WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 2, 2013

Neno La Leo; Ukiona Zinduna, Ambali Iko Nyuma…!

d1 cfadd

Ndugu zangu,
Katika dunia hii kila jambo hutanguliwa na ishara. Nimepata kuandika, kuwa Afrika mvua hainyeshi ghafla, utaziona ishara za mawingu.

Na nchi nayo ni hivyo hivyo, ishara za nchi inayoelekea kubaya huonekana mapema. Wahenga  walituambia, kuwa ukiona zinduna na ambali iko nyuma. Zinduna ni mti na ambali ni harufu itokanayo na mzinduna.

Naingiwa na mashaka juu ya kuongezeka kwenye jamii kwa

kauli zenye kuashiria shari zaidi kuliko maridhiano. Na wananchi hawako katikati ya hili, bali baadhi ya wanasiasa na wakati mwingine viongozi wa dini.

Ukweli Watanzania walio wengi hawajachoka kuishi kwa amani, bali, kuna baadhi ya wanasiasa na hata viongozi wa dini, kwa kutanguliza maslahi yao, wanahangaika kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwa Watanzania. Kwamba Watanzania wabaguane kwa misingi ya udini, siasa na hata ukabila.

Juzi hapa nimeandika makala kuzungumzia hatari ninayoiona katika hili la vyama vya siasa kuanzisha vikosi ama vikundi vya ulinzi. Na ukweli huko nyuma niliandika juu ya hatari hii katika makala zaidi ya mbili, ni kuanzia mwaka 2001 pale CUF na CCM Zanzibar walipokuwa kwenye msuguano mkubwa. Nikaandika tena baada ya Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki pale CCM na Chadema walipokwaruzana.

Na hapa nitarejea moja ya mazungumzo muhimu ya kihistoria kupata bahati ya kuyafanya; ilikuwa ni jioni  ya  Januari 24, 2012 pale nilipokutana na Marehemu Mama Mosi Tambwe ( Pichani)  nyumbani kwake Tabora Mjini.

Mosi Tambwe aliingia TANU akiwa na miaka 18.  Ni moja wa wanawake mahiri sana kisiasa wa enzi hizo. Mosi Tambwe alinisimulia, kuwa alianzia kwenye TANU Bantu Group, hiki kilikuwa ni kikundi cha vijana ndani ya TANU  ambacho baadae kikawa TANU Youth League.

Kwa kirefu kabisa Mosi Tambwe aliniambia majukumu yao  kama vijana kwa wakati huo. Ni wakati  nchi ikiwa chini ya mkoloni. Akabielezea pia majukumu hayo  yalivyobadilika baada ya uhuru. Enzi hizo vijana walikuwa wakiandaliwa kupitia TANU Youth League ili waje kuwa makada wa chama, hivyo basi, viongozi wa wananchi walionolewa vema. Walijengewa uwezo wa kujenga hoja.

Ni enzi hizo, baada ya kutoka Chipukizi, hatua iliyofuata ni Tanu Youth League. Wengine wakaenda JKT na hata Jeshini.  Azma kubwa ilikuwa kujenga Uzalendo na Umoja wa Kitaifa.

Tumekosea wapi?
Jibu; ni pale, kwa shinikizo la mabadiliko ya dunia , na kwa  shingo upande, Chama tawala kiliporidhia  kuanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. CCM ikasahau  kuratibu mabadiliko makubwa ya kikatiba ambayo yalipaswa yaendane na mabadiliko hayo ya kimfumo.

Kimsingi, hali tuliyo nayo sasa ya kuchanganyikiwa hata kwenye hili la vyama kuunda vikosi au la,  inatokana na makosa makubwa, kama taifa,  tuliyoyafanya  mwaka 1992.  Maana, ‘ Green Guards’ katika mfumo wa Chama kimoja haikuwa tatizo.

Nimeandika mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri, lakini,  wakati ni mwalimu mzuri pia. Tujifunze kutokana na mabadiliko ya wakati. Katika wakati tulio nao sasa,  vyama vya siasa havipaswi kujiundia vikundi vya ulinzi vyenye kupata hata mafunzo ya kijeshi. Ni ujasiri, kama viongozi wa sasa watazipa mgongo fikra hizi za kizamani na kuendana na mabadiliko ya wakati.

Tufanye nini?
Kama ningeombwa ushauri hii leo, basi, ningevishauri vyama vya siasa, kuwa kwa  haraka sana, viachane na harakati za kuunda vikosi au vikundi vya ulinzi. Jukumu hilo liachiwe vyombo vya usalama, hususan jeshi la polisi,  na hata makampuni ya ulinzi yenye kutambulika kisheria.  

Na vile vilivyopo vivunjwe. Maana, vikundi hivi vya ulinzi ambavyo kimsingi ni vikundi vya wanamgambo wa vyama ni  maafa tunayoyaandaa wenyewe. Kama hatutanguliza busara na hekima, basi, itakuwa ni suala la wakati tu kabla hatujajikuta kwenye dimbwi la maafa makubwa. Tumeshaziona ishara.

Majuzi hapa nilikuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kufuatilia kongamano la Amani ya Nchi yetu kwa miaka 50 ijayo. Kwa masikitiko makubwa, ukumbi ule wa Nkrumah haukujaa vijana.

Kwa vyama vya siasa, badala ya kutumia muda na rasilimali zao kufyeka mapori ya kuwaweka vijana kwenye ‘ makambi ya ukakamavu’, umefika wakati sasa wa kubadilika, kuachana na fikra hizo za kijima zenye kuturudisha nyuma miaka 50.

Huu ni wakati wa kuwajengea vijana wa vyama ‘ ukakamavu wa akili’. Na mahali kama pale Nkrumah Hall ndipo vijana wa vyama walipaswa wahamasishwe waende wakanoe akili zao. Waende wakajifunze kujenga na kubomoa hoja za wengine kwa nguvu za hoja na si hoja za nguvu.

Zimepita, zama za ‘ Umkhoto we Sizwe’. Hizi ni zama za ‘ Umkhoto we Mitwe’- Ni mapambano ya kutumia vichwa kwa maana ya akili.

Naam, ukiona zinduna na ambali iko nyuma.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment