WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 31, 2014

Muuaji huyu wilayani Tarime asakwe kwa udi na uvumba

Katuni
Tumepokea kwa masikitiko makubwa mauaji ya kutisha na kinyama yaliyotokea katika wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa siku tatu mfululizo.
Hadi kufikia juzi, imeelezwa kwamba watu takriban wanane wasio na hatia, walikuwa tayari wamekwisha kuuawa.

Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na jambazi mwenye silaha katika mji wa Tarime mkoani Mara kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu hadi juzi Jumanne. Mmoja wa watu waliouawa ni askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Zakaria Chacha Mwita, ambaye ni mtoto wa marehemu Meja Jenerali Mwita Marwa.

Mbali ya Marwa, wengine waliouawa ni aliyekuwa Mhandisi Ujenzi Wilaya ya Rorya, David Mwasi Misiwa na  mfanyabiashara Samuel Richard Mohenga.

Tunalaani kwa nguvu zote mauaji haya dhidi ya raia hao wasio na hatia yoyote na ambao walikuwa na haki yao ya msingi ya kuendelea kuishi.

Vifo vya Watanzania hao siyo tu pigo kwa familia zao hususani wategemezi wao, lakini pia ni hasara kwa Taifa kutokana na kuondokewa na sehemu ya nguvu kazi yake.
Mpaka sasa, bado haijafahamika lengo la muuaji huyo maana katika mauaji yote hayo, hayafafanui kama mhusika alichukua mali zozote.
Kwa hakika, mauaji haya yamemshtua kila mpenda amani maana kwa sasa ndugu zetu wa wilayani Tarime na vitongoji vyake, wanaishi kwa hofu kubwa. Hofu hiyo inaweza kuhatarisha uchumi wa wilaya hiyo ya kibiashara na yenye rutuba nzuri kwa kilimo kuporomoka kwa kuwa kila mwananchi hatakuwa huru na amani kufanya shughuli zake za uzalishaji mali.

Ni kwa msingi huo basi ndipo tunapoishauri serikali kwa kutumia vyombo vyake vya usalama, kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba muuaji huyo anakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Tunashukuru kwa hatua hizi za awali ambazo tayari Jeshi la Polisi nchini limeanza kuzichukua katika kumsaka mhalifu huyo.

Moja ya hatua zilizoanza kuchukuliwa kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, ni kutuma timu maalum kutoka makao makuu ya jeshi hilo inayohusisha kamisheni ya operesheni kufanya uchunguzi.

Naye Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alisema polisi wanafanya msako katika vijiji vya Kenyamanyori, Rebu, Nkende, Mogabiri na Kibumaye katika kata za Kitare, Turwa na Binagi kwenye tarafa ya Inchage wilayani Tarime.

Hata hivyo, pamoja na juhudi hizi zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi nchini, tungewaomba wananchi nao kwa upande wao, kutoa ushirikiano kwa Polisi kwa kutoa taarifa za kuwezesha mtuhumiwa huyo kutiwa nguvuni.

Tuna imani kubwa kwamba kama wananchi watakuwa tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi, kwa vyovyote vile mhalifu huyu atanaswa tu tena katika kipindi kifupi kijacho.

Tunasema atanaswa katika kipindi kifupi kijacho kutokana na ukweli kwamba mhalifu huyu ni binadamu mwenzetu ambaye bila shaka tunaishi naye majumbani mwetu na hata kama anajificha, bado anapatiwa huduma za msingi miongoni mwetu. Sisi tunawashauri Watanzania kamwe wasikubali kumficha mtu wa namna hii kwani ni mtu hatari katika jamii.

Tunachopaswa kufahamu ni kwamba leo amethubutu kuwaua watu hao wanane wasio na hatia yoyote, basi kesho haitakuwa ajabu akikugeukia wewe unayemficha na kukuua pia.
Aidha, tunashukuru pia kwa hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime kwenda kutembelea maeneo ya vijiji ambavyo wakazi wake wameuawa na jambazi hilo.
Hatua hiyo ni muhimu kwa kuwafariji waliopoteza wapendwa wao na pia inatia hamasa kwa wananchi na kujiona kwamba serikali inalichukulia tukio hilo kwa uzito unaostahili.

Hali kadhalika, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, alifafanua kuwa timu iliyotumwa eneo la tukio, ni ya wapelelezi na Intelijensia na inakwenda kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa na mkoa wa Mara kuhakikisha jambazi huyo anakamatwa ili kuondoa hofu kwa wananchi. Mauaji hayo ni mfululizo wa mauaji mengine ya kinyama mkoani Mara lakini yanayowalenga zaidi wanawake.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa mpaka sasa wanawake watano wameuawa katika mazingira ya kutatanisha kwenye wilaya za Musoma, Butiama na Rorya mkoani Mara.
Ni muhimu Jeshi la Polisi sasa likajipanga zaidi kuhakikisha kwamba wote wanaoendesha mauaji haya ya kinyama mkoani Mara wanadhibitiwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment