WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 11, 2013

Barua ndefu kwa Profesa Issa Shivji

KWAKO Komredi Profesa Issa Shivji, Shikamoo! Ni matumaini yangu u mzima wa siha njema na unaendelea vyema na harakati za kutuamsha wanyonge tuliolala usingizi fofofo wakati rasilimali na utajiri wetu ukipokwa na mabeberu mamboleo kwa kushirikiana na ‘’makuwadi wa soko huria’’ kama alivyowaita swahiba wako mpendwa marehemu Profesa Chachage (Mungu ailaze roho yake ya kizalendo mahala pema peponi).

Pia nichukue fursa hii kukupongeza kwa jinsi unavyoitumia kalamu na taaluma yako kutukomboa kifikra sisi ‘’wasakatonge’’ tulio kwenye giza totoro. Naamini bado unazikumbuka nasaha za  Mwalimu Julius Nyerere alivyowaasa wasomi kwenye kongamano la wanazuoni (Juni 27, 1966), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba jukumu kuu la mwanazuoni wa Chuo Kikuu ni kuutafuta ukweli; kuuzungumza kadiri anavyouona na kuusimamia kwa uthabiti bila kujali gharama yake. Je, na wewe upo tayari kuuzungumza na kuusimamia ukweli mpaka mwisho wa dahari?

Kwa hakika nafahamu kwamba kuusimamia ukweli kuna gharama kubwa. Lakini, kama inavyofahamika tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa, hakuna jipya linaloweza kumwandama mzalendo yeyote ambalo wasemakweli wengine duniani hawajalipitia. Wanatheolojia wanatujuza kwamba hakuna jipya chini ya jua kwa sababu yaliyokuwapo ndiyo yatakayokuwapo; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka.

Tangu dunia ya kale historia imetufunza kwamba ipo gharama ambayo kila msemakweli duniani anapaswa kuwa tayari kuilipa kwa kujiingiza kwenye jukumu la kuwa sauti ya wanyonge wasio na sauti.

Ni hatari gani inayoweza kumkabili msemakweli hapa duniani kushinda dhoruba ya mlipuko garini iliyotupokonya kipenzi chetu Profesa Walter Rodney na unyama wa maharamia wa Kenya waliomuangamiza Komredi Tom Mboya kwa sababu ya uchu wa madaraka?

Au kuna shubiri chungu namna gani anayoweza kuinywa  mwanazuoni mzalendo kupita uchungu wa korokoroni aliyoipitia Ngugi wa Thiong’o na masaibu yaliyomuandama mwana-umajumui wa Afrika Kwame Nkurumah?

Nieleze alipo mwana wa Afrika anayeweza kutoa ushuhuda wa ukatili kwa wazalendo wa Afrika kuliko unyama aliofanyiwa Patrice Lumumba wa Kongo na mamluki Mobutu Sese Seko na Bwana zake wa ng’ambo kwa sababu tu Lumumba, chambilecho Rais Eisenhower wa Marekani, alikuwa Fidel Castro wa Afrika aliyestahili kung’olewa madarakani?

Nakuuliza profesa! Ni vioja gani vinaweza kumsibu mwanazuoni kushinda vitimbi vya Rais Mobutu Sese Seko kwa Profesa Wamba Dia Wamba na vile vya Rais Milton Obote kwa Profesa Nabudara Wadada? Ni wapi ulipo msiba utakaotutoa chozi la uchungu kuliko ule wa Steve Biko aliyepokonywa uhai kikatili na makaburu?

Nijibu komredi! Kuna changamoto gani vijana wa leo tunaweza kuzipata kuliko zile mlizopitia zama za harakati zenu za ujanani kupitia chama chenu cha kiharakati cha University Students African Revolutionary Front (USARF) wewe na wenzio kina Profesa Karim Hirji, Henry Mapolu na Liundi pale Chuo Kikuu Mlimani?Niwie radhi;nilitaka kuwasahau kina Yoweri Kaguta Museveni, Zakia Meghi na Omari Mapuri! Kwa kweli siwezi kuimaliza orodha yenu.

Wakati unastaafu uhadhiri mwaka 2006, ulitueleza kinagaubaga kwamba katika kipindi chote cha maisha yako, unajivunia sana kipindi hiki cha harakati za ujanani. Lakini, kama ulivyofafanua, makomredi wengi wa miaka ile mkiwa makinda wa Chuo Kikuu ambao sasa ni wakuu wa nchi, wanasiasa nguli na maulamaa wabobezi wa fani mbalimbali, hivi sasa wanauonea soni ukweli kwamba na wao walikuwa wanaharakati wakubwa wa ujamaa enzi za ujanani kwa vile sasa wameipokea dini mpya; dini ya ubeberu inayowashushia pepo, neema na ukwasi hapa hapa duniani!

Tunafurahi kuona umechagua kuwa upande wa wanyonge. Hivi karibuni umewahi kutufunda kuhusu thamani ya kalamu ya mwanazuoni (Rejea kitabu chako cha Insha za Mapambano ya Wanyonge). Ulisema bila kumung’unya maneno kwamba silaha pekee ya mwanazuoni ni kalamu yake na kwamba ni lazima mwanazuoni aitumie kalamu yake kwa uthabiti kila anapopata nafasi kuwasemea wanyonge wasio na sauti hususani wakulima na wafugaji. (Naomba unipe ruksa niongeze ‘’na machinga  wa Tandika, Ubungo na kwingineko Tanzaniawanaofurushwa na wanamgambo bila ya kuelekezwa pa kwenda!”)

Binafsi sina maneno toshelezi kuipambanua thamani ya kalamu ya mwanazuoni wa wanyonge zaidi ya sifa zilizotolewa na ndugu Kajubi Mukajanga kwenye Shairi lake la ‘’You write’’ (Rejea kitabu cha ‘’Summons: Poems from Tanzania’’ )

Inanilazimu kuzitafsiri beti za ndugu Kajubi kwa Kiswahili kwa sababu nakala ya barua kwako nimeisambaza pia kwa umma wa wanyonge  wa uswahilini na vijijini: wanyonge ambao mfumo wetu shelabela wa elimu umewafanya wengi wao kuwa wahitimu wa shule za kata wasioweza kuunganisha hata sentesi tatu za kizungu kwa ufasaha! Ndugu Kajubi anamsifia msomi wa wanyonge kwa maneno yafuatayo;
You weep with them
    Unalia pamoja nao (wanyonge)
   You sigh with them
                  Unahema nao (wanyonge)
You suffer with them Unataabika nao(wanyonge) But you lift high Lakini unainua juu The banner of their struggle
                  Bendera ya harakati yao
 With your sacred pen
Kwa peni yako takatifu!
Naam, hayo siyo maneno yangu. Hayo ni maneno ya Kajubi kuhusu msomi wa wanyonge. Wanyonge wakiteseka, na yeye anahisi kuteseka; wakihema na yeye anatweta; wakilia na yeye anabubujikwa machozi ya uchungu! Ndiyo, ni kupitia kalamu yake iliyotukuka , bendera ya harakati za wanyonge inainuliwa juu zaidi na kupepea kudhihirisha ushindi wa umma wa walalahoi.

Kwa hakika beti hizi za Kajubi zinawahusu waandishi sampuli ya Komredi Abdilatif Abdallah. Si unakumbuka huyu bwana alipowekwa gerezani na Mzee Jomo Kenyata kwa kuhoji Kenya inakokwenda? Je, alitokwa na machozi kwa kadhia na misukosuko ya kuswekwa korokoroni? Upweke wa gerezani ulimkatisha tamaa? La hasha, si unakumbuka alivyoendelea kuandika kazi zake za kiukombozi akiwa jela kwa kutumia karatasi za chooni (toilet paper)?

Sasa turudi kwenye kiini cha barua yangu. Ili kuelewa vyema usuli wake, inanipasa nirejee nyuma kidogo. Nikiwa sekondari, nilipata bahati ya kusoma na kusimuliwa habari kuhusu weledi wa baadhi ya wahadhiri wa UDSM. Na kwa kweli baada ya kuja chuoni, nimejionea wana-akademia  waliobobea kwenye fani mbalimbali.

Wakati ule wa sekondari nilivutiwa sana niliposimuliwa habari ya Profesa Haroub Othman na wewe. Kwa kweli nilipata mshawasha mkubwa wa kukutana nanyi na kupata darasa maridhawa kutoka kwenu.

Kwa bahati mbaya, mauti yalitupokonya kipenzi chetu Profesa Haroub Othman hata kabla sijamuona. Mauti hayakutaka nipate walau nafasi ya kumtunukia kwa kupigania bila kuchoka mustakabali wa haki za binadamu, hasa upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wanyonge wasio na uwezo huko Zanzibar. Hebu haya tumuachie Rabana kwa sababu imeshanenwa kwamba kazi yake haina makosa.
Hata wewe nilikuta umekwishastaafu shughuli ya uhadhiri. Sikubahatika kukaa darasani ambamo mbele yake kuna mhadhiri aliyeitwa Prof. Issa Gulamhusein Shivji!

Mwishowe niliamua kujifariji kwa kufuata nyayo zako kila mahali. Nilinunua vitabu vyako na kuhudhuria makongamano mengi uliyohutubu. Nisingekosa mhadhara wako kirahisi, labda niwe hoi bin taabani kitandani! Swahibu zangu wanajua jinsi nilivyomkereketwawa kazi zako.

Hivyo basi mimi ni mwanafunzi wako wa nje ya darasa. Kama unavyofahamu, ulimwengu wa wanafunzi umejaa maswali: maswali yenye kufikirisha na wakati mwingine maswali yasiyo na kichwa wala miguu! Wanafunzi wasipodadisi na kuuliza maswali basi hapo  hakuna uanafunzi (bila shaka kuna ububusa au labda wanafunzi wamekuelewa kwa asilimia mia!)

Si unakumbuka wanafunzi wa Yesu walivyomsonga Masihi kwa maswali na jinsi Masahaba walivyomuandama Mtume Muhamad (S.A.W) kwa maswali ya kufikirisha? Hata wewe mwenyewe umerudia mara chungu tele kwamba tofauti ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu na wale wa chini yake ni kwamba mwanachuo anapaswa kujipambanua kwa kufanya tafiti, uchambuzi na tafakuri ya kina kwenye masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Nami mwanafunzi wako nina maswali. Barua yangu imejaa maswali ambayo ningekuuliza darasani kama ningepata bahati ya kufundishwa nawe. Na kama asemavyo Okot P’ Bitek (Rejea shairi lake la ‘’From the Mouth of Which River?), maswali yanapokosa wa kuyajibu, yanaumiza kichwa na kuchoma ndani kwa ndani zaidi ya kichomi!
Sasa ngoja nianze maswali yangu.

Wakati fulani nilikuwa wilayani kwetu Tunduru, himaya ya Chifu Machemba. Si unakumbuka jinsi huyu Bwana alivyowakoromea Wajerumani walipomtaka kusalimisha himaya yake kwao wakati ule wa kinyang'anyiro cha mabeberu kuigombea Afrika? Nayakumbuka majibu yake kwa Gavana wa Kijerumani mwaka 1890, ''Nimeyasikiliza maneno yako lakini sioni sababu ya kukunyenyekea. Bora nife kwa sababu mimi ni sultani hapa kwenye nchi yangu nawe ni Sultani kwenye nchi yako..kama una nguvu njoo mwenyewe unikamate''.

Naam, hayo yalikuwa maneno ya Chifu Machemba ambaye wajerumani walipomvamia alipambana nao mpaka tone la mwisho na kuamua kutimkia Msumbiji pale maji yalipozidi unga!

Angekuwa mbinafsi, Chifu Machemba angeweza kuingiwa na uchu na kuiuza himaya yake kwa Wajerumani lakini akachagua maisha ya upweke ya uhamishoni. Mbona watawala wengi wa Afrika ya leo hawalikumbuki darasa hili maridhawa kutoka kwa Machemba? Kwa nini washirikiane na mababeru kutorosha vito , nyara za serikali na utajiri wetu kwenda ng’ambo?

Basi nikiwa na vijana wenzangu pale Tunduru , niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na msimamo kama ule wa Chifu Machemba. Kwamba kama wanauchukia ufukara basi wakati wa uchaguzi, wasikubali kurubuniwa.

Lilipokuja suala la msimamo, nikakikumbuka kile kisa cha wewe kuukataa mwaliko uliopewa na Prof.Keneth King wa Uskochi na Prof.Bonaventura De Souza wa Ureno waliokualika kutoa mada kwenye makongamano huko kwao katika kipindi kile ambacho Marekani na washirika wao waliivamia kimabavu Irak. Uliwaeleza kinagaubaga bila kumung’unya maneno kwamba unafanya hivyo ili kuonesha mwitiko wako hasi dhidi ya uvamizi wa Marekani na washirika wake nchini Irak.

Nakumbuka ulivyotueleza wazi wakati ule kwamba ile haikuwa vita dhidi ya silaha za maangamizi kama walivyodai mabingwa wa propaganda za kivita, bali ilikuwa vita ya kugombea mafuta na kujitanua kimabavu kwa mabeberu. Nakumbuka moto uliwaka hadi ndani ya Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es laam (UDASA). Nasikia kipindi kile mulifikia hadi hatua ya kumpiga marufuku barozi wa Marekani Bwana Robert Royall kukanyaga Chuoni!

Sasa turudi kwenye kiini cha barua yangu. Kama nilivyokueleza kwenye barua yangu ya kwanza niliyokutumia wikijana, waraka wangu ni mjumuiko wa maswali kuhusu taifa letu. Maswali haya yananisumbua sana na kunichoma ndani kwa ndani kwa kukosa majibu. Nimekuwa nikijiuliza maswali haya kila wakati: najiuliza asubuhi, mchana na usiku!
Jinamizi la maswali haya linanisonga kila sehemu. kafeteria nikipata staftahi, ladha ya chakula siipati. Darasani, barabarani, chumbani na kila sehemu nayawaza maswali haya bila kupata majibu. Sasa naomba nianze maswali yangu na ni matumaini yangu kwamba utanipatia majawabu ili kukata kiu yangu.

Swali langu la kwanza linahusu itikadi ya ujamaa na kujitegemea.  kwa miaka nenda rudi, Profesa unahubiri kuhusu Azimio la Arusha. Ingekuwa kwenye muktadha wa ulimwengu wa kiroho ningekuita nabii wa Azimio la Arusha! Ni adimu kwa wewe kuwa hatibu eneo fulani bila kulitaja Azimio la Arusha.

Kwenye Tamasha la pili la kigoda cha Mwalimu Nyerere mwaka 2010 ulikwenda mbali zaidi. Ulichapisha mamia ya nakala za Azimio la Arusha na kutugawia  vijana ili tuidurusu misingi yake.

Kwenye kuta za ukumbi wa Nkrumah pale Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam pakawekwa maneno yenye kutia mshawasha ya Azimio la Arusha; ‘’Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge (wetu) ili tusionewe na kunyonywa tena.’’

Swali langu kwako ni kutaka kufahamu kiini cha wewe kuendelea kulishabikia na kulishadidia Azimio katika zama hizi. Kwa nini unalitajataja Azimio kwenye zama hizi za utandawazi wa ‘’dunia kuwa kijiji’’? Umesahau kauli ya Mwalimu Nyerere mbele ya wanahabari  kwamba inahitaji roho ngumu mithili ya ile ya mwendewazimu kulizungumzia Azimio katika zama za leo? Na wewe umeamua kuivaa roho hiyo Profesa wangu?

Si bado unakumbuka maneno ya Mzee Ruksa wakati akiling’oa Azimio la Arusha na kusimika kile walichokubaliana kule Zanzibar kwamba ‘’Likulli Ajalin Kitabun, kila kitabu na zama zake’’?

Hata majuzi wakati tunamuaga nguli wa stadi za maendeleo Profesa Goran Hyden pale hoteli ya Serena, kuna vijana walizipinga fikra za usasa za uliberali mamboleo na kukumbushia misingi ya Azimio la Arusha; misingi ya utu na usawa. Nakumbuka Baroli Mwapachu aliwang’akia vijana wale kwamba wasiendelee na fikra za Ki-maksi zisizotekelezeka katika dunia ya leo na aliwaasa wahadhiri wa UDSM waachane na mtindo wa upandikizaji wa fikra hizo kwa wanafunzi: fikra alizoziita muflisi na zilizofeli!

Nini lengo lako kulishadidia Azimio la Arusha wakati wanazuoni wa kimamboleo  wanaweka wazi kwamba kwenye dunia ya leo ya utandawazi, kuacha milango wazi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji ni suala lisilo na mbadala? Na nadhani unazisikia tambo zao kwamba nchi yetu sasa inatajwa kuwemo kwenye orodha ya mataifa ya Afrika yaliyopiga hatua katika kuweka mazingira murua ya kuvutia wawekezaji kutoka nje!

Ukitoa mada kwenye kongamano lililoandaliwa na umoja wa Sauti ya Vijana Tanzania (SAVITA) mwaka 2011, ulitupatia changamoto ya kupambana kuirejesha misingi ya Azimio la Arusha na kuisimika kwenye katiba mpya. Hata Dk. Mkenda (Sasa mwenyekiti wa Bodi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii) alitoa rai ya kuirejesha misingi muhimu ya Azimio la Arusha wakati akitoa mada kwenye kongamano kuhusu fikra za Mwalimu Nyerere lililofanyika nchini Urusi mwaka 2010.

Pia nimesoma kwenye kitabu chako cha ‘’Insha za Mapambano ya Wanyonge’’ ukibashiri kuhusu kumea kwa dalili zinazoashiria kurejea kwa misingi mikuu ya Azimio la Arusha  na kwamba dalili za wazi za ‘’ufufuo’’ wa misingi ya  Azimio la Arusha zimeanza kuonekana. Nakumbuka ulisisitiza kwamba si Azimio lote litarudi bali misingi yake mikuu. Nami naomba nikueleze mapema kwamba kila nitapozungumzia kuhuishwa kwa Azimio kwenye waraka huu, namaanisha kuhuishwa kwa misingi yake mikuu na si Azimio lote.
Unamaanisha nini kuhusu kuhuishwa kwa Azimio? Kwamba viongozi wetu hawatomiliki tena hisa kwenye kampuni za kibwanyenye? wasipokee mishahara miwili au zaidi? wasiwe wajumbe wa bodi za mashirika na makampuni ya kibeberu? Unamaanisha tutarudisha tena vijiji vya ujamaa na kutaifisha makampuni? Unamaanisha nini unaposema Azimio linarudi?

Au unamaanisha tutarudi nyuma na kuikumbatia misingi ya kujitegemea iliyosisitiza  kuacha kutembeza bakuli la kuomba misaada kutoka kwa wahisani? Unadhani tutazinduka toka usingizini na kuyakumbuka mahubiri yaliyotuonya kwamba misaada ya wahisani inahatarisha uhuru wetu? Nijuze Profesa wangu! Unamaanisha nini kuhusu ufufuo wa Azimio?

Najua hata kama  Azimio litarudi, halitowakataza tena viongozi wetu wafanyabiashara kufanya biashara na kupangisha nyumba. Na sasa tunaambiwa wana majumba na ‘’miradi’’ mpaka Arabuni na Ulaya. Nina uhakika Azimio jipya litaporudi halitoweka sharti hilo litalowakosesha raha viongozi wetu watukufu! Si unakumbuka hata mzee Kingunge alikueleza kwamba kwa hili la kuwanyima viongozi wetu kufanya biashara ya kupangisha nyumba wakati ule wa Azimio, ilikuwa ni upotofu? (Rejea mazungumzo yako na Mzee Ngombale Mwilu kwenye jarida la Chemichem toleo la pili)

Halafu kama Azimio linarudi; ni nani analirudisha? Mmetufundisha kwamba ujamaa wa kiafrika, tofauti na ule wa kisayansi wa Karl Marx na Fredrick Engels, uliletwa na viongozi waliopigania uhuru na si vuguvugu la kimapinduzi la wafanyakazi na wakulima. Uliletwa na kina Nyerere, Nkurumah na Tom mboya.
Ni viongozi gani wataolirudisha Azimio hivi leo? Ni viongozi hawahawa wanaopokea posho mbili bungeni kwa kazi ileile? Ni viongozi hawahawa wanaopayuka majukwaani  na kulalama kulaani matumizi mabaya ya serikali wakati wao wenyewe wakiendesha magari ya kifahari ya serikali na kula mlungula bila soni?

Kwamba viongozi hawa hawa wanaodaiwa kuficha maburungutu ya ndarama chafu huko Uswizi na kwingineko wataridhia kupitisha sheria yenye hata harufu tu ya Azimio la Arusha ; Sheria ya kuwabana wasijilimbikizie ukwasi wakati masikini wa kijijini kwetu Namasakata na kwingineko Tanzania wakitaabika kwa ufukara?

Unakumbuka yaliyokukuta miaka ya tisini ulipoteuliwa kuwa mwenyekiti wa tume ya ardhi? Mimi nakumbuka kilichotekea. Ulizunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi na mwishowe ukaishauri serikali kwamba udhibiti wa ardhi ( Radical Title) urudishwe kwa umma badala ya rais kama ilivyo sasa. Ulizawadiwa nini kwa ushauri wako? Nini ulipata zaidi ya maneno ya wakubwa pale wizara ya ardhi kwamba ''Prof. Shivji was so much against the Excutive, and that he tailored the Report towards this end'', yaani kwamba wewe ulikuwa mpinzani wa serikali na hivyo basi ukaisuka ripoti ili kupata hitimisho la kuipinga serikali (kwa kushauri udhibiti wa ardhi uhamishwe kutoka mikononi mwa rais!)

Una imani watu hawa sasa wamepata ubatizo mpya; ubatizo utaowapa hamu ya kulirudisha Azimio la Ujamaa? Kwamba watazirudisha zile zama za ''Tanzania ni ya wafanyakazi na wakulima'' badala ya kuziendeleza zama za ''Tanzania ina wenyewe, na wenyewe ndio wao''?

Yu wapi Nyerere wetu; Moringe wetu;  na Kawawa wetu wa kulifufua Azimio la Arusha? Nionyeshe alipo Nkurumah wetu, Sengor wetu, Kaunda wetu na Tom Mboya wa kuujenga ujamaa? Anaishi wapi Abdulrahman Babu wetu wa sasa wa kuwakusanya makomredi wenzie na kuwahubiria ujenzi wa usoshalisti kule Zanzibar na Tanzania kwa ujumla?
Nieleze Profesa! Nijibu komredi uitibu kiu yangu!

Lakini kabla hatujaendelea  na waraka wetu, naomba uniruhusu nikusimulie mchapo mmoja. Si unajua tena vijana tumejaa michapo! Na kwa kweli ujana bila michapo basi unapoteza  maana yake!

Kwa muda mrefu, nimekuwa nikijishughulisha kudodosa kuhusu maisha yenu ya ujanani. Ni katika safari hiyo ya kudodosa, nikapata bahati ya kupitia simulizi za Profesa Karim Hirji (Sasa Profesa wa Biostatistics Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili). Kwa kweli nilihamasika sana. Mzee Hirji ametusimulia kinagaubaga kuhusu vuguvugu lenu la miaka ya 1970.
Kwamba mlishiriki kilimo na wakulima katika vijiji vya ujamaa na kuzunguka mashuleni kuwahamasisha vijana kuhusu ujamaa na kujitegemea ni habari ya kusisimua kwelikweli!

Nasikia mlijitolea kufundisha vituo vya elimu kwa watu wazima. Siku hizi, licha ya utitiri wa vyuo vikuu, shule za kata hazina walimu. Vijana hatuna tena moyo wa kujitolea kama wa enzi zenu. Rafiki yangu mmoja alinieleza kuwa hawezi kujitolea wakati serikali haionyeshi kujali mustakabali wa shule hizo. Pia anasema uzalendo wenu ulichagizwa na ukweli kwamba mukiwa vyuoni serikali iliwapa kila kitu.

Nasikia mlisoma bure; kula bure; kulala bure; usafiri bure; kila kitu bure! Kama hiyo ni kweli basi uzalendo wenu ulichipua kutokana na samadi ya huduma bora mulizopewa. Au hili halikusaidia chochote?

Kwamba mlikusanya michango kuchangia harakati za FRELIMO kule Msumbiji na chama cha MPLA cha Angola ni uzalendo wa kusifiwa kwelikweli. Sio kwamba vijana wa sasa hatuchangii, la hasha! Tunachanga sana. Siku hizi vijana tunachangia harusi, kitchen party  na kuwalipia wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi ikiwemo marais! Naambiwa ninyi mlithubutu kutembelea hadi maeneo ya kivita huko msumbiji yaliyodhibitiwa na FRELIMO ili kujionea matunda ya mapambano ya wazalendo wa Msumbiji!
Siku hizi vijana tumejibatiza uanaharakati huku mioyo yetu haina hata tone la harakati ya kuinufaisha jamii. Tunajivika kiremba cha uanaharakati kwa kuvaa mashati yenye picha za Che Guevara na mavazi ya kikomredi waliyovaa kina captain Mao Tse Tung! Harakati zetu ni za kuvaa  mavazi yenye picha za  Commandante Che Guevara na Malcom X huku wengi wetu mioyo yetu imejaa kila dalili za ubeberu na ndoto za kujilimbikizia ukwasi fursa itapowadia!

Hebu tuziache habari hizi kwa muda. Ni matumaini yangu tutapata fursa ya  kuyazungumzia mambo haya kwa kina. Kama unavyofahamu, kama vijana wa sasa hatutafanya jitihada kuudurusu ujana wa wazee wa leo, kuna hatari kubwa ya kutumbukia kwenye mtego wa kushindwa kuyafahamu mazuri yao na kurudia makosa yale yale waliyoyafanya wakiwa vijana.

Naomba tuendeleze mjadala tuliouweka kiporo wiki jana. Kama unavyokumbuka, wiki iliyopita tulizungumzia kile ambacho wewe ulikiona kama dalili za wazi za kufufuliwa kwa misingi mikuu ya Azimio la Arusha. Swali langu kubwa lilikuwa ni kutaka kufahamu jinsi Azimio la Arusha litavyohuishwa. Ujamaa na kujitegemea ulikuwa mfumo wa ujamaa wa kiafrika ambao tofauti na ujamaa wa kisayansi wa Karl Marx uliojengwa kwa vuguvugu la wafanyakazi na wakulima, wenyewe uliletwa na viongozi wa kizazi cha uhuru. Nilikuuliza wiki jana kama tunao viongozi wa kisiasa hapa nchini ambao unawatumaini kulirejesha Azimio. Bado  ninasubiri jibu langu kwa shauku.

Au sijakuelewa Profesa? Pengine unamaanisha watu wenyewe watarirudisha Azimio. Kwamba umma wenyewe wa wanyonge utapigania kuirejesha misingi ya usawa? Nimesoma pahala ukirejea vuguvugu la wavujajasho kwenye maeneo ya Hanang, Loriondo, Rufiji na kwingineko Tanzania  kupinga upokwaji wa rasilimali zao bila wao kushirikishwa ipasavyo (Na sasa Mtwara hali ilikuwa tete kuhusu uvunaji na usafirishaji wa gesi asilia) unadhani hizi ni dalili za awali za ufufuo wa Azimio?

Lakini Profesa, si umetufundisha mwenyewe kwamba vuguvugu la wafanyakazi baada ya uhuru lilianza kuchipua Tanzania tangu miaka ya sabini? Nimesoma kazi zako kadhaa kuhusu kumea kwa tabaka la kibwanyenye na kuchomoza kwa vuguvugu la wafanyakazi. Jitihada zilifanyika wakati ule kuzima vuguvugu la wafanyakazi. Una hakika haya hayawezi kujirudia sasa? Ninafahamu kwamba bado unayakumbuka mabavu yaliyotumika kuwadhibiti wamasai wa Loriondo ili kupisha ‘’mwekezaji’’? Mh.Shamsa Mwangunga alisema waliofurushwa ni wakenya! Kwa Kweli nilipomsikia nilibaki mdomo wazi!
Lakini hata kama umma utakuwa na mwamko mkubwa na hamasa, tunaweza kulirejesha Azimio kama wale wanaouhamasisha umma hawana imani na Azimio?

Sikuulizi kama vuguvugu linalochipua kwa kasi kwenye kambi ya upinzani nchini ndilo unalolitumaini kurudisha misingi ya Azimio. Nimepitia maandiko ya vyama kadhaa kwenye maeneo ya itikadi, falsafa na sera. Makamanda wa ‘’peoples power’’ wameshaweka wazi kwamba wakipewa ridhaa ya kushika dola wanakusudia kujenga mfumo wa uchumi na siasa za mrengo wa kati. Hata ‘’wanangangari’’ wametueleza kwamba wanaamini katika uliberali.

Majuzi nimebahatika kupitia tamko la Mtandao wa Vikundi  vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) walilolitoa pale Morogoro wakati wa kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wetu.

Naomba nikukumbushe waliyoyasema wakulima wale: kwanza waliweka wazi sikitiko lao kuhusu kusalitiwa kwa misingi ya Azimio la Arusha na hivyo basi kukuza pengo baina ya walalahoi na walalaheri.

Pia waliweka wazi kwamba wanapinga kwa nguvu zote ukandamizaji na unyonyaji wanaofanyiwa wakulima wa Tanzania na wakoloni mamboleo kwa kushirikiana na makuwadi wa ubeberu. Nilihamasika sana niliposoma kwamba wameamua kuchukua hatua ya kukuza umoja wa wakulima wanaonyonywa na kukandamizwa.

Lakini, niligutuka kidogo niliposoma suluhisho walilolitoa kukabiliana na madhila yanayowakumba. Unajua suluhisho walilolisema katika kunusuru mustakabali wao? Kwamba watawanyima kura wanasiasa uchwara wote na pia watapiga kelele dhidi ya dhuluma kwa wakulima. Hapa nilishangaa kidogo! Ninachojiuliza ni kama wakulima hawa wanalenga kulirudisha Azimio la Arusha au wanachotaka ni maslahi bora katika mfumo uleule uliopo? Kama wanataka Azimio, watalirudishaje? Katika vyama vyetu vya siasa, ni nani watayempa kura ambaye ana ndoto na nia thabiti ya kulirudisha Azimio la Arusha?
Nitanzulie Profesa! Nitoe kizani Komredi!

Source: Raia Mwema

2 comments:

  1. Bravo !lakini kiswahili mheshimiwa kinakupa tabu L na R , mfano Loliondo Sio liriondo nk

    ReplyDelete
  2. Fikra pevu ulizoonesha ni msingi wa ukombozi wa vijana kama tukitambua nafasi yetu katika kulitengeneza taifa letu la Tanzania.

    ReplyDelete