WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 7, 2014

Neno La Leo: Profesa Amechelewa.. !


Ndugu zangu,
Profesa Mwesiga Baregu amenukuliwa na gazeti Mwananchi akisema;
 
"Bila kuweka utashi wa kujenga taifa moja, Bunge lijalo linaweza kutawaliwa na vituko. Iwapo wajumbe watakwenda kwenye Bunge la Katiba huku wakiwa na ushabiki wa vyama vyao mimi naona kutakuwa na vituko vikubwa.Tunapaswa kutambua kwamba tunakwenda kutengeneza Katiba ya Taifa na siyo kwa kuegemea masilahi ya kundi fulani" - Profesa Baregu ( Mwananchi, Februari 7, 2014)

Na kabla sijaichambua kauli ya Profesa, ngoja hapa nimkumbushe Profesa juu ya mwanafalsafa wa Kiyunani, Ptolemy, huyu alipata kuandika: "Ex Africa simper aliquid novi". Maana yake: "Kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika."

Mimi nadhani Profesa amechelewa katika kauli yake hii, maana, anachofikiri Profesa kuwa kitatokea, tayari ishara zilishaonekana, na sasa tumeanza kukiona. Na Rais Kikwete kule Mbeya majuzi ndiye aliyeweka bayana kabisa, kuwa tatizo naye ameliona, kuwa kwenye Bunge la Katiba yumkini malumbano hayatakuwa ya hoja bali hata kupimana ubavu na kwa sura za rangi za vyama.

Profesa wangu Baregu, hivyo vitakavyotokea si vituko tu, ni vioja kama anavyosema Mwanafalsafa Ptolemy. Na tujiandae na burudani za aibu kwa taifa.

Maana, nilishapata kuandika, kuwa safari nyingi za Mwafrika ni za bure tu. Tusipotanguliza busara na hekima, tutambue, kuwa kazi yote hii ya akina Jaji Warioba na wenzake nayo itakuwa ni ya bure tu. Tutakuwa tumechoma mabilioni ya fedha kwa jambo litakalohitimishwa na kutugawa zaidi kuliko kutujenga kama taifa. Maana, sisi ni wabinafsi kuliko. Hatutangulizi maslahi ya nchi bali yetu binafsi, ya makundi yetu na vyama vyetu.

Na zaidi ya miaka 15 iliyopita niliandika, kuwa Tanzania ina vyote kasoro Watanzania. Tusipowafanya wajumbe wengi ndani ya Bunge la Katiba wafikiri kama Watanzania, basi, tutaishia kuipata Katiba ya Vyama Vya Siasa na si ya Watanzania.

Maana, wanachotaka Watanzania walio wengi tayari kinafahamika kupitia rasimu ya pili ya Mabadiliko ya Katiba. Lakini, hofu iliyopo ni kutokea kwa baadhi ya Watanzania wenzetu, kupitia Bunge la Katiba, kuyateka matakwa ya umma na kupandikiza matakwa ya vyama na makundi.

Maana, kupitia Tume ya Warioba Wananchi walishausonga ugali wao na ukaiva. Lakini, kuna waliojipanga kwa kuanika kimea cha mtama, tayari kuwakorogea Wananchi togwa ili wanywe, walewe na kuendelea kulala usingizi. Wakiamka watayakuta yale yale. Na yawe ni mapambano, ya uwepo wa Katiba ya Kusongwa na Wananchi, kama ugali, na kuipinga kwa hoja, Katiba ya kukorogwa na wanasiasa, kama togwa.

Itakumbukwa, mwanzoni kabisa mwa mchakato wa Katiba, Profesa Kabudi alipata kusema, " What we are doing is Constutional building and not Constutional making". Kwamba tunachokifanya ni Ujenzi wa Katiba na si Kutengeneza Katiba.
Na katika alichokisema Profesa Kabudi swali lilikuja,je; 

" Ni kina nani wanaostahili kushirikishwa kwenye maandalizi ya ujenzi huo? Swali lingine, ni maoni yepi yanayotakiwa kupewa kipaumbele, ya wananchi au wanasiasa?
Nahofia, kuwa hatufikiri kuhusu nchi yetu tuliyozaliwa na hatma yake. Tunajifikiria sisi , makundi na vyama vyetu. Vyote vya kupita, wakati nchi itabaki.

Maana, kutengeneza Katiba ya nchi ni sawa na kulima shamba la pamoja. Na kwanini basi wenye kulima shamba moja wagombanie majembe? Hakika, huo utakuwa ni uwendawazimu, ni kwa vile, watakachopanda na kuvuna ni cha faida yao wote.

Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
0754 678 252
Iringa.

No comments:

Post a Comment