Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na wananchi wa
kijiji cha Chwaka na kuwapongeza kwa kufungua ukurasa mpya wa maelewano na
kumaliza mzozo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 kati yao na wanakijiji wa
Marumbi.
Akizungumza na wanakijiji hao waliojaa katika viwanja
vilivyopo pembezoni mwa skuli ya Chwaka Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusibni Unguja,
wakiwa na hamu na furaha ya kumsikiliza kiongozi huyo kama walivyomuomba na
yeye kutimiza ahadi yake ya kwenda kijiji hapo aliyoitoa Agosti 15
alipozungumza na wanakijiji wa Marumbi, kwa lengo la kutafuta Sulhu kufuatia
mzozo wa bahari kati ya Marumbi na Chwaka.
Katika maelezo yake Dk. Shein
aliwataka wananchi hao watambue kuwa wao ni ndugu wa damu hivyo hakuna haja ya
kugombana na hasa ikizingatiwa chanzo cha ugomvi huo ni bahari ambayo bahari
hiyo imeumbwa na MwenyeziMungu na ni ya Mungu hivyo wao wanatakiwa waitumie
ipasavyo.
Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao jinsi alivyofarajika na
kufurahishwa na risala yao waliyoelezea azma yao ya kufukia chuki, hasama na
ugomvi kati yao na wanakijiji wa Marumbi ambao ni ndugu zao wa damu.
Dk. Shein aliwakata wananchi hao wa Chwaka kutambua kuwa
kijiji hicho kina historia kubwa ya maendeleo pamoja na historia ya watu wake
ambao ni wachapa kazi mahiri hasa katika sekta ya uvuvi na wanajulikana Afrika
Mashariki yote.
“Leo kwangu ni siku ya furaha baada ya kusikia risala yenu
iliyoandikwa ikaandikika na iliyosomwa ikasomeka… Sulhu ni jambo muhimu kwani
hata Mtume wetu Muhammad (S.A.W), alifanya Sulhu iliyoitwa kwa jina la Sulhu ya
Hudaibiya”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein aliwapongeza wananchi hao wa Chwaka kwa
kuwa na hamu ya maendeleo na kukubaliana na ombi lao la kuiomba Serikali kuimarisha
uvuvi wa bahari kuu, na kuwaeleza kuwa hilo ndio lengo kuu la Serikali hivi
sasa kwa kushirikiana na wawekezaji na mchakato wake ndio unaendelea na si muda
mrefu utakamilika.
Alisema kuwa tayari Serikali imeshatuma ujumbe kwenda nchi
mbali mbali duniani zikiwemo China na Shelisheli kwa lengo la
kupanua wigo juu ya sekta hiyo ya uvuvi hasa wa bahari kuu. “Bahari kuu
haijaguswa na ndio maana zinakuja meli kutoka nje zinakuja kuwaiba samaki
wetu”,alisisitiza Dk. Shein.
Pia, Dk. Shein alieleza kuwa nchi hii ni ya demokrasia na
kila mmoja ana uhuru wa kuwa na chama chake hivyo hakuna haja ya kubaguana na
kutambua kuwa siasa sio ugomvi na kuwataka viongozi wote wa Chwaka kuwatumikia
wananchi wote bila ya kuwabagua kwani wote wanahaki ya kupata huduma za Serikali.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuziheshimu
na kuzifuata sheria na taratibu za nchi zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya
mwaka 1984 na kusisitiza kuwa hakuna nchi hata moja duniani inayotunga sheria
yenye kuwakandamiza wananchi wake.
Kutokana na hatua hiyo aliwataka wale wote wanaodai kuwa
Sheria ya Uvuvi iliyopo hivi sasa ina mapungufu watambue kuwa kuna taratibu
nyingi za kuondoa mapungufu hayo huku akisisitiza kuwa Baraza la
Wawakilsihi haliwezi kutunga Sheria kandamizi.
Alisema kuwa Zanzibar haipo peke yake hivyo ni lazima
ifuate sheria na taratibu za Kimataifa na kusisitiza kuwa Sheria zimetungwa
kwenda na wakati na ikibainika kuwa kuna kipengele kimepitwa na wakati ama
sheria yenyewe basi inaweza kubadilishwa. Dk. Shein aliwataka wananchi na
wanakijiji wa Chwaka kutunza mazingira ya bahari.
Sambamba na hayo, aliwaeleza azma ya Serikali ya kuamua
kuviwezesha vikundi vya ushirika kupitia mfuko maalum wa kujitegemea ambao
utakapozinduliwa wananchi wote watapewa taarifa kwani tayari umeshaanza
kukushanya fedha kwa madhumini hayo.
Kwa upande wa tatizo ukosefu wa huduma ya maji safi na
salama katika kijiji hicho, Dk. Shein aliwaahidi wananchi hao kuwa ataungana na
viongozi wengine kutoa mchango wake wa mabomba akiwemo Balozi Seif Idd na kueleza
kuwa serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo muhimu pamoja na
kutatua changamoto nyengine.
Nae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja ambae pia, ni Mkuu
wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis aliwapongeza wananchi wa
kijiji cha Chwaka kwa juhudi zao hizo na kuwataka watambue kuwa ustahamilivu na
uvumilivu sio udhaifu.
Mapema wakisoma risala yao, wananchi hao walieleza kuwa
watu wa Marumbi ni ndugu zao wa damu kwa hivyo suala la shari na kumwaga damu
kwa masuala ya bahari hawatoyapa nafasi tena na litabaki kuwa historia.
“Sisi watu wa Chwaka tunakupongeza kwa umahiri wako wa
udokta wa kutibu donda hili la miaka mingi kwetu, hili sasa sio ‘issue’ tena
kwa sababu wasuluhishaji wako walituunganisha pamoja na ndugu zetu wa Marumbi”,
walisema wananchi hao.
Aidha, waliiomba serikali kuwawezesha kuvua katika bahari
kuu na kusisitiza kuwa Zanzibar ina rasilimali za kutosha kuanzia
Kizimkazi Mashariki na Kaskazini Mashariki mpaka Msuka kisiwani Pemba ambako wapo samaki wengi ambao
hawajavuliwa.
Wananchi hao walitoa shukurani kwa Dk. Shein pamoja na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwashukuru viongozi wote walioshiriki katika
kuleta Sulhu ya mzozo wa Chwaka na Marumbi.
“….. na hii leo baada ya miaka 33 historia imejirea, kwa
wewe Mheshimiwa Ali Mohamed Shein kuja kwetu moja kwa moja kuzungumza na watu
wa Chwaka, hili ni somo kubwa sana kwetu juu ya upendo wako, sisi watu wa
Chwaka tunasema MwenyeziMungu akupe umri wenye mafanikio”, walieleza wananchi.
Sambamba na hayo, wananchi hao walizieleza changamoto
mbali mbali zinazowakabili katika upande wa sekta ya elimu, maji safi na salama, rasilimali za
mawasiliano ya simu, nyumba kongwe, utawala bora na nyenginezo ambapo miongoni
mwa viongozi waliohudhuria katika mkutano huo akiwemo Waziri wa Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban aliahidi kuzifanyia kazi.
Imewekwa na MAPARA
No comments:
Post a Comment