WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 2, 2013

Pinda Kortini

  Mashtaka dhidi yake yawasilishwa rasmi
  Timu ya mawakili 20 kunguruma kortini

 
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo Bisimba, akionyesha hati ya mashtaka ya kesi namba 24 ya Mwaka 2013 ya Mashauri ya Katiba dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana katika Makama Kuu jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Ringo Tenga.
Hatimaye Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Waziri Mkuu,  Mizengo Pinda na Manasheria Mkuu wa Serikali.
Katika shauri hilo lililowasishwa jana, wanaomba mahakama hiyo itoe tafsiri za kisheria katika baadhi ya Ibara ambazo wanaamini zimevunjwa na Pinda katika matamshi yake bungeni juu ya kupigwa kwa wananchi.

Kesi hiyo namba 24/2013 hata hivyo bado haijapangiwa jaji wala tarehe ya kusikilizwa.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo una takribani mawakili  20 akiwamo Haroud Sungusia wa LHRC, Francis Stolla ambaye ni Rais wa TLS na wengine 17.

Walalamikaji katika hati ya madai wana maombi mawili; moja mahakama itoe tafsiri ya kisheria katika Ibara hizo na kwamba wamewasilisha kesi hiyo ya Kikatiba chini ya sehemu ya Tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inaainisha Haki na Wajibu Muhimu.

Walalamikaji wakiongozwa na Wakili Sungusia wanaomba ufafanuzi wa kisheria katika ibara ya 100 (1) ya Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa majadiliano bungeni. Ibara hiyo inaeleza kwamba: “Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.”

Hati hiyo, inafafanua zaidi kwamba Ibara hiyo ina ubaguzi ndani yake kwani inatoa uhuru wa majadiliano bungeni hata kama mbunge atavunja haki za mtu mwingine hataweza kushitakiwa wala kuhojiwa jambo ambalo linakinzana na Ibara ya 13 (2) ya Katiba.

Ibara hiyo inaeleza kwamba: “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”

“Tunaomba mahakama hiyo itamke wazi kuwa Ibara ya 100 (1) inakwenda kinyume cha matakwa ya Ibara 13 (2), zinakinzana kwani Ibara hiyo ya 100 (1) ya Katiba inatoa haki tu kwa upande mmoja wa wabunge uhuru wao kutohojiwa na inawanyima haki ya kuwahoji au kuwashitaki wabunge wanaotoa kauli zao bungeni hata kama kauli hizo zimevunja haki za wananchi, hivyo tunaomba mahakama itamke kuwa ibara ya 100 (1) ya Katiba inakinazana na ibara hiyo.”

Ombi la pili katika hati hiyo ni mahakama hiyo itamke kuwa kauli ya Pinda ambayo ililitaka Jeshi la Polisi kuwapiga wale wote wanaokiuka amri za jeshi hilo, kama kauli hiyo nayo inalindwa na kinga iliyowekwa katika Ibara ya Ibara ya 100 (2) ya Katiba ya nchi ambayo inatoa kinga ya majadiliano ndani ya Bunge.

Ibara hiyo inaeleza kwamba: “Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.”

Katika kauli hiyo, Pinda alisema: “Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua wewe kukaidi utapigwa tu. Maana hakuna namna nyingine; lazima tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria, Sasa kama umekaidi hutaki, unaona kama wewe ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tuu kwa sababu hakuna namna nyingine, maana tumechoka sasa,” alisema Waziri Mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama baada ya kuwasilisha hati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa  LHRC, Helen Kijo-Bisimba, alisema wameamua kufungua shauri hilo kwani hakuna aliye juu ya sheria nchini na kauli iliyotolewa na Pinda ni uvunjifu wa Katiba.

Alisema Mahakama ni chombo pekee ambacho kinaweza kutoa haki katika nchi.
Kwa upande wake, Wakili Sungusia, alisema wameiomba mahakama iamue kipi kinabaki kati ya haki za binadamu na kinga ya bunge.

Alisema hadi jana walikuwa wamepokea kura na sahihi za watu 2,029 na bado zinaendelea kupigwa katika mikoa mbalimbali nchini kupinga kauli ya Pinda.

Alifafanua kuwa kituo hicho kitaunda jopo la mawakili wasiopungua 20 ambao watakuwa upande wa walalamikaji pindi shauri hilo litakapopangiwa jaji na tarehe ya kusikilizwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Raia, inayofuatilia mwenendo wa bunge, Marcus Albanie, alisema taasisi hiyo inaungana na LHRC pamoja na TLS na kwamba itamshtaki Pinda kwa wananchi kwa kuwa siyo mara ya kwanza kutoa kauli yenye utata.

Alikumbusha kwamba siku za nyuma, Pinda aliwahi kutoa kauli bungeni akitaka wanaowaua albino nao wauawe, lakini baada ya kubanwa na wananchi pamoja na wanaharakati, alilia ndani ya bunge.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment