WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, January 11, 2014

Tunawatakia maadhimisho mema ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar

Muonekano wa Mbali wa Zanzibar 
Na Mhariri

Leo Januari 12, Wazanzibari wanaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi. Mengi yametokea, mengi yametendeka, lakini kubwa zaidi ni kuwa Wazanzibari wamebaki Wazanzibari.

Huu ni wakati wa kutafakari na kujitathmini. Miaka 50 katika umri wa binadamu si haba, yaliyotokea na kutendeka Zanzibar kwa kipindi chote hicho pia si madogo.

Atakayesema kuwa hakuna maendeleo yaliyopatikana katika miaka hiyo, labda hataki kuuona ukweli, lakini kimsingi maendeleo yapo, tena siyo kidogo. Zanzibar ya mwaka 1964 siyo Zanzibar ya leo mwaka 2014.

Katika miaka hii 50 kwa kiasi fulani Zanzibar imepiga hatua, idadi ya shule imeongezeka, idadi ya hospitali na vituo vya afya vimeongezeka, hata idadi ya majengo bora imeongezeka. Miji imekua na watu pia wameongezeka, lakini bado hali ya maisha kwa jumla ni ngumu, ingawa hicho ni kilio cha dunia nzima.

Ila zipo changamoto nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi, siyo na Serikali pekee, bali hata mtu mmoja mmoja katika nafasi yake. Kuna tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na vijana kutumia dawa za kulevya.

Pengine vijana wanajiingiza katika vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na shida za maisha au sababu ya kukosa la kufanya na wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili siyo Serikali pekee bali hata wanajamii.

Kweli huduma za afya zimefika hadi vijijini, lakini ukweli unabaki palepale kuwa vituo vingi vya afya havina wahudumu wa kutosha, wala vifaa na dawa. Hili ni tatizo la Serikali. Isijivunie tu kufungua vituo vya afya hadi vijijini, lakini inapaswa kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa uhalisia wake.

Shule nyingi zimefunguliwa kila pembe ya Visiwa vya Unguja na Pemba; lakini je, elimu inayotolewa inakidhi haja? Vijana wengi leo wanashindwa kufaulu vyema mitihani yao ya Kidato cha Nne na cha Sita je, ni kwa sababu gani? Je, mazingira ya kujifunzia yanaridhisha? Je, wapo walimu wenye taaluma stahiki? Je, vifaa vya kufundishia vipo? Masuala kama haya ndiyo tunayostahili kujiuliza kabla ya kujisifu kujenga maelfu ya shule ambazo badala ya kuwa maeneo ya kujifunzia yanabaki kuwa magofu au maeneo ya kwenda kupotezea muda.

Waasisi wa Taifa letu waliahidi kupambana na maadui watatu; maradhi, ujinga na umaskini, je, mapambano dhidi ya maadui hao yamefikia wapi? Isije ikawa tunajidanganya kujenga majengo ya kutolea elimu na afya, lakini hakuna elimu inayotolewa wala afya inayopatikana, kwani kudhibiti Malaria pekee haijatosha kusema kuwa tumeweza kukomesha adui maradhi.

Kuhusu umasikini, bado asilimia kubwa ya Wazanzibari hasa waishio vijijini wanaishi katika dimbwi la umaskini, je, kwa miaka 50 ya kujitawala, Serikali imefanya jitihada gani ya kuwakomboa wananchi hawa kutokana na adui umasikini? Kipato cha Wanzanzibari walio wengi bado ni chini ya dola moja kwa siku, je, kuna jitihada gani za kuinua kipato cha mwananchi wa kawaida?

Lakini pamoja na hayo yote, kiwango cha uvumilivu wa kisiasa Zanzibar kinazidi kuongezeka siku hadi siku. Tunaipongeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwa kutuliza mori na jazba za kisiasa.

Pamoja na yote hayo, tunapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kwa kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kazi ya kuyalinda haikuwa ndogo hata kidogo, tunatarajia kuwa katika mwanzo huu wa karne mpya yatafanyika mapinduzi zaidi katika sekta za elimu, uchumi na afya ili kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Hongereni Wazanzibari kwa kutimiza miaka 50 ya kujitawala. Tunawatakia maadhimisho mema ya Sherehe za Mapinduzi. Mapinduzi Daima.

Source: mwananchi

No comments:

Post a Comment