WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, June 23, 2012

Freemasons Ni Abrakadabra! ( Makala Yangu Raia Mwema)




 Na Maggid Mjengwa,

TUNAWAPITISHA watu wetu kwenye njia yenye giza. Kwenye njia yenye matope. Kwanini?
Kwenye moja ya mashairi ya Marcelino Dos Santos wa Msumbiji  anasema; " We Must Plant".  Kwa maana ya tuna lazima ya kupanda. Dos Santos hazungumzii kupanda mbegu za mahindi au mtama, bali kupanda fikra za kimapinduzi kwa wanajamii. Fikra zitakazowasaidia kutoka katika hali iliyopo na kwenda kwenye hali nyingine iliyo bora zaidi.

Na Socrates, mwanafalsafa wa Uyunani ya kale alipata kuonekana akimulika kurunzi mchana wa jua kali. Inaandikwa, kuwa Socrates yule alizunguka sokoni na kurunzi (tochi) yenye kumulika. Watu walimwuliza, kulikoni? Socrates akawajibu; ”Kwenye nuru hii , kuna walio gizani.”

Kwa Socrates lilikuwa ni tendo la kifalsafa lenye kuelezea hali halisi. Hata katika dunia hii ya kisasa, bado tuna miongoni mwetu, walio gizani mchana wa jua kali. Angalia ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo. Ndiyo, kuna wanaohitaji kumulikiwa mwanga.

Uvumi wa Freemasons unaosambaa sasa kwenye jamii  ni dhana ya kufikirika kama ilivyokuwa kwa Babu wa Loliondo. Ya Babu wa Loliondo yalianza kwa uvumi wa  magazetini na hatimaye kugeuka kuwa moja ya majanga ya kitaifa.

Leo Watanzania tunajua, kuwa  pamoja na kutangazwa sana, Babu wa Loliondo hajamtibu  hata mgonjwa mmoja. Badala yake, amechangia kwenye vifo na mateso ya wengi. Hakika, ni sisi Watanzania ndio tuliokuwa  ' wagonjwa' wa kuendekeza abracadabra za Babu wa Loliondo.

Na uvumi huu wa sasa wa Freemasons ni abrakadabra nyingine tunayolishwa Watanzania. Ni habari za kupotosha jamii, ikiwamo jamii kuaminishwa kuwa wanachama wa jumuiya ya Freemasons ni watu matajiri na kuwa anayejiunga na Freemasons atapata utajiri wa haraka. 

Kwamba  Freemasons inahusishwa pia na nguvu za giza ikiwamo imani za kimashetani. Walioanzisha upotoshaji huu wanajua kuwa hiyo Freemasons ni jumuiya ya kimataifa kama ilivyo kwa Rottery na  Lions Club ambazo uanachama wake haupo wazi kwa yeyote yule bila kupitia wanachama wenyewe. Lakini haimaanishi kuwa wanachama wa jumuiya hizo wanajipatia utajiri wa haraka kwa kushiriki ‘ abrakadabra’ .

Leo hii hapa Tanzania kuna vijana wanaoshinda vijiweni wakiwaza tu namna ya kujiunga na Freemasons badala ya kufanya kazi. Na Freemasons pia imekuwa njia ya baadhi ya wanajamii kutetea  uvivu wao.  Freemasons inatumika pia kuwaandama wenye kufanya kazi kwa bidii na kujipatia mafanikio. Maana, leo hata anayenunua pikipiki mpya ataitwa ‘ Freemason!’

Ni wakati sasa kwa Serikali kutoa tamko juu ya hili la uvumi wa Freemasons. Iweke wazi kuwa jambo hili linakuzwa na kuwa kuna upotoshaji unaofanywa kwa makusudi. Maana, uvumi huu ukiachwa uendelee unaweza kutuletea madhara makubwa huko twendako. 

Tunajua, kuwa leo wamejitokeza matapeli wanaowahadaa wanajamii kuwa wao ni Freemasons na kuwa wanaweza kuwasaidia wengine kujiunga na mtandao huo. Wamejitokeza pia waganga  wa kienyeji wenye kufanya utapeli kwa kutangaza kuwa wana uwezo wa ‘ kiganga’ wa kuwasaidia wateja wao kujiunga  na Freemasons. Wapo wanajamii wanaopoteza fedha na mali zao kwa kutapeliwa juu ya hili la Freemasons. Ndiyo maana, kuwa ni wajibu wa Serikali kuingilia kati kuwanusuru watu wake.

Ndiyo, watu wetu wako kwenye giza. Kuna upumbavu unaendelea kwenye jamii. Ni wajibu wa Serikali yao kuwasaidia kwa kuwamulikia mwanga. Na kuna tofauti ya ujinga na upumbavu. Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka;” Kusoma si kuufuta ujinga, bali ni kuupunguza”.

Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa na ujinga wa jambo si kosa, hata profesa anaweza asijue namna ya kuchochea kuni za kuchomea mhindi mbichi. Kijana wa darasa la saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda profesa.

Lakini upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu. Na ndiyo maana binadamu kuitwa mpumbavu ni tusi. Kuitwa mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga wake. Kuwa na ujinga wa jambo fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani anayeelewa kila jambo?

Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemwuliza swali hilo. Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani amgetamka, kuwa angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.

Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndiko njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri? Haya ya ya kuendekeza abrakadabra za Freemasons ni kielelezo cha Watanzania, kama ilivyokuwa kwa Babu wa Loliondo,  kuamua kuacha kufikiri. Ndiyo, kuna waliojifunika vilemba vya ujinga. Wako  gizani, wanahitaji mwanga.

Kuna wakati Waziri  Mkuu, Mizengo Pinda, aliingilia kati na kusitisha abrakadabra ya DECI iliyokuwa ikiitafuna jamii. Pinda aliwanusuru wengi. Ni wakati sasa kwa Waziri Mkuu wetu Pinda kuingilia tena kati na kulitolea tamko hili la abrakadabra ya Freemasons.  Kufanya hivyo atawanusuru wengi.


No comments:

Post a Comment