WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, February 25, 2014

Anayeona posho haimtoshi afungashe virago’

bunge_4f64b.jpg
Dodoma. Wizara ya Fedha imepigilia msumari maombi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kutaka waongezewe posho na kusema anayeona ameacha kazi inayomlipa zaidi kwenda bungeni afungashe virago na kuondoka.
Msimamo huo umekuja siku moja tu baada ya gazeti hili kudokeza kuwa madai ya wajumbe wa bunge hilo kutaka waongezewe posho kutoka Sh300,000 za sasa kwa siku, yamegonga mwamba baada ya kamati iliyoteuliwa kuchunguza uhalali wake kusema kiwango hicho kinatosha.
Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Kificho alisema jana bila kutaja viwango, kuwa ripoti ya kamati hiyo imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi.
Madai ya wajumbe kutaka waongezewe posho, yamechafua hali ya hewa ndani na nje ya Bunge, huku baadhi ya wananchi wakipaza sauti zao na kumsihi Rais Kikwete alivunje bunge hilo iwapo wajumbe watashikilia msimamo wa kutaka nyongeza ya posho.
Jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema wanaoshiriki kutunga Katiba ni Watanzania na siyo wataalamu washauri waliokodiwa kutoka nje.
Alisema kwa msingi huo, Serikali ilitarajia kuwaona watu hao wakitanguliza uzalendo zaidi badala ya kudai malipo manono.
"Katika kutengeneza Katiba hii, hatujakodi consultants (wataalamu washauri) kutoka Uingereza, Marekani, Kenya, Uganda wala nchi nyingine yoyote... Hawa ni Watanzania na kazi wanayoifanya ni yao," alisema.
"Wangekuwa wataalamu wa kukodi wangeweza kudai malipo hayo, lakini hapa ni tofauti... wanafanya kazi yao na kila mtu anafanya kazi yake na anapaswa kujivunia kushiriki katika tendo hili la kihistoria kwa kutanguliza uzalendo," alisema.
Nchemba alisema anazielewa hoja za baadhi ya wajumbe walioibua suala la posho, lakini kwa mtazamo wake, hoja hiyo hata kama ingekuwa na mashiko kiasi gani, imewasilishwa wakati usiokuwa mwafaka. Alisema wapo makandarasi na wazabuni waliotoa huduma kwenye taasisi mbalimbali za umma lakini hawajalipwa.
Alisema kwa kawaida, Februari ni mwezi mbaya kwa kuwa baadhi ya wilaya zina historia ya kukumbwa na uhaba wa chakula hivyo kuhitaji fedha nyingi za Serikali ili kuokoa maisha ya watu katika maeneo hayo.
Pia alisema si wakati mwafaka wa kudai nyongeza hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna walimu wapya 30,000 nchini kote ambao hawajapangiwa vituo kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa stahiki zao.
Nchemba alisema mbali na walimu hao wapya kutokupangiwa vituo, walimu wengine wanadai malimbikizo ya fedha zao na kwamba hawajalipwa kutokana na ufinyu wa bajeti serikalini.
"Siku zote ukweli unauma. Nasema kama kuna mjumbe ambaye anaona huko alikokuwa kabla ya kuteuliwa alikuwa anapata pesa zaidi kuliko hii, basi kwa heshima afungashe virago na kuondoka," alisema.
Aibu kwa mjumbe
Akizungumzia suala hilo la posho, Mjumbe wa Bunge hilo, David Kafulila (picha ndogo chini) alisema ni aibu kwa wajumbe ambao wameaminiwa na Watanzania na kupewa jukumu zito la kutunga Katiba, kuanza kujadili nyongeza ya posho.
"Ninachokiona ni tatizo la standard (viwango) vya posho... hakuna standard kwamba posho ilipweje, kwa nani na kwa kiasi gani. Mtu akidai leo kwamba Sh300,000 ni ndogo tunajiuliza ni kwa standard ipi?" alihoji.
Kamati ya Posho
Kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kushughulikia madai ya nyongeza hizo, zinasema imeshauri kuwa kiwango kinacholipwa sasa kinatosha.
Kamati hiyo inaundwa na William Lukuvi, Mohamed Abood Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari na taarifa yake imekwishakabidhiwa kwa Kificho.
Mmoja wa makatibu wa bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alikaririwa juzi akisema suala la posho limetoka mikononi mwa Kificho na mapendekezo yake yameshapelekwa serikalini.
Hoja ya kutaka nyongeza ya posho iliibuliwa na wajumbe wawili ambao pia ni wabunge wa CCM, Richard Ndasa (Sumve) na Suleiman Nchambi (Kishapu).

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment