WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, January 23, 2014

Mawaziri wapya wachape kazi kuepuka jina 'mzigo'

Maoni ya katuni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alitangaza uteuzi mpya wa mawaziri na manaibu wao katika baadhi ya wizara juzi huku wengine wakibaki katika nafasi zao. Rais alitumia mamlaka yake kikatiba kufanya mabadiliko hayo baada ya kuwaengua mawaziri wanne waliokumbwa na tuhuma za kutosimamia vyema wizara zao wakati wa utekelezaji wa 'Operesheni Tokomeza Ujangili'.
Aidha, nafasi ya Waziri wa Fedha ilihitaji pia kujazwa baada ya aliyekuwa akiishikilia kufariki dunia wakati akitibiwa nchini Afrika Kusini.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete alitangaza sura mpya 10 kushikilia nafasi za uwaziri na unaibu wa wizara mbalimbali, kuwapandisha manaibu watatu kuwa mawaziri kamili, kuwaengua manaibu watano na kuwahamisha wengine kutoka wizara moja hadi nyingine. Mawaziri na manaibu wa wizara sita walibaki katika nafasi zao zilezile.

Mawaziri na manaibu wote wapya wa wizara mbalimbali waliapishwa rasmi na Rais Kikwete jana, hivyo kupata idhini ya kuanza kutumikia nafasi zao.
Sisi tunawapongeza mawaziri wote wapya baada ya kupata nafasi hizo adimu, wakiwa ni punje tu kwa idadi kutoka miongoni mwa mamilioni ya Watanzania.

Tunawapongeza pia wale wote waliopandishwa kutoka kuwa manaibu na kuwa mawaziri kamili. Tunawapongeza pia wale wote waliobakizwa madarakani ili waendelee kutumia maarifa yao katika kuziongoza wizara mbalimbali walizopo.

Bila shaka, wateuliwa wapya na wale wa zamani, ni wachapa kazi hodari, wafuasi wazuri wa maadili na tena, wenye uwezo wa kusimamia kwa vitendo sera mbalimbali za nchi kwa nia ya kuliendeleza taifa.

Na kadri tunavyoona, tunaamini kuwa mawaziri na manaibu wao wote ni watu makini. Tunaamini kuwa hakuna hata mmoja atakayemuangusha Rais na Watanzania wote kwa kutenda kinyume cha matarajio. Hakika, hilo hatuna shaka nalo kwani wote waliomo kwenye orodha ya mheshimiwa rais ni watu safi. Hawana rekodi mbaya machoni mwa umma wa Watanzania.

Hata hivyo, tunapenda kuwakumbusha kuwa wote walioteuliwa juzi na kuapishwa na Rais jana, na wote waliobaki katika nafasi zao za kuongoza wizara mbalimbali; wanapaswa kuwa makini zaidi, hasa katika eneo la uwajibikaji.

Kwamba, waache mara moja hafla za kujipongeza baada ya kupata nafasi walizopewa. Badala ya kukaa tu ofisini na kusubiri taarifa za kuletewa na wasaidizi wao, wote wanapaswa kufuatilia kwa karibu maeneo yao ya kiutawala ili kupata matokeo chanya.

Mawaziri hawa wapya na wale wa zamani waliobaki madarakani wajue kuwa kazi kubwa waliyo nayo ni kuhakikisha kuwa taifa linakabiliana vyema na changamoto mbalimbali zilizopo na kuliendeleza taifa kupitia sekta wanazozisimamia.

Tunawakumbusha kuwa dunia imebadilika, uelewa wa wananchi umeongezeka na kasi ya upashanaji taarifa miongoni imekuwa kubwa zaidi kulinganisha na miaka michache iliyopita. Kwa sababu hii, ukichanganya kushamiri kwa demokrasia, hivi sasa wananchi wamekuwa na ujasiri mkubwa wa kuwataja bila kificho mawaziri wenye kasi ya konokono katika kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili.

Hivi karibuni, baadhi ya mawaziri walijikuta katika wakati mgumu baada ya wananchi kuwabaini kuwa ni goigoi na kasi yao ndogo inachangia ustawi wa kero mbalimbali katika jamii. Mawaziri hawa wakaitwa 'mizigo', wakashtakiwa kwa chama chao tawala (CCM) na mjadala juu ya neno hilo jipya kwa viongozi wa serikali limeendelea kuwa maarufu; likiwatambulisha viongozi wasioendana na kasi inayohitajika sasa katika mchakato wa kuliendeleza taifa.

Tunaamini kuwa, kwa kuzingatia yote hayo, mawaziri na manaibu wapya watakuwa makini katika kutekeleza shughuli zao za kila siku na mwishowe kuepuka uwezekano wa kuitwa 'mizigo' au kuendelea kutambulishwa kwa jina hilo. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment