WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, January 29, 2014

Shein atema moto Z'bar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema kuwa wanaotaka mamlaka kamili ya Zanzibar waondoke.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, alitoa kauli hiyo wakati akiwahutubia wananchi na wanachama wa CCM katika mkutano wa uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Bila kutaja jina la mtu yeyote wala kikundi chao, au walau kueleza wanaotaka mamlaka kamili ya Zanzibar waondoke Zanzibar kwenda wapi, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina mamlaka yake kamili tangu mwaka 1964 baada ya Mapinduzi yaliokuwa halali na kuungwa mkono na wananchi na mataifa mbalimbali duniani.

Dk. Shein alisema Serikali ya Zanzibar ni serikali kamili yenye mihimili mitatu muhimu ya kuunda dola ambayo ni Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahakama.

“Wanaotaka mamlaka kamili ya Zanzibar nawashangaa sana kwani Zanzibar imepata mamlaka kamili tangu mwaka 1964 na inaongozwa na katiba yake ambayo inaheshimiwa,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein alisema hakuna mtu wala kikundi kinachoweza kuingilia mambo ya Zanzibar na wanaotaka serikali ya aina nyingine kwa njia ya mkato wasahau kwani jambo hilo halipo.

Alisisitiza kuwa wakati CCM inaadhimisha miaka 37 tangu kuanzishwa kwake wanaamini kwamba Muungano na Mapinduzi ndio nguzo kuu ya serikali.

Akizungumzia mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, alisema sera ya sasa ya CCM kuhusu mfumo wa Muungano ni wa serikali mbili.

“Wanaosema serikali tatu waache wasema, hiyo ndiyo sera yao, lakini na sisi tunasema sera yetu ni serikali mbili, nataka nirejee tena kwa wasiosikia kwamba nguzo ya chama chetu ni Muungano wa serikali mbili,” alisema Dk. Shein katika viwanja vya Kiembe Samaki mjini Unguja juzi jioni.

Wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya ya mtu mmoja mmoja na wakati wa kujadili rasimu ya katiba kupitia mabaraza ya katiba upande wa Zanzibar, liliibuka kundi ambalo lilitaka Muungano wa mkataba.

Wananchi hao pamoja na wanasiasa waandamizi wakiwamo wa CCM na Chama cha Wananchi (CUF) walipendekeza kuwapo kwa Muungano wa mkataba ambao pamoja na mambo mengine kuipa Zanzibar mamlaka kamili.

Walisema kuwa kuwa kuipa Zanzibar mamlaka kamili ni pamoja na kuirejeshea kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN).

Miongoni mwa waliohamasisha wananchi wapendekeze Muungano wa makataba na Zanzibar yenye mamlaka kamili ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
Kamati ya maridhiano ya Zanzibar ambayo inaongozwa na muasisi wa Chama cha Afro Shiraz (ASP), Ali Nassoro Moyo, nayo ilipendekeza Muungano wa mkataba.

Mwaka jana CCM ilimvua uanachama aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid, kufuatia kauli zake za kutaka Zanzibar yenye mamlaka kamili pamoja na Muungano wa mkataba. Mansour aliwahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya sita ya Amani Abeid Karume.

Akikabidhi taarifa na Rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete na Dk. Shein Desemba 30, mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema asilimia 60 ya Wazanzibari waliotoa maoni yao walipendekeza Muungano wa Mkataba.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment