WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, August 24, 2013

Ushindi wa Mugabe: Heri mtawala kikongwe kuliko kibaraka
MASIKINI Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, anaongoza taifa tajiri katikati ya miba na joto kali. Ni nani atamwonea wivu kwa zawadi pekee ya kuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe huru?

Fikiria utata katili unaomkabili, dunia ya nchi za Magharibi imemkaba koo kwa sababu tu ya kutenda dhambi kuu ya kisiasa ya kushusha bendera ya Uingereza – “Union Jack” nchini Zimbabwe na kuwaamuru walowezi weupe kwa yeye kutii na kuheshimu matakwa ya wazalendo walio wengi, na kuendelea kuvunjilia mbali mfumo hasi na usio wa haki wa umilikaji wa ardhi miaka 13 iliyopita.

Kuanzia hapo, alianza kuondoa taratibu upendeleo, ulafi na maslahi ya wazungu wachache waliojiona mabwana zaidi kuliko wazalendo. Hatua hiyo ilisababisha walowezi mamluki kuondoka kwa wingi Zimbabwe na wale wenye nia njema kwa Zimbabwe na Wazimbabwe walibakia. Kwa hili, nchi za Ulaya na Marekani zilimwita mtawala dikteta na adui wa demokrasia na hivyo kuiwekea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi. Nasi baadhi ya Waafrika, kwa ujinga wetu na umamluki, tukaitika mwangwi huo kwa kumwona vivyo hivyo.

Robert Mugabe

Mugabe, kwa kukerwa na uzandiki huu wa nchi za Magharibi, hususan Uingereza, alijitoa kwenye Umoja wa Jumuiya ya Madola inayoongozwa na Malkia wa Uingereza akiita kuendelea kuwa mwanachama ni upuuzi na utumwa mambo leo.

Katika uchaguzi wa hivi karibuni, Mugabe, mwenye umri wa miaka 89, amepata ridhaa nyingine ya wananchi wake kuiongoza Zimbabwe. Mwangwi umesikika tena kutoka nchi za Magharibi, nasi kwa ujinga wetu tumedakia kwamba, Mugabe, kwa vigezo vya Magharibi ni dikteta na kikongwe asiyefaa kuongoza taifa enzi hizi za “dotikomu”.

Lakini mbona hatuwaulizi wazandiki hawa waseme; kati ya Mugabe na Malkia Elizabeth wa Uingereza, ni nani mzee aliyetawala muda mrefu kuliko mwenzake?  Mbona dunia haimshutumu Malkia huyo kwa kukaa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, ambao ni muda mrefu kuliko mtawala yeyote duniani?

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, Umoja wa Ulaya (EU) hususan Uingereza na Marekani, zimekuwa mstari wa mbele kumhujumu Mugabe na Serikali ya Zimbabwe tangu mwaka 2000 pale Mugabe alipotaifisha ardhi na mashamba ya wazungu wachache na kuwagawia wazalendo walio wengi badala ya wazalendo hao kuendelea kuwa manamba katika mashamba ya walowezi.

Ni kweli kwamba, baada ya hatua hiyo, uchumi wa Zimbabwe umetetereka, lakini si kwa sababu ya sera za Mugabe zenye kujali wanyonge, bali ni kutokana na uhasama wa kizandiki wa nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo kufikia hatua ya kuitenga na kuinyima ushirikiano kimataifa.

Kwa wanaoielewa vyema historia ya Uhuru wa Zimbabwe, watanielewa ninapotumia neno “uzandiki” wa nchi za Magharibi. Na kwa wale miongoni mwetu wanaomshutumu Mugabe kwa hilo, bora wakaacha kujidhalilisha kwa kujifanya kenge kwenye msafara wa mamba, msafara wasioujua wala kuwahusu.

Uzandiki wa Uingereza unaanzia Novemba 11, 1965, wakati huo huo Rhodesia (baadaye Zimbabwe) ikiwa koloni la Uingereza; ilipomruhusu mlowezi wa Kiingereza na haini, Ian Smith, kujitangazia uhuru kwa mabavu (Unilateral Declaration of Independence) – UDI, kuwa mtawala wa Rhodesia. Kufuatia hatua hiyo, mwaka 1969, wazalendo wa Zimbabwe walianzisha vita vya msituni vya ukombozi (Chimrenga) kuung’oa utawala huo wa kidhalimu.

Na pale vita vya ukombozi dhidi ya Smith vilipopamba moto kufikia hatua ya kuung’oa utawala wake, mlowezi huyo alibadili mbinu kutaka kukabidhi Uhuru bandia kwa vibaraka wa Kiafrika, Askofu Abel Muzorewa na Chifu Jeremiah Chirau, na kuibatiza nchi kuitwa “Zimbabwe – Rhodesia”.  Kama isingekuwa Mwalimu Julius Nyerere kumkabili ana kwa ana na kwa hoja pevu, Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Magareth Thatcher, Uingereza ilikuwa karibu kumtambua Askofu Muzorewa kama Waziri Mkuu wa Zimbabwe – Rhodesia “huru”.

Na katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Julai 1979, Mwalimu, kwa mara nyingine alipambana na Thatcher kikamilifu na kufanikisha kuundwa kwa kamati maalumu iliyoandaa mapendekezo ya Katiba ya Zimbabwe chini ya Mwalimu Nyerere mwenyewe.  Mapendekezo hayo ndiyo yaliyofanikisha kutungwa kwa Katiba ya Zimbabwe ambayo ilitoa uzito mkubwa na wa pekee kwa suala la ardhi.

Mwaka huo huo, mazungumzo juu ya Uhuru wa Zimbabwe yalifanyika huko Lancaster House, Uingereza kwa majuma 14 na kuwa mazungumzo marefu ya pekee katika historia ya mazungumzo kama hayo kwa nchi huru za Afrika. Hapo, suala la Ardhi lilikuwa zito kuliko yote kuwafanya wazalendo, Robert Mugabe na Joshua Nkomo, kusitisha mazungumzo mara mbili kuja Dar es Salaam kupata ushauri wa Mwalimu Nyerere.

Na ilipobainika kwamba suala hilo lilikuwa gumu kuweza kupata ufumbuzi kwa mashauriano pekee, Mwalimu alimteua na kumtuma aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania wa wakati huo, Joseph Sinde Warioba (ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini), kwenda Uingereza kuhudhuria mkutano huo ili kuokoa jahazi kwa upande wa Zimbabwe.

Baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa, ni pamoja na Serikali ya Uingereza kuwalipa fidia katika kipindi cha miaka 20 (kufikia mwaka 2000), walowezi waliokuwa wakimiliki ardhi ili hatimaye ardhi hiyo irejeshwe serikalini kuwezesha kugawiwa bure kwa Wazalendo.

Hii ilikuwa agenda nzito na tete kwa Waingereza na kwa wazalendo pia, kwani kutofanya hivyo kungekaribisha vita nyingine kwa wazalendo kurejea msituni kuendeleza mapambano waweze kunyakua ardhi kutoka kwa walowezi hao.

Kwa upande wa pili, ilikuwa simanzi kwa wazungu kuachia ardhi waliyomiliki kwa karibu karne nzima, na hawakuwa na pa kwenda.
Kwa kuwa vita ilionekana kuwa na madhara zaidi kwa wazungu na kwa Serikali ya Uingereza pia, serikali hiyo ilichagua kukubali kulipa fidia kwa walowezi kuepuka mapambano ya silaha kwa mara nyingine. Makubaliano mengine yalikuwa ni kutenga viti 20 vya Bunge kwa wazungu, kwenye Bunge lenye viti 100 katika kipindi cha mpito cha miaka mitano hadi mwaka 1985.

Kati ya makubaliano hayo mawili, ni hili la viti 20 vya Bunge tu ndilo lililotekelezwa; na hilo la kulipa fidia lilipuuzwa na Serikali ya Thatcher hadi alipong’atuka madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Mkuu John Major wa Chama cha Conservative, ambaye naye alishindwa baadaye na Tony Blair wa Chama cha Labour.

Blair alikataa kulipa fidia licha ya kukumbushwa mara nyingi na Mugabe juu ya kutimiza ahadi hiyo.

Robert Mugabe, baada ya kubaini uhuni huo wa Serikali ya Uingereza, hakuwa na subira tena, hivi kwamba miaka 20 ya makubaliano ilipotimia mwaka 2000, alianza kuwapokonya walowezi ardhi na mashamba na kuzua mtafaruku miongoni mwa nchi za Ulaya, hususan, Uingereza, ikiungwa mkono na shoga yake, Marekani.

Baadhi ya hatua nchi hizo zilizochukua dhidi ya Zimbabwe ni pamoja na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na safari za Mugabe kwenda nchi hizo kuzuiwa au kudhibitiwa.

Hatua nyingine ya kipuuzi iliyochukuliwa dhidi ya Mugabe, ni kuvuliwa baadhi ya shahada (Mugabe ana shahada saba) alizopata kutoka nchi hizo, kana kwamba kufanya hivyo kungempunguzia akili, maarifa na uwezo wa kufikiri.

Ili kuhakikisha Mugabe anaondolewa madarakani kwa njia ya sanduku la kura na wapinzani, mwaka 2000, wazungu walianzisha harambee ya kuchanga fedha, ndani na nje ya Zimbabwe kuanzisha Chama cha upinzani cha “Movement for Democratic Change” (MDC), na kumpachika uongozi wa Chama kibaraka wao, Morgan Tsvangarai, mbumbumbu mwenye elimu ya darasa la nne na ambaye alikuwa mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi nchini Zimbabwe kupambana na Mugabe kwenye chaguzi.

 Morgan Tsvangarai


Huku kikipewa nguvu na misaada lukuki na walowezi, MDC kilipanda chati haraka haraka na kujidhihirisha kuwa chama kikuu cha upinzani dhidi ya ZANU – PF cha Mugabe. Pamoja na kuwa hivyo, MDC hakijaweza kukitikisa ZANU – PF chenye mizizi sehemu za vijijini ambako wazalendo wanyonge hawajasahau fadhila ya Mugabe kwao kwa  kuwapatia ardhi na huduma zingine muhimu za kijamii.

Lengo la MDC ni kuhakikisha walowezi wanarudishiwa ardhi na mashamba yao yaliyotaifishwa kikitwaa madaraka. Ni dhambi kuu hii ya MDC inayomfanya Mugabe asing’atuke madarakani kuruhusu kwa kile ambacho amekuwa akirudia kulaani, “nchi kwenda kwa mbwa”.

Mugabe amesema mara nyingi kuwa yuko radhi kukabidhi madaraka kwa mzalendo mwingine yoyote, lakini “si kwa huyu (Tsvangarai) kibaraka wa wazungu”. Amehoji, kwa nini wazalendo waendelee kukosa ardhi ya kulima ndani ya Zimbabwe yao huru? Amekejeli kwa kusema, wanaohoji ushindi na uongozi wake wajinyonge.

Dunia ya wapenda haki, tukiwemo sisi “Wabongo”, inapaswa kumuunga mkono Rais Mugabe, Rais pekee barani Afrika aliyebakia, anayeweza kuyaambia Mataifa makubwa “shut up” – “nyamaza” na yakatikisika yasimfanye kitu. Watawala dhaifu wanaokosana na mataifa hayo, mara nyingi wamepinduliwa kwa nguvu ya mataifa hayo, kwa sababu hawana msingi au uungwaji mkono wa watu wao; lakini si kwa Mugabe.

Mugabe ni kikongwe wa miaka 89 mwenye kujali maslahi ya taifa la Zimbabwe na wananchi wake. Amekataa kuwa mateka wa ukoloni mambo leo na ubeberu wa mataifa makubwa. Kwa upande wa pili, Morgan Tsvangarai, mwenye umri wa miaka 61 ni wa damu mpya, lakini ni mateka wa ukoloni mamboleo, ubeberu na ufisadi wa kimataifa kuweza kuuza nchi na wananchi wake kwa nyang’au hao.

Kama uongozi ni tunu kwa taifa, heri kuongozwa na mzee kama Mugabe kuliko kuongozwa na kijana msaliti kama Tsvangarai. Na hili liwe somo la kutosha kwa Watanzania wakati huu wa kinyang’anyiro cha kumpata Rais ajaye mwaka 2015.

Si hivyo tu, suala la ardhi na rasilimali za taifa nchini Zimbabwe liwe funzo kwetu.  Wakati Mugabe anatengeneza historia chanya kwa kurejesha ardhi iliyoporwa na wageni mikononi mwa wazalendo, sisi, kwa ujinga tunakabidhi ardhi kwa wageni kwa kisingizio cha uwekezaji ili kukaribisha usetla utakaowageuza wananchi kuwa manamba katika nchi yao huru.

Wakati Wazimbabwe wanawapiga mieleka wagombea urais vijana mafisadi, vibaraka na wauza nchi, na kuchagua wazee wenye hekima na busara kuongoza nchi; sisi kwa ujinga, tunabeza hekima, busara na uadilifu katika uongozi kwa kutekwa na ubeberu wa mitaji, umamluki na usaliti kwa taifa.

Niambieni, kama leo Mwalimu angefufuka na kusimama kugombea urais, nani angethubutu kujilinganisha naye na kutoa changamoto bila kujiaibisha? Je, Mwalimu ni kijana?

Niambieni, kama Edward Moringe Sokoine angefufuka leo na kugombea urais, nani kati ya hawa wa enzi za “dotikomu” angejilinganisha naye kutaka kugombea bila kuanguka kabla ya kusimama?

Kwa jinsi ambavyo imekuwa rahisi kwa mataifa ya kibeberu kushinikiza na kuamuru hatima yetu kisiasa na kiuchumi kupitia viongozi mamluki, ndiyo kunakofanya uhuru wetu kuwa kichekesho. Lakini si kwa kiongozi kama Rais Mugabe ambaye daima amesimama kutetea uhuru wa nchi yake.

Na kwa udhaifu huu wa viongozi, tumegeuka kichekesho na jamvi la wageni; tunalilia umoja, lakini tunatenda kwa utengano; tunalilia uhuru kama taifa, lakini tunajenga utegemezi kwa mataifa ya kibeberu.

Tunapenda kuona ustawi wetu na wa taifa, lakini tunatumikia umasikini wa kujitakia. Tumegeuka taifa la ombaomba katikati ya utajiri tulioruhusu kuporwa chini ya sera za uwekezaji usiojali. Lakini si kwa kiongozi kama Rais Mugabe, aliyeweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi kwa wageni.

Wakulima na wafanyakazi wetu wanagharimia uzandiki huu kwa jasho na machozi kuneemesha tabaka la watawala wasiotaka kuona ukweli wa maisha duni ya wanyonge hao. Tabaka hili la watawala limepofuka kwa hofu, hofu ya kuwaogopa watu wao wenye njaa, wenye kuvaa matambara na umma unaofupika umri wa kuishi kwa umasikini, kwamba siku moja watasema “imetosha” na kutenda yasiyotarajiwa.

Haya yote hayaonekani machoni, wala kusikika masikioni mwa viongozi wenye ukwasi wa kupora, kwa sababu wamehakikishiwa “usalama” na dunia ya ubeberu wa mitaji kuwa, “msihofu enyi kundi dogo, kwa kuwa baba yenu (ubeberu) amekwishawapa ule ufalme wa ulaji”.

Kwa kundi hili na mabwana zao, kiongozi kama Rais Robert Mugabe, mwenye kusimamia na kutetea maslahi ya nchi na wananchi wake ni “gaidi”. Na kwa nini tumekubali kutunga sheria ya ugaidi hapa kwetu bila kutafiti mantiki yake na hatima ya uhuru wetu, chini ya sheria hii ya kibabe?

source://www.raiamwema.co.tz: Joseph Mihangwa

No comments:

Post a Comment