WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, March 29, 2015

Hali ya Gwajima bado tete

  Polisi, waumini wavutana hospitali inayofaa

Askofu wa Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat Gwajima akiwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), hospitali ya TMJ ya jijini Dar es Salaam JANA.
Wakati hali ya kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, ikiwa tete kwa siku mbili mfululizo, Jeshi la Polisi na waumini wa Askofu huyo wanadaiwa kuvutana hospitali inayofaa kumpa matibabu. 
 
Askofu Gwajima, alizimia ghafla juzi majira ya saa 2: 45 usiku akiwa kwenye chumba cha mahojiano katika Kituo cha Polisi KATI, baada ya kutuhumiwa kumkashifu na kumtukana kiongozi wa kanisa la Katoliki JIMBO kuu la Dar es Salaam, Mwadhama kadinali Polycap Pengo.
 
Hata hivyo, mara baada ya kutokea tukio hilo, Askofu huyo alichukuliwa akiwa katika hali ya kuzirai na kuanza kuzungushwa katika hospitali tofauti wakati waumini walitaka apelekwe Hospitali ya TMJ Mikocheni, Jeshi la polisi lilitaka apelekwe hospitali za Jeshi na Muhimbili.
 
Tukio hilo ambalo NIPASHE ililishuhudia, lilianza majira ya saa 3:00 usiku alipopoteza fahamu hadi majira ya saa 8:00 usiku ambapo walikubaliana apelekwe Hospitali ya TMJ ambako anaendelea kupatiwa matibabu.
 
HALI ILIVYOKUWA POLISI KATI
Baada ya kuwasili kituoni hapo majira ya saa 8:15 alasiri, alikwenda moja kwa moja katika chumba  maalumu kilichoandaliwa kwa ajili ya kuhojiwa tuhuma zinazomkabili.
 
Mahojiano rasmi yalianza majira ya saa 8:45 mchana. 
Ilichukua  muda wa saa saba ndani ya chumba hicho, na ilipofikia saa 1.05 usiku, hali ya Askofu Gwajima ilibadilika ghafla.
 
Baadhi ya askari na viongozi wenzake walionekana kujaribu kutumia njia mbalimbali ikiwamo kumpeleka chooni ili kumrudisha hali yake ya kawaida, lakini ilishindikana.
 
Aliporudi ndani, aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu kitu ambacho kilizusha taharuki ndani ya ukumbi huo.
 
CHANZO CHA KUZIMIA 
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho kilieleza, hali yake ilibadilika ghafla baada ya kuanza kuhojiwa kuhusu mali anazomiliki ikiwamo helikopta aliyoinunua hivi karibuni.
 
Aidha mambo mengine aliyotakiwa kueleza ni uhusiano wake na wanasiasa mashuhuri pamoja na akaunti anazomiliki na njia anazopata pesa.
 
“Mahojiano yalikwenda vizuri, lakini ilipofikia zamu ya kumhoji mali anazomiliki na ile helikopta aliyonunua, ghafla alibadilika na kuanza kutoka jasho kwa wingi na kuzimia,” kilisema chanzo hicho. Akithibitisha jambo hilo, Mchungaji Yekonia Behanaze alikiri kuwepo kwa maswali hayo, lakini alilalamikia namna alivyokuwa akihojiwa na askari hao kwamba haukufuata hali ya kibinadamu.
 
“Unajua hawakuwa na misingi mizuri ya kupata maelezo, walihojia mambo mengi sana hata yale tuliyoamini yangekuwapo tuliona hayakuzingatiwa badala yake iliegemea umiliki wa vitu,” alisema Mchungaji Behanaze.
 
ATEMBEZWA AKIWA AMEZIMIA
Baada ya kuzirai aliondolewa ndani ya chumba hicho ili kumuwahisha hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.
 
Hata hivyo, kulitokea mabishano makali KATI ya polisi na viongozi wa kanisa hilo, ambapo upande wa polisi ukitaka kumpeleka katika Hospitali za serikali, viongozi hao waling’ang’ania kwenda Hospitali ya TMJ.
Ilipofika Saa 3:00 usiku, polisi walimchukua  na kumuingiza katika GARI lenye namba T 215 aina ya Noah na kumpeleka Hospitali ya Kilwa ROAD inayomilikiwa na jeshi hilo.
 
Hapo alitibiwa kwa muda wa saa tatu na ilipofika saa 5:08 usiku alichukuliwa na GARI la wagonjwa lenye namba DFP 6309 na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
 
Msafara wote ulikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, ambapo wakati akielekea Muhimbili, msafara huo ulikatisha mitaa ya Kurasini, Kariakoo, Faya na kuishia Hospitali ya Muhimbili majira ya saa 5:18, usiku. Hata hivyo,  pande mbili hizo KATI ya polisi na waumini ziliendelea kushindana kuhusu hospitali inayofaa kumtibia.
 
Wakiwa Hospitali ya Muhimbili, viongozi wa kanisa hilo ndugu na jamaa wa Gwajima waliendelea kushinikiza kuondolewa hapo ili apelekwe TMJ ambako walidai ndipo alipokuwa daktari wake.
 
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na polisi wakiwaeleza Muhimbili ndiyo Hospitali Kuu na watakubaliana nao endapo madaktari watashauri kuondolewa kwa barua maalum.
 
Ilipofika majira ya saa 6:00 usiku GARI la wagonjwa kutoka Hospitali ya TMJ lenye namba T 786 BYK liliwasili na kukaa tayari kumchukua.
Saa 7:00 usiku Askofu Gwajima alitolewa hospitalini hapo akiwa bado amezirai na kuingizwa katika gari hilo na kumkimbiza Hospitali ya TMJ. Katika msafara huo, magari yalipita mitaa ya Upanga, daraja la Selander, Morocco na hatimaye  hospitalini hapo na kulazwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
 
HALI YAKE KWA SASA
Hata hivyo taarifa zilizopatikana kutoka Hospitali ya TMJ, zinaeleza bado hali yake si nzuri kutokana na kutorejewa na fahamu.
Kwa mujibu wa daktari anayempatia matibabu, Dk. Photonatus Mazigo, hali ya mgonjwa wake bado ni mbaya japokuwa kuna dalili ya kupata fahamu taratibu.
“Kwa ujumla hali ya mgonjwa siyo ya kuridhisha, hajazinduka tunachokifanya ni kumpatia tiba ili arejee katika hali yake ya kawaida,” alisema Dk. Mazigo.
 
DK. SLAA: TUMUACHIE MUNGU
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, alikwenda kumjulia hali kiongozi huyo na kusema kwa sasa Watanzania wasitafute chanzo, badala yake wamuachie Mungu amsaidie apone haraka.
 
Alisema hawezi kuzungumzia hali ya Askofu Gwajima kwa kipindi hiki kwa sababu jukumu hilo anaachiwa daktari anayemtibia.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Hoja ya Prof. Mbele: Vyama vya siasa vijitegemee


Ninaandika ujumbe huu kwa wa-Tanzania wenzangu. Ninatoa hoja kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tuachane na utaratibu wa sasa wa serikali kuvipa ruzuku vyama vya siasa.

Fedha inayotolewa na serikali KAMA ruzuku kwa vyama vya siasa ni kodi ya walipa kodi wote, na wengi wao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ruzuku hii ni hujuma dhidi ya hao walipa kodi ambao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ni hujuma, ingawa imehalalishwa kisheria. Sheria na haki si kitu kile kile. Ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini ulikuwa ni hujuma dhidi ya haki.

Fedha inayotolewa kwa vyama hivi ni nyingi sana, mamilioni mengi ya shilingi kila mwezi. Ni fedha ambazo zingeweza kununulia madawati na vitabu mashuleni, kulipia mishahara ya walimu au madaktari, kukarabati barabara, kuwanunulia baiskeli walemavu wanaotambaa chini, kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi ambayo yanaoza katika mikoa KAMA vile Ruvuma, na kadhalika.

Kutoa ruzuku kwa chama kimoja tu, KAMA kingekuwepo kimoja tu, tayari ni hasara na hujuma. Sasa tunavyo vingi, na hasara ni kubwa mno. Utitiri wa vyama unavyoongezeka, hali itazidi kuwa mbaya. Huduma za jamii zitaendelea kuzorota, na hata kutoweka, kwa fedha kutumika kama ruzuku kwa vyama vya siasa.

Kama kweli vyama hivi vina maana kwa wanachama wao, wanaweza kuvichangia vikastawi bila tatizo. Vyama kama Simba, Yanga, Maji Maji, na Tukuyu Stars havitegemei ruzuku. Wanachama, kwa mapenzi waliyo nayo kwa vyama vyao, wanaviwezesha kuwepo na kustawi, na hawako tayari vitetereke. Wako tayari kuvichangia wakati wowote ikihitajika. Nini kitawazuia wanachama wa vyama vya siasa kufanya vile vile, kama kweli vyama hivi vina maana kwao?

Sisi raia ambao si wanachama wa vyama vya siasa TUNA wajibu wa kuanza kampeni ya kushinikiza itungwe sheria ya kufuta ruzuku kwa vyama vya siasa, ili kuokoa fedha, ziweze kutumika kwa huduma muhimu kwa jamii yetu.

Kama umevutiwa na makala hii na ungependa kufuatilia zaidi mawazo yangu ya kichokozi na kichochezi, utayapata kwa wingi katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.


  • Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Prof. Mbele: Hapa Kwetu

MATOKEO YA UCHAGUZI WA CHAMA CHA ACT WAZALENDO


Zitto akihutubia wajumbe wakati wa uchaguzi wa ACT

Mwanasiasa kijana, Zitto Kabwe, amechaguliwa kuwa kiongozi wa chama kipya cha siasa cha upinzani ACT Wazalendo, katika uchaguzi uliokamilika usiku wa kuamkia leo Jumapili Machi 29, 2015.

Kwa mara ya kwanza chama hicho ambacho katika katiba yake kinaonesha patakuwa na Viongozi Wakuu, wakiongozwa na Kiongozi Mkuu wa chama, Mwenyekiti wa chama, Makamu Wenyeviti wawili kutoka BARA na Zanzibar, Katibu Mkuu, na Manaibu Makatibu Wakuu wawili kutoka pande zote za Muungano na kitakuwa chini ya Uenyekiti wa Mwanamama Mwanasheria msomi.

Matokeo hayo yanaonyesha, Mwanamama huyo, ANNA Mghwirim, ndiye aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Makamu Mwenyekiti Bara, Shaban Mambo, na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Ramadhan Suleiman Ramadhan.

Katibu Mkuu na Manaibu wake wanasubiri mapendekezo ya Kamati Kuu ya chama ambayo ilitarajiwa kukamilisha kazi yake mapema alfajiri ya Jumapili. 

Pichani kiongozi huyo wa chama, Zitto Kabwe, akilakiwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika kwenye ukumbi wa Kadinali Rugambwa, Oysterbay jijini Dar es Salaam, Jumamosi Machi 28, 2015. 

Zitto alichaguliwa kuwa Kiongozi wa chama hicho, nafasi ambayo kwa Katiba ya chama hicho ndiyo ya juu zaidi. 

Chama hicho kinazinduliwa rasmi Jumapili Machi 29, 2015 kwenye ukumbi wa Diamond JUBILEE jijini Dar es Salaam


Zitto akionyesha alama ya chama ambayo ni "Uwazi"


Zitto akihutubia wajumbe


Zitto akipongezwa



Wajumbe wakiserebuka, wakati wa uchaguzi huo


Wajumbe wakifurahi kwa kushikana mikono kuonyesha umoja


Wajumbe wakipiga kura






Askofu Gerald Mpango akiongoza sala


Mzee Kastiko, akiwakilisha waislamu kuomba dua


Aliyekuwa Katibu Mkuu wa muda wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba, akihutubia






Msimamizi wa uchaguzi huo, Profesa Kitila Mkumbo





  • Taarifa hii imenukuliwa kutoka kwenye blogu mbalimbali mtandaoni.
  • SOURCE WAVUTI

Sunday, March 22, 2015

NIMEJIUNGA NA ACT ILI KUENDELEA KUWEKA MBELE MASLAHI YA TAIFA - ZITTO KABWE

Zitto akiongea na wanahabari leo katika ukumbi wa mikutano ndani ya Hoteli ya Serena, Dar.

Maelezo ya Ndugu Zitto Kabwe aliyoyatoa katika Mkutano na Waandishi wa Habari kufuatia Kung’atuka Ubunge na Kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo
Jumapili, 22 Machi 2015, Serena Hoteli, Dar es Salaam
Ndugu Waandishi wa habari, wanachama na wapenzi wa ACT-Wazalendo na wote mliohudhuria mkutano huu,
Kama mnavyojua siku ya Ijumaa tarehe 19 Machi 2015 ilikuwa siku yangu ya mwisho kuhudhuria bunge la kumi linaloendelea Mjini Dodoma. Baada ya kung’atuka ubunge kufuatia kukoma uanachama wangu wa chama nilichotumia kuingia Bungeni, wengi mliniuliza ‘what is next?’
Sasa ninapenda kuwataarifu, kama ambavyo baadhi yenu tayari mnajua, kwamba jana siku…
Zitto akiongea na wanahabari leo katika ukumbi wa mikutano ndani ya Hoteli ya Serena, Dar.

Maelezo ya Ndugu Zitto Kabwe aliyoyatoa katika Mkutano na Waandishi wa Habari kufuatia Kung’atuka Ubunge na Kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo
Jumapili, 22 Machi 2015, Serena Hoteli, Dar es Salaam
Ndugu Waandishi wa habari, wanachama na wapenzi wa ACT-Wazalendo na wote mliohudhuria mkutano huu,
Kama mnavyojua siku ya Ijumaa tarehe 19 Machi 2015 ilikuwa siku yangu ya mwisho kuhudhuria bunge la kumi linaloendelea Mjini Dodoma. Baada ya kung’atuka ubunge kufuatia kukoma uanachama wangu wa chama nilichotumia kuingia Bungeni, wengi mliniuliza ‘what is next?’
Sasa ninapenda kuwataarifu, kama ambavyo baadhi yenu tayari mnajua, kwamba jana siku ya Jumamosi tarehe 20 Machi 2015 nilijiunga rasmi na Chama cha ACT - Wazalendo na kukabidhiwa kadi na Mwenyekti wa Tawi la Tegeta. Hii ilikuwa ni moja kati ya siku muhimu kabisa katika maisha yangu ya kisiasa. Na kwa leo kwa kweli nisingependa nizungumzie mgogoro uliokuwepo kati yangu na viongozi wangu wa chama cha zamani wala kile kilichotokea Bungeni. Hayo yote mnayajua, yameandikwa sana na yameshapita. Sasa ni wakati wa kusonga mbele. Rais Kwame Nkrumah alipata kusema "forward ever, backward never". Na kama nilivyosema Bungeni, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Kwa hiyo leo nitazungumzia uanachama wangu katika chama changu kipya cha ACT - Wazalendo.
Tuna vyama 22 kwa sasa. Na kwa kweli wengi watakuwa wanajiuliza kwa nini nijiunge na chama kipya ambacho kimeanzishwa juzi tu na ambacho pengine wanachama wake bado wanajaa katika kiganja cha mkono?
Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote. Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii. Uadilifu ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu yote ya ubunge nimepigania uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini kwamba ni moyo wa utumishi wa umma. Nimefurahi kwamba kati ya misingi kumi ya ACT-Wazalendo, uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu kabisa ya misingi hiyo. Uwazi ni sehemu ya jina la chama hiki. Yote haya yamenifanya nione kwamba sitojiona mgeni katika chama hiki. Huku ndiko nyumbani kwangu kisiasa na katika utumishi wa umma.
Nimejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa maendeleo. Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za Taifa lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana, wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja. Tunataka tufungue ukurasa mpya wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi yetu. Siasa za masuala ya vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi, wajasirialimali, wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na katika kuondoa umaskini.
Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu, afya, hifadhi ya jamii, na ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu namna endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia sehemu yake.
Mwezi Oktoba mwaka 1966 Mwalimu Nyerere alipokea maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ikulu. Maandamano yale yalichochewa na kasi kubwa ya rushwa na maisha ya kifahari ya viongozi (wabenzi). Mwalimu alifoka kwa kuuliza “ Tunajenga nchi ya namna gani”? Hatimaye Azimio la Arusha likatangazwa.
Chama hiki kipya kimeanzishwa katika mazingira yale yale ya mwaka 1966. Ni wakati wa kujiuliza na kupata majawabu ya aina ya nchi tunayojenga. Sisi ACT – Wazalendo tumeona jawabu ni kurudi kwenye misingi. Waingereza wanasema ‘back to the future’ Let the new beginning begin.
Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Zitto Zubeir Kabwe
Dar es Salaam, 22 Machi 2015.


SOURCE: GLOBAL PUBLISHER