WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, October 21, 2012

Hawa ndiyo maadui wa Waisalam na Uislam @MohamediMtoi

21/10/2012

Ndugu zangu.


Tunapokuwa tunajiuliza mhemuko wa udini unatoka wapi au nani wameusababisha na kuuasisi, si vibaya tukajua maadui wakuu kwa upande wetu Waislamu. Ukimjua adui ni rahisi kupambana naye na ni nusu ya ushindi kwenye vita ya kutafuta haki au usawa au kuondoa tunao uita unyanyasaji kwa waislamu au mfumo kristo kama wengine wanavyopenda kuita (Mimi sio muumini wa dhana ya mfumo Kristo) maana nimeona wakati wote Waislamu wenzangu wakishika nafasi kubwa Serikalini, kwenye mashirika ya umma na hata mashirika binafsi.



Siuoni mfumo Kristo kama unavyoitwa au kama baadhi ya Waislamu wenzangu wengine wanavyotaka kuaminisha umma wa Kiislamu juu ya hii dhana. 



Nasema sioni kwa kuwa bado naamini katika uwezo na si mfumo Kristo, siuoni kwa kuwa hii nchi ni ya Wakristo, Wapagani, Waislamu, Wahindu na dini nyingine. 



Siuoni mfumo Kristo kwa kuwa nimeshuhudia watu kama kina Omari Mahita, na Said Mwema wakiwa viongozi wa vyombo ambavyo mara kadhaa vimesababisha mauaji ya Waislamu wenzetu na ndugu zetu Wakristo. 



Mtanisamehe bure wenye mtazamo tofauti na wangu lakini siuoni mfumo Kristo nikimwangalia JK na Makamu wake. Siuoni mfumo Kristo nikimuangalia wajina wangu Mohamedi Shein na Seif Shariff Hamad. Siuoni mfumo kristo nikimwangalia Chande Othman yule jaji mkuu na Othman Rashid, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Si uoni hata nikiungalia kwenye Wizara na Taasisi nyingine za Serikali.



Wanaoongela mfumoKristo hawana uthibitisho wa kutosha kuhalalisha madai yao ambayo kwa sasa nayaita hayana mashiko bali yametawaliwa na ukame wa maono na kiangazi cha fikra kinachopiga macho pazia mchana wa jua kali.



Kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu, lazima tutambue kuwa adui wa Waislamu siyo Wakristo, Wapagani, Wahindu au dini nyingine zinazopatikana kwenye huu ulimwengu.



Lazima tujue kuwa sisi ni ndugu tunaohitaji kuishi kwa upendo na kuvumiliana bila kuathiri imani zetu, na ikitokea lazima tutafute njia za amani kupata suluhu.



Kwa mtazamo wangu hawa ndio maadui wakubwa wa Uislamu kwa Tanzania.



1. Adui namba moja kwa Waislamu ni kutokuwa na mashule na vyuo vingi vyenye kutoa elimu bora kwa vijana wa Kiislamu na hata wale wa upande wa pili wanaokuja kuitafuta elimu. Najua kuna watu watapinga sana lakini ukweli mchungu lazima tuuseme ili tupate pa kuanzia. Mtakuwa mashahidi hata shule tulizonazo hazifanyi vizuri sana kwenye mitihani ya Kitaifa lakini pia hata mashule yetu hayana mfumo wa kuandaa Masheikh walioiva kwenye elimu dunia na akhera. Mimi napendekeza harakati zetu ziwe kwenye kujenga mashule ya viwango pamoja na kuajiri walimu bora bila kujali dini zao ili kuwaandaa vijana bora wanaoendana na kasi ya sayansi na teknolojia kuelekea soko la ajira ya ushindani na pia viongozi bora wa dini.



2. Ni kukubali kufanywa nyezo ya CCM kupata uhalali wa kutawala kwa kura za Waislam. Lazima tujue kuwa CCM wametutumia vya kutosha na kutudanganya vya kutosha, sasa tuseme basi! Mfano, Wametudanganya swala la Mahakama ya Kadhi wakati wa kampeni za 2010, Waislamu waliotaka tuwe na Kadhi kwa kauli hadaa ya CCM wakapiga kura za kuhadaiwa lakini baada ya matokeo wakatugeuka! Huku ni kuonekana kuwa tu-malofa wa kudanganywa. Tuunge mkono chama ambacho hakitatugawa lakini pia ambacho hakitatugawa na kuharibu umoja wetu wa kitaifa.



3. BAKWATA imekuwa ni kama taasisi ya CCM. Wanamuweka wanayemtaka wao. Lazima tupiganie BAKWATA iwe chombo huru cha Waislamu na tuwaweke viongozi wenye maono mapana tunaotaka sisi, na siyo CCM,  hii itasaidia kurejesha imani kwa BAKWATA. Napendekeza vigezo vya kuiongoza BAKWTA viwe ni kwa kiwango cha PhD kwa kuangalia uwezo wa elimu akhera na elimu dunia, lakini pia pamoja na uwezo wa kuongoza na kusimamia mambo. Chuo Kikuu cha MUM kinaweza kusaidia kuratibu kupatikana wataalamu na watendaji wengine wa BAKWATA ambao nao kiwango cha chini cha kuanzia kiwe Shahada moja na kuendelea.



4. Kutokufuata mafundisho ya mtume. Mtume wetu Muhammad S.A.W alikuwa mwema, mwingi wa hekima na busara. Lazima tuyafuate mafundisho yake na kukumbushana mema na kukatazana mabaya. Uislamu haujajengwa kwenye misingi ya uhasama, vurugu, fujo, chuki na mambo mengine mabaya. Uislamu umejengwa kwenye misingi ya usafi wa matendo mema, kumcha Mungu, ukarimu, na kuhurumia na kuwajali wengine. Tukiyafanya haya tutawaepuka wale wanaoutumia Uislamu wetu kama daraja ambalo baadaye hutuchafua wote. Mfano, wale walioingia kuchoma na kuvunja Makanisa na kuiba sadaka, baadhi ya vifaa vya Kanisa na mikate.



"Uislamu ni unadhifu" hii ni moja ya tafsiri ya hadithi za mtume wetu kipenzi Muhammad S.W.A.



Tuyafuate mafundisho yake kwa matendo ili tumuenzi kipenzi chetu.

---
Imeandikwa na Mohamedi ‘Moudy’ Mto


Source: http://www.wavuti.com

No comments:

Post a Comment