Viongozi wa kikristo wakiongoza maombi mbele ya kanisa la KKKT Mbagala siku moja baada ya kushambuliwa na kuharibiwa.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Viongozi wa dini waiunga mkono Serikali kuhusu udini VIONGOZI wa dini zote katika Mkoa wa Kilimanjaro wameungana kuunga mkono jitihada za Serikali kupambana na wanaharakati wa kidini ambao wanatumia dini kucheza siasa kwa nia ya kuvuruga amani ya utulivu ambao umedumu nchini kwa miaka mingi. Miongoni mwa mambo mengine, viongozi hao wameitaka Serikali kuangalia upya sera ya usajili wa taasisi za kidini nchini kwa nia ya kupunguza na hata kumaliza joto la uvunjivu wa amani kwa kutumia mgongo wa dini. Aidha, viongozi hao wameishauri Serikali kuchukua hatua kali za kupambana na vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu kupitia kisingizio cha dini ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaotumia mwanya wa dini kuingiza siasa katika dini na hivyo kuvunja amani. Msimamo huo wa viongozi wa dini umeelezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa jana, Jumanne, Oktoba 30, 2012, wakati alipokutana na viongozi hao ambao wamewasilisha matamko yao kwake katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Mkoa wa Kilimanjaro mjini Moshi. Matamko hayo yanahusu vurugu za karibuni katika Jiji la Dar es Salaam ambazo zilihusisha uvunjifu wa amani. Viongozi hao wakiongozwa na viongozi wao – Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro Sheikh Ramadhan Salim, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro Sheikh Shaaban Rashid na maaskofu Glorius Shoo, Martin Shao na Isaac Amani wakiwasilisha madhehebu ya Kikristo ya Wakatoliki, KKKT, Pentecoste na TAG na imani mbali mbali za dini ya Kiislamu walifika Ikulu Ndogo kuwasilisha salamu kwa Rais Kikwete. Ujumbe wa viongozi hao ulifanana kabisa. Wote walilaani kudhalilishwa kwa Kitabu Kitakatifu cha Quran kwa kukojolewa na kijana mmoja, kitendo ambacho kilisababisha kuvamiwa na kuchomwa kwa makanisa ya Kikristo na kuibiwa kwa mali kutoka kwenye makanisa hayo. Baba Askofu Martin Shao amemwambia Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais tumekuja kukusalimia na kutoa tamko letu la kuunga mkono jitihada za Serikali yako katika kukabiliana na uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha dini kama ilivyodhihirika katika siku chache zilizopita.” Naye Sheikh Shaaban Rashid amemwambia Rais Kikwete: “Hatukubaliani na mambo mawili, moja ni kunajisiwa kwa Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu cha Quran na pili ni kuvunjwa na kuharibiwa kwa Nyumba za Ibada kama ilivyoonyeshwa katika matukio ya Mbagala kule Dar es Salaam. Tunaunga msimamo wa Serikali yako katika kukabiliana na mambo haya.” Naye Mwenyekiti wa Bakwata katika Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Ramadhan Salim amemwambia Rais Kikwete: “Tumefadhaishwa na kitendo cha kunajisiwa Kitabu cha Mungu – imepata kutokea pale Dodoma, imepata kutokea Boma Ng’ombe Mkoa wa Kilimanjaro na sasa Mbagala, Dar es Salaam. Tunalaani pia vitendo vya kuvunja, kuharibu na kuchoma moto nyumba za ibada.” Ameongeza: “Tunaomba Serikali kuchukua hatua tatu. Moja ni kuhakikisha kuwa hukumu ya uadilifu inafikiwa katika kesi zinazowakabili waliohusika na vitendo hivi. Pili Serikali iangalie upya sera za uandikishaji wa taasisi za kidini na tatu Serikali itoe msimamo kamili na sahihi kuhusu jambo hili badala ya taarifa za matukio haya kutolewa na vyombo vya habari.” Naye Askofu Martin Fataely Shao amesema: “Tunasikitishwa na vitendo na matukio ya uvunjifu wa amani, utulivu na mshikamano. Tunasikitishwa na kuibuka kwa vikundi vinavyodhalilisha dini na imani ya watu wengine kwa kutumia vyombo vya habari na hasa redio. Hatukubaliani na vitendo vya kukashifu dini na imani za watu wengine.” Akizungumza katika shughuli hiyo kwenye siku ya tatu ya ziara yake ya siku nne katika Mkoa wa Kilimanjaro, Rais amewashukuru sana viongozi hao wa dini. “Leo nitalala usingizi mzuri kwa kuwa mmetoa maneno ya kuponya nchi yetu. Nawapongezeni kwa uamuzi wa kukutana na kufikia uamuzi huu.” Rais Kikwete amesema kuwa kwa muda sasa amekuwa anaona dalili za Tanzania kupelekwa pabaya siyo kwa tatizo la ukabila bali kwa tatizo la udini kwa sababu ni dhahiri kuna watu hawafurahishwi na utulivu wa Tanzania na wangependa kuiona Tanzania ikikumbwa na matatizo ya ukosefu wa amani na utulivu kama baadhi ya nchi majirani. Amesema kuwa ni dhahiri wako wanarahakati wa dini zote kubwa mbili ambao wanatumia dini kujipenyeza katika ajenda za kisiasa na hivyo kuvuruga amani na utulivu. “kazi ya wanaharakati hawa ni kukashifu dini za wenzao. Uzuri sheria za nchi hii zinatosha kukabiliana na hali hii. Tunatoa uhuru wa watu kuabudu lakini hatutoi uhuru wa watu kudhalilisha dini za watu wengine.” Rais Kikwete amewahakikishia viongozi hao wa dini kuwa Serikali yake haitalala katika kuhakikisha kuwa Tanzania haiingii katika uvunjifu wa amani na utulivu kwa kisingizio cha dini.“Nataka kuwahakikishia kuwa Serikali yenu iko macho. Kamwe, hatutaruhusu uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha dini. Nyie mmeonyesha mfano. Na sisi hatuwezi kuiachia nchi kutumbukia katika matatizo.”
source Mjengwa blog
No comments:
Post a Comment