WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, August 11, 2013

Amani hii ni tunu, tuienzi na kuilinda

Maoni ya Katuni

Jitihada kubwa za kuhimiza amani na usalama kudumishwa nchini zimekuwa zikifanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali katika nyakati tofauti.

Makundi mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakihamasishwa kila wakati kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote bila kujali tofauti za kidini, rangi, kabila, jinsia na maeneo ya uzawa.

Wakati huu ambapo Watanzania wamekuwa katika sherehe za Eid El Fitr, viongozi wa kitaifa wameshiriki katika ibada hizo kwa kuwakumbusha Watanzania kutokukubali umoja wetu kusambaratishwa kwa vigezo vya mitafaruku ya udini.

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal wakati akizungumza katika Baraza la Eid El Fitr mjini Tabora juzi, alisisitiza kuwa Watanzania wakatae kabisa kugawanywa kwa misingi ya udini na kwamba ni busara kwa waumini wa dini na madhehebu kujenga utamaduni wa kuvumiliana hasa zinapotokea hitilafu miongoni mwao.

Dk. Bilal alitumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania kumaliza tofauti za kidini kwa kukaa pamoja na kutafuta muafaka kwa njia ya majadiliano ya amani na upendo pasipo kutawaliwa na jazba wala chuki, huku akiwakumbushia waumini wote kauli na angalizo la Rais Dk. Jakaya Kikwete kuwa vita vya dini havina mshindi.

Makamu wa Rais aliwakumbusha Watanzania kuwa pamoja na Tanzania kuwa kisiwa cha amani, baadhi ya mataifa hayatutakii mema, yanatuangalia kwa jicho la husuda na kutuombea mabaya.

Aidha, wanatuombea tufike mahali tuharibikiwe ili wao wafurahi, suala ambalo endapo tutashikamana na kuzitupilia mbali tofauti zetu, hilo halitatokea kwani katu "dua la kuku halimpati mwewe".

Alisisitiza kuwa amani katika taifa au jamii yoyote ni sharti la kwanza katika mchakato wa kuleta maendeleo, hivyo ana imani kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kujenga maadili mema katika taifa hili na kwamba watu wakishiba imani ndani ya nafsi zao na wakaelewa na kuzingatia mafundisho, maovu yataondoka miongoni mwao.

Wito wake kwa viongozi wa dini na madhehebu yote nchini ni wahakikishe kuwa wanatumia nafasi zao vyema kuwajenga waumini wao kimaadili, ili wawe raia bora watakaosaidia kudumisha na kuendeleza sifa na heshima ya taifa letu kuhusu kutunza na kuilinda amani.

Tukio la kumwagiwa tindikali kwa wasichana wawili raia wa Uingereza huko Zanzibar wiki hii ni moja ya matukio yanayoliweka taifa katika sura mbaya duniani, na tayari baadhi ya vituo vya runinga kama CNN vimelitangaza tukio hilo kwa uzito mkubwa.

CNN kupitia kipindi chake cha Out Front imeonesha kuwa Tanzania siyo salama tena na kwamba watu wanaotaka kutembelea nchini humu, lazima wachukue hatua za tahadhari. Hayo yote yanatuhusu kama taifa kupambana nayo kwa gharama yoyote.

Binadamu wote humheshimu na kumwogopa Mungu, viongozi wa dini wanamwakilisha Mungu katika kuwaongoza waumini wao hapa duniani ili waishi kwa imani na matarajio kama inavyoagizwa katika vitabu vya madhehebu yao. Na kwa uhakika, hakuna dhehebu linalohamasisha waumini wake watende dhambi na kumuasi Mungu, kwao amani, upendo na kuheshimiana ni kipaumbele kikuu kwa madhehebu yote.

Tunaamini kuwa viongozi wa dini ni mhimili mkubwa katika kutatua tofauti za kidini, na ndiyo maana tunazo sababu za kumpongeza Makamu wa Rais kwa wito alioutoa kwa viongozi wa dini kumaliza tofauti zilizopo kwa kuzungumza bila jazba wala hasira. Viongozi hao ndiyo dira kwa waumini wao, viongozi wa dini wanao uwezo mkubwa wa kushawishi na kudumisha maelewano miongoni mwao.

Tunaamini pia kuwa nchi hii itabaki kuwa nchi salama ya amani na utulivu na ambayo itaendelea kupigiwa mfano na nchi nyingine. Uhuru wa kuabudu katika taifa hili umejengewa misingi ndani ya Katiba na kutokana na ukweli huo, kila mmoja anapaswa kuheshimu imani au dini ya mwenzake pasi na kujiona imani au dini yake ni bora zaidi.

 Yote hayo amewahi kuyasema pia mara nyingi Rais wetu, Dk. Jakaya Kikwete kila anapopata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini kuhusu mustakabali wa amani ya taifa letu. Amani hii ni tunu, tuilinde kwa nguvu zetu zote. Mungu ibariki Tanzania na watu wake.   
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment