aliokuwa akiupata Savimbi, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa UNITA, iliyokuwa ikipigana vita vya msituni dhidi ya Serikali ya Angola chini ya MPLA.

Sababu nyingine ilikuwa kwa Mobutu kuwasaidia Wahutu ambao walikuwa kipenzi cha Ufaransa ilibidi aondolewe ili kuhakikisha kuwa Wamarekani wanalishika na kulidhibiti eneo lote la Maziwa Makuu.

Ikumbukwe kuwa wakati huo Rais Bill Clinton ambaye hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC, ndiye aliyekuwamadarakani wakati huo na alifanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa shughuli za kijasusi zinaendeshwa katika mtindo ambao utakuwa na manufaa zaidi kiuchumi na siyo kisiasa kama ilivyokuwa wakati wa vita baridi.

DRC ilikuwa muhimu kwa majasusi wa Marekani, hasa kwa uzarishaji wa madini ya coltan ambayo hutumika kutengenezea simu za mkononi, madini hayo hayapo sehemu nyingine yoyote duniani zaidi ya DRC.

Clinton alihakikisha kuwa anafanya kila awezalo kuondoa ushawishi wa Ufaransa nchini Sudan kwa kuwataka viongozi wa SPLA wakati huo, Kanali John Garang na wengine wadai uhuru kamili na siyo utawala wa shirikisho kutoka Sudan ili mradi Ufaransa ikose mafuta yaliyokuwa yakichimbwa kutoka Sudan Kusini.

Waandishi hao wamebainisha kuwa Marekani ilitoa dola 100 milioni ili kumsaidia Laurent Kabila kuanzisha jeshi la watoto waliokuwa wakijulikana kama Kadogoo wakiwa na malengo ya kumwondoa Mobutu.

Kufikia mwaka 1997, Shirika la Kijasusi la Marekani (NSA) lilikuwa imejenga vituo vya kuendesha shughuli za kijasusi ili kunasa taarifa za mawasiliano kupitia simu, nukushi, redio katika sehemu mbalimbali za eneo la Maziwa Makuu kama vile, Fort Portal nchini Uganda, Kigali Rwanda na Kongo Brazaville.

Ufaransa ambayo ilikasirishwa na jinsi Marekani ilivyofanikisha kuwaondoa vibaraka wake katika DRC na Rwanda ilihakikisha kuwa inawaandaa wanajeshi ambao walimpindua Rais Pascal Lissouba wa Congo Brazaville ambaye alikuwa ni kipenzi cha Marekani.

Chanzo:Mwananchi

Saturday, August 24, 2013

Kikwete azindua baraza la ‘vigogo’


 


Dodoma. Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete jana alizindua Baraza la Ushauri linalounda na wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu na baadaye baraza hilo likamchagua Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuwa mwenyekiti wake wa kwanza huku katibu wake akiwa Pius Msekwa.

Katika hafla ya uzinduzi wa baraza hilo, iliyohudhuriwa na wazee hao isipokuwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour kwa sababu za kiafya, Rais Kikwete aliwamwagia sifa marais wastaafu, Mwinyi na Benjamin Mkapa kuwa ni sawa na kamusi ya mageuzi makubwa yaliyotokea nchini nyakati uongozi wao.

Kuhusu Mwinyi, Kikwete alisema ni mwasisi wa mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa kuwa aliwezesha taifa kuondoka katika uchumi wa dola kuingia uchumi soko, huku Mkapa akipokea mabadiliko hayo na kuyaendeleza katika mfumo wa vyama vingi.

Baada ya uzinduzi huo, wazee hao walikaa kwenye kikao chao cha kwanza kujadili “mambo ambayo wangeona yanafaa”, ambako waliwachagua Mwinyi na Msekwa kuwaongoza.

Waliohudhuria uzinduzi huo ni Mkapa, Mwinyi, Msekwa, John Malecela na Amani Abeid Karume.

Baraza hilo tayari linatambuliwa ndani ya Katiba ya CCM, lilitokana na mapendekeo ya Kamati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama iliyoundwa mwaka 2011.

kwa lengo la kushauri namna ya kufanya mageuzi mbalimbali ndani ya chama.

Rais Kikwete alisema wao ndani ya chama , hawana hofu ya kuwatumia wazee hao kwa njia hiyo kwa kuwa itakuwa njia mwafaka ya kutoa ushuri wao kwa namna watakavyoona inafaa.

Alipuuza madai kwamba wazee hao wanaondolewa kwenye vikao vya uamuzi, akisema mbali na mapendekezo ya Kamati ya Mukama, pia wazee hao walikuwa wanachoka kuitwa mara kwa mara kwenye vikao.

“Tumekuwa tukiwaita kwenye vikao vyetu na wao wanahoji, ’kwanini mnatusumbua nyinyi hamuwezi kuamua wenyewe, wanasema kama kuna jambo la muhimu sana…wanasema ‘sisi tumeshatimiza wajibu wetu na nyingi timizeni wajibu wenu,” alisema.

Alisema hata kwenye vikao, wastaafu hao walikuwa wanaona taabu kuzungumza kwa kuhisi kuwa wangeweza kuonekana wanamwingilia mwenyekiti, jambo ambalo halitakuwapo wakiwa peke yao, kwa kuwa watakaa na kuamua nini cha kushauri na namna ya kushauri.

source: mwananchi

YANGA YAUA, SIMBA, AZAM ZACHECHEMEA



YANGA leo imeanza ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibamiza Ashanti mabao 5-1 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Jerry Tegete aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matano. Mabao mengine yalifungwa na Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Nizar Khalfan wakati bao la kujifariji la Ashanti lilifungwa na Shabani Juma.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simba ilibanwa mbavu na wenyeji Rhino Rangers baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2.

Mabao yote mawili ya Simba yalifungwa na kiungo mchacharikaji, Jonas Mkude wakati mabao ya Rhino Rangers yalifungwa na Iman Niel na Saad Kipanga.

Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Mtibwa ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Juma Luizio dakika ya nne kabla ya Aggrey Morris kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 19.

JKT Mgambo ilishindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKT Ruvu, Coastal Union iliichapa JKT Oljoro mabao 2-0 mjini Arusha, Mbeya City ilitoka suluhu na Kagera Sugar mjini Mbeya, Prisons ilipokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Ruvu Shooting
 
source: liwazo zitto blog

Ushindi wa Mugabe: Heri mtawala kikongwe kuliko kibaraka




MASIKINI Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, anaongoza taifa tajiri katikati ya miba na joto kali. Ni nani atamwonea wivu kwa zawadi pekee ya kuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe huru?

Fikiria utata katili unaomkabili, dunia ya nchi za Magharibi imemkaba koo kwa sababu tu ya kutenda dhambi kuu ya kisiasa ya kushusha bendera ya Uingereza – “Union Jack” nchini Zimbabwe na kuwaamuru walowezi weupe kwa yeye kutii na kuheshimu matakwa ya wazalendo walio wengi, na kuendelea kuvunjilia mbali mfumo hasi na usio wa haki wa umilikaji wa ardhi miaka 13 iliyopita.

Kuanzia hapo, alianza kuondoa taratibu upendeleo, ulafi na maslahi ya wazungu wachache waliojiona mabwana zaidi kuliko wazalendo. Hatua hiyo ilisababisha walowezi mamluki kuondoka kwa wingi Zimbabwe na wale wenye nia njema kwa Zimbabwe na Wazimbabwe walibakia. Kwa hili, nchi za Ulaya na Marekani zilimwita mtawala dikteta na adui wa demokrasia na hivyo kuiwekea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi. Nasi baadhi ya Waafrika, kwa ujinga wetu na umamluki, tukaitika mwangwi huo kwa kumwona vivyo hivyo.

Robert Mugabe

Mugabe, kwa kukerwa na uzandiki huu wa nchi za Magharibi, hususan Uingereza, alijitoa kwenye Umoja wa Jumuiya ya Madola inayoongozwa na Malkia wa Uingereza akiita kuendelea kuwa mwanachama ni upuuzi na utumwa mambo leo.

Katika uchaguzi wa hivi karibuni, Mugabe, mwenye umri wa miaka 89, amepata ridhaa nyingine ya wananchi wake kuiongoza Zimbabwe. Mwangwi umesikika tena kutoka nchi za Magharibi, nasi kwa ujinga wetu tumedakia kwamba, Mugabe, kwa vigezo vya Magharibi ni dikteta na kikongwe asiyefaa kuongoza taifa enzi hizi za “dotikomu”.

Lakini mbona hatuwaulizi wazandiki hawa waseme; kati ya Mugabe na Malkia Elizabeth wa Uingereza, ni nani mzee aliyetawala muda mrefu kuliko mwenzake?  Mbona dunia haimshutumu Malkia huyo kwa kukaa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, ambao ni muda mrefu kuliko mtawala yeyote duniani?

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, Umoja wa Ulaya (EU) hususan Uingereza na Marekani, zimekuwa mstari wa mbele kumhujumu Mugabe na Serikali ya Zimbabwe tangu mwaka 2000 pale Mugabe alipotaifisha ardhi na mashamba ya wazungu wachache na kuwagawia wazalendo walio wengi badala ya wazalendo hao kuendelea kuwa manamba katika mashamba ya walowezi.

Ni kweli kwamba, baada ya hatua hiyo, uchumi wa Zimbabwe umetetereka, lakini si kwa sababu ya sera za Mugabe zenye kujali wanyonge, bali ni kutokana na uhasama wa kizandiki wa nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo kufikia hatua ya kuitenga na kuinyima ushirikiano kimataifa.

Kwa wanaoielewa vyema historia ya Uhuru wa Zimbabwe, watanielewa ninapotumia neno “uzandiki” wa nchi za Magharibi. Na kwa wale miongoni mwetu wanaomshutumu Mugabe kwa hilo, bora wakaacha kujidhalilisha kwa kujifanya kenge kwenye msafara wa mamba, msafara wasioujua wala kuwahusu.

Uzandiki wa Uingereza unaanzia Novemba 11, 1965, wakati huo huo Rhodesia (baadaye Zimbabwe) ikiwa koloni la Uingereza; ilipomruhusu mlowezi wa Kiingereza na haini, Ian Smith, kujitangazia uhuru kwa mabavu (Unilateral Declaration of Independence) – UDI, kuwa mtawala wa Rhodesia. Kufuatia hatua hiyo, mwaka 1969, wazalendo wa Zimbabwe walianzisha vita vya msituni vya ukombozi (Chimrenga) kuung’oa utawala huo wa kidhalimu.

Na pale vita vya ukombozi dhidi ya Smith vilipopamba moto kufikia hatua ya kuung’oa utawala wake, mlowezi huyo alibadili mbinu kutaka kukabidhi Uhuru bandia kwa vibaraka wa Kiafrika, Askofu Abel Muzorewa na Chifu Jeremiah Chirau, na kuibatiza nchi kuitwa “Zimbabwe – Rhodesia”.  Kama isingekuwa Mwalimu Julius Nyerere kumkabili ana kwa ana na kwa hoja pevu, Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Magareth Thatcher, Uingereza ilikuwa karibu kumtambua Askofu Muzorewa kama Waziri Mkuu wa Zimbabwe – Rhodesia “huru”.

Na katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Julai 1979, Mwalimu, kwa mara nyingine alipambana na Thatcher kikamilifu na kufanikisha kuundwa kwa kamati maalumu iliyoandaa mapendekezo ya Katiba ya Zimbabwe chini ya Mwalimu Nyerere mwenyewe.  Mapendekezo hayo ndiyo yaliyofanikisha kutungwa kwa Katiba ya Zimbabwe ambayo ilitoa uzito mkubwa na wa pekee kwa suala la ardhi.

Mwaka huo huo, mazungumzo juu ya Uhuru wa Zimbabwe yalifanyika huko Lancaster House, Uingereza kwa majuma 14 na kuwa mazungumzo marefu ya pekee katika historia ya mazungumzo kama hayo kwa nchi huru za Afrika. Hapo, suala la Ardhi lilikuwa zito kuliko yote kuwafanya wazalendo, Robert Mugabe na Joshua Nkomo, kusitisha mazungumzo mara mbili kuja Dar es Salaam kupata ushauri wa Mwalimu Nyerere.

Na ilipobainika kwamba suala hilo lilikuwa gumu kuweza kupata ufumbuzi kwa mashauriano pekee, Mwalimu alimteua na kumtuma aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania wa wakati huo, Joseph Sinde Warioba (ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini), kwenda Uingereza kuhudhuria mkutano huo ili kuokoa jahazi kwa upande wa Zimbabwe.

Baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa, ni pamoja na Serikali ya Uingereza kuwalipa fidia katika kipindi cha miaka 20 (kufikia mwaka 2000), walowezi waliokuwa wakimiliki ardhi ili hatimaye ardhi hiyo irejeshwe serikalini kuwezesha kugawiwa bure kwa Wazalendo.

Hii ilikuwa agenda nzito na tete kwa Waingereza na kwa wazalendo pia, kwani kutofanya hivyo kungekaribisha vita nyingine kwa wazalendo kurejea msituni kuendeleza mapambano waweze kunyakua ardhi kutoka kwa walowezi hao.

Kwa upande wa pili, ilikuwa simanzi kwa wazungu kuachia ardhi waliyomiliki kwa karibu karne nzima, na hawakuwa na pa kwenda.
Kwa kuwa vita ilionekana kuwa na madhara zaidi kwa wazungu na kwa Serikali ya Uingereza pia, serikali hiyo ilichagua kukubali kulipa fidia kwa walowezi kuepuka mapambano ya silaha kwa mara nyingine. Makubaliano mengine yalikuwa ni kutenga viti 20 vya Bunge kwa wazungu, kwenye Bunge lenye viti 100 katika kipindi cha mpito cha miaka mitano hadi mwaka 1985.

Kati ya makubaliano hayo mawili, ni hili la viti 20 vya Bunge tu ndilo lililotekelezwa; na hilo la kulipa fidia lilipuuzwa na Serikali ya Thatcher hadi alipong’atuka madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Mkuu John Major wa Chama cha Conservative, ambaye naye alishindwa baadaye na Tony Blair wa Chama cha Labour.

Blair alikataa kulipa fidia licha ya kukumbushwa mara nyingi na Mugabe juu ya kutimiza ahadi hiyo.

Robert Mugabe, baada ya kubaini uhuni huo wa Serikali ya Uingereza, hakuwa na subira tena, hivi kwamba miaka 20 ya makubaliano ilipotimia mwaka 2000, alianza kuwapokonya walowezi ardhi na mashamba na kuzua mtafaruku miongoni mwa nchi za Ulaya, hususan, Uingereza, ikiungwa mkono na shoga yake, Marekani.

Baadhi ya hatua nchi hizo zilizochukua dhidi ya Zimbabwe ni pamoja na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na safari za Mugabe kwenda nchi hizo kuzuiwa au kudhibitiwa.

Hatua nyingine ya kipuuzi iliyochukuliwa dhidi ya Mugabe, ni kuvuliwa baadhi ya shahada (Mugabe ana shahada saba) alizopata kutoka nchi hizo, kana kwamba kufanya hivyo kungempunguzia akili, maarifa na uwezo wa kufikiri.

Ili kuhakikisha Mugabe anaondolewa madarakani kwa njia ya sanduku la kura na wapinzani, mwaka 2000, wazungu walianzisha harambee ya kuchanga fedha, ndani na nje ya Zimbabwe kuanzisha Chama cha upinzani cha “Movement for Democratic Change” (MDC), na kumpachika uongozi wa Chama kibaraka wao, Morgan Tsvangarai, mbumbumbu mwenye elimu ya darasa la nne na ambaye alikuwa mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi nchini Zimbabwe kupambana na Mugabe kwenye chaguzi.

 Morgan Tsvangarai


Huku kikipewa nguvu na misaada lukuki na walowezi, MDC kilipanda chati haraka haraka na kujidhihirisha kuwa chama kikuu cha upinzani dhidi ya ZANU – PF cha Mugabe. Pamoja na kuwa hivyo, MDC hakijaweza kukitikisa ZANU – PF chenye mizizi sehemu za vijijini ambako wazalendo wanyonge hawajasahau fadhila ya Mugabe kwao kwa  kuwapatia ardhi na huduma zingine muhimu za kijamii.

Lengo la MDC ni kuhakikisha walowezi wanarudishiwa ardhi na mashamba yao yaliyotaifishwa kikitwaa madaraka. Ni dhambi kuu hii ya MDC inayomfanya Mugabe asing’atuke madarakani kuruhusu kwa kile ambacho amekuwa akirudia kulaani, “nchi kwenda kwa mbwa”.

Mugabe amesema mara nyingi kuwa yuko radhi kukabidhi madaraka kwa mzalendo mwingine yoyote, lakini “si kwa huyu (Tsvangarai) kibaraka wa wazungu”. Amehoji, kwa nini wazalendo waendelee kukosa ardhi ya kulima ndani ya Zimbabwe yao huru? Amekejeli kwa kusema, wanaohoji ushindi na uongozi wake wajinyonge.

Dunia ya wapenda haki, tukiwemo sisi “Wabongo”, inapaswa kumuunga mkono Rais Mugabe, Rais pekee barani Afrika aliyebakia, anayeweza kuyaambia Mataifa makubwa “shut up” – “nyamaza” na yakatikisika yasimfanye kitu. Watawala dhaifu wanaokosana na mataifa hayo, mara nyingi wamepinduliwa kwa nguvu ya mataifa hayo, kwa sababu hawana msingi au uungwaji mkono wa watu wao; lakini si kwa Mugabe.

Mugabe ni kikongwe wa miaka 89 mwenye kujali maslahi ya taifa la Zimbabwe na wananchi wake. Amekataa kuwa mateka wa ukoloni mambo leo na ubeberu wa mataifa makubwa. Kwa upande wa pili, Morgan Tsvangarai, mwenye umri wa miaka 61 ni wa damu mpya, lakini ni mateka wa ukoloni mamboleo, ubeberu na ufisadi wa kimataifa kuweza kuuza nchi na wananchi wake kwa nyang’au hao.

Kama uongozi ni tunu kwa taifa, heri kuongozwa na mzee kama Mugabe kuliko kuongozwa na kijana msaliti kama Tsvangarai. Na hili liwe somo la kutosha kwa Watanzania wakati huu wa kinyang’anyiro cha kumpata Rais ajaye mwaka 2015.

Si hivyo tu, suala la ardhi na rasilimali za taifa nchini Zimbabwe liwe funzo kwetu.  Wakati Mugabe anatengeneza historia chanya kwa kurejesha ardhi iliyoporwa na wageni mikononi mwa wazalendo, sisi, kwa ujinga tunakabidhi ardhi kwa wageni kwa kisingizio cha uwekezaji ili kukaribisha usetla utakaowageuza wananchi kuwa manamba katika nchi yao huru.

Wakati Wazimbabwe wanawapiga mieleka wagombea urais vijana mafisadi, vibaraka na wauza nchi, na kuchagua wazee wenye hekima na busara kuongoza nchi; sisi kwa ujinga, tunabeza hekima, busara na uadilifu katika uongozi kwa kutekwa na ubeberu wa mitaji, umamluki na usaliti kwa taifa.

Niambieni, kama leo Mwalimu angefufuka na kusimama kugombea urais, nani angethubutu kujilinganisha naye na kutoa changamoto bila kujiaibisha? Je, Mwalimu ni kijana?

Niambieni, kama Edward Moringe Sokoine angefufuka leo na kugombea urais, nani kati ya hawa wa enzi za “dotikomu” angejilinganisha naye kutaka kugombea bila kuanguka kabla ya kusimama?

Kwa jinsi ambavyo imekuwa rahisi kwa mataifa ya kibeberu kushinikiza na kuamuru hatima yetu kisiasa na kiuchumi kupitia viongozi mamluki, ndiyo kunakofanya uhuru wetu kuwa kichekesho. Lakini si kwa kiongozi kama Rais Mugabe ambaye daima amesimama kutetea uhuru wa nchi yake.

Na kwa udhaifu huu wa viongozi, tumegeuka kichekesho na jamvi la wageni; tunalilia umoja, lakini tunatenda kwa utengano; tunalilia uhuru kama taifa, lakini tunajenga utegemezi kwa mataifa ya kibeberu.

Tunapenda kuona ustawi wetu na wa taifa, lakini tunatumikia umasikini wa kujitakia. Tumegeuka taifa la ombaomba katikati ya utajiri tulioruhusu kuporwa chini ya sera za uwekezaji usiojali. Lakini si kwa kiongozi kama Rais Mugabe, aliyeweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi kwa wageni.

Wakulima na wafanyakazi wetu wanagharimia uzandiki huu kwa jasho na machozi kuneemesha tabaka la watawala wasiotaka kuona ukweli wa maisha duni ya wanyonge hao. Tabaka hili la watawala limepofuka kwa hofu, hofu ya kuwaogopa watu wao wenye njaa, wenye kuvaa matambara na umma unaofupika umri wa kuishi kwa umasikini, kwamba siku moja watasema “imetosha” na kutenda yasiyotarajiwa.

Haya yote hayaonekani machoni, wala kusikika masikioni mwa viongozi wenye ukwasi wa kupora, kwa sababu wamehakikishiwa “usalama” na dunia ya ubeberu wa mitaji kuwa, “msihofu enyi kundi dogo, kwa kuwa baba yenu (ubeberu) amekwishawapa ule ufalme wa ulaji”.

Kwa kundi hili na mabwana zao, kiongozi kama Rais Robert Mugabe, mwenye kusimamia na kutetea maslahi ya nchi na wananchi wake ni “gaidi”. Na kwa nini tumekubali kutunga sheria ya ugaidi hapa kwetu bila kutafiti mantiki yake na hatima ya uhuru wetu, chini ya sheria hii ya kibabe?

source://www.raiamwema.co.tz: Joseph Mihangwa