WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, January 23, 2014

Tunahitaji viongozi wa aina gani?

 
Rais Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Mwaka huu na ujao ni miaka ya chaguzi za viongozi wa Serikali za Mitaa, Madiwani na Wabunge watakaodumu kwa miaka mitano ijayo. Ni wakati mwafaka kujiuliza aina ya viongozi tunaowahitaji.
Je, tunahitaji viongozi wavivu na wachumia tumbo au wenye uchungu wa maendeleo na jinsi ya kutatua matatizo ya wananchi? Tunahitaji kufanya tafakuri jadidi katika jambo hili kabla ya muda wa kampeni na kupiga kura.

Tuanze na wenyeviti wa serikali za mitaa. Wamekuwa watendaji wazuri katika maeneo yao? Wameyafanyia kazi mambo waliyoahidi wakati wa kuomba kura? Wameziacha ofisi zao kwa muda kwenda kuona matatizo ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi au walikuwa viongozi waliozipenda zaidi ofisi zao kusubiri wananchi waliohitaji kuandikiwa barua, kupigiwa mihuri na kupokea asilimia ya fedha za mauzo ya viwanja na nyumba?

Je, waliitisha mikutano ya kila baada ya miezi miwili au mitatu kuwaeleza wananchi mafanikio waliyopata na matatizo waliyokumbana nayo? Kamati za Mazingira na Afya, Ulinzi na Usalama, Uchumi, Maji, Miundombinu n.k. zimetekeleza malengo yaliyoainishwa? Kama jibu ni ‘hapana’ kilichokwamisha ni nini? Wenyeviti wametimiza ahadi zao kwa asilimia ngapi?

Je, wanaeleza mapato na matumizi ya fedha zilizopatikana kutokana na miradi ya mitaa yao na walizopewa na Halmashauri za Miji na Majiji? Wanafaa kuchaguliwa tena au la? Haya ni baadhi ya maswali wanayopaswa wananchi kujiuliza kabla ya uchaguzi.
Baada ya hao tuchambue walichofanya madiwani kwa muda waliokaa madarakani.

Wametimiza waliyowaahidi wapiga kura au wamekuwa wakifanya mikutano kwenye majumba ya wananchi usiku kuomba kura za kutaka waendelee na nafasi zao huku wengine wakieleza nia ya kugombea ubunge? Kama wameshindwa kwenye udiwani watawezaje hekaheka za ubunge?

Wabunge nao wamewafanyia nini wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015? Ikumbukwe tu kuwa wakati walipokuwa wakifanya kampeni waliahidi mambo mengi yanayowezekana na yasiyowezekana. Kwa mfano mgombea alipoomba kura aliahidi akichaguliwa atajenga barabara, atamaliza tatizo la maji, atahakikisha hospitali za jimbo lake zinakuwa na dawa za kutosha n.k.

Waliotoa ahadi hizo ingedhaniwa wangetoa fedha mifukoni mwao kumbe ni kuwaghilibu wapiga kura ili wavutiwe kuwapigia kura. Badala ya kusema wangeishinikiza serikali ijenge barabara, madaraja, kuwapatia maji na umeme, kuongeza matundu ya vyoo katika shule za msingi na madawati, eti waliahidi kufanya wao na wenye fikra finyu waliamini!

Wengi wao baada ya kuchaguliwa walishindwa kurudi kwa wapiga kura kuwashukuru bali walifanya hivyo walipopewa nafasi ya kutoa hoja zao Bungeni. Huko walifanya vituko vya aina yake kwani walitumia muda mrefu kuwashukuru wapiga kura waliowachagua. Kwamba kuchaguliwa kwao ni uthibitisho kuwa vyama vyao vinapendwa na ndivyo vinavyoweza kuwatoa wananchi katika dimbwi la umasikini lakini vingine vinaganga njaa!

Baada ya kuchaguliwa walibaki kwa muda mfupi tu majimboni mwao na kutumia muda mwingi mijini, hasa Dar es Salaam wakiwasiliana na watu mbalimbali jinsi ya kuanzisha miradi yao. Uchaguzi unapokaribia ndipo hujitokeza tena kutoa ‘misaada’ kwa wananchi. Kuna wanaodai kuwa hutoa misaada hiyo kwa fedha zao lakini hawasemi kila jimbo la uchaguzi hutengewa fedha kusaidia maendeleo. Wananchi wanaelewa hili?
Hebu tuwafuatilie walipokuwa Bungeni.

Walikuwa wawakilishi wa kweli wa wananchi au walitetea zaidi itikadi za vyama vyao na kusahau matatizo ya wananchi waliowapa kura? Baadhi walikuwa watoro ama kuchelewa kuingia Bungeni na hata walipoingia walisinzia na kugonga meza kwa kila lililosemwa na wabunge wa vyama vyao hata kama hayakuwa na tija kwa wananchi.

Wengine tangu mwanzo mpaka mwisho wa vikao vya Bunge hawakuchangia lolote. Inakuwa kama walikwenda Bungeni kusikiliza kejeli, kurushiana vijembe, kuzomeana na hata kutukanana kana kwamba wabunge wa vyama vingine waliingia Bungeni kwa ‘bahati mbaya!’ Kwani katika nchi ya vyama vingi kuna chama chenye haki pekee ya kuwa na wabunge?

Baadhi walitumia muda mwingi n-nje ya Bunge. Kuna wakati takriban robotatu ya wabunge hawakuwapo Bungeni kwani walikuwa kwenye shughuli zao. Mara kadhaa mbunge baada ya mwingine alisimama kukosoa na kupinga kwa nguvu bajeti ya wizara fulani lakini mwishowe alihitimisha kwa kusema anaiunga mkono kwa asilimia 120! Alichokuwa akipinga ni nini hata avutiwe kuiunga mkono kabla ya kusikia kauli ya mwisho ya waziri wa wizara husika?

Wananchi wanaofadhaishwa na wabunge wa aina hiyo na kuonesha nia ya kugombea katika uchaguzi unaofuata ili wawe wawakilishi wa kweli wa wananchi, huwa nongwa kwa wabunge waliopo. Hulalamika Bungeni wakisema kuna watu wanaopitapita kuzengea majimbo yao. Kwani wana hatimiliki inayowaharimisha wengine kugombea katika majimbo hayo?

Ingawa yanayotokea ndani ya Bunge ni vijembe, kuzomeana na kutetea itikadi za vyama vyao, yanapokuja masuala ya masilahi, wote huweka kando tofauti zao na kuwa wamoja kama walivyo ndege wa rangi moja ambao huruka pamoja. Tujiulize: Tunahitaji viongozi wa aina gani?
marobarnabas@yahoo.com 
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment