UVUMILIVU HUJENGWA NA MISINGI
GANI?
Taifa letu katika siku
hizi za karibuni limeendelea kugubikwa na wimbi la matendo ambayo yanaashiria
uvunjaji wa amani ambayo Viongozi wetu waanzilishi wa Taifa hili wazee wetu hayati Abeid
Aman Karume na Mwalimu Julius Nyerere, walifanya kazi kubwa kuasisi Amani
na Umoja wa kitaifa ambao umekuwa ni kioo cha Taifa letu katika macho ya
kimataifa.
Tumeendelea kuona matukio
ya kutisha yakiendelea kutokea sehemu mbalimbali kama vile Zanzibar, Dar es
salaam, Arusha na kwingineko wakati kundi moja likijiona kuwa lina haki zaidi
kuliko kundi nyingine na kusababisha hata wananchi kadhaa kupoteza maisha na
mali zao.
Naanza kwa kujiuliza kuwa
je fujo za aina hii zinapotokea ambazo zinasababisha uvunjaji wa makusudi wa
amani pengine dhidi ya jamii au kundi nyingine, na kundi ambalo linatendewa
vibaya kwa kudhalilishwa au hata kuharibiwa mali zao na halichukui hatua ya kulipa
kisasi mara moja na kusababisha maafa makubwa kwa amani ya Taifa swali hapa ni je kundi hilo
linakuwa katika hali ya subira au uvumulivu? Je kama wako kwenye subira, subira
yao itaisha lini na nini kitatokea?
Je na viongozi wetu nao wanakuwa na subira
au uvumilivu? Wa
kuto chukua hatua inayostahili ili kukomesha fujo ana matendo hayo ya uvunjaji
wa amani?
Kwa haraka haraka
tu Uvumilivu ni uwezo wa, au ni mazoezi ya, kutambua na kuheshimu imani au
matendo ya wengine; uvumilivu uko katika kila nyanya ya maisha yetu, kuanzia
maisha yetu ya kila siku;
TATIZO katika
maisha ya kawaida sana, swala la uvumilivu halizungumzwi sana, tunachokiona
sana ni mazungumzo ya kulipa kisasi;
Nafikiri itakuwa jambo
njema kama tutaendelea kufundisha na kuhubiri uvumilivu katika nyanya zote. Pengine
fujo hizi ambazo taifa linaendelea kujionea zikizidi kujitokeza zingeweza
kukoma au kupungua.
Uvumilivu huongelewa sana
kwa mapana hasa katika maswala ya uongozi, uongozi ni hali ya kuongoza nchi
katika mwelekeo wa kuleta maendeleo na ni ukweli kama mwandishi mmoja alipowahi
sema kuwa “KUONGOZA watu na hasa wa watu wazima ni kazi nzito inayohitaji
mtu anayepewa jukumu hilo kuwa makini, vinginevyo mambo yanaweza kuwa magumu na
hatimaye kuangukia katika mtego wa udikteta.
Hii inatokana na
kukosekana mambo makubwa matatu ambayo ni ufahamu au maarifa, hekima na
hasa uvumilivu. Kiongozi asiye mvumilivu anaweza kujikuta anatumia mabavu
kutawala ili watu wajue kuwa yupo, ana nguvu na ana mamlaka”.
Na hii falfasa ambayo huangukia kwa wananchi vile vile pale ambapo wanakuwa
hawana uvumilivu;
Ni ukweli ulio wazi
kuwa kiongozi anatakiwa kuwa, mtulivu, mvumilivu na anayetumia zaidi
hekima kuliko mabavu”, kiongozi anatakiwa Kuwa na msimamo wa
uvumilivu ni moja ya kazi ngumu zaidi miongoni mwa viongozi dhidi ya wananchi
katika jamii. Ni ukweli ambao haufichiki kuwa viongozi hawakuzaliwa
wakiwa wavumilivu, lakini lazima tujifunze kuwa wavumilivu. Na hii ni kweli
hata kwa jamii inatupasa kuvumiliana na kumaliza tofauti zetu kwa busara ya
majadiliano.
Katika siasa uvumilivu wa
kisiasa unakuza utamaduni wa utawala bora na ukomavu wa demokrasia; na
Kwa demokrasia kufanya kazi vizuri, wananchi lazima kuwa tayari kuvumilia na
kuvumiliana.
Dhana ya uvumilivu ni ya
msingi sana kwa maendeleo kwani inaruhusu mawazo mapya ndani ya jamii; kupitia
dhana hii ya uvumilivu, kiongozi anakuwa tayari kukubali na
kuheshimu maoni na mawazo ya watu wengine na haki zao kwa uwazi na uhuru.
Katika hali hii,uvumilivu huruhusu kuwepo kwa vyombo huru vya habari
kutumika kama chombo muhimu kuwahabarisha wananchi na kuwasilisha madai yao kwa
viongozi wao.
Demokrasia inahitaji
vyombo vya habari ambavyo hugeuka kuwa daraja la mawazo kati ya viongozi na
waongozwa. Vyombo huru vya habari husaidia wananchi kuelewa
taratibu ambazo zinaimarisha demokrasia.uvumilivu wa viongozi huru utasaidia
kueneza demokrasia na uwajibikaji kwani wananchi wataweza kukosoa
serikali na ujumbe kufikishwa serikalini bila kuogopa.
Ni ukweli kuwa Falsafa
ya Uvumilivu hufunza na kuwakumbusha viongozi na wananchi wake
kuwa wanatakiwa kuishi kulingana na fikira njema. Mwenye kuifuata falsafa ya
uvumilivu hayuko tayari kuamsha fikra mbaya za uvunjajiwa amani bali daima
atajitaidi kuziepusha kwa kuendeleza uamuzi wa uwazi na kwa kutumia
njia ya utulivu wa hekima kupitia uzoefu makini wa kimantiki: Kiongozi
mwenye uvumilivu daima hutafakari, na kuziweka fikira mahali pamoja kabla ya
kufanya uamauzi.Msingi wa kimaadili wa falsafa ya uvumilivu kama mtaalam
mmoja alivyo wahi kusema kuwa kwa ufupi tunaweza kusema kuwa uvumilivu
umesheheni nini?
Kwa wananchi wa Tanzania
bado tuna kila sababu ya kuendelea kuenzi na kuthamini uvumilivu miongoni
mwetu; uvumilivu kati ya wananchi wa dini tofauti, kusikilizana na kushauriana
kwa faida ya taifa letu; tukiweza kuutumia uvumilivu katika kiwango cha juu
tutafanikiwa kuondoa chuki ambayo inaanza kueneakatika taifa letu;
Kwa ufupi Uvumilivu
tunaweza kuueleza kuwa:
- Tendo lililojaa subira kubwa,
- Tendo lililojaa utu,
- Tendo ambalo linaashiria Ukuaji wa demokrasia
Ni ukweli ambao haufichiki
kuwa sisi kama wananchi tukiweza
kuvumiliana katika maisha yetu ya kawaida, na kuweza kukosoana bila kugombana mara
moja hurudisha imani ya wananchi, upendo na matumaini kati wananchi wao
kwa wao au dhidi ya serikali yao; Tukumbukwe kuwa Ingawa watu wengi kufikiria
uvumilivu ni upole na kuto wajibika la hasha uvumilivu ni uwajibikaji
ulio jaa busara na subira;
- Kwa nini uvumilivu wetu unatoweka katika kipindi hiki cha sasa?
- Ni kweli kuwa hakuna nafasi ya wananchi kuvumiliana katika kuchangia hoja katika mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Taifa letu au pale kunapotokea kutofautiana?
- Kuna maswali mengi sana ya kujiuliza hasa katika kipindi hiki ambapo kuna mwendelezo wa fujo.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA TUJALIWE TUWEZE KUDUMISHA UVUMILIVU
No comments:
Post a Comment