WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 27, 2013

Wabunge CCM wavuana nguo


 


 *Lugora, Filikunjombe washambuliwa mbele ya Pinda
*Wajibu mapigo, Lugora asema acheni unafiki
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana waliumbuana na kushutumiana wazi mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao chao katika ukumbi wa Msekwa mjini hapa ambako waliumbuana na kushutumiana waziwazi.
Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kilifanyika baada Spika wa Bunge, Anne Makinda kuahirisha mjadala wa makadirio ya mtumizi ya fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Spika aliahirisha mjadala wa makadirio hiyo uliokuwa uhitimishwe jana, baada ya wabunge wengi kuonyesha nia ya kuyakwamisha kutokana na kutoridhishwa na jitihada za Serikali za kukabiliana na kero ya maji nchini.

Chanzo chetu kilichokuwa katika kikao hicho kilisema mjadala ulipoanza, Pinda aliizungumzia kwa kifupi Wizara ya Maji na kuonyesha jinsi Serikali ilivyokubali kwa dhati kurekebisha makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara hiyo.

Baada ya hoja hiyo, chanzo hicho kilisema Waziri Mkuu aliwasilisha hoja nyingine iliyowataka wabunge wa CCM kuchangia posho zao za siku moja kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

“Hoja hiyo ilipopita, Nyoka wa Shaba (Kangi Lugora, Mbunge wa Mwibara), alisimama na kuhoji ni kwa nini chama kimekubali kusaidia uchaguzi wa madiwani wakati huwa hakisaidii kesi za uchaguzi za wabunge.

“Si unajua Nyoka wa Shaba naye ana kesi mahakamani, sasa ndiyo maana akaamua kuhoji iweje yeye hasaidiwi na chama wakati huo huo anaambiwa asaidie uchaguzi wa madiwani.

“Alipomaliza kusema hivyo, akasimama Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba. Aliposimama aliwashutumu moja kwa moja Lugora na Filikunjombe (Deo, Mbunge wa Ludewa).

“Akasema wabunge hao badala ya kuisaidia Serikali wanapokuwa bungeni, wao wamekuwa wakiishambulia jambo ambalo halileti picha nzuri kwa wananchi.

“Akasema kitendo cha Filikunjombe kusema bungeni kwamba Serikali ina miwani ya mbao hakikuwa kizuri… akasema ‘hawa wenzetu hatuko nao na kwa kuwa mwezi ujao tutaonana na Mwenyekiti wa Chama (Rais Jakaya Kikwete) nitasema mengi’.

“Alipomaliza kusema hayo akasimama Kibajaji (Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera). Kibajaji akaungana na Nkumba, akawashambulia Lugora na Filikunjombe kwamba wanaiua Serikali kutokana na maneno yao bungeni.

“Akasema kama Lugora ana kesi mahakamani ni bora akakabiliana nayo mwenyewe kwa sababu inaonekana hayuko pamoja na chama,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Baadaye alisimama Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alimshutumu Lugora kwamba kitendo chake cha kuliambia Bunge kuwa kuna baadhi ya mawaziri wanajihusisha na dawa za kulevya, kinawaweka njia panda wananchi kwa kuwa wanahisi wabunge wao ambao ni mawaziri, nao wamo kwenye orodha hiyo ikizingatiwa kuwa hakuwataja majina.

“Pia, akahoji kama wabunge wana kero zao ni kwa nini wasiwafuate mawaziri na kuzungumza nao badala ya kuwasema bungeni.

“Kisha, alisimama Mangungu (Mbunge wa Kilwa Kaskazini) ambaye alionyesha wasiwasi juu ya majaji wanaosikiliza kesi za uchaguzi.

“Yeye akasema kesi nyingi za uchaguzi ambazo CCM inashindwa ni kwa sababu majaji wengi wanaichukia CCM na wanaipenda Chadema.

“Baadaye aliungwa mkono na Dk. Chami (Dk. Cyril Chami, Mbunge wa Moshi Vijijini) ambaye alidiriki kumtaja jaji mmoja kwa jina kwamba ana upendeleo wa wazi wazi kwa Chadema.

“Kisha, alisimama Mbunge wa Karagwe (Gosbert Blandes) na akatoa ushauri kwamba kuna haja chama kusaidia majimbo ya uchaguzi na wakati huo huo, viongozi wakuu wa chama waende kwa wananchi kama wanavyofanya viongozi wa Chadema.”

Mbali na hao, chanzo hicho kilimtaja Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia kwamba alimshutumu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kwamba hakusaidia wakati wa vurugu zilizotokea hivi karibuni mjini Mtwara.

“Ghasia alianza kwa kusema kwamba, siku hizi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, anafanya ziara za mara kwa mara jimboni kwake Mtwara Vijijini lakini CCM haijali.

“Pia akamlalamikia Waziri Nchimbi kwamba wakati wa vurugu za wananchi mkoani Mtwara alimpigia simu lakini hakupokea na hata alipomtumia ujumbe mfupi wa simu hakumjibu.

“Akahoji pia kwamba iweje wakati wa vurugu zote Mtwara, nyumba zinazochomwa ni za wabunge wa CCM wanawake na nyumba za wabunge wanaume hazichomwi, akahoji kuna kitu gani hapo,” kilisema chanzo hicho.

source Mjengwa Blog

No comments:

Post a Comment