WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 12, 2014

Sheria ichukue mkondo wake dhidi ya Sitti

Katuni

Hatimaye mwishoni mwa wiki, mrembo wa Taifa mwaka huu 'Redd's Miss Tanzania 2014', Sitti Mtemvu, alilivua rasmi taji hilo kwa kile alichodai kuchoshwa na kuandamwa na vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na watu mbalimbali.

Sitti ambaye waratibu wa urembo walianza kumfuatilia kumshawishi kushiriki shindano hilo tangu mwaka juzi, alifanikiwa kuibuka mshindi wa taji hilo katika kinyang'anyiro kilichofanyika usiku wa Jumamosi ya Oktoba 11, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, baada ya kushinda taji hilo siku moja baadaye, taarifa za awali zilionekana kwenye mitandao ya kijamii zikianika hati yake ya kusafiria ikionesha ilitolewa Februari 15, 2007 na muda wake wa kutumika mwisho ukiwa ni Februari 14, 2017.

Katika hati hiyo yenye namba AB 202696 ilitolewa jijini Dar es Salaam ikiwa na jina la ukoo la Mtemvu huku mawili ya awali yakiwa Sitti Abbas, ilionesha mshindi huyo pia wa kitongoji cha Chang'ombe na Redd's Miss Temeke amezaliwa Mei 31, 1989 hivyo umri wake ni miaka 25.

Pia NIPASHE liliona taarifa za mrembo huyo za Taasisi ya Explore Talent ikionesha kuwa ana miaka 25, anaishi Dallas, Tx, urefu wake ni 5'8, umbo lake ni la kati, asili yake ni Mwafrika na rangi ya macho yake ni kahawia.

Katika harakati za kuzidi kutafuta ukweli wa umri sahihi wa mrembo huyo, habari zaidi zilida kuwa Sitti alizaliwa katika hospitali binafsi (jina tunalo) ambayo iko wilayani Ilala jijini na si Temeke kama ilivyoelezwa kwenye cheti kipya kilichotolewa Septemba 9, mwaka huu ambacho kinataja tarehe yake ya kuzaliwa ni Mei 31, 1991.

Tayari Mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga, amemtangaza aliyekuwa mshindi wa pili katika kinyang'anyiro hicho, Lilian Kamazima kuwa mrithi wa taji hilo kwa mujibu wa kanuni za shindano hilo.

Habari zisizo rasmi zinaeleza kuwa uamuzi wa Sitti kulivua taji hilo ulitokana na uamuzi uliofikiwa katika kikao kizito kilichofanyika wiki iliyopita kati ya Kamati ya Miss Tanzania, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Vijana, Habari Utamaduni na Michezo.

Inaelezwa kwamba Kamati ya Miss Tanzania ilitakiwa kutangaza kumvua taji hilo Sitti kutokana na kubainika kwamba alidanganya umri, lakini kwa kile kilichodaiwa ni kuficha aibu na kujaribu kukwepa mkono wa sheria ikamtaka yeye binafsi kutangaza kulivua.

Kwanza kabisa tunaipongeza Wizara ya Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa juhudi kubwa walizozifanya kulifuatilia kwa kina sakata hilo hadi kufikia hatua ya mrembo huyo kuona anastahili kulivua taji hilo kutokana madai ya kughushi vyeti vya kuzaliwa.

Lakini bado wadau wa michezo na Watanzania kwa ujumla wanasubiri kupata jibu sahihi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu umri sahihi wa Sitti na si kuishia tu kulivua taji hilo. 

Tunaamini kama kweli Sitti hakudanganya umri angesimama kidete katika kuvitetea vyeti vilivyompa sifa ya kushiriki kinyang'anyiro hicho na asingediriki kulivua taji hilo kirahisi wakati akitambua kwamba hiyo ni kashfa kwake.

Kitendo alichodaiwa kukifanya Sitti kimeichafua Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita) na taifa kwa ujumla, kwani ni dhahiri hata vyeti vya kuzaliwa hapa nchini kwa sasa vitaonekana si kigezo sahihi cha kuthibitisha umri wa Mtanzania.

NIPASHE tunataka kuona Wizara ya Mambo ya Ndani 'ikifunguka' katika hili, na kuuweka hadharani umri sahihi wa Sitti huku hatua kali zikichukuliwa dhidi yake kama kweli alighushi vyeti hivyo kwa kuwa hili si jambo la kufumbia macho hata kidogo katika ustawi wa taifa letu.

Tunatambua Sitti kulivua taji hilo ni hatua ya kwanza kwa mujibu wa kanuni za shindano hilo, na ya pili ni wizara husika kumchukulia hatua za kisheria kama kweli kughushi vyeti ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia chafu kama hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment