WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 30, 2011

KATIBA BORA NI ZAO LA MAAMUZI YA BUSARA NA SIO MAANDAMANO NA KUSUSIA MAJADILIANO



BUSARA ALIYOIONYESHA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE YA KUANZA KUKUTANA NA VYAMA VYA UPINZANI KUJADILI MCHAKATO WA KATIBA MPYA TUMEzIPOKEA KWA FURAHA KUBWA;

 “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Novemba 29, 2011, ametia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011. Hatua hiyo ya Mheshimiwa Rais kutia saini Muswada huo inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali katika kikao kilichopita cha Bunge. Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010.”


Kama taifa inatupasa kukumbuka kuwa  mabadiliko ya katiba ni madai ya msingi na matakwa ya lazima kama nchi hii inataka kujenga na kudumisha amani ya kweli na kuleta maendeleo kwa watu wake; wazo la serikali na vyama vya siasa na zsasi zingine zinazojishughulisha na sheria  ni msingi kuendelea kutambuka kuwa  Safari hii  ya utungaji wa katiba ni ya Muhimu sana ; hivyo ni wajaibu wao  kuhakikisha kuwa wananchi waweze kujua zaidi kuhusu katiba, wawe tayari kutoa mawazo ili tume au kamati itakapowatembelea wawe na kitu cha kusema, watakapoachwa hivi hivi hawatakuwa na cha kuzungumza; je vyama na asasi kwa sasa hivi zimeandaa mkakati gani wa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia maoni; tatizo nilionalo kama vyama vitaendelea kulumbana vyenyewe vuifahamu kuwa havina nafasi ya kumsaidia mwananchi wa katika kujinasua katika hali duni kwani katiba na utungaji wake itabakia kwa wanansiasa, wasomi na wanjanja wachache.


Tukiangalia wenzetu kama Marekani pamoja na  uwezo wao  na maendeleo yao bado Katiba ni chombo cha wananchi na sio chombo cha chama Fulani, na katiba yao imejengwa katika msingi mkubwa sana wa uhuru ambao umewekwa katika katiba yao.
Jukumu la wanasiasa kuwaelimisha wananchi kuhusu marekebesho ya  kutungwa kwa katiba mpya ni la muhimu sana kwani wananchi wengi  hawajui katiba ya zamani inamabo gani ni ina matatizo gani, hivyo wasipoelimishwa hata mabadiliko yanayokusudiwa hayatakuwa na msisimko wowote kwao na itabaki tu kuwa je watawezaje kutoa maoni ya katiba  mpya wakati hawajui  mapungufu amabayo yamo katika katiba iliyotumika kwa ktakribani miaka hamsini sasa.


Kwa serikali vyama vya siasa, vyama vya upinzani na Asasi zinazojihusiha na maswala ya katiba, tunaviomba sana katika mchakato huu mzima wa uandikaji wa katiba mpya  vitumie nafasi hii vizuri kwa kujadiliana juu ya Katiba mpya, kwa kudumisha utamaduni wa kuvumilia maoni yanayotofautiana, sambamba na kuwa na mtazamo chanya na kutanguliza taswira nzuri ya Taifa kwa masilaha ya wananchi wote, vijana, akina mama, wanaume, wazee, matahira na wengineo wote, kwa maana ndiyo inayosimamia maisha yao.




Nakumbuka  Profesa Shivji katika moja ya mikutano ya changamoto ya katiba mpya ya Tanzania aliwahi sema kuwa  “mchakato wa upatikanaji wa kabisa mpya ni fursa muhimu ya kurejesha mwafaka kwa majadiliano kuliko ilivyo sasa ambako kuna kila dalili za kuelekea katika magomvi na mapambano”


Kwa maneno mengine Professor Shivji  anatukumbusha kuwa Katiba inatakiwa Ni ya  wananchi, ndio wananchi  lazima wawe  wenye uamuzi wa aina ya serikali wanayotaka kuwa nayo na inawaongozaje, wananchi ndio msingi wa madaraka yote nchini. Kwa maneno mengine Katiba inatakiwa itoke kwa wananchi. Siyo katika kuipigia kura tu bali katika uandikaji wake. Katiba ambayo haitoki kwa wananchi na haiweki ushiriki wa juu kabisa wa wananchi kutoka mwanzo haiwezi kudai kuwa ni katiba ya wananchi hao.

Kwa mtazamo wangu na wengine wengi ambao sio wanansiasa au wasomi  tunatamani kuwa Katiba Mpya iwe ni kumbu kumbu endelevu na kwamba, kasoro zilizojitokeza kiasi cha kutibua mori na hali ya watanzania, iwe ni changamoto ya kuwa makini zaidi katika mchakato mzima wa uandikaji wa Katiba Mpya, mzaha wowote unaweza kulitumbukiza Taifa katika maafa makubwa lazima usipewe nafasi kwani tunatamani katiba yetu iwe kama ile ya Merakani ambayo imesimama na inatekelezeka. 


Kama Mwalimu Nyerere alivyowahi sema katika moja ya mikutano yake kuwa  Katiba ni sheriamama, iguse msingi wa mambo makuu yatakayoongoza sheria, sera na mifumo ya kitaifa. Hii ni dhamana nyeti inayopaswa kuwashirikisha wataalam kutoka katika medani mbali mbali za maisha nchini Tanzania. Wanasiasa waepuke kishawishi cha kudhani kwamba, wao ndio wanaopaswa kusimamia na kuongoza mchakato huu, wajitahidi kushiriki kama watanzania wengine kwa kuchangia mawazo yao

Katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba tuzingatie,  
·  Tunaomba Busara  na hekima za Rais wetu zitumike sana wakati huu; 

·    Katiba Mpya inapaswa kuwa ni mali ya watanzania wote kwa kuwa mchakato mzima unawashirikisha watanzania wengi zaidi kwa njia ya moja kwa moja au uwakilishi wao. Chombo kitakachopewa dhamana ya kusimamia kuandika Katiba Mpya, kwanza kabisa kikubalike na watanzania wengie, hii itakuwa ni hatua kubwa hata kuweza kuridhia kile kitakachoandikwa. Miongozo itolewe katika lugha inayoeleweka na fasaha ili kuwa na tafsiri sahihi na rahisi kwa watanzania wa kawaida kabisa



·        Washauri wa mheshimiwa Rais tunawaomba wamshauri Mkuu wetu wa nchi kwa masilahi ya Taifa na sio vinginevyo wakizingatia kuwa serikali yetu kwa hivi sasa inaingia katika kipindi muhimu sana cha kulipitisha Taifa letu katika wakati huu kwa maendeleo ya wananchi wote na sio kikundi kidogo cha watu;




· Katiba yetu ikamilishwe kutungwa kwa majadiliano na makubaliano ya umoja wa kitaifa na sio kwa vitisho vya Migomo na maandamano na shinikizo la vyama kwa masilahi binafsi. 

·   ili kupata Katiba makini inayozingatia mafao ya wengi kuna haja kwanza kabisa kuwa na utulivu wa kimawazo, busara na hekima vitumike zaidi, kwa kuzingatia umoja wa kitaifa na upendo kati ya watu. Masilahi ya taifa yapewe kipaumbele cha kwanza na kamwe ubinafsi usiruhusiwe kutawala zoezi nyeti kama hili.



·        Ebu tuache  malumbano wakati huu ni mzuri kwa vyama vya siasa tanaznia pamoja  asasi zanazojishughulisha na mambo ya  sheria kutumia muda huu kuwafundisha  wananchi katiba ya zamani na waone hayo mapungufu yake halafu wapate kutoa maoni  yanayolingana na mahitaji yao na sio kufuata mkumbu wa mahitaji ya wanasiasa kama inavyoendeleahivi sasa;

HITIMISHO;

Kwa msingi huu vyama vyote yaani  CCM, CHADEMA, CUF, NCCR, TLP na Vyama vingine vya siasa vikumbuke kuwa “Katiba ya nchi si mali ya chama au mtu binafsi na wala si mali ya kiongozi fulani, ni mali ya watu wote raia wa Tanzania na wala katiba isipatikane kwa shinikizo la kukundi chochote cha watu”


kama Dk Salim Ahamed Salim aliwahi sema kuwa “Chama tawala na chama kikuu cha upinzani vijue tunaangalia mustakhabali wa taifa letu, lazima uelewano uwepo malumbano si mazuri japokuwa ni sehemu ya siasa, lakini akaonya kwamba yasiruhusiwe yakasababisha nchi ikafika pabaya. Ninachoomba chama tawala na Chadema wafikirie mwafaka na kuangalia mustakhabali wa taifa, kama hakuna maafikiano si jambo zuri kwa taifaKwa hali ya kisiasa hivi sasa ni lazima mjadala uwe wa nia njema lengo ni kuendeleza makubaliano na si kuhitilafiana. Tujenge na kuimarisha undugu na mishikamano wetu na kuonyesha uzalendo na uongozi madhubuti wa taifa letu,”


kwa hiyo tunavyoelekea kupata katiba mpyaa ifikapo mwaka 2015 kama serikali ilivyohaidi, Tanzania kama nchi ambayo imeingia katika mfumo wa vyama vingi miaka ya 90, inahitaji mabadiliko au katiba mpya yenye misingi YA UPANA NA UWAZI WA DEMOKRASIA na misingi mipya ya kuongoza vyama vingi na mawazo mapya ya Jamii kwa msingi huu kama sisi kama Taifa tutafanikiwa kupata katiba mpya basi tukakuwa  tumejijengea  katiba  iwapo vile vile tutaweza kujumuisha kwenye uandikaji wa katiba mpya kwa maoni ya wananchi hapo tutakuwa tumejijengea  Utawala wa Demokrasia ya umma.


Tunaendelea kumpongeza mheshimiwa Rais kwa busara yake ya kuanza kukutana na vyama vya upinzani CHADEMA, katika kufikia muafaka na kushauriana katika kuboresha uandikaji wa katiba mpya; tunamwomba mheshimiwa Rais aendelee kukutana na wale wote wenye nia njema, katika kuboresha katiba yetu mpya;


MUNGU IBARIKI TANZANIA KATIKA MAANDALIZI YA KATIBA MPYA

Monday, November 28, 2011

Kilichotokea Vikao Vya CCM Dodoma: Tafsiri Yangu


Ndugu zangu

Waafrika sisi tu mahodari sana wa kufunga safari, lakini, huwa hatupangi safari. Kuna tofauti ya kufunga safari na kupanga safari.  Kuna tofauti pia ya kuwa na mipango na mikakati na kuwa na mipango na mikakati sahihi.
Mara nyingi wenye kupanga safari zao, na hata kuwa na mipango na mikakati sahihi hufanikiwa zaidi. Na ndivyo ilivyo kwenye siasa.

Kule Dodoma tumeshuhudia ’ Vita vya wenyewe kwa wenyewe’ ndani ya CCM.  Inahusu safari ya kuelekea 2015, na si kitu kingine.  Kule Dodoma CCM hawakutoka WaMOJA . Wametoka kwenye mapande  makubwa mawili na mafungu mengine madogo madogo.

Na CCM ya sasa ina makundi, walau hili wamekiri rasmi CCM wenyewe.  Na kwenye kuelekea 2015 tunayaona makundi makubwa mawili; lile linaloongozwa na Edward Lowassa na la akina Samwel Sitta. Kule Dodoma  tumeushudia mnyukano wa wazi wa makundi  haya yakiwahusisha pia vijana wa chama hicho. 

Yote haya yanatoa fursa kwa upinzani kufanya vizuri kama itatumia vema fursa hii ya  Wana- CCM wanaonyukana wenyewe kwa wenyewe.  Huu ni wakati kwa Wapinzani kuwaonyesha Watanzania kuwa CCM ni chama cha kawaida tu na unaweza kuwepo mbadala wa chama hicho. Ni wakati pia kwa wapinzani  kuongeza nguvu ya  kusukuma hoja  ya kuandikwa Katiba Mpya itakayowashirikisha wananchi katika hatua zote.

Na mpambano ule wa Dodoma, katika hali inayoweza hata kumstajabisha  Lowassa mwenyewe,  umempa sio tu ushindi Lowassa na kundi lake, bali pia,  Lowassa ametoka kwenye vikao vile akiwa, walau kwa wakati huu,  na nguvu nyingi zaidi za kisiasa ndani ya chama hicho .  Inaonekana ’ jeshi la Lowassa’ ni kubwa, limesambaa  na lina nguvu za kimikakati. Ndio, Edward Lowassa amenufaika sana  kisiasa na vikao vya chama chake kule Dodoma.

Na mwananchi wa kawaida anasemaje?

Namwuliza , Andrew, kijana dereva wa teksi hapa Iringa;  “ Unasemaje kuhusu yaliyotokea Dodoma CCM?”
”Lowassa hayumo!” Ananijibu.
”Una maana gani?”  Namwuliza.
”Tuliambiwa Lowassa ni fisadi kumbe hayumo.”

Dereva wa teksi anaonyesha kufurahi kuujua  ukweli. Swali ni hili; Je, aliousikia dereva wa teksi ni ukweli kamili?   Hivyo basi, waliomwaminisha dereva wa teksi kuwa Lowassa ni fisadi wana mtihani wa kuja na ushahidi wa kumtia hatiani mtuhumiwa ili nao waaminike. 

Na katika hili nayakumbuka maandiko ya  mwanafasihi  Kezilahabi: “ Siku hiyo ikifika utaona ishara itakayokuongoza. Utakapofika pale ambapo kila binadamu lazima afike utajua hukukosea; kwani njia ya kwenda huko inajulikana kwa wote na inakwenda moja kwa moja bila kupinda.


Huna haja ya kusoma kitabu chochote kupata maelezo ya kwenda huko wala hakuna haja ya kusikiliza mahubiri. Hakuna  utalaamu unaohitajika  maana utajikuta umefika. Utakapofika utamkuta  amekaa peke yake akiwatazama  wale wengine . Hao wengine  utawatambua maana  ni ndugu zako wote.

Wengi kati yao  ndio wale waliokuwa askari wa mwanga. Wale ambao hutaweza kuwatambua atakumbulisha kwao  na wewe utachukua nafasi yako.  Usistuke utakaposikia majina yao; maana, wengi kati yao wana majina  makubwa. Utawakuta wanafanya jambo fulani. Wewe pia fanya kama wao bila kuuliza bila manung’uniko na usikate tamaa. Kwa sasa hivi subiri  ishara” ( E. Kezilahabi, Nagona)

Ni kina nani wamejeruhiwa Dodoma?

Nape Nnauye hawezi kuwa mwana- CCM mwenye furaha kwa  wakati huu.  Nahofia kuna hesabu za kisiasa alizozichanganya vibaya sana.  Kama mwenezi wa chama alijichanganya sana kwenye  kuilezea kwa umma dhana ya ’ Kujivua Gamba’ . Badala ya kuonekan kuwa ni mkakati wa mabadiliko ya jumla kwa CCM Nape aliitumia dhana hiyo kuwahukumu WanaCCM wenzake . Hivyo basi,  kuonekana zaidi kuwa ni mbinu ya kutaka kuondokana nao ili kupisha njia kwa watu wa kundi lake.  Na hapo ndio kwenye tatizo la msingi kwa Nape. Kwamba anaonekana kuwa na kundi lake kuelekea 2015. 

Kujichanganya kwa Nape kimsingi kumewapa fursa akina Lowassa na wenzake kupanga mashambulizi na kuyatekeleza kwa mafanikio makubwa.  Na kama kuna mtu aliyejeruhiwa vibaya kwenye vikao vya Dodoma ni Nape Moses Nnauye.  Ana lazima ya kujipanga  na kurudisha mashambulizi ili kulinda heshima yake na hata taswira  yake kwa jamii.  Hivyo hivyo kwa Samwel Sitta na wenzake.  Dakika 45 za kuongea peke yake kwenye ITV hazikumwongezea nguvu Samwel Sitta na kundi lake na labda kinyume chake. 

 Je, ina maana vita ndani ya CCM  ndio imekoma?
Hapana, huu ni mwanzo tu, vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM vitaendelea na moto wake kuongezeka.  Mwakani  kuna uchaguzi wa ndani ya chama  hicho. Tulichokiona Dodoma ni ’ rasha-rasha’ tu.   Kutoka Dodoma makundi yanayohasiamiana ndani ya CCM yatazidi kupambana  mikoani, wilayani  na hata kwenye kata. Watazidi kupambana pia kupitia vyombo vya habari. Yote ni katika kuhakikisha wanajipanga  kushika nafasi muhimu  kwenye uchaguzi ujao wa chama chao, nafasi zitakazohakikisha wagombea wao wanapata tiketi za kuwania urais na hatimaye kushika dola. 

Na Lowassa na wenzake wana kibarua kigumu cha kuwabadilisha   WaTanzania kutoka kile walichoaminishwa kabla .   Ni kibarua kigumu kama vile kumwambia  mtu kuwa rangi nyekundu si nyekundu tena bali ni nyeupe.  Kwamba alichokuwa akiamini mtu huyo siku zote kuwa ndicho, sicho.  Ni watu hawa  hawa ambao hawakupata tabu jana  kujibu swali  la je, fisadi mkuu ni nani? Na anayefuatia….?


Je, uchaguzi wa ndani ya  CCM ukimalizika  mwakani ndio mwisho wa vita?

Hapana, kundi  litakaloibuka na ushindi wa  jumla litahamishia mapambano yake kwa wapinzani wa chama na mgombea wao Urais walio nje ya chama chao. Kwa ilivyo sasa mashambuzi yanaweza kuelekea kwa Chadema.  Hiki ni chama   chenye nguvu  na ushawishi mkubwa kwa wananchi  kwa sasa.

Hivi ni Lowassa tu aliyeibuka mshindi kule Dodoma?
Hapana, kuna  MwanaCCM mwingine aliyetoka Dodoma kimya kimya huku kikapu chake kikiwa kimejaa mavuno. Ni Fredrick   Tluway Sumaye.  Msomaji  lishike jina hili. Huyu bwana  hadi wakati huu anazicheza karata zake vizuri sana. Yaelekea mafunzo yake ya Uongozi aliyoyapata kule Havard Marekani  yanamsaidia.
Si tulimsikia  Sumaye  kule Dodoma akisimama na kumtetea ’ majeruhi’ mwenzake Lowassa bila kutamka kuwa naye, Sumaye  ni ’ majeruhi’ wa  ’ Siasa uchwara’ kama anavyoziita Rostam Aziz.  Sumaye ana  mitaji ya kisiasa anayowekeza.

Je, ni kweli Lowassa ana nguvu na ushawishi mkubwa kisiasa?

Nikijibu hapana nitaongopa. Edward Lowassa ni mwanasiasa mahiri na mwenye ushawishi mkubwa ndani na hata nje ya chama chake.  Wanaomjua Lowassa wanasema ana vitu viwili vikubwa;  authority na humbleness. Kwamba ana uwezo wa kushawishi na kufanya vitu vifanyike na pia ni mnyenyekevu. Hilo la mwisho kuna wanaosema Lowassa anaweza kuongea na mtu mdogo sana, lakini atahakikisha hajibu simu ya mtu mwingine mpaka amalize mazungumzo na anayeongea nae.

Nikiwa Bagamoyo  kwenye mkutano wa masuala ya elimu juma la jana kuna hoja ilizuka juu ya shule za sekondari za kata. Kikundi cha majadiliano nilichokuwamo kiliwajumuisha watendaji wa elimu kutoka Wilaya mbali mbali za  Tanzania.
Swali likaulizwa; ” Ilikuaje sekondari za kata zikajengwa kwa kasi vile?”
” Ni Lowassa!” Alijibu mmoja wa washiriki.
Alifanyaje? Akauliza mwingine.
”  Waliokuwa wakiratibu michango ya elfu kumi kumi kutoka kwa Watumishi walitwambia; Lowassa anataka tumpelekee orodha ya ambao hawakulipa michango hiyo, si orodha ya waliyolipa. Ni kwa njia hiyo kila mmoja  wetu akachangia na shule zikajengwa.  Ni nani anayetaka jina lake lifikishwe kwa Lowassa?” Alimalizia kwa kuuliza mmoja wa wanakikundi cha majadiliano.

Na kwa yaliyotokea Dodoma   kuna watakaoshika tama na kusema, kumbe, Edward Lowassahajamalizwa kisiasa! Je, akina Mwakyembe hawakufahamu, kuwa simba humwui kwa risasi ya kumpapasa masikioni?
 Kama ni mchezo wa ngumi, basi, kwa mpinzani wa Lowassa, akubali, kuwa kummalizaLowassa , awe tayari kucheza raundi zote 12.

Naam, tutayaona mengi mengine huko twendako, tuombe uhai.

Maggid  Mjengwa
Iringa,
Jumatatu, Novemba 28, 2011
http://mjengwa.blogspot.com

Habari kwa hisani ya Mwandishi Mashuhuri na mwanafilosofia- Maggid Mjengwa;

Tuesday, November 22, 2011

MAENDELEO YA TASNIA YA FILAMU TANZANIA NA SHEHERE YA MIAKA 50 YA UHURU




Katika kelekea kusherekea miaka hamsini ya uhuru  kama wadau wengi walivyowahi kusema kuwa  "ANGALAU sasa Watanzania tunaweza kujivunia muvi (filamu) za nyumbani”

Kanumba aliwahi kusema kuwa “Filamu za kitanzania zina historia ndefu tofauti na wengi wanavyofikiria. kuliwahi kuwepo na filamu kama vile Fimbo ya Mnyonge (1974), Harusi ya Mariam(1983) na Yomba Yomba(1983) na nyinginezo ambazo ziliwahi kutamba sana enzi hizo. Baadaye idara ya filamu ikapotea kabla ya kupigwa kikumbo na sanaa ya maigizo” aliendelea kusema kuwa      

"Mabadiliko yapo,tena makubwa sana.Kwanza utaona kwamba mimi nilipoanza nilianzia kwenye kucheza tamthiliya na hivi sasa nimeacha kucheza tamthiliya na badala yake nacheza filamu peke yake. Hivi sasa ili aone ninachofanya inabidi ununue filamu”.

Maneno haya ya Msanii maarufu wa tasnia ya filamu Tanzania Kanumba yanaukweli ndani yake na yanaashiria kuwa kumekuwapo kwa maendeleo ya ukuaji wa tasinia ya filamu kutoka hatua moja hadi nyingine katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru;  

Wasanii wote wa Filamu wa hapa Nyumbani wake kwa wanume wanahitaji kupongezwa, kwa kuthubutu katika kufanikisha ukuaji wa tasnia ya filamu Tanzania; wasanii kama Steve Kanumba, Vincent Kigos (Ray), Blandina Chagula (Johari), Emmanuel Myamba (Pastor), Jacob Stephen (JB), Aunti Ezekiel, Steve Mangere (Nyerere), Irene Uwoya, Jackline Wolper Wema Sepetu Monalisa nimewataja baadhi na wengine wote ambao wanaendelea kukuza fani hii ya filamu Tanzania. Binafsi ninafahamu ugumu wa technolojia na mazingira ambayo yana mchango mkubwa sana katika ubora wa tasnia hii ya filamu. kweli kazi ni ngumu.Pia nawapongeza si kwa sababu eti wanatengeneza film nzuri ,Hapana ,ni kwa sababu wachache waliojitokeza katika fani hiyo wamethubutu katika kuleta  mapinduzi makubwa sana ya tasnia hii;


Tasnia ya filamu Kwa taifa linaendelea kuwa ni kioo cha jamii, basi kuna kila sababu ya   Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wasanii ambao ndiyo kioo cha jamii yetu; Nia ya wasanii ni kufikisha ujumbe kwa jamii,ujumbe ambao utaibadilisha jamii, utaielimisha kwa kupitia maudhui hayo ya  kuburudisha.  Ujumbe ambao utaleta mabadiliko chanya kwa jamii na siyo mabadiliko hasi, ambayo yanaliengua taifa katika mhimili wa kujisifu kupitia tamaduni zetu wenyewe.

Sina uhakika kutika kipindi hiki cha miaka 50 Wasani wetu wa tasnia ya filamu wameshawahi kujiuliza maswali  haya

·        Mimi ni nani?
·        Thamani yangu ya usanii katika tasnia ya filamu  inatokana na nini?
·        Je ni mambo gani ambayo yamejitokeza katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru na maendeleo ya filamu Tanzania
·        Ugumu wa soko la filamu katika kipindi hiki umekuwaje?
·        Je wasanii wa filamu wamekabiliwa na Ukosefu wa   creativity katika filamu zao?
·        Je namna gani kama wasanii mnakuza vipaji vyenu au mnabaki kuutafuta umaarufu baada ya kutafuta njia ya kujiendeleza na kukuza vipaji vyenu ili kazi zenu ziwe bora zaidi kwa faida yenu na taifa kwa ujumla wake?
·        Kwa nini  wasanii wetu wanakuwa wagumu wakianza kufanikiwa  wakatenga pesa na kwenda kujiendeleza kama Chuo cha sanaa bagamoyo? 
·        Ni kweli kuwa  Wasanii wengi hujibweteka na vipaji vyao wanapoanza kufanikiwa na kuanza kufanya anasa nyingi  na kuanza kujidhalilisha na kuanza kupoteza utu wao na fani yao na hatimaye "kufulia"


Kama wasanii wetu watafanikiwa kuyajibu maswali haya, hii itawasaidia kutambua kwamba thamani ya mtu haitegemei watu wengine wala wanavyosema, hata si umbo alilo nalo, bali ni hali ya ndani. Thamani ya mtu ipo ndani ya utu wake, yaani nafsini mwa mtu mwenyewe. 


Je ni ushauri gani wasanii wetu wanatakiwa waufuate ili kuimarisha sanaa zao na maendeleo yao?

·  shauri wajiendeleze kimasomo na kuijishughulisha na maswala ya maendeleo kuliku ubishoo usiokuwa na maana.


·  Suala la kuigiza uhalisia mimi naamini ni kitu kinachowezekana


·   Ni vema kuiga hekima na busara za waliondelea na kuacha yale yasiyofaa


·        Ili filamu iuze nakala nyingi siyo lazima wahusika wavae nusu uchi au waonyeshe matendo ya aibu, bali ni umahiri wa kuigiza,kipaji na nidhamu katika uigizaji.


·     Wasanii wetu wanatakiwa kukuna vichwa sana na kubadilika kulingana na dunia inavyokwenda.


·        Kupunguza matendo ya ambayo yanakiuka maadili  na kuacha tabia za uhuni kwa wasanii wote wa kike na wa kiume heshima ya kila mtu sio uhuni ni maadili mema, na kuwajibika kwa ajili ya mafanikio yao binafsi.

ni ukweli kuwa katika kipindi hiki cha miaka 50, Mimi nafikiri kosoro ambazo zimeelezwa, waigizaji wetu na waongazaji wa filamu wazichukue kama changamoto.  Ni kweli kuwa kwa sasa Soko limetanuka bado lakini Safari bado ni ndefu japo kwa wasanii angalau inatia moyo. Kwa hili pengine ushahidi tunao kutoka kwa Kanumba na Ray ambao wamewashukuru wateja wao kwa kuwawezesha  kumiliki usafiri wa gharama kubwa kupitia kazi zao.





Wasanii wote wakumbuke kuwa maendeleo yao yataendelea kupatikana tu kama watakuwa tayari kubadilika; tunazipenda kazi zenu lakini lazima ziwe katika kiwango bora cha kuangaliwa kulingana na maudhui ya kufundisha na sio kuwa kazi ambazo kila siku wanatuonyesha kitu kimoja chenye maudhui yanayofanana.


Kuelekea miaka 50 ya uhuru ni vyema wanafilamu wetu mkabadilika kwa masilahi yenu wenyewe na taifa kwa ujumla; mbembwe nyingi ambazo hazina tija hazitawasaidia sana kujinasua kwenye ugumu wa maisha ya kisanii bali creativity katika utendaji  na uandaaji wa filamu zenu ndio silaha pekee ya mafanikio yenu;

MUNGU IBARIKI TASNIA YA FILAMU TANZANIA IENDELEE KUSONGA MBELE

Friday, November 18, 2011

AMANI YA KWELI HULETA MATUMAINI;




JE AMANI TUYAHUBIRI SASA KUELEKEA MIAKA HAMSINI YA UHURU WA TAIFA LETU INAMWELEKEO WA KULETA MATUMAINI NA MAENDELEO KWA TAIFA LETU?

JE AMANAI HUZAA UPENDO MIONGONI MWETU?
JE HIVI SASA TUNAHUBIRI AMANI AU UNAFIKI  WA KUBOMOA TAIFA kwa masilahi binafsi?

Mwandishi  Ezekiel Kamwaga, KATIKA MOJA YA MAKALA ZAKE  aliwahi andika kuwa  “Bila ya UPENDO miongoni mwa Watanzania, taifa hili halitakwenda popote. Tutabaki tu kuwa nchi ya manyang’au”.

Wakati tuapojianda kusherekea miaka hamsini  ya uhuru wa taifa letu kuna mambo mengi tumejifunza na tunaendelea kujifunza katika kuhakikisha kuwa amani ambayo waasisi wetu wametuachia  hatuko tayari kuipoteza; tatizo langu je mikakati yetu ya kudumisha amani yetu ni imara au inayumba kwa hivi sasa? Na kama inayumba inayumbishwa na nini?

Ni ukweli ambao hatuwezi kuuficha kuwa kwa hivi sasa wananchi wengi  wanajaribu kutathimini uzoefu wa sera za vyama vyao ambao ndio chimbuko  linalotumika kuidumisha amani nchini. wananchi na wananchama katika kipindi hiki cha sasa wanachukua kwa hamu fursa hii ya demokrasia  ili kushiriki katika shughuli za vyama vyao katika kuleta maendeleo, lakini pengine kwa wengine wanaishiwa na hamu mara moja baada ya kuona pengine ni kwa namna gani chama kinaweza husika katika kuhatarisha amani kwa kuleta vurugu, na hivyo kuhatararisha utawala wa sheria ndani ya  demokrasia huru  ambayo huwa kama ni  kikwazo kwenye fikra bunifu katika fursa  ya kujenga  amani ya kweli.

Kama nilivyowahi kusema huko nyuma katika makala zangu kuwa tusipo ongeze jihudi za  uwekezaji wa elimu ya uraia (civic education) kwa wananchi na wanachama wa vya vyama mbalimbali vya siasa amani tunayotamani kuitunza itabaki kuwa ni ndoto; ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelewa haki zao za msingi na matumizi ya sheria ndani ya demokrasia, hii ni fursa pekee katka kuhakikisha  kuwa tunakuwa na amani yenye vigezo vya juu vya ubora, lakini  tukishindwa kufanya hivyo tutaendelea kudhoofisha sana juhudi zetu za kudumisha amani na upendo katika taifa letu.

Katika kipindi hiki tukiwa tunajiandaa kusherekea miaka hamsini ya uhuru  wa taifa letu si vibaya kujiuliza  amani bora inapatikanaje? Au amani bora hujengwa na watu au inashushwa tu kama neema kwetu kama taifa kutoka Kwa Mwenyezi Mungu?

Je yale yanayofanyika hivi sasa sehemu mbali mbali ya nchi yetu na wanachama mbalimbali wa vyama vya siasa na kusababisha vurugu kwa kivuli cha demokrasia, ni sehemu ya kudumisha amani yetu? Je wananchi na wananachama wa vyama husika wanaelewa nini wananchofanya au ni kufuata tu mkumbo bila kuelewa kwa undani kwa nini kitu fulani kinatokea na kwa nini mimi nikipiganie? Je ni kwa sababu kiongozi wangu ndio amesema nifanye hivyo? Au kwa vile rafiki yangu amefanya hivyo?

Nionavyo mimi Kama wananchi na wananchama wa vyama mbalimbali watendelea kufuata kila jambo kwa mkumbo kwa kweli Watabaki wamefungiwa katika hali ya hasara, bila uwezo wa kushindana; watakuwa wakitumika katika uchumi na utamaduni wa utandawazi kwa masilahi ya wachache na kuwajengea umaarufu watu wachache na pengine kwa undani na hawatakuwa na masilahi na wengi.  Na wataendelea tu  kudumaza vichwa vyao na kuwatia ganzi ya usikivu na utiifu, badala ya kuwapatia ujuzi na kuwapa nyenzo wanazohitaji kuwafanya wabunifu na watu wa fikra, watabaki kama tulivyo leo: wenye mapungufu, tusiotimilika, usiowashindani, na, kama kundi, maskini kiuchumi.

Lakini siyo lazima iwe hivyo. Maamuzi tunayofanya leo yanaweza kuwasaidia wananchama  kuwa watetezi wa mawazo yao wenyewe, pamoja na mitazamo na misimamo yao. Wananchama wanahitaji kuwa na ufahamu na ujuzi unaoweza kutumika katika mazingira yanayobadilika. Wanahitaji uhodari na imani ya kuamini silika zao. Wanahitaji nidhamu ya kufikia kilele cha uwezo wao.

Pengine vyama vyetu vimejikita katika mawazo yaliyokuwa sahihi kwa wakati uliopita. Wengi wetu tumezoea kufikiri kuwa siasa na vyama vya siasa ni sehemu tu ya propaganda ambayo  wanasiasa wanajifunza kutoa propaganda pengine kwa  kukariri kilichoandikwa ndani ya ilani ya chama husika hata kama hawaelewi na hawawezi kupambanua vizuri. Kwa kufanya hivyo nafikiri tunalenga kuwajengea hofu ya kuvunja sheria na madhara yake. Ikiwa hivyo basi vyama vyetu vinajiendesha kwa kuwatisha na kuwajengea wachama nidhamu ya woga ili wafanye yanayotarajiwa kutoka kwao nafikiri ina madhara makubwa kwa kuzingatia kuwa;

1    Kila mmoja anakubali kuwa watu wazima wana nafasi muhimu katika kuelekeza makuzi yamawazo yao ndani ya chama.

2    Tatizo ni wengi wa wananchama hawa  wanatoka katika  katika mazingira ambayo hawafahamu sana elimu kuhusu haki zao za msingi ndani ya vyama vyao na nje ya vyama vyao wamebakia kuwa na kiwango kidogo sana cha uwezo wanaohitaji ili kufanikiwa katika kueelewa na kumbambanua maswala mbali mbali ya  kisiasa.

3    mara nyingi inawezekana kuwa viongozi wa vyama wanaweza  kulazimisha utiifu kwa muda mfupi na kujenga chuki na uasi kwa muda mrefu miongoni mwa wananchi wa jamii moja. Wananchama  wengi wa vyama kutokana na kukosa elimu ya uraia  wanabaki kuwa wananchama watiifu na waoga wanajifunza kuendana na njia zilizozoeleka za kuwa na za kufikiri na, kwa hiyo, hawaendelezi stadi za lazima kuleta majibu muafaka kwa matatizo mapya.

Je, huku siyo kuwa tunashindwa, licha ya kudhani tumefanikiwa kuwaelimisha wananchama wetu? Kutokana na mahitaji yetu ya haraka ya watu wabunifu na wenye fikra?  Je tunajifunza nini kutokana na migomo, machafuko ambayo yanasababisha watu kujeruhiwa katika kipindi hiki tunavyoelekea kusherekea miaka hamsini ya uhuru wetu?

Nafikiri kama tutafanikiwa kuwafanya wananchama wetu wawe na elimu  ya uraia na itasaidia Kukuza utambuzi:  kujifunza wajibu wao katika kuhusiana na wengine. Ukuaji kimaadili: Kupitia miundo ya kidemokrasia na uwajibikaji, kuwa mfano mzuri wa kuigwa, na sera endelevu, elimu bora ya uraia  huendeleza uwezo wa wananchi  kushiriki kutekeleza sera hizo na kuonyesha hali ya kujali kama raia. Elimu bora  hupalilia viwango dhahiri vya maadili ambavyo huwasaidia wananchi kujijengea ndani mwao mfumo wa maadili kwa maisha yao yote.

Kama tutafanikiwa kuwa na Vyama bora vya siasa vitasaidia sana kuleta haya yafuatayo;

• kujenga nidhamu chanya ndani ya chama chake na vyama vingine,

• kudumisha  kuheshimu na utu wa kila mwananchi wa taifa letu.

• kuimarisha amani ambayo sisi kama taifa tunaipigania kuilinda kwa nguvu zote.

 Ni ukweli kuwa katika kipindi hiki cha miaka Hamsini ya uhuru, wananchi walio wengi wamebaki kwenye kifungo cha mzunguko wa hali ngumu na umaskini wa kujua haki zao za msingi kwa ukosefu wa elimu bora ya uraia. Wananchi wengi wamebaki kuwa wapokeaji na watekelezaji wa sera za viongozi wao hata kama sera hizo haziwanufaishi wao wananchi.

Kupitia elimu ya uraia tunajifunza kuwa  Kuongoza ni kuwasiliana.  Ili uongozi uwepo, tunahitaji walao watu wawili ambao kwa kiasi fulani wanashirikiana na kuhusiana.  Kwa maneno menginekatika duru za kisiasa tunahitaji chama zaidi ya kimoja ili kuleta ushindani wa kimaendeleo;Hakuna awezaye kuongoza akiwa katika upweke.  Kwa hiyo, uongozi ni mojawapo ya aina za mawasiliamo. Kuna uhusiano mkubwa kati ya jinsi mtu anavyoongoza na jinsi anavyowasiliana na wengine;

Je katika kipindi hiki cha miaka hamsini tumeongoza vipi? Au tumewasiliana vipi katika kuliletea taifa hili tija ya maendeleo kwa kigezo cha amani na utulivu?


Hayati Mwalimu Nyerere katika harakati zake zote za uongozi  alijua anahitaji sana hali ya amani, utulivu na ushirikiano katika kujenga nchi mpya, nchi huru. Mwalimu alitambua vile vile nchi ilikuwa na makabila mengi zaidi ya 120 yaliyokuwa na lugha, mila na desturi zinazotofautiana, na ingekuwa vigumu kuongoza watu wasioelewana kifikra, na tofauti nyingine nyingi.

Alijua tofauti hizi zingeweza kuchochea chuki na hivyo kuondoa matumaini ya kuwa na amani na maendeleo. Baba wa taifa Mwalimu Nyerere alifahamu kuwa watanzania kuelimishwa juu ya haki zao ili waweze kuzidai si kuvunja amani, amani ya kweli ni ili ambayo imejengwa katika misingi ya ukweli, haki na democrasia ya kweli. Amani ya kweli ni uwepo wa haki na uwajibikaji wa viongozi.

Kwa hiyo tunakila sababu ya kuhakikisha kuwa amani ambayo tunayo tunaendelea kuilinda kwa nguvu zote; tunawaomba wapinzani waendelee kutufunua kuikosoa serikali pale ambapo inakiuka na inashindwa kuwajibika; ni ukweli kuwa mengi tulikua hatuyajui tunafikiri kila kitu kinachofanywa na serikali ni sawa. Analisho kwa vyama vya upinzani tunaomba chonde chonde tupitisheni katika barabara sahihi ya kudai haki zetu au unapoiwajibisha serikali, tunatamani sana amani ambayo tunayo iendelee kuwako kwa miaka mingine hamsini inayokuja, vurugu na hasira zitahatarisha amani yetu;

MUNGU IBARIKI TANZANIA NA TUENDELEE KUKUMBUKA KUWA “Bila ya UPENDO miongoni mwa Watanzania, taifa hili halitakwenda popote. Tutabaki tu kuwa nchi ya manyang’au”. NA ISIYO NA AMANI YA KWELI.