WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, August 19, 2013

AG Zanzibar: Mwarobaini wa Muungano Serikali tatu

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, 

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema mfumo wa muundo wa Muungano wa Serikali mbili ni ghali zaidi kwa Zanzibar, huku akipendekeza Serikali tatu zitaipunguzia Zanzibar gharama.

Akifungua Baraza la Katiba Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar jana, Othman alisema chini ya mfumo wa sasa wa Muungano, maofisa wa Zanzibar wamekuwa wakipishana kila uchao Dar es Salaam kufuatilia masuala mbalimbali ya SMZ.

“Jamani Serikali mbili ni ghali kwetu Zanzibar kuliko wao, ndiyo maana wamekuwa hawashughuliki,” alisema Othman na kuongeza:

“Hakuna hoja za msingi za kuwa na Serikali mbili.”
Alisema ikiwa mtu atafanya utafiti kwenye idara na wizara mbalimbali Zanzibar, atabaini karibu kila siku maofisa wamekuwa wakienda bara kufuatilia masuala mbalimbali.

Kuhusu mfumo wa Serikali tatu, Othman alisema mfumo huo ni imara na utaimarisha Muungano, kuonya kwamba mfumo wa Serikali mbili unaweza kuwa sababu ya kuvunjika kwa Muungano.

Alisema Serikali tatu zitadumisha Muungano, kwa sababu zitakuwa zinaweka bayana kila maslahi ya mshirika.

“Nawaambieni Muungano utavunjika kwa Serikali mbili, kwa sababu wapo watu kule wanaichukia Zanzibar, lazima tujenge misingi ya kulinda Muungano,” alisema.

Othman alisema kujificha kwa Tanganyika kwenye Serikali ya Muungano, ni fitna kubwa katika Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

“Uruhani wa Tanganyika ndiyo fitna kubwa ya Muungano, Mzee Jumbe (Rais wa awamu ya pili Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi), alitaka kuja na hirizi ya huyu ruhani akamchukue na akamzike,” alisema Othman na kuongeza:

“Lakini akadhalilishwa mbele za watu kwa kuambiwa eti hajui hesabu moja na moja anasema tatu, hivi kweli Mzee Jumbe msomi mzima hajui hesabu.”
“Huu uruhani wa Tanganyika ndiyo fitna kubwa ya Muungano, ipo haipo. Lakini akipanda kichwani anasema nipo, sasa inataka kutumia jina letu la pamoja,” alisema.

Pia, alitolea mfano uruhani wa Tanganyika kuwa ni suala la michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halina uhalali wa kuwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu siyo suala la Muungano.

“Leo kama tutaifungulia kesi kushtaki TFF kwamba haiwakilishi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutashinda,” alisema.

Katika hatua nyengine, Othman alinafanisha vyama vya siasa kuwa ni sawa na duka, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuelewa kuwa siyo busara kuweka rehani nyumba kwa sababu ya kupata kilo ya mchele dukani.
Alisema duka ni jambo la uchaguzi wa mnunuzi, anaweza kununua duka hili leo kesho akaenda kutafuta mahitaji kwingine, hivyo suala la nchi ni jambo la msingi zaidi.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment