WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 9, 2013

MAJANGA : Mhadhiri UDSM auawa kinyama Dar,Wazungu wamwagiwa tindikali Z'bar,JK asema tukio limeitia aibu nchi

Rais Jakaya Kikwete akitoka kuwajulia hali raia wawili wa Uingereza Kristie Trup na Katie Gee waliolazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam baada ya kumwagiwa tindikali huko Zanzibar juzi. Kushoto kwa Rais ni Mganga Mkuu wa Aga Khan, Dk Jaffery Dharsee .  

Dar/Zanzibar. Mauaji, mashambulizi ya kudhuru mwili na uporaji vimeendelea kuchafua taswira ya Tanzania baada ya juzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuuawa kwa kupigwa risasi na watu ambao hawajafahamika, raia wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali na mfanyabiashara kuporwa zaidi ya Sh40 milioni.
Jana, Rais Jakaya Kikwete alikwenda Hospitali ya Aga Khan kuwajulia hali raia hao wawili wa Uingereza waliomwagiwa tindikali huko Zanzibar, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) akisema tukio hilo limetia aibu kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
Mauaji
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alisema jana kuwa mauaji ya Mhadhiri huyo Msaidizi katika Idara ya Uhandisi na Teknolojia, Patrick Rweyongeza (32) yalitokea juzi saa saba mchana maeneo ya Magomeni Tanesco, Dar es Salaam, wakati marehemu alipokuwa ndani ya gari lake akielekea katikati ya jiji.
“Alipofika maeneo hayo alivamiwa na watu waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Boxer ambao walimpiga risasi ya kifua upande wa kulia kisha kutokomea.”
“Baada ya kupigwa risasi alipelekwa Muhimbili lakini kabla ya kuanza kupatiwa matibabu alifariki dunia,” alisema Kamanda Wambura.
Alisema hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. “...Tunaendelea na upelelezi kufahamu tukio hilo lililofanywa na watu hao kama ni la ujambazi au kisasi.”
Akizungumza nyumbani kwa mjomba wa marehemu Mbweni, Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Uhandisi, Dk John Mahunza alisema Rweyongeza alikutwa na mkasa huo baada ya kutoka benki kuchukua fedha kwa ajili ya shughuli za ofisi.
“Baada ya kuchukua fedha hizo Ubungo, alipanda gari kuelekea Magomeni na kufika maeneo ya Tanesco, walimzingira na kumlazimisha kufungua mlango, lakini aligoma na wakampiga risasi,” alisema.
“Baada ya kumpiga risasi mkononi, walimpora bahasha iliyokuwa na fedha... nadhani wale walikuwa wanamfuatilia tangu alipokuwa benki hadi anatoka.
Dk Muhunza alisema marehemu alipata shahada yake ya kwanza mwaka 2004 chuoni hapo na baadaye shahada ya uzamili katika chuo kimoja cha London, Uingereza. Alifundisha chuoni hapo masomo ya Numerical Method na Building Design kwa miaka mitatu.
“Marehemu alikuwa na mpango wa kwenda kuchukua shahada ya uzamivu katika chuo kimoja London na alikuwa hajaoa.”
Msemaji wa familia, Damas Kayanda alisema marehemu anatarajiwa kuagwa leo kwa shughuli za ibada kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu Raphael na kesho utasafirishwa kwenda Tabora kwa maziko.
Tindikali
Wasichana hao wawili walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe wakiwa katika matembezi ya kawaida juzi usiku.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadamu Khamis Mkadamu alisema tukio hilo lilifanywa na vijana wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa.
Mkadamu alisema Wazungu hao walikuwa walimu wa kujitolea katika Shule St Monica, Tomondo, Zanzibar.
Alisema waathirika hao wamedhurika kiasi kikubwa katika maeneo ya kifua na mikononi na baada ya tukio hilo, walipelekwa Hospitali Kuu ya Zanzibar na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Mganga Mkuu wa Aga Khan, Dk Jaffery Dharsee alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na hali za wasichana hao akisema hajapata ruhusa kutoka kwa ndugu wa familia.
Maofisa mbalimbali wa Ubalozi wa Uingereza nchini walifika hospitalini hapo kuwajulia hali wagonjwa hao.


Uporaji
Majambazi wanne walimvamia mfanyabiashara wa vifaa vya magari na kumpora zaidi ya Sh40 milioni alizokuwa akipeleka benki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marieta Minangi alisema tukio hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi kwenye makutano ya Mitaa wa Livingstone na Kiungani, Dar es Salaam wakati mfanyabiashara huyo aliyefahamika kwa jina moja la Bupedra akiwa na dereva wake kwenye aina ya Toyota Hiace.
Alisema walipofika katika eneo hilo walivamiwa na watu wanne waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Boxer na walisimamisha gari hilo kisha kupiga risasi moja hewani na kuvunja kioo cha dirisha cha mlango wa mbele kwa nondo na kumtaka Bupedra awape fedha hizo zilizokuwamo kwenye begi haraka.
“ Watu hawa walikuwa wanajua kila kitu kilichomo kwa sababu waliposimamisha gari walitaka wapatiwe fedha haraka na walipatiwa na kutokomea, “ alisema Kamanda Marieta.
Alisema polisi wanamshikilia dereva wa gari hilo kwa upelelezi wa tukio hilo ambalo hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Imeandikwa na Talib Ussi, Zanzibar, Minael Msuya, Bakari Kiango na Daria Erasto Dar es Salaam.
source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment