Waandishi Wetu
POLISI nchini wamepanga kusambaratisha mtandao unaodhamini na kuchapisha vipeperushi vinavyohamasisha kufanyika kwa maandamano, kutaka kutolewa kwa Katibu wa Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake.
Hatua hiyo imekuja baada ya waumini hao kupanga kufanya maandamano Novemba Mosi, ambayo yatahamasisha mahakama hiyo kutoa dhamana kwa kiongozi wa taasisi hiyo na wenzake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema wataanza kufanya msako wa wote wanaohamasisha, wanaochapisha na wanaotoa vipeperushi ili kuwakamata.
“Tunafuatilia wadhamini na wachapishaji wa vipeperushi kwani ni chanzo cha uchochezi na upotevu wa amani nchini,” alisema Kova.
Kova alisema maandamano hayo ambayo yamepangwa na waumini hao yanatishia amani , wananchi watashindwa kwenda kazini na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Hatuna mazungumzo tena kwa suala lolote litakalotishia uvunjifu wa amani hasa kwa yeyote atakayefanya maandamano bila kibali, hatutangalia anatoka dini gani au chama gani hivyo polisi itafanya kazi yake na kuwachukulia hatua kali,” alisema Kova na kuongeza:
“Kisheria kumtishia mtu siyo lazima utumie bomu, bali unaweza ukatumia kauli au vipeperushi kama hivyo vya maandamano.”
Alisema wazazi watakaoruhusu watoto wa shule kufanya maandamano watachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani, ikiwezekana kufungwa mwaka mmoja jela.
“Nimesikia wanataka kuwahusisha watoto wasiende shule, ili wafanye maandamano ambayo yanazuiwa na sheria ya mtoto kutofanya maandamano,” alisema Kova na kuongeza:
“Sisi tutahakikisha sheria inachukua mkondo wake, kama kuna mtu amefikishwa mahakamani kuna taratibu zake za kupata dhamana, siyo kufanya maandamano haramu.”
Pia, aliwaomba wananchi wasishiriki maandamano hayo kwani yataleta madhara makubwa kwa familia zao kwa wale watakaokamatwa.
“Hii inajidhihirisha pale utakapotembelea familia za wale waliokamatwa katika maandamano yaliyopita, watoto wanashindwa hata kwenda shule kutokana na kukamatwa kwa wazazi wao na wanakosa nauli na chakula,” alisema Kamanda Kova.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment