WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, April 24, 2013

Rais Kikwete, watawajibika kwa mdomo au vitendo?

NI Jumatano nyingine tunakutana tena katika safu ya ya Jicho la Mtanzania. Wiki iliyopita, tulijadili suala la afya ya mama na mtoto, mada ambayo nilipokea michango mingi kwa njia ya simu na barua pepe.
Napenda kuwashukuru wasomaji wote walioguswa na mada hiyo. Jumatano ya leo nitazungumzia mpango maalumu wa kutathmini utendaji kazi wa viongozi wa Serikali, uliozinduliwa wiki iliyopita na Rais Jakaya Kikwete.

Ni jambo lililo wazi kuwa nchi yetu pamoja na kuwa na rasilimali nyingi ukilinganisha na nchi nyingine za Kiafrika kama jirani zetu Rwanda, bado imekuwa nyuma kimaendeleo. Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa uchumi wa nchi yetu, umekuwa lakini wananchi wake wanaishi kwenye umaskini mkubwa.

Moja kati ya sababu zinazotolewa na wachambuzi wa mambo kuhusu Tanzania kuwa maskini, wakati ikiwa na rasilimali nyingi ni usimamizi mbaya wa rasilimali za nchi. Viongozi wetu hawajaweza kuwajibika ipasavyo kusimamia rasilimali zetu na hii inakwenda mpaka kwenye sekta ya huduma.

Wiki iliyopita, naweza kusema kuwa nchi yetu iliandika historia mpya ya kujaribu kuweka utaratibu ambao utawafanya viongozi wa umma, wajenge tabia ya kufanya kazi kwa malengo na ufanisi, baada ya kuzinduliwa kwa mpango maalumu wa kutathimini utendaji kazi wa viongozi.

Tukio hili la kupongezwa ni matokeo ya ziara ya Rais Kikwete nchini Malaysia aliyoifanya mwaka 2011, ambako alikwenda pamoja na mambo mengine, kuhudhuria mkutano wa kibiashara ulioitwa mkutano wa Lankavi.

Akizungumzia mpango huo, Rais Kikwete alisema ni busara kwa nchi kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa kimaendeleo kama Uingereza, Vietnam na Malaysia ambazo zinatekeleza mpango huo.

“Nchini Malaysia, mpango huu unafanya vizuri zaidi, waziri akishindwa kutekeleza miradi aliyopangiwa, akaitwa kwa Waziri Mkuu, ina maana ameshindwa kazi na hawezi kuendelea tena kuwa waziri,” alisema Kikwete.

Alisema kuwa mpango huo mpya una lengo la kutoa majukumu kwa kiongozi mmoja mmoja, ili aweze kutoa matokeo mazuri ya kazi zake na kwamba hilo ndilo litakalomfanya aendelee na wadhifa wake.

Kwa kuanzia, wizara zitakazoanza kutekeleza mpango huo ni Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Chakula, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Maji.

Katika tukio hilo, mawaziri wa wizara zilizo katika mpango huo, walisimama na kuahidi kutekeleza majukumu yao chini ya mpango huo na kwamba hivi sasa watendaji mbalimbali wa wizara hizo wako kwenye mafunzo maalumu kuhusu mpango huo.

Mpango huu umekuwa na faida kubwa kwa nchi ambazo zimekuwa zikiutumia na leo nitajaribu kueleza namna ambavyo umeweza kuleta mabadiliko kwa jirani zetu, Rwanda.

Miaka 18 iliyopita, Rwanda ilikuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe na zaidi ya watu 800,000 waliuawa kutokana na vita hivyo, huku wengine wengi wakikimbia nchi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani ikiwamo Tanzania.

Lakini leo, Rwanda chini ya Rais Paul Kagame, imeweza kuujenga uchumi wake ulioharibiwa vibaya na vita na kuwa moja kati ya nchi chache za Kiafrika, ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.

Pato la ndani la Rwanda limekuwa kwa asilimia nane katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Rwanda haina madini, mafuta wala gesi kama ilivyo nchi yetu. Lakini kupitia rasilimali chache na vivutio vichache vya utalii pamoja na kilimo imeweza kuushangaza ulimwengu. Hii ni kwa sababu ya usimamizi mzuri wa rasilimali ambao pia ni matokea ya utaratibu kama ambao umezinduliwa hapa kwetu Tanzania.

Miundombinu Rwanda imekuwa kwa kasi ya ajabu, watu waliounganishwa kwenye gridi ya taifa, wameongezeka kutoka watu 91,000 mwaka 2006 hadi 215,000 mwaka 2011. Upatikanaji wa elimu umeimarika ambapo asilimia ya watoto wanaomaliza darasa la saba ni 79 kufikia mwaka 2011 juu ya malengo ya asilimia 58 ambayo ilijiwekea.

Tanzania tumesherehekea miaka 51 ya Uhuru, huku tukiwa hatuna Shirika la Ndege la Taifa lililo imara. Wenzetu Rwanda shirika lao limeanza mwishoni mwa mwaka 2002, lakini leo hii limekuwa na linasafirisha abiria zaidi ya nchi 15 duniani.

Rais Kagame aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akisema kuwa maendeleo ya kweli ya nchi yake, hayatatokana na misaada ya wafadhili bali katika uwekezaji wa kuwajengea uwezo watu wake.

Mwaka 1995 bajeti ya Rwanda ilikuwa ikitegemea wafadhili kwa asilimia 100, lakini mwaka 2011 ilishuka mpaka asilimia 40. Bajeti yetu ni tegemezi kwa wahisani kwa asilimia 40 kama Rwanda wakati tukisherehekea miaka 51 ya Uhuru.

Kusajili biashara Rwanda kama unakila kinachohitajika, itakuchukua siyo zaidi ya siku tatu. Karibu kila kitu kinafanyika kwa njia ya kompyuta na kumekuwa na ufanisi mkubwa.

Haya yanayotokea Rwanda siyo miujiza. Ni matokeo ya utaratibu wa kuwajibika unaokwenda na malengo ambayo viongozi huwekewa na kutakiwa kuyatimiza pasipo kuwa na visingizio na usimamizi thabiti wa utaratibu huo.

Katika nchi ya Rwanda ambayo mpango huo unatekelezwa, kiongozi wa umma anaposhindwa kufikia malengo yaliyowekwa katika wizara ama idara yake, anahesabika kuwa ameshindwa kazi na anatakiwa kuachia ngazi na kumpisha mtu mwingine.

Nafasi ya uwaziri Rwanda siyo lelemama kama hapa kwetu, ambapo mtu akiteuliwa waziri anafanya sherehe ya kujipongeza. Mawaziri wa Rwanda wanawekewa malengo ambayo wanaposhindwa kuyafikia wanatakiwa kuachia ngazi na Kagame hana msamaha na hilo.

Tanzania ni hodari wa kuwa na mipango. Mipango yetu ni mizuri kiasi kwamba hata majirani zetu wamekuwa wakiiga. Tatizo kubwa ni utekelezaji wake na ndiyo maana nimekuwa na wasiwasi kama kweli pamoja na uzuri wa mpango huu, utekelezaji wake utafanikiwa.

Fedha za walipa kodi masikini wa Tanzania, zimetumika kufanikisha mpango huu kutekelezwa hapa nchini na kwa hiyo ni matumaini ya Watanzania wengi kuona mabadiliko katika utendaji wa Serikali.

Ni wazi kuwa kama kutakuwa na ufuatiliaji wa kutosha katika utekelezaji wake, viongozi wazembe watajikuta wakijifukuzwa kazi wenyewe na kuwaacha wachapa kazi wakiendelea.

Rwanda ni mfano mzuri wa kuwa na uongozi imara wanaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika nchi. Kwa kipindi kifupi pamoja na uchache wa rasilimali, imeweza kupiga hatua kubwa ya kiuchumi, kiasi cha kuwashangaza magwiji wa kiuchumi duniani. Kwa nini isiwe sisi Tanzania?

Moja kati ya mambo yanayotufanya tusisonge mbele kimaendeleo, ni kulindana hasa inapotokea kiongozi ameboronga. Ni mara nyingi tumesikia na kuona watendaji wa Serikali wakiboronga katika utendaji kazi wao bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi yao.

Nakubaliana na nia nzuri ya Rais Kikwete ya kuanzisha utaratibu huu, ila ni muhimu sana kuwepo na ufuatiliaji wa karibu na viongozi wanaoshindwa kufikia malengo yaliyowekwa wasionewe huruma wala haya. Mungu ibariki Tanzania!

source:  Mtanzania; Justin Damian

No comments:

Post a Comment