WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, February 3, 2014

Yanga, Azam zaua

Mrisho Ngasa aliyeshika kichwa akishangilia pamoja na wachezaji wenzake wa Yanga baada ya kufunga bao wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Goli  pekee kutoka kwa mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngasa lilitosha kuwashushia wageni wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Mbeya City waliobaki 10 uwanjani kipigo chao cha kwanza msimu huu, lakini walikuwa ni Azam FC waliobaki kileleni mwa msimamo baada ya kuisambaratisha Kagera Sugar kwa mabao 4-0.
Matokeo hayo yaliiacha Azam kileleni ikiwa na pointi 36, moja juu ya Yanga huku Mbeya City wakibaki katika nafasi ya tatu kwa kuwa na  pointi 31 baada ya mechi 16.

Simba yenye pointi 30 kufuatia kutoa kipigo kikali cha 4-0 dhidi ya JKT Oljoro juzi, imebaki katika nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 15. Itakuwa na fursa ya kuipita Mbeya City katika nafasi ya tatu kama itashinda mechi yao ya mkononi dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini Jamhuri Morogoro keshokutwa.

Ngasa aliifungia Yanga goli la kuongoza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa shuti kali la kutokea nje ya 18 ambalo kipa wa Mbeya City, David Burhani, aliruka kuufuata mpira bila ya mafanikio katika dakika ya 15.

Licha ya timu hizo kushambuliana kwa mpira wa kasi, goli hilo lilibaki hadi wakati wa mapumziko.

Matumaini ya kusawazisha goli hilo ya Mbeya City ambayo imekuwa gumzo nchini katika msimu wake wa kwanza kwenye ligi, yalipata pigo baada ya refa Abdalla Kambuzi kutoka Shinyanga kumtoa Steven Mazanda kwa kadi ya pili ya njano baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Yanga katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
Mbeya City kubaki 10 uwanjani kuliwapa nguvu Yanga ambao walilishambulia goli la wageni mfululizo lakini matokeo hayakubadilika.
Yanga walionekana kudhamiria kushinda mechi hiyo tangu mapema kwani dakika ya kwanza tu Msuva alikaribia kufunga goli la kuongoza lakini shuti lake lilipaa juu ya lango na dakika nne baadaye kipa Burhani alidaka shuti la Frank Domayo.

Wageni walijibu mapigo kwa kuraribia kufunga katika dakika ya 6 wakati Mwagane Yeya aliposhindwa kuunganisha krosi ya Deus Kaseke.

Burhani pia alidaka kiufundi shuti la Msuva katika dakika za 71 kabla ya mtokeabenchi Hamis Kiiza kushindwa kufunga katika dakika ya 74 baada ya shuti lake kwenda nje wakati kipa huyo wa Mbeya City akiwa ametoka langoni.

Hadi mechi unamalizika hapakuwa na mabadiliko katika matokeo.

Hata hivyo, kulitokea vurugu wakati askari walipompiga mchezaji wa Yanga,Shaaban Kondo aliyekuwa hajavaa sare pale alipokuwa akitaka kuingia katika vyumba vya kuvalia wachezaji wenzake. Polisi walionekana kutomtambua kama ni mchezaji wa Yanga na akaondoka akiwa amebebwa kwenye gari la polisi.

Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Mganda Brian Umony alifunga mara mbili na Himid Mao na Kelvin Friday wakaongeza moja kila mmoja na kuibakisha timu yao kileleni.

Umony alifunga goli la kuongoza katika dakika ya 13 akitumia pasi ya kupenyezewa ndani ya boksi kutoka kwa Kipre Tchetche na Mganda huyo akaongeza la pili katika dakika ya 48 kufuatia krosi ya Himid Mao.

Mtokeabenchi Friday kisha akafunga la tatu kufuatia pasi ya pasi ya Kipre katika dakika ya 51 na kufanya magoli mawili ya ndani ya dakika sita kuwachanganya kabisa Kagera Sugar.

Kipa wa Azam, Mwadini Ali, alihusika katika goli la nne pale mpira wake mrefu aliopiga hadi katikati ya uwanja kumkuta Friday ambaye naye alipiga shuti la juu kuelekea langoni mwa Kagera Sugar na katika kujaribu kuokoa shambulizi, kipa Agaton Antony wa Kagera akiwa nje ya boksi akaupiga kichwa mpira uliotua miguuni mwa mtokeabenchi Jabir Aziz aliyefunga katika lango tupu dakika saba kabla ya mechi kumalizika.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment