WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 11, 2013

Mwalimu Nyerere na ukombozi wa kifikra

LEO Jumatano pale Nkrumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yanafanyika maadhimisho ya Tano ya Tamasha la Kigoda cha Mwalimu.

Nina hakika, Watanzania wanazidi kutambua, kuwa  Mwalimu Nyerere, pamoja na upungufu wake wa kibinadamu, katika uhai wake, siku zote alisimama upande wa wanyonge walio wengi.

Mwalimu aliitazama zaidi Tanzania kuliko chama alichokiongoza. Na kuna wakati, kwa maneno yake mwenyewe, Nyerere alitamka; CCM si baba wala mama yangu. Mwalimu alikuwa tayari kuikana CCM lakini si kuikana Tanzania.

Mwalimu alidhamiria kuwakomboa Watanzania kifikra ili waondokane na unyonge na umasikini wao. Hakika  Nyerere alikuwa kiongozi wa kanuni, kilichokufa ni kiwiliwili, fikra zake ziko hai na atabaki milele katika mioyo ya Watanzania wengi.
Naam, Mwalimu aliwataka Watanzania waamke. Na hapa nilipata kusimulia kisa kinachotukumbusha wajibu wetu wa kuamka sasa kutoka usingizi wa pono.

Hapo zamani palipata kutokea watu watatu. Watu hao walikuwa na ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika. Akatokea bwana mmoja akawakabidhi mikungu mitatu ya ndizi. Akawapa pia bahasha yenye barua ndani yake. Akawaagiza; "pelekeni mikungu hiyo ya ndizi nyumbani kwa rafiki yangu".

Njiani watu wale wakajisikia njaa kali. Wakautafuna mkungu mzima wa ndizi. Walipofika mwisho wa safari, wakaikabidhi mikungu ya ndizi na barua ile kwa mwenyeji wao.

Mwenyeji aliisoma kwanza barua ile, akawashukuru. Kisha akasema; "Naiona mikungu miwili. Je, uko wapi mkungu wa tatu wa ndizi? Watu wale walitahayari. Walishangaa sana, kuwa bwana yule amebaini, kuwa  njiani wamekula mkungu mzima wa ndizi!

Walirudi nyumbani wakiamini, kuwa bahasha ile waliyopewa ilikuwa na macho. Iliwaona wakati waliposimama njiani na kula ndizi zile.

Ikatokea tena, wanaume wale wakatumwa na bwana yule yule. Waende mji ule ule na kwa rafiki yake yule yule. Wapeleke tena mikungu mitatu ya ndizi. Njiani wakajisikia tena njaa kali. Wakaambizana; tusimame na tule mkungu mzima wa ndizi. Lakini, tuhakikishe, kuwa   mmoja wetu ameichukua bahasha  tuliyobeba. Aiweke ardhini, kisha aifukie kidogo na mchanga. Halafu aikalie, bahasha isiweze kabisa kuona wakati tunatafuna mkungu wa ndizi!

Wakamaliza kuutafuna mkungu wa ndizi. Wakahakikisha wametupa maganda  porini. Wakafika kwa mwenyeji wao. Wakakabidhi mikungu miwili ya ndizi na bahasha. Wakashangaa sana, kuwa hata safari hii, mwenyeji wao amewauliza tena ulipo mkungu wa tatu wa ndizi. Wakabaini, kuwa humu duniani kuna maarifa ya kusoma na kuandika.

Na hata sasa, miaka 18 baada ya kifo cha Mwalimu, jamii yetu imo katika vuguvugu la mjadala juu ya  kero ya ufisadi uliotamalaki. Wananchi wamebaini, kuwa kuna "mikungu yao ya ndizi" inaliwa njiani na watu waliotakiwa kuifikisha kwa wananchi. Wananchi wameanza kuguna na kuhoji.  Naam, wakati umebadilika.

Wananchi sasa wanawahoji  viongozi  waliowapa dhamana ya kuwatumikia. Wanawatuhumu kwa matendo yao maovu. Wananchi wana haki ya kuhoji na kudadisi. Wana haki ya kupewa majibu ya ufafanuzi, si majibu ya kubezwa. Inahusu rasilimali zao. Inahusu haki zao.

Hapa tunauona mgogoro kati ya baadhi ya waliokabidhiwa dhamana na wale wanaowaongoza. Ni kweli, kuwa baadhi ya viongozi na watendaji wetu ni wenye kutenda maovu na wasiotanguliza maslahi ya umma, bali yao binafsi. Kuukana ukweli huo si tu ni kuwadharau wananchi, bali ni kuwatukana.

Na wakati huu tukielekea kwenda kuandika Katiba Mpya ieleweke, kuwa inahusu mustakabali wetu kama taifa. Si suala la vyama vya siasa vilivyopo. Inatuhusu sote kama taifa.

Tunajua leo, kuwa viongozi wenye kutenda maovu na wasiowajibika kwa maslahi ya umma ni wachache, wamo ndani ya CCM, wamo ndani ya kambi ya upinzani. Wamo pia nje ya vyama vya siasa.

Ni wajibu wa wanaCCM wenye kukitakia mema chama chao na nchi yao, kupambana na waovu  hao ndani ya chama chao. Ni wajibu wa wanachama wa vyama vya upinzani wenye kuvitakia mema vyama vyao na nchi yao, kupambana na waovu  ndani ya vyama vyao. Ni wajibu wa hata tulio nje ya siasa za vyama, kushiriki mapambano hayo.

Mapambano haya ni ya lazima, maana, tunashuhudia wachache wenye kuhujumu rasilimali za taifa  wanavyoonyesha pia dharau  kwa umma. Wanaamini, kuwa fedha zao zitanunua haki mahakamani. Kuwa  zitawafunga pia midomo baadhi ya wanahabari.

Hata pale inapotokea wakasikia wananchi kwa wingi wao wanalalamikia jambo, au hata kuwazomea, basi,  kama ilivyokuwa kwa watu wale waliotumwa mikungu ya ndizi, nao hushangaa na kujiuliza; hivi wananchi hawa wamejuaje kuwa tunafuna rasilimali zao wakati wenye macho ya kuona na kutetea tumewakalia?

Marehemu Bob Marley ni mmoja wa wasanii mahiri waliopata kutokea humu duniani. Msanii huyu alipata kuimba; unaweza kuwapumbaza watu wachache kwa kipindi fulani, lakini huwezi kuwapumbaza watu wote kwa wakati wote! Nahitimisha.

source: Raia Mwema: Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment