WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 24, 2014

Migiro, mustakabali wa nchi u-mikononi mwako
KATIKA mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika majuzi, inaweza kabisa kusemwa, kuwa Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Asha -Rose Migiro ndiye Mtanzania pekee kwa sasa aliyebebeshwa dhamana kubwa ya kuuongoza, kuusimamia na kuhakikisha unahitimishwa salama, mchakato wa nchi yetu kupata Katiba Mpya inayotokana na utashi wa wananchi, na si wa wanasiasa na vyama vyao. Hii ni dhamana kubwa. Ni heshima kubwa aliyopewa Asha-Rose Migiro. Hakika, iinaweza kusemwa, kuwa mustakabali wa nchi yetu uko mikononi mwake.

Ni dhamana yenye kumtaka aliyepewa, kuitanguliza haki. Namna yoyote ile, ya kwa makusudi au kwa hila, kujaribu kuipindisha haki, na hivyo kuwanyima walo wengi haki, itapelekea kwenye kupanda mbegu za chuki na ulipaji wa visasi. Mbegu za utengano kama taifa. Ni dhambi tutakayohukumiwa nayo kwa siku ama miaka ambayo hata sisi tutakuwa tumeshatangulia mbele ya haki. Na siku zote, hukumu ya kutotenda haki, kwa kudhamiria au kwa hila, hutolewa humu duniani, na huko tunakokwenda.

Na hakika, kama Mtanzania, mzaliwa na mzalendo wa nchi hii, nimefarijika kuisikia kauli ya awali ya Asha- Rose Migiro. Amenukuliwa akitamka; kuwa  moja ya majukumu atakayoyafanya ni kuhakikisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya unakwenda kama ulivyopangwa, huku akisisitiza kuwa hawezi kukipendelea CCM katika mchakato huo. Na akazidi kuongeza;

“Nitasimamia mchakato wa Katiba katika kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye Bunge la Katiba na baadaye Kura ya Maoni. Jambo zuri ni kwamba mchakato huu unakwenda kwa mujibu wa sheria. Nawahakikishia Watanzania nitafanya kazi kwa uaminifu na kujituma,” amenukuliwa akisema Waziri Migiro.

Na nyongeza hapa ni kuwa, kwa Asha-Rose Migiro, umma na umwamini, kuwa sio tu hawezi kukipendelea CCM ( Chama chake) katika mchakato huu, bali, haitarajiwi akipendelee chama chochote, kikundi chochote au mtu yeyote. Anatakiwa aipendelee Tanzania. Atangulize maslahi ya nchi kwa kutazama zaidi leo, kesho, keshokutwa na mtondogoo. Kwamba vyama vya siasa na viongozi wanakuja na kuondoka, lakini nchi itabaki.

Na ikumbukwe, katika hili la Katiba, yanayokuja ni mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika tangu mwaka 1977. Ni pale ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo wa 1977 yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa chama tawala na hata mfumo wa uongozi wa serikali.
Nimepata kuandika, kuwa katika dunia hii, mabadiliko ya kijamii husababisha mabadiliko ya kisiasa. Wanasosholojia wanasema, kuna sababu mbili zenye kufanya mabadiliko hayo; sababu za ndani ya jamii husika (endogenous) na sababu za nje ya jamii (exogenous).

Kwa upande wetu, tunaona kuwa, sababu za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma kwenye kufikia hatua hii ya kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.

Na kwa jamii yetu kwa upana wake, ina sababu za msingi  za kuyafurahia mabadiliko haya yanayokuja. Ni mabadiliko yenye kuleta matumaini mapya.

Na Rais kikwete , hadi kufikia hatua hii, ameonyesha ujasiri wake mkubwa  wa kiuongozi. Ni katika kuyafanya hata yale ambayo hayakufikiriwa kabla kwamba yangefanyika katika nchi hii.

Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni  nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi  au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini. Na imani ya wananchi kwa taifa na viongozi wao ni shina la matumaini  yao. Katiba yetu inayokuja  chachu ya kurudisha mioyo ya uzalendo kwa taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz: Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment