WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 28, 2014

Neno Fupi La Leo: Bunge La Katiba Na Kisa Cha Risasi Ya Mwisho...!

Ndugu zangu,
Jana katika nyakati tofauti nimefuatilia mjadala wa rasimu ya kanuni za Bunge hilo.
Kuna wakati nimejiuliza; hivi wote mle ndani wanajua maana ya dhamana kubwa waliyobeba kwa ajili ya nchi hii, leo na kesho?
Kwamba hawapaswi kuonyesha aibu ile ya kujikita kwenye kujadili mustakabali wa taifa kwa kuvaa miwani ya makundi na vyama vyao vya siasa. Kuingia kwenye ushabiki kama wa Simba na Yanga. Maana, inahusua masuala ya msingi yaliyo mbele ya uhai wa vyama vya siasa.
Katiba ni dira ya nchi. Ni ramani ya kutuongoza Watanzania wa leo na wajao, bila kujali makundi na vyama vya siasa.
Kwa WaTanzania, madai ya kupata Katiba mpya ni madai halali yanayotokana pia na kukosekana kwa Haki, Uwazi na Uwajibikaji, hususan kutoka kwa baadhi ya wenye kupewa dhamana za uongozi.
Watanzania ni kama kisa cha wanakijiji waliokuwa kwenye shida ya njaa ya miaka hamsini. Na katika kuhangaika kwao,na kwa risasi yao ya mwisho waliyobaki nayo kwenye gobore moja na la pekee kijiji kizima, wamekaa kikao na kujadili wafanyeje ili wampate mwenzao atakayekwenda mbugani kuwinda mnyama ili aokoe njaa yao.
Na Jemedari wao, baada ya kutafakari, amewateulia mwenzao anayedhaniwa kuwa makini na mahiri kwa uwindaji. Mwenye uwezo wa kulenga shabaha, na hivyo, kuitumia vema risasi hiyo moja iliyobaki kwenye kumlenga nyati na kumwangusha. Kwamba abebe gobore lenye risasi moja, na aingie nalo msituni kuifanya kazi hiyo.
Aliyekwenda mbugani nyuma amewaacha wengi wenye matumaini ya kuusikia mlio wa gobore utakaoshiria mnyama mkubwa ameangushwa mbugani.
Na hakuna habari mbaya, kama wanakijiji wale watakapousikia mlio huo na kukimbilia mbugani kujionea. Na huko wamkute mwenzao ameitumia risasi ile ya mwisho kwa kumlenga na kumwangusha nyani badala ya nyati waliyemtarajia!
Na kwa mila za wanakijiji wale, nyani haliwi,na ni mwiko.
Na Bunge la Katiba lijione kuwa lina fursa adhimu ya kutimiza ndoto ya Watanzania ya kupata Katiba Bora yenye kukidhi mahitaji ya sasa na hata miaka mia moja ijayo.
Kwa Wabunge wa Bunge la Katiba kwenda Dodoma na kurudi na nyani badala ya nyati, sio tu kutawakatisha tamaa Watanzania, bali, kutawafanya Watanzania wawadharau Wabunge hao na hata kuhoji uzalendo wao kwa nchi yao waliyozaliwa.
Ni Neno Fupi La Leo.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)

No comments:

Post a Comment