WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 31, 2014

Muuaji huyu wilayani Tarime asakwe kwa udi na uvumba

Katuni
Tumepokea kwa masikitiko makubwa mauaji ya kutisha na kinyama yaliyotokea katika wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa siku tatu mfululizo.
Hadi kufikia juzi, imeelezwa kwamba watu takriban wanane wasio na hatia, walikuwa tayari wamekwisha kuuawa.

Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na jambazi mwenye silaha katika mji wa Tarime mkoani Mara kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu hadi juzi Jumanne. Mmoja wa watu waliouawa ni askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Zakaria Chacha Mwita, ambaye ni mtoto wa marehemu Meja Jenerali Mwita Marwa.

Mbali ya Marwa, wengine waliouawa ni aliyekuwa Mhandisi Ujenzi Wilaya ya Rorya, David Mwasi Misiwa na  mfanyabiashara Samuel Richard Mohenga.

Tunalaani kwa nguvu zote mauaji haya dhidi ya raia hao wasio na hatia yoyote na ambao walikuwa na haki yao ya msingi ya kuendelea kuishi.

Vifo vya Watanzania hao siyo tu pigo kwa familia zao hususani wategemezi wao, lakini pia ni hasara kwa Taifa kutokana na kuondokewa na sehemu ya nguvu kazi yake.
Mpaka sasa, bado haijafahamika lengo la muuaji huyo maana katika mauaji yote hayo, hayafafanui kama mhusika alichukua mali zozote.
Kwa hakika, mauaji haya yamemshtua kila mpenda amani maana kwa sasa ndugu zetu wa wilayani Tarime na vitongoji vyake, wanaishi kwa hofu kubwa. Hofu hiyo inaweza kuhatarisha uchumi wa wilaya hiyo ya kibiashara na yenye rutuba nzuri kwa kilimo kuporomoka kwa kuwa kila mwananchi hatakuwa huru na amani kufanya shughuli zake za uzalishaji mali.

Ni kwa msingi huo basi ndipo tunapoishauri serikali kwa kutumia vyombo vyake vya usalama, kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba muuaji huyo anakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Tunashukuru kwa hatua hizi za awali ambazo tayari Jeshi la Polisi nchini limeanza kuzichukua katika kumsaka mhalifu huyo.

Moja ya hatua zilizoanza kuchukuliwa kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, ni kutuma timu maalum kutoka makao makuu ya jeshi hilo inayohusisha kamisheni ya operesheni kufanya uchunguzi.

Naye Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alisema polisi wanafanya msako katika vijiji vya Kenyamanyori, Rebu, Nkende, Mogabiri na Kibumaye katika kata za Kitare, Turwa na Binagi kwenye tarafa ya Inchage wilayani Tarime.

Hata hivyo, pamoja na juhudi hizi zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi nchini, tungewaomba wananchi nao kwa upande wao, kutoa ushirikiano kwa Polisi kwa kutoa taarifa za kuwezesha mtuhumiwa huyo kutiwa nguvuni.

Tuna imani kubwa kwamba kama wananchi watakuwa tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi, kwa vyovyote vile mhalifu huyu atanaswa tu tena katika kipindi kifupi kijacho.

Tunasema atanaswa katika kipindi kifupi kijacho kutokana na ukweli kwamba mhalifu huyu ni binadamu mwenzetu ambaye bila shaka tunaishi naye majumbani mwetu na hata kama anajificha, bado anapatiwa huduma za msingi miongoni mwetu. Sisi tunawashauri Watanzania kamwe wasikubali kumficha mtu wa namna hii kwani ni mtu hatari katika jamii.

Tunachopaswa kufahamu ni kwamba leo amethubutu kuwaua watu hao wanane wasio na hatia yoyote, basi kesho haitakuwa ajabu akikugeukia wewe unayemficha na kukuua pia.
Aidha, tunashukuru pia kwa hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime kwenda kutembelea maeneo ya vijiji ambavyo wakazi wake wameuawa na jambazi hilo.
Hatua hiyo ni muhimu kwa kuwafariji waliopoteza wapendwa wao na pia inatia hamasa kwa wananchi na kujiona kwamba serikali inalichukulia tukio hilo kwa uzito unaostahili.

Hali kadhalika, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, alifafanua kuwa timu iliyotumwa eneo la tukio, ni ya wapelelezi na Intelijensia na inakwenda kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa na mkoa wa Mara kuhakikisha jambazi huyo anakamatwa ili kuondoa hofu kwa wananchi. Mauaji hayo ni mfululizo wa mauaji mengine ya kinyama mkoani Mara lakini yanayowalenga zaidi wanawake.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa mpaka sasa wanawake watano wameuawa katika mazingira ya kutatanisha kwenye wilaya za Musoma, Butiama na Rorya mkoani Mara.
Ni muhimu Jeshi la Polisi sasa likajipanga zaidi kuhakikisha kwamba wote wanaoendesha mauaji haya ya kinyama mkoani Mara wanadhibitiwa.
 
CHANZO: NIPASHE

Chadema kususia Bunge la Katiba ikiwa...


Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema wabunge wa chama chake watasusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa hoja ya kuundwa kwa Serikali tatu itapingwa na wabunge wa CCM, Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu ametaka kuvunjwa kwa Muungano.

Akihutubia kwenye Uwanja wa Tubuyu nje kidogo ya Mji wa Morogoro juzi, Mbowe alisema wabunge wa chama chake wataandamana nchi nzima kufikisha ujumbe kwa wananchi kwamba maoni yao yamepingwa na wabunge wa CCM walio wengi.

"Tutawaeleza wananchi kwamba maoni ya CCM ndiyo yameonekana ya maana kuliko ya wananchi ambao ni wengi zaidi," alisema Mbowe kwenye mkutano huo ambao ni sehemu ya Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko - M4C Pamoja Daima.

Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya maoni na kubaini kuwa asilimia 62 ya Watanzania wanataka Serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.

"Serikali ya CCM haitaki kusikia maneno Serikali tatu wanasema sera yao ni ya Serikali mbili, wanafanya kila hila ili kuikataa hoja hiyo. Natangaza kwamba wakifanya hivyo tutasusia na kwenda kuwashtaki kwa wananchi," alisema Mbowe.

Aliongeza kwamba wataandamana kuanzia Kagera hadi Mtwara kuwaeleza wananchi kwamba hoja yao imepingwa na CCM.

Mbowe alisema baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa kashfa dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwamba amechukua maoni ya Chadema.

"Wanakosea hayo si maoni ya Chadema, bali ni maoni ya wananchi, Warioba amezingatia maoni ya wananchi," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema Katiba inayotafutwa si ya chama, bali ni ya Watanzania na kwamba inashangaza CCM kuipinga hoja Serikali tatu.

"Tunafahamu wanaogopa kuikubali hoja ya Serikali tatu kwa sababu wanafahamu huo ndiyo utakuwa mwisho wao wa kuwa madarakani," alisema Mbowe huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Alisema CCM wanaelewa kwamba kukiwa na Serikali tatu, Chadema kitashinda Tanganyika na CUF Zanzibar katika uchaguzi wowote utakaoitishwa.

"Kwa hiyo hivi sasa wana wasiwasi kweli, wanatafuta kila njia ya kuichakachua hoja ya Serikali tatu lakini wafahamu kuwa Chadema wanaifuatilia hoja hiyo kwa ukaribu," alisema.

Aliwataka wananchi kufuatilia Bunge Maalumu la Katiba litakapoanza mwezi ujao ili kuangalia wabunge wao wanavyowawalisha katika suala hilo muhimu.

Hata hivyo, Mbowe alisema chama hicho kikishinda katika uchaguzi wa mwaka 2015 hakitahangaika kulipa kisasi kwa kuwachukulia hatua za kisheria viongozi, bali kitajikita kutafuta maendeleo.

"Wasituogope tutasamehe kama alivyosamehe aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Hatutalipa kisasi tukiingia Ikulu, kwa sababu hakuna binadamu asiye na makosa. Tutaelekeza nguvu zetu kuwaletea maendeleo Watanzania," alisema Mbowe.
Jussa na Muungano

Akihutubia mkutano wa kampeni katika Jimbo la Kiembesamaki jana, Jussa alisema hakutakuwa na maendeleo yatakayofikiwa Zanzibar ikiwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hautang'oka.

Jussa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la CUF, alisema Zanzibar yenye watu milioni 1.5 haiwezi kuwa na tatizo la watu kukosa ajira lakini sera na mipango ya kiuchumi imekuwa ikikwama katika utekelezaji wake kutokana na kukosa mamlaka kamili.
Alisema Zanzibar haiwezi kukopa katika taasisi za kimataifa bila ya kuwekewa dhamana na Waziri wa Fedha wa Muungano wakati Zanzibar ni nchi na kuwataka wananchi kutumia kura zao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuleta mabadiliko ya kiutawala.

"Hakuna sababu ya vijana Zanzibar kukosa ajira, kuna watu wasiozidi milioni 1.5, Muungano umefika wakati ung'oke, ndiyo kikwazo cha maendeleo ya Zanzibar na watu wake kiuchumi na kisiasa," alisema Jussa.

Alisema mradi wowote unaobuniwa Zanzibar hauwezi kupata mfadhili bila kuwekewa dhamana na Serikali ya Muungano na kukwama kwa juhudi zote za kujiunga na jumuiya za kimataifa akitolea mfano Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Alisema Rais wa Zanzibar amepoteza mambo muhimu chini ya mfumo wa Muungano ikiwa ni pamoja na kutopigiwa mizinga 21 akiwa nje ya nchi, kupeperusha bendera ya Zanzibar, kutokagua gwaride na kupigiwa wimbo wa Taifa la Zanzibar.

"Haya ya sasa si mamlaka kamili, wapi Dk Shein alikokwenda akapigiwa mizinga 21 au alipeperushwa wapi bendera ya Zanzibar wakati wa safari zake za nje?" alihoji Jussa.

source: mjengwa blog

Thursday, January 30, 2014

Azam yaing’oa Yanga kileleni


Mshambuliaji wa Azam Kipre Tchetche akipiga shuti langoni mwa timu ya Rhino Rangers huku mabeki wa
Dar es Salaam. Azam wamekalia usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya  Yanga kulazimishwa sare 0-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Azam wamekalia uongozi ligi hiyo baada ya kuichapa Rhino Rangers kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, na kufikisha pointi 33, huku Yanga wakiwa na  pointi 32 na Mbeya City (31) wakibaki nafasi ya tatu baada ya kulazimishwa sare 1-1 na Ruvu Shooting.

Mshambuliaji Kipre Tchetche ameendelea kuibeba Azam baada ya kuifungia bao pekee dakika 26, kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiunganisha pasi ya Mohamed Kone.

Tchetche amefikisha mabao tisa hadi sasa akiwa nyuma kwa bao moja kwa kinara wa ufungaji Amisi Tambwe wa Simba mwenye magoli 10.

Tanga; Mabingwa watetezi Yanga, watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi  walizozipata katika kipindi cha kwanza baada ya kupata kona sita katika dakika 30 za kwanza kabla ya wenyeji Coastal Union kuamka.

Kiungo Haruna Niyonzima alikosa bao baada ya shuti lake kudakwa na Shaabani Kado dakika 12, mashabiki wa Yanga dakika 29 walirusha chupa za maji uwanjani kupinga uamuzi wa mwamuzi wa mchezo huo, Simon Mbelwa, Pwani.

Wenyeji Coastal Union waliamka dakika ya 30, na kuanza kushambulia, lakini mashuti ya Yayo Lutimba, Haruna Moshi na Kenneth Masumbuko yaliokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa Deo Munishi wa Yanga.
Mlandizi, Wenyeji Ruvu Shooting wameipunguza kasi Mbeya City baada ya kuilazimisha sare 1-1 kwenye Uwanja wa Mabatini

Shooting walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Jerome Lembele dakika 4, kabla ya City kusawazisha kupitia Deus Kaseke dakika 14.

Kagera Sugar wameendelea kusuasua baada ya kulazimisha sare 0-0 na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kaitaba.

Mashabiki Yanga wapata ajali Tanga
Mashabiki wanaodhaniwa wa Yanga, wamepata ajali wakiwa safarini kuelekea mkoani Tanga kuishangilia timu yao ikivaana na Coastal Union.

Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Tange karibu na Tanga mjini jana wakiwa kwenye gari lao aina ya Toyota Noah.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Polisi wa Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki katika ajali hiyo alikuwepo Meneja wa Bendi wa Jahazi Modern Taarab, Ally Boha ambaye yeye ni majeruhi.

Aliwataja wengine waliopata majeraha ni dereva wa gari hilo aliyemtaja kwa jina moja la Yasini, Kondo Karume na Mbaraka Madenga ambao wote wamepata matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo.

“Haikuwa ajali ndogo, lakini kikubwa cha kushukuru kuwa waliokuwepo kwenye ajali hiyo wote wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya mkoa wa Tanga.
Vikosi

Coastal: Shaaban Kado, Hamad Hamis, Abdu Banda, Mbwana Hamisi, Juma Nyoso, Jerry Santo, Daniel Lyanga, Chrispine Wadenya, Yayo Lutimba, Haruna Moshi, Kenneth Masumbuko

Yanga: Deogratius Munishi, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na David Luhende.

Imeandaliwa na Burhan Yakubu (Tanga), Sosthenes Nyoni  (Dar), Msafiri Sanjito (Pwani), na William Paul (Kagera)

SOURCE: mwananchi blog

YANGA WAMEMNUNUA WAPI EMMANUEL OKWI?




Na BARAKA MBOLEMBOLE
Wakati ligi kuu ikianza, mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi, Mganda, Emmanuel Okwi amekuwa mmoja wa watazamaji mwenye thamani kubwa. Je, Yanga wameingia ' mkenge' katika usajili wake?. Hili linaweza kuwa swali ambalo majibu yake yapo wazi. Kwanza, Okwi ni mchezaji wa Etoile du Salehe ya Tunisia ambao walimnunua kutoka timu ya Simba.

Kwa nini yupo Yanga?. Alikuwa akiichezea timu ya SC Villa ya kwao Uganda kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita akitokea Etoile. Narudia tena, alikuwa akiichezea Villa kwa mkopo. Fifa ilimruhusu Okwi kucheza Villa kwa muda wakati kesi tatu zinazomuhusu Mganda huyo zikitafutiwa mhuafaka. Okwi kwa upande wake anadai kuwa Watunisia hao walivunja mkataba kwa kushindwa kumlipa pesa zake kama ilivyotakiwa. Simba nao wanadai malipo yao kutoka kwa Etoile.

Okwi aliruhusiwa kuichezea Villa ili kulinda kiwango chake, na wala hakuwa mchezaji anayemilikiwa na timu hiyo. Alizuiwa kuichezea timu ya Taifa ya Uganda katika michuano inayoendelea ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani, CHAN, kwa kuwa alikuwa Villa kwa mkopo kutoka timu ya ng'ambo. Ila, ni Villa ndiyo wanaosemekana kumuuza Okwi kwa timu ya Yanga. Kwa mamlaka gani?. Hadi hapa Yanga watakuwa wameliwa. Kwa kuwa Okwi ni mchezaji wa Etoile si Villa.

Yanga wamemsaini Okwi huku wakijiaminisha kuwa wapo sahihi. Wanaamini Okwi ni mchezaji huru au wa Villa. Ila, alitakiwa kucheza Villa kwa miezi sita, lakini akaitumikia miezi isiyozidi miwili tu na kununuliwa. Caf, Shirikisho la soka Afrika wamemuhidhinisha Okwi kuichezea Yanga. Kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji imemzuia matumizi yake hadi watakapopata ufafanuzi kutoka FIFA, Shirikisho la soka ulimwenguni. 
Ndiyo, wapo sahihi kwa kuwa FIFA, ndiyo waliosema mchezaji huyo acheze Villa kwa miezi sita wakati kesi zake zikishughulikiwa. 

FIFA, wanaweza kumruhusu Okwi kuchezea Yanga kwa maslai ya kipaji chake. Ila, wanaweza pia kumzuia endapo watajua kuwa mchezaji huyu amekiuka maagizo yao ya awali ambayo walimwambia acheze Villa. Inawezekana mchezaji huyo akaonekana tapeli, kwa kuwaadaa Yanga wakati akijua fika mkataba wake upo Etoile. Wapo wachezaji walioshinda vita kama hii ya Okwi, ila wapo pia walioingia katika vifungo vya FIFA. 

Huenda Yanga wakamtumia Okwi siku za mbele, ila kwa sasa ni uhalali wa mchezaji huyo. Kama, Etoile wataendelea kushikilia msimamo wao kuwa hawajui mchezaji wao mahali alipo, Okwi ataoneka ni mtoro. Endapo, Okwi ataonekana ni halali madai yake anaweza kulipwa fidia na Etoile, ila kasheshe ni wapi ambapo Villa walipata kibali cha kumuuza Okwi kwa timu ya Yanga?

Kila upande udai una wanasheria wake. Duh!. Lakini mwanasheria wa Okwi anaweza kuwa mjanja zaidi, mwenye akili zaidi, kwa kuweza kupata saini na mamillioni ya Yanga kwa ufafanuzi wake wakati akimpigia debe mteja wake kuwa hana tatizo. Kama sheria iliwekwa ili ivunjwe, na kama mikataba siku zote inaweza kutenguliwa, Yanga watamtumia Okwi, ila tusije kushangaa FIFA, wakisema mchezaji huyo mali ya Etoile. Yanga walimnunua wapi Emmanuel Okwi? Labda hapa ndipo kuna hoja ya msingi.

Source: shaffih Dauda blog

Wednesday, January 29, 2014

Mbowe apaisha homa serikali 3

 
Helkopta iliyobeba viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikitua katika uwanja wa mikutano wa Uhuru mjini Bukoba kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa hadhara.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema iwapo kutakuwa na uchakachuaji wa rasimu ya Katiba mpya na kuondoa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya mfumo wa serikali tatu, chama hicho hakitakubali na hatua madhubuti zitachukuliwa.
Mbowe aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Biharamulo mkoani Kagera na Chato, mkoani Geita.

Alisema katika Bunge Maalum la Katiba, vyama vya upinzani na wengine wanaounga mkono mfumo wa serikali tatu katika Bunge hilo ni wachache, lakini hawatakuwa tayari kukubali wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao ni wengi wakijaribu kuvuruga.

“ Kama noma na iwe noma, Chadema haitakubali wabunge wa CCM kupindisha na kukataa kupitisha serikali tatu, tuko tayari kwa lolote iwe kupigana ngumi na mieleka kuhakikisha kinaeleweka kuhusu serikali tatu,” alisisitiza Mbowe.

Alisema wananchi wengi wameonyesha kutaka serikali tatu, lakini wachache ambao ni CCM wanapinga na kwamba Chadema haitawaangusha wananchi bali itawatetea kuhakikisha wanachokitaka kinafanikiwa.

Mbowe alisema Katiba ni uhai wa Watanzania, hivyo ni bora siasa zikawekwa kando na kutanguliza uhai wa wananchi.

Mbowe alisema katiba za vyama zipo kwa ajili ya vyama vyenyewe, lakini Katiba ya nchi ni kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo inapaswa kuheshimiwa.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kama wanataka nchi itamalaki, ni vyema wakaheshimu maoni ya wananchi wengi ya kuwapo kwa serikali tatu.

Alisema Chadema inataka Katiba inayotengenezwa sasa iondoe makovu ya muda mrefu ambayo yaliwaumiza Watanzania.

Kwa mujibu wa Mbowe, zipo taarifa kuwa CCM wameanza kukaa vikao vya kukataa rasimu ya Katiba kwa sababu hawataki serikali tatu zilizopendekezwa na kwenye rasimu hiyo na kusisitiza kwamba jambo hilo halitakubalika bali watapambana ili njama hiyo isifanikiwe.

Mbowe anaendelea na ziara yake na leo anatarajia kufanya mikutano mbalimbali mkoani Iringa.

SLAA: VIJANA JIANDIKISHENI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akizungumza jana mjini iringa, aliwataka vijana kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.

Akiwahutubia wananchi katika viwanja vya Mwembetogwa, Dk. Slaa pia aliwataka vijana nchini kuachana na propaganda ambazo hazina maana yoyote kwao.

Sambamba na hilo, aliwatahadharisha Watanzania kuwa kwa sasa nchi inaingia kwenye deni la Sh. trilioni 25 huku wananchi wakililipa taratibu bila wao kujua na kuhoji kuwa deni hilo limetokana na nini.

Alisema mwishowe wananchi ndiyo watakaoumia kwa kukatwa kupitia kodi.

LISSU ALIA NA WASALITI
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, akiwahutubia wakazi wa mjini Dodoma katika viwanja vya Barafu jana, alisema hawataacha kuwashughulikia wale wote watakaobainika kukihujumu chama hicho.

Naye Mwenyekiti cha Baraza la Vijana la Chadema Taifa (Bavicha), John Heche, ambaye aliambatana na Lissu katika ziara hiyo, alisema ni lazima daftari la kudumu la wapigakura lirekebishwe kwani hadi sasa kwa mujibu wa sensa ya baraza hilo, takribani vijana milioni 5.5 nchini kote hawajajiandikisha kwenye daftari hilo.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Biharamulo; Agusta Njoji, Dodoma na George Tarimo, Iringa.
 
CHANZO: NIPASHE

Shein atema moto Z'bar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema kuwa wanaotaka mamlaka kamili ya Zanzibar waondoke.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, alitoa kauli hiyo wakati akiwahutubia wananchi na wanachama wa CCM katika mkutano wa uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Bila kutaja jina la mtu yeyote wala kikundi chao, au walau kueleza wanaotaka mamlaka kamili ya Zanzibar waondoke Zanzibar kwenda wapi, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina mamlaka yake kamili tangu mwaka 1964 baada ya Mapinduzi yaliokuwa halali na kuungwa mkono na wananchi na mataifa mbalimbali duniani.

Dk. Shein alisema Serikali ya Zanzibar ni serikali kamili yenye mihimili mitatu muhimu ya kuunda dola ambayo ni Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahakama.

“Wanaotaka mamlaka kamili ya Zanzibar nawashangaa sana kwani Zanzibar imepata mamlaka kamili tangu mwaka 1964 na inaongozwa na katiba yake ambayo inaheshimiwa,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein alisema hakuna mtu wala kikundi kinachoweza kuingilia mambo ya Zanzibar na wanaotaka serikali ya aina nyingine kwa njia ya mkato wasahau kwani jambo hilo halipo.

Alisisitiza kuwa wakati CCM inaadhimisha miaka 37 tangu kuanzishwa kwake wanaamini kwamba Muungano na Mapinduzi ndio nguzo kuu ya serikali.

Akizungumzia mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, alisema sera ya sasa ya CCM kuhusu mfumo wa Muungano ni wa serikali mbili.

“Wanaosema serikali tatu waache wasema, hiyo ndiyo sera yao, lakini na sisi tunasema sera yetu ni serikali mbili, nataka nirejee tena kwa wasiosikia kwamba nguzo ya chama chetu ni Muungano wa serikali mbili,” alisema Dk. Shein katika viwanja vya Kiembe Samaki mjini Unguja juzi jioni.

Wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya ya mtu mmoja mmoja na wakati wa kujadili rasimu ya katiba kupitia mabaraza ya katiba upande wa Zanzibar, liliibuka kundi ambalo lilitaka Muungano wa mkataba.

Wananchi hao pamoja na wanasiasa waandamizi wakiwamo wa CCM na Chama cha Wananchi (CUF) walipendekeza kuwapo kwa Muungano wa mkataba ambao pamoja na mambo mengine kuipa Zanzibar mamlaka kamili.

Walisema kuwa kuwa kuipa Zanzibar mamlaka kamili ni pamoja na kuirejeshea kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN).

Miongoni mwa waliohamasisha wananchi wapendekeze Muungano wa makataba na Zanzibar yenye mamlaka kamili ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
Kamati ya maridhiano ya Zanzibar ambayo inaongozwa na muasisi wa Chama cha Afro Shiraz (ASP), Ali Nassoro Moyo, nayo ilipendekeza Muungano wa mkataba.

Mwaka jana CCM ilimvua uanachama aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid, kufuatia kauli zake za kutaka Zanzibar yenye mamlaka kamili pamoja na Muungano wa mkataba. Mansour aliwahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya sita ya Amani Abeid Karume.

Akikabidhi taarifa na Rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete na Dk. Shein Desemba 30, mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema asilimia 60 ya Wazanzibari waliotoa maoni yao walipendekeza Muungano wa Mkataba.
 
CHANZO: NIPASHE

Monday, January 27, 2014

bunge la katiba kizungumkuti


arioba_28998.jpg

Dar es Salaam. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bado ina upungufu ambao utaathiri utendaji wa Bunge Maalumu, ambalo huenda likaanza Februari 11 mwaka huu, mjini Dodoma.
Sheria hiyo Namba 8 ya 2011, imeishafanyiwa marekebisho mara mbili yakiwamo ya Februari 2012 na Novemba 2013, lakini mabadiliko hayo yameacha kasoro ambazo zinapaswa zifanyiwe tena kazi, kupitia Bunge. (JM)

Kasoro zipo katika Kifungu cha 22 kinachohusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum, pamoja na kifungu cha 24 kinachozungumzia Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo wanavyoanza kutekeleza wajibu wao.

Kupitia Sheria ya Marekebisho (Na:2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013, Bunge katika mkutano wa 12, liliwapa mamlaka Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, 'kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge Maalumu'.

Watendaji hao kwa mujibu wa sheria ndio watakaoteuliwa kuwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu baada ya Rais kutangaza kuitishwa kwa Bunge hilo, lakini kiapo chao kitasubiri hadi pale watakapochaguliwa Mwenyekiti na Makamu wa Bunge hilo.

Sheria husika inaweka sharti kwamba ikiwa Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Muungano basi Katibu atoke upande mwingine na kinyume chake. Hivyo lazima wasubiri uchaguzi huo ili wajue ni nani Katibu na Naibu Katibu.

Kifungu cha 24 (2) kinasema: "Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu, watashika nyadhifa zao kwa misingi kwamba, endapo Mwenyekiti atachaguliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Katibu wa Bunge Maalumu atatoka upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano".

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tayari baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Bunge na ile ya Baraza la Wawakilishi (BLW) wameanza maandalizi ya awali katika moja ya hoteli za jijini Dar es Salaam.
Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah mbali na kukiri kuanza kwa maandalizi hayo, hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa maelezo kuwa lazima ashirikiane na Katibu wa Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, kutokana na mkanganyiko mkubwa uliopo katika Sheria hiyo, ni dhahiri watendaji hao watapata wakati mgumu katika kuanza kutekeleza majukumu, hasa katika kuteua wajumbe wa sekretarieti ya Bunge hilo.

Uteuzi wa wajumbe hao kwa mujibu wa kifungu cha 24 (4) unapaswa kufanywa na Katibu kwa kushauriana na Naibu wake, nafasi ambazo hazitakuwapo hadi pale Mwenyekiti na Makamu wake watakapochaguliwa. 

CHANZO MWANANCHI

Saturday, January 25, 2014

YANGA YAANZA MZUNGUKO WA PILI KWA KUTOA KIPIGO - YAICHAPA ASHANTI 2-1

 Raha ya ushindi.....Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao pili la timu hiyo dhidi ya Ashanti United.
 Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao pili la timu hiyo dhidi ya Ashanti United, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga imeshinda 2-1. Kutoka kushoto ni Frank Domayo, Simon Msuva na David Luhende. Yanga imeshinda 2-1.
 Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la ushindi wa timu yao dhidi ya Ashanti United. 
 Idd Seleman wa Ashanti United akimiliki mpira huku akizongwa na mchezaji wa Yanga, Simon Msuva.
 Davidi Luhende wa Yanga akiipangua ngome ya Ashanti wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika leo.
 David Luhende akimtoka Hussein Mkongo wa Ashanti wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
 David Luhende wa Yanga, akipiga mpira uliozaa bao la pili la timu yake. Huku Hussein Mkongo (kulia), akiwa hana la kufanya.
Benchi la ufundi la Yanga likiongozwa na  Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm (kulia), Kocha Msaidizi, Charles Boniface na Kocha wa Makipa Juma Pondamali.
Moja ya heka heka zilizotokea katika lango la Yanga.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm akitoa maelekezo kwa wachezaji wake.
 Kocha wa Ashanti, Abdallah Kibaden akitoa maelekezo kwa wachezaji wake.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm akibadilishana mawazo na David Luhende wakati wa mapumziko.
 
source: Shaffih Dauda Blog

Friday, January 24, 2014

Migiro, mustakabali wa nchi u-mikononi mwako




KATIKA mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika majuzi, inaweza kabisa kusemwa, kuwa Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Asha -Rose Migiro ndiye Mtanzania pekee kwa sasa aliyebebeshwa dhamana kubwa ya kuuongoza, kuusimamia na kuhakikisha unahitimishwa salama, mchakato wa nchi yetu kupata Katiba Mpya inayotokana na utashi wa wananchi, na si wa wanasiasa na vyama vyao. Hii ni dhamana kubwa. Ni heshima kubwa aliyopewa Asha-Rose Migiro. Hakika, iinaweza kusemwa, kuwa mustakabali wa nchi yetu uko mikononi mwake.

Ni dhamana yenye kumtaka aliyepewa, kuitanguliza haki. Namna yoyote ile, ya kwa makusudi au kwa hila, kujaribu kuipindisha haki, na hivyo kuwanyima walo wengi haki, itapelekea kwenye kupanda mbegu za chuki na ulipaji wa visasi. Mbegu za utengano kama taifa. Ni dhambi tutakayohukumiwa nayo kwa siku ama miaka ambayo hata sisi tutakuwa tumeshatangulia mbele ya haki. Na siku zote, hukumu ya kutotenda haki, kwa kudhamiria au kwa hila, hutolewa humu duniani, na huko tunakokwenda.

Na hakika, kama Mtanzania, mzaliwa na mzalendo wa nchi hii, nimefarijika kuisikia kauli ya awali ya Asha- Rose Migiro. Amenukuliwa akitamka; kuwa  moja ya majukumu atakayoyafanya ni kuhakikisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya unakwenda kama ulivyopangwa, huku akisisitiza kuwa hawezi kukipendelea CCM katika mchakato huo. Na akazidi kuongeza;

“Nitasimamia mchakato wa Katiba katika kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye Bunge la Katiba na baadaye Kura ya Maoni. Jambo zuri ni kwamba mchakato huu unakwenda kwa mujibu wa sheria. Nawahakikishia Watanzania nitafanya kazi kwa uaminifu na kujituma,” amenukuliwa akisema Waziri Migiro.

Na nyongeza hapa ni kuwa, kwa Asha-Rose Migiro, umma na umwamini, kuwa sio tu hawezi kukipendelea CCM ( Chama chake) katika mchakato huu, bali, haitarajiwi akipendelee chama chochote, kikundi chochote au mtu yeyote. Anatakiwa aipendelee Tanzania. Atangulize maslahi ya nchi kwa kutazama zaidi leo, kesho, keshokutwa na mtondogoo. Kwamba vyama vya siasa na viongozi wanakuja na kuondoka, lakini nchi itabaki.

Na ikumbukwe, katika hili la Katiba, yanayokuja ni mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika tangu mwaka 1977. Ni pale ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo wa 1977 yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa chama tawala na hata mfumo wa uongozi wa serikali.
Nimepata kuandika, kuwa katika dunia hii, mabadiliko ya kijamii husababisha mabadiliko ya kisiasa. Wanasosholojia wanasema, kuna sababu mbili zenye kufanya mabadiliko hayo; sababu za ndani ya jamii husika (endogenous) na sababu za nje ya jamii (exogenous).

Kwa upande wetu, tunaona kuwa, sababu za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma kwenye kufikia hatua hii ya kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.

Na kwa jamii yetu kwa upana wake, ina sababu za msingi  za kuyafurahia mabadiliko haya yanayokuja. Ni mabadiliko yenye kuleta matumaini mapya.

Na Rais kikwete , hadi kufikia hatua hii, ameonyesha ujasiri wake mkubwa  wa kiuongozi. Ni katika kuyafanya hata yale ambayo hayakufikiriwa kabla kwamba yangefanyika katika nchi hii.

Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni  nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi  au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini. Na imani ya wananchi kwa taifa na viongozi wao ni shina la matumaini  yao. Katiba yetu inayokuja  chachu ya kurudisha mioyo ya uzalendo kwa taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz: Maggid Mjengwa