WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, January 6, 2014

JK: Tofauti ya maoni ya Katiba si dhambi

 
Rais Kikwete akihutubia mjini Unguja katika kilele cha matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Jakaya Kikwete, amesema kutofautiana maoni ya mabadiliko ya Katiba, si dhambi kwani hadi sasa Tanzania haijapata Katiba nyingine na kwamba yaliotolewa ni maoni ambayo yatajadiliwa na Bunge la Katiba na hatimaye kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana kwenye viwanja vya Maisara Sulemain mjini Unguja katika kilele cha matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Kikwete aliamua kuzungumzia jambo hilo baada ya UVCCM kuponda mapendekezo ya rasimu ya Pili ya Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, kuhusu mabadiliko ya mfumo wa Muungano kutaka uwe wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.

“Kazi ndiyo imeanza, kama ni mkoko ndiyo kwanza unaalika maua, wananchi wenyewe wataamua kwa ridhaa yao lipi wataliafiki na lipi watalikataa lisiwamo kwenye Katiba mpya ijayo, wananchi kaeni na wabunge wenu ili kujua mnalolitaka na msilo litaka,” alisema.

Aidha, alisema kuna baadhi ya watu wanapita na kupotosha umma kwa kusema kuwa Katiba mpya imekamilika, jambo ambalo si la ukweli na kuitaja hatua inayofuata ni rasimu hiyo kujadiliwa na Bunge la Katiba na baadaye kupigiwa kura na wananchi, hivyo maoni yanayotolewa kuikosoa Tume siyo dhambi.

Alisema bado wananchi wanayo nafasi pana ya kuendelea kutoa maoni yao na kutaka aina ipi ya Katiba na kwamba si lengo la Taifa kuunda Katiba ya kundi fulani au watu kuzuiwa kutoa maoni yao.

Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Rais Kikwete aliwataka vijana kuendelea kuyathamini na kuyaenzi kwani yalitokomeza unyanyasaji, dhulma na ukandamizaji uliofanywa na wakoloni.

Alisema yalikuwa ni Mapinduzi yaliyoondoa matabaka, uonevu na ukandamizaji wa haki kwa walio wengi ambao walibaguliwa na kunyimwa fursa za kibinadamu.

Wakati huo huo, Rais Kikwete, ameisifu Zanzibar kuwa ni nyota inayong’ara ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria katika Afrika.

Rais Kikwete amesisitiza kuwa siyo tu kwamba Zanzibar inaongoza katika Afrika, lakini ni mfano wa kuigwa duniani.

Aidha, ameisifu na kuipongeza Zanzibar kwa kuvuka lengo la Shirika la Afya Duniani (Who) la kuhakikisha kuwa wananchi hawatembei umbali wa zaidi ya kilomita tano kufuata huduma ya afya.

Zanzibar imeshuka kutoka umbali wa kilomita tano kama inavyopendekezwa na Who hadi kufikia kilomita tatu.

Rais Kikwete pia amekisifu Kikosi Maalum cha Kupambana na Magendo (KMKM) cha Zanzibar kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya majini na kudumisha utulivu ambao Tanzania imeushuhudia katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele cha sherehe zake kitakuwa Januari 12, mwaka huu.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza mwishoni mwa wiki na mamia ya wananchi, maofisa na askari wa KMKM baada ya kuifungua rasmi hospitali kubwa na ya kisasa ya kikosi hicho kwenye eneo la Kibweni mjini Zanzibar.

Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kikazi katika Zanzibar, alifungua rasmi hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kuhusu mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi (SMZ) katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye nyanja mbalimbali, Rais Kikwete alisema Zanzibar imekuwa na mafanikio makubwa na ya kujivunia katika kipindi hicho.

Alitaja moja ya mafanikio makubwa kuwa ni katika sekta ya afya ambako miongoni mwa mambo mengine, Zanzibar imefanikiwa kufuta ugonjwa wa malaria.

Alikuwa anazungumzia takwimu za Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Duni Haji, ambaye alimweleza Rais Kikwete kuwa mwaka 2007, vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria vilikuwa asilimia 3.1, lakini mwaka 2011 asilimia hiyo ilikuwa imeshuka hadi sifuri. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment