SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa yake ya uchunguzi kuhusu kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, umeibuka utata wa mali alizokuwa akimiliki, huku akidaiwa kumiliki utajiri wa kutisha likiwamo jengo la ghorofa.
Habari za kiuchunguzi zilizopatikana zinaeleza kuwa mbali ya jengo hilo, Kamanda Barlow anadaiwa pia kumiliki magari zaidi ya saba yakiwamo malori mawili aina ya Fuso, malori mawili ya mchanga, gari dogo aina ya Toyota Cresta pamoja na Toyota Hilux Double Cabin.
Magari hayo yanadaiwa kuhifadhiwa eneo la Nyakato mjini Mwanza, yakisimamiwa na mfanyabiashara mmoja kwa niaba yake.
Mbali na magari hayo kamanda hyo anatajwa kumiliki nyumba ya kifahari mkoani Mara, ambayo aliijenga alipokuwa RPC mkoani humo, huku nyumba nyingine ikiwa maeneo ya Capri-Point jirani na Ikulu ndogo mkoani Mwanza, inayoelezwa kuwa aliinunua baada ya Serikali kutangaza uuzaji wa nyumba zake kwa watumishi wake.
Umiliki wa mali hizo umeibua maswali mengi, wengi wakitaka kujua iwapo zinalingana na kipato cha Kamanda Barlow, licha ya kuwa na cheo cha Kamanda wa Polisi wa mkoa.
Jengo la orofa
Moja ya mali za Kamanda huyo ambazo zimeanza kuwa gumzo mjini Mwanza ni jengo la ghorofa ambalo ujenzi wale ulikuwa ukiendelea katika kiwanja Namba 173 Block G, eneo la Nyakato Mahina kwa kibali Na. 6400 (Building Permit), kilichotolewa na ofisi ya Mhandisi Jiji la Mwanza kikiruhusu kujenga jengo la ghorofa tatu.
Mhandisi wa Jiji la Mwanza, Boniface Nyambele alikiri Kamanda Barlow kuomba kibali cha kujenga jengo la ghorofa katika kiwanja hicho na kwamba, hata ujenzi wake walikuwa wakiufuatilia kwa karibu.
“Kibali kilichotolewa hapa kilikuwa ni kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa tatu, alipoanza ujenzi alieleza kuwa anataka kujenga ghorofa tano, lakini baada ya kukagua jengo hili tulikuta foundation yake ikiwa na uwezo wa kuhimili ghorofa tatu tu, tulimzuia,” alisema Nyambele.
Hata hivyo, mmoja wa wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa marehemu Kamanda Barlow, aliwasisitiza kujenga ghorofa tano.
Alisema kwamba kila mara kamanda huyo alikuwa akiwaeleza kuwa masuala ya vibali kutoka Jiji wanapaswa kumwachia yeye licha ya wakaguzi kumkatalia.
“Baada ya kuwa tumejenga hapa ,mwezi mmoja kabla ya kufariki alituita na kumweleza fundi wetu mkuu kuwa alikuwa amebadili mawazo ya kujenga jengo la ghorofa tatu na kwamba, mpango wake sasa ulikuwa ni kuongeza ghorofa nyingine mbili juu,” alisema mmoja wa wasimamizi wake wa ujenzi na kuongeza: “Alipoelezwa kama kisheria haikubaliki, alidai hayo hayamuhusu atasimamia yeye huko kwenye sheria.”
Mwandishi wa habari hizi alifika eneo linapojengwa ghorofa hilo na kushuhudia ubao unaoonyesha kuwa kibali cha ujenzi wa jengo hilo kimetolewa kwa Liberatus Barlow.
Hata hivyo, majuma machache kabla ya kifo chake, eneo hilo la ujenzi kulitokea wizi wa nondo za ujenzi, ambapo baada ya tukio hilo mwangalizi wa jengo hilo na baadhi ya mafundi wake walikamatwa na kuwaweka mahabusu kwa siku nne katika Kituo cha Polisi Nyakato Mwatex huku ikielezwa kuwa kamanda huyo aliwatoa baada ya kukubaliana nao kumlipa nondo zilizopotea.
“Siku ya wizi huo ujenzi ulisimama na tulikamatwa na kulazimishwa kulipa nondo 10 alizodai zimeibwa, lakini msimamizi wetu nakumbuka aliamua kulipa yeye badala yetu na kesi iliishi baada ya kuwekwa ndani siku nne. Alilipa nondo 60 badala ya 10 na huo ulikuwa mwisho wake wa kuendelea na kazi pamoja nasi, ” alisema kijana huyo aliyewahi kufanya kazi ya kibarua katika jengo hilo.
Umiliki wa magari na utata wake
Mali nyingine zinazodaiwa kumilikiwa na Kamanda Barlow ni pamoja na magari, ambapo katika idadi ya magari hayo, gari moja aina ya Toyota Hilux ambalo ndilo alipata nalo ajali limeonekana kuwa na utata katika umiliki wake kutokana na namba hiyo ya usajili kubainika kuwa siyo yake kwa vile ilisajiliwa kwa gari aina ya Nisan Premier inayomilikiwa na wamiliki wawili.
Ingawa umiliki wa magari mengine unadaiwa kusajiliwa kwa majina ya mfanyabiashara maarufu jijini Mwanza, lakini umiliki wa gari ambalo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alipotangaza kifo cha kamanda huyo, alilitangaza pia kuwa ni mali ya marehemu, imebainika kuwa alilipata wiki moja kabla ya kifo chake.
Katika uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, imebainika kuwa hata bima ya gari hilo iliyoonyesha imekatwa kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar, ilikuwa haitambuliki.
Kamanda Barlow alilichukua gari hilo kwa mmoja wa wafanyabiashara jijini Mwanza, ambaye bado jeshi hilo la polisi linamsaka kutokana na utata wa umiliki wake, kuonyesha namba hiyo siyo halisi ya gari hilo.
Meneja wa Tawi la Kampuni ya Bima Zanzibar Mkoa wa Mwanza, Suzan Masele alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alisema kuwa stika ya bima ya gari hilo alilokuwa nalo Kamanda Barlow, wamefuatilia kwenye mfumo wao wa malipo wakabaini kuwa haipo.
"Tumeangalia katika system (mfumo) yetu hakuna bima ya malipo hayo, kwa hiyo ni feki," alisema.
Aidha, utata wa umiliki wa gari hilo pamoja na bima yake ulithibitishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, ambaye alisema jijini Mwanza kuwa jeshi lake lilikuwa likiendelea na uchunguzi wa umiliki wa gari hilo, pamoja na bima yake kujua ukweli na jinsi lilivyoingia mikononi kwa marehemu siku kadhaa kabla ya kifo chake.
“Suala la gari alilokuwa akilitumia marehemu mpaka siku mauti yanamkuta, pamoja na bima yake, hatuwezi kulieleza hapa, kwa sasa bado tunachunguza,” alisema IGP, alipoulizwa na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumaliza kutoa taarifa za awali za uchunguzi wa kifo Kamanda Barlow.
---
Imeandikwa na Frederick Katulanda, Mwanza via mwananchi
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment