WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, January 2, 2014

Waziri wa Fedha afariki dunia

marehemu Dk William Mgimwa akisoma bajeti ya wizara yake bungeni. 

Dar es Salaam na Iringa. Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Iringa, William Mgimwa amefariki dunia jana katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.
Habari zilizopatikana jana kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake, Habib Awesi zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli amefariki leo mchana tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kusema Waziri Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa 6:20).
“Kinachofanyika kwa sasa ni maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye kadiri zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na alishirikiana kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa limepoteza mtu makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea, jambo ambalo lilimfanya awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara (Fedha),” alisema Ndugai.
Kikwete atuma rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitoa taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,” ilisema taarifa yake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu... Natoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Steven Muhapa alisema jana kuwa wamepokea kwa mshituko kifo cha mbunge wao.
Muhapa alisema halmashauri yake imepata pigo la mwaka, kwani walikuwa na mipango mingi ya kutekeleza chini marehemu Mgimwa lakini sasa imeyeyuka... “Alisaidia sana kutuletelea wafadhili kutekeleza ahadi mbalimbali alizoahidi... ni mapenzi ya Mungu.”
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema Mkoa wa Iringa umepoteza mtu muhimu, mahiri na mchapakazi... “Pamoja na kwamba alikuwa CCM, hakubagua mtu. Niliwahi kumpa ushauri mara kadhaa akauchukua ushauri wangu na kuufanyia kazi.”
Mwenyekiti PAC
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amemwelezea marehemu kwamba alikuwa ni mtu mnyenyekevu na hakuwa na ubaguzi katika kutekeleza wajibu wake akiwa kiongozi wa Serikali.
“Kwa kipindi kifupi nilichofanya naye kazi kwa karibu, kwanza kwenye Kamati ya Fedha, nikiwa mkaribishwa kama Waziri wa Fedha kivuli, kisha kwenye kamati ndogo niliyounda kuhusu miradi ya umeme ya Mchuchuma, Liganga na Ngaka na baadaye akiwa Waziri wa Fedha, jambo la msingi nililoliona kwake ni unyenyekevu na heshima kubwa aliyonayo kwa watu wengine.
“Hakusita kuomba ushauri licha ya kuwa na tofauti za kivyama na kwa kweli ni Waziri wa Fedha niliyeelewana naye zaidi kuliko wengine wote waliopita nikiwa ama Waziri Kivuli au Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu.”
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Florence Majani, Joseph Zablon (Dar) na Geofrey Nyang’oro (Iringa).

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment