WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, August 31, 2013

Kingunge Anaangalia Miaka 50 Nyuma, JK Anaangalia Miaka 50 Mbele !

kingunge_bd410.jpg

Ndugu zangu,

Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru ni mmoja wa wanasiasa ninaowaheshimu sana. Nimemsikia Kingunge tangu nikiwa na miaka saba.

Lakini, kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere, hakuwa malaika, Kingunge naye ni mwanadamu kama wengine. Si malaika.

Nimeyasikia mawazo ya Kingunge juu ya Serikali Tatu na hata Uraia wa Nchi Mbili. Ni mawazo yake, nayaheshimu, ingawa, kwa mtazamo wangu, Kingunge hayuko sahihi kwenye yote mawili.

Na hapa nitalizungumzia hili moja tu la mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba juu ya muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Kimsingi haya ni mapendekezo yenye kutokana na maoni Wananchi. Hivyo, Tume imewasilisha tu. Si mapendekezo ya Jaji Warioba au wajumbe wake.
Hii ni tofauti kubwa na mazoea ya ' Ukale' ya Mzee Kingunge ambayo hata sasa anataka yafuatwe; kuwa jambo kubwa la muundo wa Muungano liachiwe Chama Cha Mapinduzi na vikao vyake.

Ni jambo jema kwa mwanadamu kujifunza kutokana na historia, lakini, si jambo jema kwa mwanadamu kuwa mtumwa wa historia. Ni bahati mbaya, kuwa Mzee wetu mpendwa, Kingunge Ngombare Mwiru, anataka tubaki kwenye utumwa wa historia. Hatutaki.

Na hakika Mzee Kingunge anapaswa kuelewa, kuwa nchi hii ni zaidi ya Chama cha Siasa. Na chama cha siasa kilicho madarakani hakiongozi mawe. Na hata kama kingekuwa kinaongoza tumbiri, bado kingekumbwa na changamoto ya uwepo wa tumbiri wenye kutaka mabadiliko, kulingana na mahitaji ya wakati.

Tukubali, kuwa yalifanyika makosa makubwa ya kiuongozi huko nyuma. Ni pale masuala makubwa ya kitaifa kuachwa maamuzi yake kufanywa na kundi dogo la watu kwa kutumia nyadhifa za uongozi wa chama. Kwenye masuala makubwa ya nchi Chama kiliamua juu ya vichwa vya watu bila kushirikisha mawazo ya wananchi wenyewe, iwe kwa kupitia kura za maoni au kukusanya tu maoni ya makundi wakilishi. Huo ni msingi wa manung'uniko mengi ya sasa.

Kwangu mimi, Jakaya Kikwete ni mwanamageuzi wa kweli ambaye, kama kiongozi, ameonyesha ujasiri mkubwa wa kuzipa mgongo fikra za ukale na kuiangalia zaidi nchi na mustakabali wake kwa miaka mingi ijayo. Anafanya hivyo bila kujali nani au chama gani kitakuwa madarakani.

Wakati Mzee Kingunge na wahafidhina ( wasiotaka mabadiliko) wengine ndani ya mfumo uliopo wanatoka mahandakini huku wakihaha kujaribu kuurudisha nyuma mshale wa mabadiliko chanya kwa jamii , Jakaya Kikwete anaonekana, kuwa sio tu amesimama imara katika kuhakikisha mshale wa saa ya mabadiliko chanya kwa nchi unakwenda mbele, bali, unakwenda mbele kwa kasi.

Ni imani yetu, Wananchi walio wengi, kuwa Jakaya Kikwete hatakatishwa tamaa wala kuyumbishwa katika kukamilisha ajenda yake njema ya mabadiliko chanya kwa jamii ya Watanzania kuelekea miaka 50 ijayo.

Mzee Kingunge aelewe pia, kuwa wakati umebadilika. Kuwa ya mwaka 1974 alipojiunga na TANU ni tofauti na ya sasa, mwaka 2013. Huu ni wakati wa kiongozi kuonyesha uwezo wa kusoma alama za nyakati. Hivyo, kujitahidi kuendana na mabadiliko ya nyakati.
Hiyo pia ndio tafsiri ya kuwa ' Kiongozi wa Kisasa na Kimaendeleo'- A modern and progressive leader. Jakaya Kikwete kwa sasa yumo kwenye kundi hilo.

Na wenzake ndani ya CCM wakimsaidia katika kazi yake, basi, ni fursa pia kwa Chama chao kuiteka tena mioyo ya Wananchi wengi, mijini na vijijini. Maana, kati ya ambayo yanawachosha wananchi ni kukosekana kwa mawazo ya usasa na ya kimaendeleo kutoka kwa miongoni mwa viongozi wa CCM. Ni moja ya sababu ya chama hicho kupungukiwa na mvuto hususan kwenye kundi kubwa la vijana.

Na hakika, hata kama hatuoni leo, historia itakuja kumkumbuka Jakaya Kikwete kama mmoja wa viongozi Wana-Mageuzi ndani ya Chama chake CCM, na nchi kwa ujumla.
Maggid.
Iringa.
0754 678 252

Comments!
Thabit Molly Ni kweli japo na mimi napingana na wewe katika suala la uraia wA NCHI MBILI
41 minutes ago · Like · 1

Goddy Semwaiko sijakuelewa Maggid. hujaeleza Kingunge kaongea nini na kwa point zipi wewe unapishana nae. hebu nifafanulie tuweze kuchangia na kujadiliana. naona umetumia muda mwingi kumlaumu, nadhani na yeye ana uhuru wa mawazo na mchango wake. Haya mimi sijamsikia huyu babu kaongea nini, nihadithie
36 minutes ago · Like · 2

Thabit Molly Kama uko Tz fatilia magazeti yote yameongelea alichoongea mzee Kingunge jana@Goddy Semwaiko
29 minutes ago · Edited · Like · 1

Maggid Mjengwa Baada ya kukaa kimya muda mrefu, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingune Ngombale-Mwiru, ameibuka na kuwatupia lawama viongozi wa CCM, kwa kutaka kupenyeza suala la uraia wa nchi mbili ndani ya Katiba Mpya.Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, ...See More
32 minutes ago · Like · 2

Goddy Semwaiko OK. Mimi sioni tatizo na naungana mkono moja kwa moja na huyu mzee. Nakubaliana nae kabisa, kama hoja ya muhimu inajadiliwa na kundi dogo la watu na kutumia fursa yao kutengeneza Kitabu wanachokiita Ufafanuzi wa Rasimu ya Katiba, sidhani kama watu hao wana haki ndani ya kundi kubwa la wanachama. Sasa Maggid wewe unalalamika nini hapo? Kiasi cha kumshambulia huyu mzee???
27 minutes ago · Like

Maggid Mjengwa Goddy, nimejikita kwenye Serikali Tatu. Kingunge hataki Serikali Tatu, anataka tubaki tulikokuwa. Hayuko sahihi. Kwa mtazamo wangu. Hata la Uraia wa nchi mbili napingana nae. Nitalifafanua.
14 minutes ago · Like

Goddy Semwaiko Mimi Naona serikali tatu ni tatizo Kubwa mno, na gharama zisizo na sababu. Kama serikali moja haiwezekani, basi serikali mbili ziangaliwe upya. Ingawa najua upande wa pili hawataki kusikia swala la serikali mbili. Mimi binafsi kwakweli serikali tatu ni kudanganya wenyewe, kwani haiwezi kudumu wala hakutakuwa na la msingi kwa hii serikali ya muungano.
 
Kuhusiana na swala la Uraia wa nchi mbili pia, sioni umuhimu, na swala la fursa na uwekezaji, bado wanaotaka kuwekeza nchini mwao wanaweza tu, mbona kuna wawekezaji ambao si raia wa nchi hii na wanafanya vizuri kibiashara? Iweje raia anaepata fursa huko nje ashindwe kuwekeza hapa, hata kama akiukana uraia wa nchi hii, anaweza kuwekeza kama mgeni, tena atakuwa mgeni mwenye kujua in and out. Swala la uwekezaji kutetea uraia wa nchi mbili nalo naliona halina mashiko....
Leta hoja Maggid...

source: mjengwa blog

No comments:

Post a Comment