TUESDAY, OCTOBER 30, 2012
KAMATI YA LIGI YAIKUMBUSHA YANGA KUMALIZANA NA NJOROGE KUEPUKANA NA ADHABU YA KUSHUSHWA DARAJA - VITUO VYA TV NA REDIO SASA RUKSA KUTANGAZA NA KUONYESHA LIGI KUU KWA MAKUBALIANO MAALUM
1. Kamati ya Ligi jana
(Oktoba 29,2012) ilifanya kikao pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya
Vodacom kujadili mambo kadhaa, likiwemo tukio la Jumamosi iliyopita la kuzuia
televisheni na radio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga
picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari. Kamati
ilifanya mazungumzo na mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
(TASWA), Juma Pinto kuhusu msukosuko huo na kufikia muafaka katika masuala
yafuatayo:
a- kwamba uamuzi wa kuzuia
vituo vya redio na televisheni kutangaza moja kwa moja ulikuwa sahihi lakini
una kasoro katika utekelezaji kwa kuwa hayakuwepo mawasiliano rasmi kwa vyombo
vya habari na pia haukutoa muda wa kutosha kwa vyombo hivyo vya habari kufanya maandalizi
kwa kadri ya utashi wa klabu za Ligi Kuu.
b- Kwamba Kamati ya Ligi
haijakataza redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, bali vituo vya
redio ambavyo vinataka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu vifanye
hivyo bila ya kuweka matangazo ya wadhamini na kama matangazo hayo ya moja kwa
moja yatadhaminiwa, basi vituo hivyo havina budi kuwasiliana kwa maandishi na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa maelekezo zaidi.
c- Kwamba vituo vya redio
vitakavyotaka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, ni lazima zitamke
mashindano hayo kuwa ni “Ligi Kuu ya Vodacom”.
d- Kwamba vituo vya
televisheni vitakavyotaka kutangaza moja kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, ni
lazima viingie mkataba na TFF ambao utaaridhiwa na klabu husika. Kwa sasa,
kituo cha televisheni cha Star TV hakitaruhusiwa kurusha matangazo ya moja kwa
moja ya michezo hiyo hadi hapo mkataba utakaposainiwa na tunatumaini mkataba
huo utasainiwa kabla ya mechi za kesho na hivyo kuwapa fursa wapenzi wa soka wa
maeneo mbalimbali kuendelea kushuhudia Ligi Kuu ya Vodacom.
e- Kwamba vituo vya
televisheni vitakavyotaka kuchukua picha kwa ajili ya habari zinaruhusiwa
kufanya hivyo. Endapo kituo hicho kitaonyesha mchezo uliorekodiwa, hatua
zitachukuliwa dhidi ya kituo hicho.
f- Kamati inaomba
radhi kwa usumbufu uliosababishwa na uamuzi huo, lakini inazidi kusisitiza kuwa
uamuzi huo ulifanywa kwa lengo zuri la kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha
vitakavyoziwezesha klabu kujimudu kiuchumi na kuifanya Ligi Kuu ya Vodacom
iendeshwe kwa ubora zaidi.
2. Kocha mkuu wa timu ya
taifa ya Tanzania, Kim Poulsen amerejea Dar es salaam baada ya kufanya ziara
kwenye visiwa vya Pemba na Unguja ambako alishuhudia mechi sita za Ligi Kuu ya
Grand Malta kuanzia Oktoba 19, 2012 hadi Oktoba 26, 2012 visiwani Zanzibar.
Poulsen alishuhudia mechi baina ya Falcom na Bandari iliyoisha kwa Falcom
kushinda kwa mabao 3-1 na pia mechi baina ya Duma na Bandari ambayo iliisha kwa
Bandari kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Mechi hizo mbili zilifanyika kisiwani Pemba.
Poulsen pia alishuhudia mechi zilizofanyika kwenye
Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja ambako Mtendeni iliibwaga Chipukizi kwa mabao
2-1; Mundu na Jamhuri (0-1), KMKM na Zimani Moto (1-0); na Mafunzo dhidi ya
Chuoni iliyoisha kwa Mafunzo kulala kwa mabao 3-0.
Poulsen amefurahishwa na ziara hiyo na kusema kuwa ni
kitu kizuri kwake na kwa soka la Tanzania kwa ujumla. Poulsen alisema kuwa
amefurahishwa na mapokezi aliyopata visiwani Zanzibar na kukishukuru Chama cha
Mpira wa Miguu cha Zanzibar (ZFA) kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wote
akiwa Zanzibar.
Hata hivyo, Poulsen alisema hawezi kueleza kwa sasa
kama ameona wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha Taifa Stars, lakini
akasema amevutiwa na viwango vya wachezaji wengi.
3. TFF inapenda tena
kuihimiza klabu ya Yanga kumalizana na mchezaji wake wa zamani, John Njoroge
Mwangi kabla ya Novemba 2, 2012 ili ijiepushe na adhabu kaili inayoweza
kuchukuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa
mujibu wa barua ya FIFA, iwapo Yanga haitakuwa imemlipa mchezaji huyo na
kusiwepo na mawasiliano yoyote, shauri hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya
Nidhamu ya FIFA itakayokutana Novemba 14, 2012 kutathmini hukumu iliyotolewa
mapema Januari mwaka huu.
4. Mchezo namba 10 wa Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) baina ya Morani na Polisi Tabora uliokuwa uchezwe Kiteto
mjini Tabora Oktoba 31, 2012, sasa utachezwa Novemba 01, 2012 baada ya treni
ambayo Morani walikuwa wakisafiria kutoka kupata matatizo njiani wakati
wakitoka Kigoma ambako walicheza na Kanembo.
5. TFF inapenda kutoa
ufafanuzi wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari leo, likiwemo
gazeti la Habari Leo na Daily News, vikimnukuu rais wa TFF, Leodegar Tenga
akisema kuwa amewataka watu wanaotaka kugombea uongozi wa shirikisho watangaze
nia ili wapate kujadiliwa. Waandishi walioandika habari hiyo hawakumnukuu
vizuri Rais Tenga wakati akizungumzia masuala ya uchaguzi na hivyo kupotosha
maana nzima ambayo Ndg. Tenga alitaka iwafikie wapenzi wa michezo na hasa mpira
wa miguu. Rais Tenga alivitaka vyombo vya habari vianzishe mjadala
utakaowashirikisha wapenzi wa mpira wa miguu ili waelezee wanatarajia nini
katika miaka ijayo na hivyo kuwafanya viongozi watakaochaguliwa kufanya kazi
kwa utashi wa maoni hayo ya wananchi. Tunaelewa kuwa Rais Tenga ni muumini wa
kuheshimu katiba, sheria na kanuni na hivyo hawezi kutoa kauli ambayo inakiuka
mchakato wa uchaguzi wa TFF kwa kuwataka wanaowania uongozi kutangaza nia sasa
badala ya kusubiri muda wa kikanuni ufike. Ikumbukwe katika kikao chake na
wahariri aliwahi kuulizwa swali kama hilo na akasema kuwa akijibu lolote
atakuwa amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kuwa itamaanisha anaanza kampeniu kabla
ya muda. Ni vizuri waliohusika wakafanya masahihisho ili kuzuia habari zao kutafsiriwa
tofauti na wadau wa mpira wa miguu na hivyo kuweka uwezekano wa kuvuruga
mchakato wa uchaguzi.
6. TFF imebadilisha tarehe
ya kuanza kuchukua fomu kwa watu wanaotaka kugombea uongozi wa Chama cha Mpira
wa Miguu cha Dar es salaam (DRFA) kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato wa
uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa kanuni. Kamati ya Uchaguzi ya DRFA ilitangaza
jana kuwa uchukuaji fomu ungeanza leo, lakini DRFA iliandikiwa barua jana
kuelezwa kuwa mchakato huo sasa utaanza kesho na uchaguzi utafanyika Desemba
12, 2012.
Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA utakuwa kama
ifuatavyo:
30/10/2012 Kamati ya Uchaguzi DRFA kutangaza uchaguzi na nafasi Zinazogombewa kwa mujibu wa katiba ya DRFA
31/10/2012 Kuanza kuchukua fomu za kugombea uongozi
04/11/2012 Mwisho wa kurudisha fomu ifikapo saa 10:00 alasiri
05-09/11/2012 Kamati ya Uchaguzi DRFA kupitia fomu za waombaji uongozi na kutangaza matokeo na kubandika kwenye mbao majina ya
waombaji uongozi.
10-14/11/2012 Kutoa fursa ya pingamizi dhidi ya waombaji uongozi. Pingamizi ziwasilishwe kwa katibu wa Kamati ya Uchaguzi DRFA na wawekaji pingamizi wazingatie Ibara ya 11 (2) ya Kanuni
za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
15-17/11/2012 Kujadili pingamizi, usaili na kutangaza matokeo ya usaili na kuwajulisha kwa maandishi.
18-20/11/2012 Kukataa rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA
21-25/11/2012 Rufaa kusikilizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kutangaza matokeo ya rufaa (Kama hakuna rufaa, Kamati ya Uchaguzi
ya DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi
wanazogombea na kuanza kampeni).
26/11/2012 Baada ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi
zao na kuanza kwa kampeni
12/12/2012 Uchaguzi
SOURCE: Shaffih Dauda Blog
No comments:
Post a Comment