WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 20, 2013

Siri ya waliofeli kidato cha nne 2012 nje nje



MKANGANYIKO wa gredi za ufaulu, pamoja na mambo mengine, ulichangia kuleta matokeo mabaya ya wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2012, imebainika.
Aidha, utafiti wa Raia Mwema uliofanyika katika mikoa 13 nchini, umebaini pia kwamba mabadiliko ya ufundishaji na utungaji mitihani kutoka kwenye msisitizo wa nadharia kwenda kwenye msisitizo wa ujuzi, na usahihishaji,  nayo ni kati ya sababu nyingi za matokeo hayo mabaya ya wahitimu wa mwaka jana na mengine ya miaka kadhaa ya nyuma.
Timu ya uchunguzi wa kiuandishi wa habari ya Raia Mwema mwanzoni mwa mwezi huu ilizuru Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Mbeya, Manyara, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Rukwa,  Singida, Pemba na Shinyanga ikitembelea shule za sekondari 48, zikiwamo zilizoshika nafasi za chini kabisa katika matokeo hayo na ikihojiana na baadhi ya walimu wakuu, walimu, wanafunzi, wadau mbalimbali wa elimu na jamii inayoishi jirani na shule hizo.
Taarifa zinaonyesha kwamba kwa maeneo makuu: Gredi, ufundishaji na utungaji mitihani kulenga wanafunzi kutumia zaidi ujuzi; si walimu wala wanafunzi waliopewa taarifa rasmi ya kutosha ili wajiandae kwa mabadiliko hayo makubwa katika maeneo ya kutahini na ufundishaji.
Utafiti huo pia umeonyesha ya kuwa shule nyingi zilizofanya vibaya sana katika matokeo hayo ya mwaka jana ni za Kata, ambazo wahitimu wake, kama walivyokuwa wa shule  nyingine zilizofanya vizuri kiasi mwaka 2012, ni wale ambao wakiwa kidato cha pili walifanya mtihani wa mchujo, wakashindwa, lakini wakaruhusiwa kuendelea na shule kwa uamuzi wa Serikali.
Lakini ukiacha sababu hizo za gredi, ufundishaji na utungaji mitihani, nyingi za shule hizo zina upungufu mkubwa wa walimu, ama walimu waliopo hawana hamasa kwa kukosa maslahi; wengi wao wako katika mgomo baridi tangu katikati ya mwaka jana pale Serikali ilipotungua katika Mahakama Kuu madai yao yaliyoendana na mgomo mkubwa wa nchi nzima; ni shule ambazo hazina nyumba za walimu zinazoweza kuitwa kuwa ni nyumba; hazina maktaba; hazina maabara; hazijawahi kufikiwa na wakaguzi; ziko kwenye mazingira mabaya; na jamii inayozizunguka haina mwamko wa kutosha wa elimu.
Si tu kwamba shule hizo hazina miundombinu hiyo ya ufundishaji na mazingira mazuri, bali pia hazina wafanyakazi ambao si wa taaluma ya ualimu, kama wa maabara, uhasibu, afya na walinzi, jambo ambalo hufanya wakuu wa shule kufanya kazi za ziada katika mazingira ya upungufu mkubwa wa walimu huku na wao wakihitajika kufundisha.
Ni katika mazingira hayo taarifa ya mabadiliko katika utaratibu wa muda mrefu wa gredi za ushindi inakuwa habari kubwa. Alama zinazofahamika kwa muda mrefu ni A- alama 81 hadi 100; B- alama 61 hadi 80; C-alama 41 hadi 60; D- alama 21 hadi 40 na F- alama 0 hadi 20.
Kwamba alama hizo zimekuwa zikibadilishwa na Baraza la Mitihani (NECTA) katika kile kinachojulikana kuwa ni standardisation ni taarifa iliyowatisha wengi. Ni hali iliyowaathiri kwa aina ya pekee watahiniwa wa mwaka 2012, hata kama kwa miaka karibu mitano ya nyuma matokeo ya kidato cha nne, na hata ya kidato cha sita, yamekuwa yakionyesha kuserereka kuelekea chini.
Vyanzo kadhaa vya habari vinasema alama hizo sasa ziko katika makundi ya A-alama 85 hadi 100; B-alama 65 hadi 84; C-alama 50 hadi 64; D-alama 35 hadi 49 na F alama 0 hadi 34.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Azania, Dar es Saalam, Bernard Ngozye, anasema matokeo hayo mabaya yaliwashangaza wadau wa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam kiasi cha wao kukutana na kuhoji Baraza la Mitihani kujua chanzo ni nini.
Anasema Machi mwaka huu walikutana na maofisa wa Baraza la Mitihani na ndipo hapo walipoambiwa kwamba Baraza lilirekebisha gredi, taarifa hiyo wakiisikia kwa mara ya kwanza.
“Matokeo hayo yalitufadhaisha sana. Ni kweli hapa hatuna walimu wa kutosha. Watahiniwa hawakusoma vizuri masomo ya sayansi kwa kuwa sisi sote hapa ni walimu wa masomo ya sanaa. Lakini tulikuwa tunataraji walau wachache watapita katika madaraja ya nne au tatu.
“Walikuja hapa wenzenu. Niliwaambia haya haya. Mmoja baadaye akaniuliza kama nilikuwa ninajua kwamba gredi za Baraza ziko juu, nikasema hapana,” anasema Fredy John, Mkuu wa Shule ya Sekondari Chitekete, Newala, Mtwara, ambayo ni kati ya shule 10 zilizofanya vibaya zaidi kitaifa.
“Nami matokeo haya yamenishangaza sana.  Shule yangu haina matatizo ya walimu, maabara wala maktaba, lakini imefanya vibaya tofauti na matarajio yetu,” anasema Sid Moir, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Katoke Lweru, Muleba, Kagera.
Anaongeza Moir: “Kilichonisikitisha ni kuona wanafunzi ambao tangu kidato cha kwanza hadi cha nne walionyesha uwezo mkubwa kimasomo wanatoka na ufaulu wa daraja la nne. Ndoto zao zote za kusomea udaktari zimeyeyuka.”
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Hamisi Maulidi anasema hakuna mabadiliko yoyote katika alama za madaraja ya ufaulu wa wanafunzi na kwamba kama kuna taarifa hizo, ni za kupuuza.
"Hicho kitu umekitoa wapi? Hizo ni habari za kupuuza, alama hazijabadilika zimebaki kuwa zile zile hazijabadilika" alisema Maulidi.
Lakini habari kutoka ndani ya Idara ya Ukaguzi Elimu, Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza, zinasema uko mchakato unaoendelea wa kufanyia mabadiliko alama hizo ndani ya Baraza la Mitihani huku Mkuu wa Shule ya Sekondari Mukituntu, Ukerewe, Mwanza, Valence Magesa, akisema hawana taarifa za ukweli wa mabadiliko hayo, wao wanajua zinazotumika ni zilizokuwapo tangu zamani.
"Hapana. Hatujui kama kuna mabadiliko hayo ya alama za madaraja ya ufaulu. Wakibadili si lazima walimu na wanafunzi wawe na taarifa? Haya mabadiliko hayapo," alisema Magesa.
Habari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi zinasema hata hivyo kwamba kwa muda sasa imekuwapo tofauti kubwa kwenye mfumo wa kupanga alama na madaraja ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya sekondari kati ya Baraza la Mitihani na shule.
Raia Mwema limeambiwa kutoka wizarani kwamba zipo tofauti katika viwango vya alama zinazotumika, vya shuleni vikiwa chini ya vile vinavyotumiwa na Baraza hatua ambayo inatafsiriwa na baadhi ya walimu kuwa inachangia katika matokeo mabovu ya wanafunzi wao.
Taarifa zinasema kinachoichanganya zaidi wizara sasa ni ukweli kwamba standardisation imekuwa ikifanyika kwa miaka nenda rudi lakini matokeo hayakuwahi kuwa mabaya kama ilivyotokea mwaka jana.
Lakini msemaji wa Baraza la Mitihani, John Nchimbi, katika kukoleza mkanganyiko wa matokeo hayo ya mwaka jana,   ameliambia Raia Mwema kwamba Baraza halijawahi kubadili alama za ufaulu.
“Sisi tangu Baraza lianzishwe hatujawahi kubadili wastani wa masomo, wastani bado upo uleule. Hatuwezi kubadili bila ya kuwashirikisha watu wa Wizara ya Elimu. Lazima tupate baraka zao, hata huko nenda ukaulize watakueleza hivyo hivyo.  Sijui kwa sasa wastani unaanzia ngapi, lakini nitakufahamisha baada ya kupitia. Kwa sasa sina uhakika sana,” alisema Nchimbi.
Mbali na mabadiliko ya gredi, mabadiliko mengine yanayoelezwa kuchangia katika matokeo mabaya ya mwaka jana ni ya ufundishaji na utungaji mitihani ambayo nayo hayakufanyiwa maandalizi ya kutosha.
Chini ya mabadiliko hayo mwanafunzi anayehitimu anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza, si kukariri, na ufahamu wa masuala mbalimbali yakiwamo ya kitaifa na kimataifa.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Aquinas, iliyoko Halmashauri ya Mtwara, Sister Maureen Cariaga OSB, anasema kubadili mitaala ni jambo la kawaida kulingana na mazingira ya wakati husika, lakini mabadiliko hayo yawe yamefanyiwa maandalizi ya kutosha.
“Hapa kwetu matokeo hayakuwa mabaya. Tuna walimu wa kutosha na mahitaji yote yapo. Tunachuja vizuri wanaoingia kidato cha kwanza, tunafuatilia maendeleo yao mpaka juu. Hata mchujo wa walimu ni mgumu kidogo. Ninaweza kusema kwamba mabadiliko kutoka kwenye nadharia kwenda kwenye ujuzi nayo yatakuwa yamechangia ushindi kushuka.
“ Hapakuwa na muda wa kutosha wa maandalizi kwa walimu na wanafunzi. Si kwamba hili la mabadiliko ni jambo baya, hasha. Lakini maandalizi ya kutosha ni muhimu. Tulitakiwa tujiandae pengine kuanzia mwaka 2009,” anasema Sister Maureen ambaye shule yake ni kati ya zilizofanya vizuri mkoani Mtwara.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bureza, Muleba, Theonestina Deogratias, na makamu wake,  Fredius Banywani,  wanalalamikia utungaji wa mitihani.
“Setting (utungaji) wa mitihani ulikuwa tofauti na uliozoeleka,” anasema mwalimu Theonestina.
Alitoa mfano wa somo la  Historia kwamba  mtihani ulitungwa kwa namna ambayo mwanafunzi alitakiwa ajieleze kwa maneno yake kwa kuingia ndani zaidi  na si kutegemea  maelezo aliyoyasoma kwenye kitabu peke yake.
Jambo kama hilo pia lililalamikiwa na Mkuu wa Shule ya Katoke Lweru, Moir,  ambaye alisema ya kuwa katika  mtihani wa Uraia,  yalitungwa maswali yanayoegemea zaidi uelewa wa masuala yanayotokea nchini na duniani kwa ujumla, masuala ambayo yanahitaji mwanafunzi kuwa mfuatiliaji mzuri wa magazeti, redio na televisheni.
“Mwanafunzi anayesoma shule ya bweni si rahisi  kuwa mfuatiliaji wa vitu hivyo,” alisema.
Lakini ofisa mmoja wa elimu kutoka Ofisi ya Elimu ya Mkoa wa Lindi ameliambia Raia Mwema kwamba matokeo mabaya ya wahitimu wa mwaka 2012 hayawezi kuelezwa kwa sababu moja tu au mbili.
“Tunaweza kutaja mitaala au hata mabadiliko hayo ya ufundishaji na utungaji, lakini ukweli unabaki kwamba hatutapata jibu la hakika la nini kinachotokea mpaka sote tuamue kushughulikia elimu kwa jinsi inavyopasa.
“Kwa hiyo ofisa elimu hana jibu la moja kwa moja la nini hasa chanzo cha matokeo mabaya. Huko nyuma tulikwisha kusema kwamba kwa Mikoa kama hii ya Lindi, iliyo pembezoni, ipewe upendeleo wa kibajeti. Uamuzi huo ukakubalika lakini ukabaki kwenye nyaraka tu.
“Tuna Wakaguzi wa Kanda, lakini kawaulize kwa mwaka jana walikagua shule ngapi? Hawana usafiri, na hata kama wakipata gari, hawawezi kupata mafuta kwa sababu hakuna bajeti ya mafuta,” anasema ofisa huyo akiomba asitajwe.
Msemaji wa Baraza la Mitihani, John Nchimbi anasema Baraza la Mitihani halihusiki na mabadiliko katika ufundishaji. Kazi hiyo ni ya taasisi nyingine.
“Sisi hatuhusiki katika mabadiliko ya ufundishaji. Lakini Taasisi ya Elimu watakusaidia. Nakumbuka utaratibu wa ufundishaji na kuandaa maswali ulibadilika tangu mwaka 2005, lakini mtihani wa kwanza uliotungwa kwa muundo huo ulikuja miaka mitatu baadaye (2008).
“Katika mtindo huu mwanafunzi anafundishwa kuelewa, si kukariri, yaani mwanafunzi anatakiwa kuelezea kwa kina namna alivyoelewa. Hiyo ni tofauti na zamani kwani wakati huo mwanafunzi alikuwa anaelezea kwa ufupi tu.
“Walimu walipewa semina na sisi baada ya hapo tukaliacha suala hilo kwa Taasisi ya Elimu. Hatuhusiki tena, tunachosubiri ni kuwatahini tu na kutoa matokeo,” alisema Nchimbi.
Wakufunzi wa Chuo cha Ualimu Katoke, Muleba, Kagera, wanaeleza kasoro nyingi zilizosababisha ufaulu mdogo zikitokana na elimu nchini kushuka kwa jumla.
Wanasema nia ya Serikali ya kutaka kila mtoto afike sekondari bila kujali uwezo wake, imechangia pia kwa kiwango kikubwa kufeli kwa wanafunzi wengi.
Wanasema ya kuwa nia ya Serikali ilikuwa ni nzuri lakini utekelezaji wake umekuwa mbaya kwani  uliingiliwa na wanasiasa  ambao wengi walifanya mbinu za kulazimisha wanafunzi wa  darasa la saba wafaulu kwa wingi kuingia sekondari.
Wanasema ya kuwa baadhi ya madiwani na hata wakuu wa wilaya, walifanya kila linalowezekana kufaulisha wanafunzi wengi kama mtaji wao wa kisiasa ili  waonekane kuwa ni wachapa kazi hodari.
“Inapendeza masikioni kusikia kwamba shule imefaulisha wanafunzi kwa asilimia 80 au 90, lakini hao wanafunzi wamefaulu kwa kiwango cha kuridhisha au wamesukumwa tu? 
“Hilo ndilo jambo la kujiuliza, na ukichunguza utakuta wengi walisukumwa ili wanasiasa na watendaji waweze kutamba kwenye majukwaa ya kisiasa,”  alisema  mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari ya Bwanjai iliyoko  Mugana, Wilaya ya Misenyi, Kagera, ambaye hakutaka jina lake litajwe katika suala hilo.
Aliongeza:  “Serikali inatamba kwamba imeongeza shule za sekondari kutoka 1,700 hadi 4,000  ili wote waliofaulu waingie sekondari, lakini  ilijiandaa na changamoto za kuwa na walimu wa kutosha? Kuwa na shule zenye maabara na maktaba?  Jibu ni hapana. Sasa tunashangaa vipi tunapokuwa na idadi kubwa ya waliofeli?”
Alisema ya kuwa shule nyingi zimejengwa lakini nyingi zina matatizo mengi kama vile ukosefu wa nyumba za walimu na hazina maabara wala maktaba kwa ajili ya watoto kujisomea.
“Mazingira kwa ujumla hayatoi nafasi kwa mwanafunzi kuwa na ari ya kusoma, hivyo anakuwa pale shuleni kwa ajili ya kuhudhuria tu masomo na si kusoma kwa nia ya kufaulu ili aendelee na elimu ambayo tunasema haina  mwisho,”  aliongeza.
Ni habari ya wazi kwamba kwa muda mrefu  nchi ina upungufu mkubwa wa walimu, utafiti wetu kuhusu walimu, hata hivyo, umeonyesha kitu cha ziada: Katika upungufu huo mkubwa, walimu wa sanaa ni wengi kuliko wa sayansi, kiasi kwamba katika shule nyingi zilizotembelewa na waandishi wetu, masomo ya fizikia, kemia, baiolojia na hesabu hayafundishwi kwa vidato vya tatu na nne.
Shule  ya  Sekondari Rungwa ya Manyoni, Singida ni kati shule zilizofanya vibaya katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 kwa watahiniwa wote 18 waliofanya mtihani huo kupata daraja sifuri.
Shule hiyo ambayo inamilikiwa na serikali, ilianzishwa mwaka 2007 kwa nguvu za wananchi wa vijiji vitatu vya Rungwa, Magembe na Kintanula ambavyo kwa pamoja vinaunda Kata ya Rungwa.
Ina upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu. Wanafunzi waliotahiniwa mwaka jana wanasema katika kipindi chote cha miaka minne hawakuwahi kufundishwa masomo ya hesabu, fizikia, kemia na baolojia kutokana na masomo hayo kukosa walimu.
Mmoja wa watahiniwa wa mwaka jana, Daudi Reffi (23) anasema: “Waalimu wawili waliopo wanafundisha masomo ya sayansi ya jamii tu kama historia, jiografia na yale ya lugha kama Kiingereza na Kiswahili. Hatukuwahi kufundishwa masomo mengine.”
Daudi sasa ni dereva na fundi wa pikipiki (bodaboda) na anasema hana mpango wa kusoma tena. Amekatishwa tama na hali ya mambo.
Anaeleza: “Masomo tuliyofanyia mitihani ni Historia, Kiswahili, Uraia na Kiingereza lakini hayo mengine ya sayansi hakuna aliyefanya mtihani wake kwa kuwa hatukuwahi kufundishwa.”
Maneno ya Daudi yanathibitishwa na Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mhangwa Masanja, ambaye anaeleza kuwa  tangu mwaka 2007, baada ya kuanzishwa, shule hiyo haikuwahi kuwa na walimu zaidi ya wawili kwa wakati moja kwani kila walimu waliopangwa shuleni hapo hutafuta uhamisho kabla hata ya mwezi kumalizika.
 “Kwa sasa tupo walimu wawili tu ambao tunalazimika kufundisha wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, na bado pia hakuna walimu wa masomo ya sayansi na hesabu ingawa kuna taarifa kuwa wanakuja walimu wapya watatu,”anaeleza mwalimu Masanja.
Anaongeza mwalimu Masanja: “Kwa kweli hali ni ngumu. Walimu wawili hawawezi kufundisha wanafunzi 113, kwa masomo yote, na kumaliza syllubus itakayomfanya mwanafunzi kufanya mitihani yake kwa mafaniko”.
Moja ya sababu zinazofanya walimu kuikimbia shule hiyo ni mazingira magumu ya shule hiyo ambayo iko zaidi ya kilomita 350 kutoka Makao Makuu ya Mkoa wa Singida, na kilomita 250 kutoka Manyoni, ambako ni Makao Makuu ya Wilaya. Takwimu katika Mikoa ya Mbeya na Rukwa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya walimu wa sekondari ni wa masomo ya sayansi jamii ama sanaa. Walimu wa masomo ya sayansi hawazidi asilimia tano.
Miongoni mwa shule za sekondari zilizotembelewa na waandishi wetu katika mikoa hiyo ni Shule ya Sekondari Sumbawanga yenye walimu 37 na kati ya hao 32 ni walimu wa masomo ya sanaa, lakini hayo ndiyo masomo ambayo wanafunzi wamefeli zaidi ikilinganishwa na ya sayansi yenye walimu watano lakini wanafunzi wakifaulu zaidi.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sumbawanga, Modesta Kivagala, anathibitisha hoja ya wingi wa walimu wa masomo ya sanaa katika shule yake na matokeo mabovu ya wanafunzi katika masomo hayo.
“Walimu wa arts ni wengi lakini ndiyo masomo ambayo wanafunzi wanafeli zaidi, walimu wa sayansi ni wachache lakini wanafanya kazi, hapa shuleni tupo walimu 37, kati ya hao walimu 32 ni wa masomo ya arts,” anasema.
Kwa mujibu wa matokeo ya elimu ya kuhitimu kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Sumbawanga, kati ya wanafunzi 151 waliofanya mtihani, 85 walifeli, 61 waliambulia daraja la nne, sita daraja la tatu na wanne daraja la pili.
Hali hiyo ya kuwa na walimu wengi wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari nchini inajitokeza hata katika Shule ya Sekondari Ipepa iliyopo katika Kata ya Molo eneo la Makuzani, wilayani Sumbawanga. Pamoja na na shule hiyo kuwa na idadi nzuri ya walimu, wanafunzi 62 kati ya 87 waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari mwaka jana walifeli. Alifaulu mmoja kwa kiwango cha daraja la tatu, 13 daraja la nne huku daraja la kwanza na la pili wakikosekana.
Akizungumzia hali ya matokeo katika shule hiyo, mwalimu Diwed Kikoti anasema: “Walimu wapo wa kutosha. Lakini wengi ni wa masomo ya arts.”
Tatizo la bajeti ya elimu limekuwa likijirudia katika maoni ya utafiti na hali mkoani Shinyanga inaelezea jinsi bajeti ilivyo na umuhimu.
Kwa Wilaya ya Shinyanga; mwaka 2012/2013, wakati shule za msingi zilitengewa Sh. bilioni moja kwa mwaka huo, na Sh. 25m za matumizi mengine kwa mwezi, shule za sekondari zilitengewa Sh. 309m kwa mwaka na Sh. 2m tu za matumizi mengineyo kwa mwezi, kiasi ambacho hakiwezi kukidhi ukaguzi na uendeshaji wa shule hizo, licha pia kwamba fedha hazipatikani kwa wakati mwafaka; na hata zinapopatikana mara nyingi zimetumika kwa shughuli tofauti kwa Halmashauri za Wilaya na Miji zenye kukabiliwa na ukata mara kwa mara, kwa lengo la kuzirejesha baadaye, wakati huo huduma kwa shule hizo zikiendelea kudidimia.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Kigoma, Simoni Humbi anasema tatizo jingine ni kwamba baadhi ya walimu kuanzia ngazi ya msingi na sekondari hawana moyo wa uzalendo kwa Taifa lao na ndiyo maana hata shule zao zinapofanya vibaya wanashangilia badala ya kusikitika.
Anasema zamani wakati Watanzania wamejawa na uzalendo kwa Taifa lao, walimu walikuwa wakisikitika na baadhi yao kufikia hata hatua ya kutoa machozi pindi shule zao zinapotoa matokeo mabaya, lakini katika miaka hii ya sasa hakuna mwalimu anayeshtuka wala kusikitishwa na matokeo mabaya.
Akizungumzia hoja za kwamba mishahara midogo kwa walimu na Serikali kutowajali na kutowalipa stahili zao ndicho chanzo cha kuporomoka kwa elimu nchini alisema kwa uzoefu wake wa takriban miaka 40 katika utumishi wa umma, hakuna watumishi serikalini wanaopewa kipaumbele katika madai yao kama kada ya ualimu.
“Dhana ya uzalendo imeshuka. Siku hizi hakuna uzalendo wa mwalimu kwa mwanafunzi wake. Zamani mwanafunzi akifeli, mwalimu anasikitika kweli kweli…lakini leo, mwanafunzi akifeli walimu wanapongezana. Tukiweka utaifa mbele, elimu yetu itarejea kwenye mstari. Kuna shule zina kila kitu, lakini wanafunzi wamefeli,” alisema Humbi.
Mmoja wa wadau wa elimu nchini, Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, anasema dawa ya matatizo ya elimu nchini ni kuirejea ripoti ya Tume ya Makweta.
“ Mwishoni mwa miaka ya 1970, na mwanzoni mwa miaka ya 1980, Mwalimu Julius Nyerere aliona matatizo ya mfumo mbovu wa elimu na ndiyo maana kabla ya kuondoka madarakani, yaani mwaka 1981, aliunda tume ya Jackson Makweta, kuangalia namna ya kupata mwongozo sahihi kwa mfumo wa Kitanzania unaoendana na desturi zetu, ili tushindane na ulimwengu kupambana na maadui watatu.
“Miaka miwili baadaye tume ya Makweta ilikamilisha kazi yake lakini ripoti haikufanyiwa kazi mpaka 1995 ndipo ikaandikwa Sera ya Elimu ya Taifa ambayo chini ya aliyekuwa waziri wa elimu wakati huo, Profesa Philemon Sarungi, “ anasema Mbatia.
Anasema Mbatia kuhusu ripoti hiyo ya Makweta: “ Ripoti hiyo ya wakati wa Sarungi ilikuwa na makosa sana, yaani kwa kifupi ilichakachuliwa.”
Kwa mujibu wa Mbatia, bila pia kuwahudumia ipasavyo walimu ni ndoto kuirejesha elimu mahali pazuri kwa vile matatizo yanayowakumba walimu ni kukosa kuthaminiwa, mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwemo kulipwa stahili zao kwa wakati na makazi.
“Hakuna uwiano sawa wa walimu na wanafunzi. Ni kawaida mwalimu mmoja wanafunzi  25, lakini huko mikoani na hata Dar es Salaam kuna shule zina walimu wawili tu ama watatu, walimu vijijini wanakimbia kwa sababu hakuna heshima, hawapewi motisha, mazingira ya kazi ni mabovu.
“Niliwahi kutembelea Mkoa wa Kigoma, Kata ya Nyangabo, Shule ya Msingi Reli Mpya, pale  mwalimu mkuu hana pa kulala, kuna kibanda ni ofisi ya mtu anasubiri ofisi ikifungwa ndipo alale. Nimekagua madaftari ya wanafunzi wameandika makosa na wamewekewa tiki. Unamuandaa vipi mtu huyu kufaulu mtihani wa kidato cha nne,” alihoji Mbatia. Wadau wa elimu wakiwamo walimu wa muda mrefu, maofisa wa elimu na hata watumishi wa idara mbalimbali zinazosimamia elimu wanalinyooshea kidole Baraza la Mitihani la Taifa, wakielezea kuwa limechangia kwa kiasi kikubwa matokeo mabaya na mkanganyiko katika matokeo.
Maeneo ambayo wadau hao wanayataja ni pamoja na ubadilishaji wa mifumo na wataalamu bila kuwapo maandalizi ya kutosha pamoja na kutokuwapo kwa umakini miongoni mwa watendaji wa Baraza katika kusimamia mifumo mipya iliyoingizwa kwa nia ya kuboresha mitihani.
“Hadi sasa mitambo mipya iliyofungwa na baraza inasumbua kwa sababu tu uongozi ulilazimisha kuondoa mifumo ya zamani kwa haraka badala ya kufuata ushauri uliotolewa na wataalamu kwamba mitambo mipya ifanye kazi sambamba na mifumo ya zamani ili kuepuka mikanganyiko inayotokea sasa,” anasema mtaalamu mmoja ambaye ni mtumishi mwandamizi serikalini.
Anasema pamoja na kufungwa kwa mitambo mipya, wataalamu ambao waliandaliwa kwa kazi hiyo waliondolewa na kuwekwa wapya ambao hawajaandaliwa wala kufanyiwa tathmini ya weledi na maadili yao na hivyo wanashindwa ama wanafanya kazi chini ya kiwango. Mfano wa matatizo ya wataalamu hao ni mkanganyiko uliotokea kwa matokeo ya mitihani ya elimu ya Dini ya Kiislamu na matokeo mengine ambayo baadhi ya wanafunzi walibainika kupewa alama wasizostahili.
Mkanganyiko katika mitihani ya elimu ya Dini ya Kiislamu ulitokana na uzembe katika kuingiza alama katika mitambo bila kubadili kifaa cha kufanyia hesabu na hivyo kusababisha kuwapo kwa hisia potofu kwamba wahitimu walionewa kwa sababu ya imani zao.
“Islamic Knowldge walifanya mitihani miwili badala ya mitatu iliyozoeleka, sasa mashine ya kugawanya haikurekebishwa ikaachwa igawanye mara tatu wakati mitihani ilifanywa miwili, matokeo yake wahitimu wote walipunjwa alama za jumla,” anasema mtumishi huyo wa serikali.
Msemaji wa Baraza la Mitihani, John Nchimbi, anakiri tatizo hilo akisema, “Mashine inasetiwa kuchakata matokeo, miaka yote mtihani wa dini ya Kiislamu ilikuwa inafanyika kurasa tatu, baada ya mtaala kubadilika ikawa inafanyika karatasi mbili. Na mashine ikawa imezoea kuchakata karatasi tatu ikawa inagawanya kwa tatu badala ya mbili.
“Kulikuwa na technical problem wanafunzi wa somo la Dini ya Kiislamu wanafunzi wakawa wanapata alama pungufu. Lakini tatizo hilo tulilibadilisha haraka baada ya kuligundua,” anasema Nchimbi bila kueleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika, ambao wanahusika pia na kuathiri watahiniwa katika mitihani mingine.
Eneo la usahihishaji nalo limezungumzwa na wadau mbalimbali wakiwamo watumishi wa idara za elimu katika wilaya mbalimbali na walimu, ambao wanasema kwa sasa utaratibu wa upatikanaji wa wasahihishaji umekuwa hauzingatii viwango kama zamani na hivyo kujikuta wakienda wasahihishaji wasio na uwezo na wasio waadilifu.
“Kwa kweli sasa ni tatizo maana walimu wenye uzoefu na waadilifu siku hizi wanaachwa na wanakwenda watoto wadogo ambao hawana uwezo na wasiojali maadili ya kazi na hivyo kwenda kufanya kazi kwa maslahi yao na si kuzingatia maadili,” anasema Ofisa Mwandamizi wa serikali kisiwani Pemba, ambaye ni mwalimu kitaaluma.
Kutokana na baadhi ya wasahihishaji kutokuwa na uzoefu, na kulipwa kwa kila nakala za mtihani wanazosahihisha, baadhi wamekuwa wakifanya kazi kwa haraka kiasi cha kupoteza umakini ili waweze kupata malipo zaidi.
Msemaji wa Baraza, John Nchimbi anakiri kuhusu wasahihishaji kulipwa kwa jinsi hiyo lakini anasema hana takwimu ni kiasi gani wanalipwa kwa kila mtihani lakini akitaja vigezo vya walimu wanaopewa kazi ya kusahihisha mitihani kuwa ni:
“Anayefaa kusahihisha kidato cha nne awe mwalimu ambaye ameshafundisha miaka mitatu tangu amepata diploma ya ualimu. Kwa kidato cha sita ni yule ambaye amefundisha miaka mitatu tangu amepata shahada ya ualimu.
“Namna tunavyowapata tunatuma barua kwa mikoa yote na katika barua hiyo tunaambatanisha vigezo vyetu. Mwalimu Mkuu anapendekeza majina na sisi tunatuma katika kamati za mitihani mkoa, wao wanaangalia nidhamu na vigezo vingine.
“Pia tunataka mwalimu awe na afya nzuri maana zoezi la usahihishaji linachukua muda mrefu, ni mwezi mmoja kwa kidato cha nne, kidato cha sita ni siku 19 mpaka 20. Lakini chochote kinaweza kutokea kutokana na jinsi mitihani ilivyo,” anasema Nchimbi.
Hayo yakiendelea timu yetu ya watafiti imepata taarifa kwamba baadhi ya wasahihishaji wa mitihani ya mwaka jana walirejeshwa vituoni kwao kutokana na kugundulika kuwa hawakuwa na vigezo tosha.
“Kwa kawaida mwalimu akija kituoni kuanza zoezi la usahihishaji lazima awe na barua kutoka kwa Mwalimu Mkuu, na akija mwalimu ambaye hana utambulisho huwa tunamrudisha alikotoka. Sijasikia kuhusu walimu waliorudishwa mwaka jana lakini kama walikuwapo sishangai maana walisharudishwa wengi kwa mtindo huo wa kudanganya.
“Kwa kawaida walimu ambao watafukuzwa kwa kutotimiza vigezo tunachukua walimu wengine walio katika (data base yetu), maana tuna taarifa za walimu waliowahi kuitwa miaka ya nyuma. Tunaagiza walimu wakuu wa shule husika ili kama walimu hao wapo kazini 
tunawaita kuziba ombwe hilo.”

source: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment