WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, August 24, 2013

Na ya DECI hatimaye tumevuna aibu..!
Juzi Mahakama ya Kisutu iliwatia hatiani wahusika wa kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) kwa kuwaadhibu kifungo cha miaka mitatu au faini ya jumla ya shilingi milioni 21. Mmoja ameachiwa huru.

Washtakiwa hao ni  Mchungaji Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saiguran ole Loitginye na  Samwel Mtares. Pia Mahakama hiyo iliiamuru serikali Benki Kuu (BOT) kuhakiki mali zote za DECI nchi nzima na kwarudishia wateja wanaoidai DECI chochote.

Naam, haya ni mavuno ya aibu kwa taifa, maana, tulichelewa kuchukua hatua za haraka kuwanusuru wanyonge wenye kupoteza kidogo walicho nacho kutokana na hadaa ya watu wengine wenye majina makubwa. Na wengine ni viongozi wa dini. Wote hawa wanashiriki kwenye kuwatepeli wananchi wanyonge. Na kibaya ni kuwa utapeli huu unaendelea hata leo, kupitia migongo ya imani.
Naam, nimepata kuandika, kuwa tunawapitisha  watu wetu kwenye njia yenye giza. Kwenye njia yenye matope.  Kwa nini?

Socrates,  mwanafalsafa wa Uyunani ya kale alipata kuonekana akimulika kurunzi mchana wa jua kali. Inaandikwa, kuwa  Socrates yule  alizunguka sokoni na kurunzi (tochi) yenye kumulika.  Watu walimwuliza, kulikoni? Socrates akawajibu; ”Kwenye nuru hii , kuna walio gizani.”

Kwa Socrates lilikuwa ni tendo la kifalsafa  lenye kuelezea hali halisi. Hata katika dunia hii  ya kisasa,  bado tuna miongoni mwetu,  walio gizani  mchana wa jua kali. Angalia ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo. Ndiyo, kuna  waliohitaji kumulikiwa mwanga.

Na kuna tofauti ya ujinga na upumbavu.  Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka; ” Kusoma si kuufuta ujinga, bali ni kuupunguza”. Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa na ujinga wa jambo si kosa, hata profesa anaweza asijue namna ya kuchochea kuni za  kuchomea hindi bichi likachomeka. Kijana wa darasa la saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda profesa.

Lakini, upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu. Na ndiyo maana binadamu kuitwa mpumbavu ni tusi. Kuitwa mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga wake. Kuwa na ujinga wa jambo fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani anayeelewa kila jambo?

Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemwuliza swali hilo. Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani angetamka, kuwa angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.

Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndio njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri? Haya ya  DECI na hata ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo ni kielelezo cha Watanzania kuamua kuacha kufikiri. Kuna umma uliojifunika vilemba vya ujinga. Umma uko gizani, unahitaji mwanga.

Yumkini wakatokea Watanzania wenzetu,  wakaoteshwa na Mungu juu ya  dawa za tiba kwa mwanadamu. Na hapo wakaingiza suala la imani.  Na wakatokea hao wanaosema wanaweza wakafanya maombi na miujiza ikatokea, kwa wasioona wakaona, wasiosikia wakasikia. Ni uongo. Ni abrakadabra. Na wenye mamlaka wanawaachia watu hawa kuendelea na abrakadabra zao. Kuwadhulumu wanyonge.

Katika dunia hii serikali hupendwa na watu, lakini, si vema na busara, kwa serikali za dunia kutaka kujipendekeza kwa watu. Kuna mambo yenye kupendwa na watu, na watu wakawa na haraka ya kutaka kuyafanya. Lakini, kama serikali itahitaji kufuata taratibu ili kinachopendwa na watu kifanyike, basi, serikali haina namna nyingine, bali kufuata taratibu.

Walau katika hili la DECI tulimwona  Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisimamia taratibu. Waziri Mkuu Pinda kasimamisha wimbi lile la DECI. Kuna wengi walishutumu, lakini , hao hao, leo wanaishukuru Serikali. Maana, DECI nayo ilikuwa ni Abrakadabra. Na hukumu ya Mahakama ya juzi imethibitisha hilo.

Sousrce: www.raiamwema.co.tz: Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment