WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, August 5, 2013

Tumejifunza nini Uchaguzi Zimbabwe?



Uchaguzi Mkuu nchini Zimbabwe ulimalizika Jumatano iliyopita, ambapo Rais Robert Mugabe wa Zanu-PF aliibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 61 ya kura, huku mpinzani wake, Morgan Tsvangirai wa MDC akipata asilimia 34 ya kura. Kwa ushindi huo, Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 89 ataapishwa kuongoza tena nchi hiyo kwa muhula wa saba mfululizo.

Hata hivyo, ushindi wa Rais Mugabe umelalamikiwa na MDC, kwamba kulikuwa na rafu nyingi na wizi wa kura, hivyo chama hicho kesho kitawasilisha pingamizi katika Mahakama Kuu kupinga ushindi huo. Chama hicho pia kimesema kitawasilisha waraka wa upungufu wote uliojitokeza kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kitaiomba jumuiya hiyo iitishe kikao cha dharura kuujadili.

Wakati waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika (AU) na SADC wakisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki, wenzao wa Jumuiya ya Ulaya (EU) walisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi, ikiwa ni pamoja na udhaifu katika mchakato wa upigaji kura na ukosefu wa uwazi. Hata hivyo, waangalizi wa AU na SADC walisema kulikuwa na hitilafu katika Daftari la Wapigakura, kwani baadhi ya wapigakura hawakuruhusiwa kupiga kura wakati walikuwa na sifa za kufanya hivyo.

Sio nia yetu hata kidogo kuingia kwenye malumbano na mijadala inayoendelea hivi sasa mahali pengi duniani kuhusu uchaguzi huo. Wala hatuna mamlaka kisheria na kikatiba kusema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki ama ulikuwa kinyume chake. Hii ni kwa sababu wenye mamlaka hiyo ni Wazimbabwe wenyewe na mamlaka zilizoko kisheria nchini humo.
Hivyo, lengo letu ni kuona kama kuna somo lolote ambalo nchi yetu itakuwa imejifunza kutokana na uchaguzi huo wa Zimbabwe. Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo na kuthibitishwa na waangalizi wa SADC, AU na EU ni kasoro zilezile ambazo zimekuwa zikitokea katika chaguzi mbalimbali katika nchi nyingi barani Afrika.

Tunaweza kusema kwamba kujirudia kwa kasoro hizo ni uthibitisho kwamba viongozi wa Serikali na vyama tawala katika nchi nyingi za Afrika hawajawa na utashi wa kisiasa wa kuendesha na kusimamia chaguzi huru na za haki na kuhakikisha kwamba nyanja za ushindani zinakuwa sawa na linganifu kwa kila mshindani.

Moja ya kasoro kubwa zinazojirudia ni tume za uchaguzi kushindwa kuratibu na kuhakiki majina ya wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura. Kama tulivyoshuhudia hapa Tanzania katika chaguzi zote zilizopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwa makusudi au kwa uzembe tu imekuwa ikishindwa kuhakikisha kwamba Daftari hilo linahakikiwa mara kwa mara ili kila mwenye sifa ya kupiga kura anapata haki hiyo.

Pamoja na kupigiwa kelele nyingi, Nec imeweka pamba masikioni.Wapigakura wengi wananyimwa haki ya kupiga kura kutokana na Daftari hilo kuwa na kumbukumbu na takwimu zilizopitwa na wakati. Nec inazembea kuingiza majina mapya ya watu waliofikisha umri wa kupiga kura na pia haifuti majina ya watu waliokufa. Tumebakiza wakati mfupi kuingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Matokeo ya hali hiyo bila shaka ni vurugu na uvunjifu wa amani. Nec isirudie makosa ya nyuma, ipate somo la Uchaguzi wa Zimbabwe na kwingineko barani Afrika.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment