Sunday, October 21, 2012
Katibu Mkuu wa CUF
Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi ya wapenzi wa chama hicho katika
viwanja vya Buguruni jijini Dar es Salaam.
Wafuasi na wapenzi
wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati
akiwahutubia katika viwanja vya Buguruni jijini Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mkurugenzi
wa ulinzi na usalama wa ADC Bw. Al-Badawi akizungumza katika mkutano wa hadhara
wa CUF baada ya kuamua kurejea CUF akitokea ADC. Kabla ya kwenda ADC na baadae
kurejea CUF Al-Badawi alikuwa mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke
Katibu Mkuu wa CUF Maalim
Seif Sharif Hamad akimkabidhi shati la chama hicho kijana Joseph Christian
ambaye alikuwa katibu mwenezi wa CHADEMA tawi la Chuo Kikuu Dodoma. Joseph
amekihama CHADEMA na kujiunga na CUF kwenye mkutano wa hadhara huko Buguruni
jijini Dar es Salaam. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR
Katibu Mkuu wa Chama Cha
Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea kutetea
na kutekeleza sera yake ya kuwaunganisha watanzania popote walipo bila ya
ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema operesheni
mchakamchaka hadi mwaka 2015 iliyozinduliwa na chama hicho hivi karibuni
imekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo, na kwamba tayari imeanza kuleta
mafanikio katika mikoa iliyoanza kutekelezwa ukiwemo mkoa wa Arusha.
Maalim Seif ametoa kauli
hiyo katika viwanja vya Buguruni jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwahutubia
wafuasi na wapenzi wa chama hicho kwenye mkutano maalum wa hadhara uliolenga
kuwakaribisha wanachama wapya na kuwapokea wanachama walioamua kurejea CUF
baada ya kukihama na kuhamia vyama vyengine.
Katika mkutano huo Maalim
Seif aliwapokea na kuwapa kadi za chama hicho wanachama kadhaa walioamua
kurejea chama hicho wakitokea chama cha ADC wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi
wa ulinzi na usalama wa ADC Bw. Al-Badawi.
Kabla ya kujiunga na ADC,
Bw. Al-Badawi alikuwa mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke, na sasa ameamua kurejea
CUF kwa kile alichokieleza kuwa ni ubabaishaji ndani ya chama hicho kipya
kinachohusishwa na mbunge wa jimbo la Wawi Mhe. Hamad Rashid Mohd.
Maalim Seif ambaye pia ni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema Tanzania imekuwa ikipita katika
kipindi kigumu cha migogoro na uvunjifu wa amani, mambo ambayo yanapaswa
kupigwa vita ili kurejesha hali ya amani na kuvumiliana.
Amedai kuwa chanzo kikuu
cha migogoro ya kijamii ikiwemo ya ardhi na mizozo ya kidini inatokana na
kutokuwepo kwa mikakati imara ya kuendesha nchi, na kwamba viongozi wanapaswa
kujifunza kutokana na migogoro hiyo, ili kuweka mikakati imara ya kuendesha
nchi kwa uhakika.
“Nchi haiendeshwi kwa
kuigiza, bali kwa kuwa na viongozi wenye dira ya mabadiliko kwa maendeleo ya
wananchi”, alisisitiza Maalim Seif.
Amesema kutokana na
viongozi kutokuwa na dira na mikakati imara ya kuendesha nchi, Watanzania
wameshindwa kunufaika na rasilimali za nchi yao ambazo ni nyingi na zinaweza
kuwabadilisha kiuchumi.
Amefafanua kuwa iwapo
wananchi watanufaika moja kwa moja na rasilimali zao, wataweza kuzitunza na
kuzilinda ili ziwe endelevu, na kwamba kinyume chake ni kuzihujumu rasilimali
ambazo watahisi haziwanufaishi.
“Popote pasipo na haki
hakuna amani, tunataka kila Mtanzania ajihisi kuwa ana haki sawa katika nchi
hii, sio kuwa na raia wa madaraja, yaani daraja la kwanza, la pili na la
tatu”,alifahamisha huku akishangaliwa na umati wa watu waliojitokeza kwenye
mkutano huo.
Katika hatua nyengine,
aliyekuwa katibu mwenezi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika
tawi la Chuo Kikuu Dodoma bw. Joseph Christian amejiengua katika chama hicho na
kujiunga na CUF.
Akizungumza katika mk
utano huo bw. Joseph
amesema ameamua kujiengua CHADEMA na kujiunga na CUF kwa madai kuwa chama hicho
kimekuwa kikiendeshwa kwa misingi ya undugu na ukabila, na kuwatelekeza vijana
wenye lengo la kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini.
Amewatahadhamisha vijana
kuwa makini na sera za chama hicho na kuacha kukurupuka kuvamia sera za vyama
wasivyovifahamu.
Nae Mwenyekiti wa ADC
Wilaya ya Kinondoni Bw. Saburi Mtoro, ambaye pia ameamua kukihama chama hicho
na kujiunga na CUF amemuahidi Katibu Mkuu wa CUF kuwa wanachama wote wa ADC
katika Wilaya hiyo watajiunga na CUF.
Imewekwa na MAPARA
No comments:
Post a Comment