Habari imeandikwa na Lucy Lyatuu via HabariLeo
BARAZA la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT) limeomba radhi kwa kitendo cha kukojolewa Kitabu Kitukufu cha Korani.
Pia limeiomba Serikali kushirikisha mabaraza yote ya kidini kuunda tume huru itakayosimamia na kuishauri juu ya uendeshaji taasisi na jumuiya za kidini nchini.
Halikadhalika limeitaka Serikali kubana wahusika wa uvunjwaji wa makanisa na kurejesha mali zilizoibwa na kulipa fidia za uharibifu wa kuchoma makanisa 10 yaliyoko Tanzania Bara.
Tamko hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Askofu Dk Mwigulu Kilimba likitokana na mkutano wa siku mbili wa maaskofu na wachungaji zaidi ya 1,000 waliokutana kujadili vurugu na ghasia za kuchomwa moto makanisa, Biblia kuchanwa na kupigwa kwa watumishi wa Mungu hivi karibuni.
Alisema vurugu hizo zilitokana na kitendo cha mtoto kukojolea Korani Mbagala jijini Dar es Salaam, kitendo kilichowahuzunisha na kuwafadhaisha.
“Baraza linaomba radhi kutokana na kitendo hicho, kwani kama mmoja asingemshawishi mwenziwe, yaliyotokea yasingetokea,” alisema Dk Kilimba na kuongeza kuwa kitendo cha kukojolea Korani hakijawafurahisha.
Alisema baada ya kitendo hicho, vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani zilitokea na Baraza linaiomba Serikali irejee misingi ya Katiba kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia isiyo na dini, ili kusaidia kuondoa hisia za kundi moja la dini kuona watawala wako upande wa dini fulani.
Kwa mujibu wa Dk Kilimba, Baraza limeiomba Serikali kushirikisha mabaraza yote ya kidini nchini na kuunda Tume Huru itakayokuwa na jukumu la kusimamia na kuishauri Serikali juu ya uendeshwaji wa shughuli za taasisi na jumuiya za kidini.
“Jambo hili litasaidia kubainisha mipaka ya kiutendaji kwa shughuli za kidini na mamlaka ya nchi, hivyo kuondoa dhana ya kutaka kuingiza udini kwenye siasa,” alisema Dk Kilimba na kuwaomba waumini kuendelea kudumisha hali ya utulivu na amani.
Aliiomba Serikali itambue kuwa macho na wapenda amani nchini wanasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa kwa watuhumiwa wa matukio ya uvunjwaji wa makanisa Zanzibar na Tanzania Bara.
Siku za karibuni nchi imekuwa katika vurugu za kidini ambapo wafuasi wa dini ya Kiislamu wamekuwa wakifanya maandamano na kushambulia makanisa huku wakiyachoma moto na kupora mali zilizomo na pia baadhi ya magari yakipondwa mawe na kuharibiwa.
Sehemu ya vurugu hizo ilichangiwa na mtoto mwenye umri wa miaka 14 kukojolea Kitabu cha Korani kutokana na ubishani na mtoto mwenziwe aliyemtishia kuwa akifanya kitendo hicho atageuka panya au nyoka.
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment