WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, April 10, 2013

Neno La Leo: ' Jogoo Mwembamba' Kaapishwa Urais- Ni Uhuru Kenyatta


2 4f64f

Ndugu zangu,
SIASA za Afrika zina yasiyolingana na siasa za wenzetu wa mataifa mengine. Afrika aliyechafuliwa sana anaweza kuibuka akawa msafi kama aliyesafishwa na sabuni ya punda. Na hasa, kama katika kuchafuliwa huko kutakuwa na shaka ya wanyonge kuhisi aliyechafuliwa  kaonewa.
Naam, wanyonge wengi Afrika wanauzoefu wa kuonewa.

Niliandika saa kadhaa tu baada ya matokeo ya uchaguzi wa Kenya kuanza kutangazwa; Kuwa kuna kila dalili kuwa Uhuru Kenyatta anaelekea kwenye ushindi.

Hiki ndicho nilichoandika;

"Afrika ukikuta jogoo wawili wanagombana, basi, hapo hapakosi mashabiki. Na kila shabiki aliyesimama kutazama mpambano wa majogoo hao, ujue, kuwa ana jogoo wake anayemshabikia.

Na jogoo anayemshabikia akishindwa pambano, shabiki ataondoka akisononeka. Kuna ambao watakosa hata hamu ya chakula siku hiyo. Kisa? Jogoo wake kagalagazwa!

Na kama jogoo mmoja ni mnene na mwingine ni mwembamba, ujue, kuwa jogoo mwembamba ana mashabiki wengi.

Ukifuatilia mwenendo wa Uchaguzi wa Kenya kuna dalili kuwa Uhuru Kenyatta ambaye pia anatuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai anaelekea kwenye kupata ushindi.
Moja ya tafsiri ya jambo hili ni ilivyo kwenye fikra za wapiga kura ambao ni wengi ni watu wa kawaida- kuwa Uhuru anaonewa, hata na mataifa ya nje. Kwamba mambo ya Kenya yao yanaingiliwa pia na wasio Wakenya, tena Wazungu.

Wakenya wana historia ya mapambano magumu ya kudai uhuru kutoka kwa ' Wazungu'- ni tangu enzi za Mau Mau.

Pamoja na utajiri wake, bado Wakenya wengi wa kawaida wanamwona Uhuru kama mtu wanayefanana naye. Ni mwanadamu kama wengine. Huko nyuma Uhuru amekuwa na historia ya matatizo binafsi pia ya kimaisha, ikiwamo matatizo ya pombe, hivyo ya kifamilia pia. Wakenya wengi wanaishi wakijisikia kuwa wananyanyaswa na kuonewa. Wanamwona Uhuru Kenyatta kuwa ni mtu anayeonewa pia.

Hivyo, yawezekana kuna kura za ' kuonewa huruma' ambazo Uhuru Kenyatta anaweza kuzipata, hata kutoka kwa watu wa kabila la Wajaluo. Wanaojiona ' wanafanana naye'.

Na lingine ambalo laweza kutokea ni ukweli, kuwa katika matatizo mengi wanayoyakabili Wakenya kwa sasa, kuna ambao wanaikumbuka ' Bora ya jana' ya Mzee Jommo Kenyatta. Wanaikumbuka historia. hivyo, kuna Wakenya waliopiga kura za ' nostalgie'- Kura za ' Zilipendwa'.

Kuna Wakenya wengi walimpenda Mzee Jommo Kenyatta. Bado wanakumbukumbu za ' Fuata Nyayo'. Na Uhuru naye anaitwa ' Kenyatta'- Jina lake la pili. Ni mwana wa Mzee wa ' Fuata Nyayo.

Naam, Nyayo zilishapotea. Kuna wenye hamu ya kuzitafuta. Wanaamini Uhuru atawasaidia kuziona. Na tusubiri tuone.”
Na liwe Neno La Leo.
Maggid,
Iringa

No comments:

Post a Comment